Tuesday, May 30, 2017

SIMULIZI, NILIKIONA CHA MOTO USRITHI WA BABU SEHEMU YA 33

ZULIA LA FAKI
 
NILIKIONA CHA MOTO URITHI WA BABU 33
 
ILIPOISHIA
 
“Kumbe babu  yako alikuwa na mke jini, ndiyo  maana alipata utajiri ghafla! Lakini hakuwahi kunieleza hata siku moja. Alikuwa  msiri sana”
 
“Huyo jini sasa amejitokeza kwangu na anataka nimrithi ili anipe utajiri aliokuwa nao  babu yangu”
 
“Sasa ulitaka nikupe ushauri gani?”
 
“Nimkubalie au nimkatalie?”
 
Mganga baada ya kutafakari aliniambia.
 
Umefanya vizuri kuja kwangu. Mimi nitakupa ushauri mzuri”
 
“Nitakushukuru sana”
 
“Usikubali. Huyo  jini atakusumbua sana na pengine atakuja kukuua. Sasa nimeanza kugundua kuwa hata babu yako aliuawa na huyo jini”
 
SASA ENDELEA
 
Maneno ya mganga huyo yakanishitua.
 
“Kumbe hivi viumbe vina madhara makubwa?” nikamuuliza
 
“Wewe hujui tu. Hawa viumbe si wazuri. Uliona wapi jini akaolewa na binaadamu?”
 
“Sijawahi kuona”
 
“Sasa ujue kuwa hicho kitu hakiwezekani. Huyo jini anakilazimisha kwa nia mbaya. Amemuua babu yako, sasa anataka kukuua wewe”
 
Nikabaki nimepigwa na butwaa la mshangao.
 
“Wewe angalia vituko na miujiza aliyokufanyia ndipo utajua ana madhara ya kiasi gani”
 
“Sasa nifanye nini ili niweze kuepukana naye?”
 
“Njoo kesho asubuhi, nitajua jinsi ya kukusaidia. Huyo hawezi kuondoka mwenyewe mpaka  nimuondoe mimi”
 
“Sasa hapo kesho utakuja kumuondoa?”
 
“Nitamuondoa na utaishi kwa usalama. Wewe ni binaadamu, wajibu wako ni kuoa binaadamu mwenzako mzae watoto na sio jini. Kama utaoana  na jini mtazaa watoto gani? Mtazaa binaadamu au majini?”
 
Mganga aliniuliza swali hilo  lakini sikuwa na jibu. Nikaona kweli ushauri wa kumrithi yule jini haukuwa na maana.
 
“Kama ulivyoniambia nitakuja kesho unishighulikie” nilimwambia mganga huyo kabla ya kuagana naye.
 
Nilipoondoka nyumbani kwa mganga huyo niliona  mawazo yake yalikuwa sahihi. Si tu ningejitafutia  matatizo  mimi mwenyewe kwa kukubali kuishi  na jinni bali pia sikuwa na uhakika tungezaa watoto wa aina gani.
 
Kama tungezaa watoto wa kijini wasingekuwa na manufaa kwangu na hata kama watoto hao wangekuwa ni binaadamu bado wasingekuwa binaadamu kamili, wasingeweza kuishi na watu wengine.
 
Lakini kulikuwa na kitu kilichojificha ambacho nilikuwa sikijui. Nilikuwa sijui  kwamba yale maneno ya yule mganga yalikuwa  ni ya roho mbaya. Alikuwa akitia  fitina ili mimi nisimrithi yule mwanamke wa kijini kwa kuona kwamba nitaidi utajiri wa bure.
 
Lengo lake la kuniambia niende kesho lilikuwa ni kutafuta  mbinu  ili amchukue yeye jini huyo.
 
Asubihi ya siku ya pili yake nikaenda tena kwa mganga huyo.
 
“Sasa mwanangu unajua hii kazi haitafanyika hapa. Itafanyika shanbani kwangu. Itabidi twende shamba” akaniambia.
 
“Sawa. Tunaweza kwenda. Gari lipo”
 
Mganga akaandaa vifaa vyake. Akawachukua wasaidizi wake wawili ambao bila shaka alishawaeleza tunakwenda shamba kufanya nini.Tukaondoka  na  gari.
 
Shamba hilo lilikuwa kule kule  Chanika lakini lilikuwa mbali kidogo.  Akaniambia tuingize gari ndani ya shamba hilo. Nikaliingiza gari na kulisimamisha mbele ya nyumba yake ya miti na udongo iliyokuwa katikati ya shamba.
 
Tukashuka na kuingia kwenye ile nyumba.
 
Kwa  jinsi  nilivyofahamu baadaye ni kuwa ili aweze kumchukua Maimun alitaka kwanza aniue mimi na ndiyo madhumuni ya kunipeleka huko shamba.
 
Baada ya kuniua alitaka achukue damu yangu na kuioga mwilini mwake kisha ajipake mafuta ya waridi.
 
Tulipoingia kwenye ile nyumba nikaambiwa nikae chini. Kwanza  kilianza kisomo. Nilisomewa na watu watatu bila  kuambiwa ninasomewa nini.
 
Baada ya kisomo hicho mganga alikoroga dawa kwenye kikombe akanipa ninywe.
 
“Kunywa hii dawa” alinaimbia kisha akaongeza.
 
“Nitakupa na dawa nyingine ya kuoga”
 
Kumbe ile haikuwa dawa. Ilikuwa sumu! Alitaka niinywe ili  nife pale pale na kisha wanitoe damu kabla haijakauka.
 
Kile  kikombe nilikipokea nikakisogeza midomoni mwangu ili ninywe ile dawa niliyoambiwa. Hapo hapo niliona kikombe kinabetwa. Kikanitoka mkononi na kuanguka chini.  Sumu iliyokuwamo ikamwagika. Yule mganga na wasaidizi wake walikuwa wameshangaa. Aliyenibeta kikombe hakuonekana!
 
Ghafla nikasikia mganga anapigwa kibao  cha nguvu na kuanguka chini. Alivyoanguka alinza kutokwa  na povu mdomoni. Wale wasaidizi wake walipoona hivyo walitimua mbio.
 
Nikabaki nimekaa nikiwa sijui kinachoendelea. Ikabidi niinuke na kumtazama yule mganga. Nikaona amekauka. Tukio hilo likanishitua.
 
Nikatoka nje ya ile nyumba kuwatazama wale waliokimbia lakini sikuwaona.  Nikasikia ninaitwa ndani ya gari langu. Niliposogea kwenye mlango nikamuona Maimun amekaa kwenye siti ya upande wa pili wa dereva.
 
“Ingia twende zetu” akaniambia.
 
Nikafungua mlango wa gari na kujipakia.
 
“Washa gari tuondoke”
 
Nikawasha gari.
 
“Umeuona  upuuzi wako?” Maimun akaniuliza.
 
Kwa vile nilikwenda pale  kwa ajili ya kumfukuza yeye, sikujibu kitu. Nilihisi pengine upuuzi aliokusudia ulikuwa ni huo.
 
“Sisi tunakubaliana kitu vizuri halafu wewe unakwenda kwa mganga! Ulikwenda kwa mganga kufanya nini?” Maimun akaniuliza.
 
Kwa kweli nilitahayari aliponiuliza hivyo. Nikaendelea kubaki kimya.
USIKOSE Uhondo huu kesho hapahapa

No comments:

Post a Comment