Thursday, May 4, 2017

SIMULIZI ZA FAKI A FAKI, NILIKIONA CHA MOTO URITHI WA BABU SEHEMU YA 21

ZULIA LA FAKI, 0655 340572
 
NILIKIONA CHA MOTO URITHI WA BABU 21
 
ILIPOISHIA
 
“Mmmh…! Mganga akaguna. Baada ya kuwaza kidogo aliniambia.
 
“Nakumbuka kulikuwa na msichana alikuwa akimsumbua sana babu yako. Huyo anaweza kujua siri ya mali ya babu yako. Babu yako alikuwa akimpenda na alifikia kumshirikisha kwenye biashara zake”
 
Mganga aliponimbia hivyo nilishituka, nikamuuliza.
 
“Aliwahi kukutajia jina lake?’
 
“Aliwahi kunitajia lakini muda ni mrefu nimelisahau”
 
“Sio  Ummy?”
 
“Sawasawa. Ni Ummy Nasri…”
 
“Lakini huyo msichana si alikufa?”
 
“Mimi sijui kama alikufa”
 
Hapo sasa nikaona nimueleze mkasa mzima wa Ummy Nasir.
 
SASA ENDELEA
 
Wakati wote nilipokuwa nikimueleza mganga huyo, alikuwa amenikazia macho kama vile nilimueleza kitu kigeni ambacho hakuwahi kukisikia.
 
Nilipomaliza maelezo yangu aliniambia
 
“Subiri”
 
Alichukua kipande cha ubao akauchorachora vistari kwa kutumia chaki. Alichora mara ya kwanza akafuta. Akachora mara ya pili akafuta. Alipofuta mara ya tatu alifungua kitabu akasoma kisha  akatikisa kichwa.
 
“Nikwambie ukweli. Mimi ni mganga  na  nimeshafanya kazi hii kwa zaidi ya miaka thelathini sasa,  sijawahi kuona ramli yangu ikiwa  na  kiza kama leo” Mganga akaniambia.
 
Nilishituka kidogo.
 
“Sijakuelewa. Unaponiambia ramli yako ina kiza una maanisha nini?” nikamuuliza.
 
“Ninamaanisha kwamba sina ninachoona. Ramli imefunga. Hapa ninaona  kiza kitupu”
 
“Inapokuwa hivyo inadhihirisha nini?”
 
“Inadhihirisha kwamba tatizo lako halitambuliki au kwa maneno mengine nimeshindwa  kulifumbua”
 
“Ni kwa sababu gani?”
 
“Sijui”
 
“Kwa hiyo huyu msichana atakuwa ni mzuka kama alivyonieleza mwenyewe”
 
“Inawezekana”
 
“Sasa kama yeye ni mzuka ni kwanini ananitokea mimi?”
 
“Hilo jambo liko nje ya elimu yangu. Siwezi kujua”
 
“Kwa hiyo unanishauri nifanye nini?”
 
“Kwa tatizo kama hili, mimi ninakushauri nenda polisi. Huyu mwanamke atakamatwa na atajieleza”
 
“Sidhani kama polisi watashughulikia suala hili”
 
“Mimi  naamini watalishughulikia”
 
“Basi nitakwenda kuripoti polisi”
 
Mazungumzo yangu na mganga huyo yakaishia hapo hapo.  Wakati niko kwenye gari nikirudi, niliamua nifuate ushauri wa yule mganga wa kwenda polisi kwa sababu sikuwa na mahali pengine pa kwenda kuomba msaada.
 
Wakati ninakwenda kwa mganga huyo nilikuwa na furaha kutokana na imani kuwa tatizo langu lingepatiwa ufumbuzi. Lakini  wakati ule narudi  nilikuwa nimepatwa na wasiwasi hasa kutokana na maelezo ya mganga kwamaba anaona kiza  kitupu.
 
Kwanini aniambie anaona kiza kitupu? Tafsiri ya kiza ni kitu gani? Kifo au uzima? Nilikuwa nikijiuliza bila  kupata jibu.
 
Licha ya mganga huyo kutonifumbulia chochote juu  ya kitendawili  cha Ummy,  jambo mmoja  lilikuwa wazi kwamba lile suala lilikuwa gumu na si la mzaha.
 
 
Niliamua niende kituo cha ppolisi cha Kinondoni. Nilipofika nilikutana na polisi waliokuwa kaunta ambao baada ya kuwaeleza tatizo langu  walinipeleka ofisini kwa Inspekta Amour.
 
“Una tatizo gani?” Inspekta huyo akaniuliza.
 
Nikamueleza. Maelezo yangu yalianzia kupigiwa simu na Ummy. Sikutaka kueleza kuhusu ziara yangu ya nchi tatu nilizozitemnbelea ambapo Ummy aliua watu watatu.
 
Nilimueleza inspekata huyo  kwamba nimekuwa nikipigiwa simu na msichana ambaye sikuwa nikimfahamu akinitaka nikutane naye kwa ajili ya kunipa siri ya mali ya babu yangu aliyekuwa amefariki.
 
Nikaendelea kumueleza kuwa mara ya kwanza aliniita katika hoteli mmoja iliyoko Masaki ambako nilikwenda kumuona na kuzungumza naye.
 
Hapo pia sikutaka  kueleza ukweli wa tukio hilo isipokuwa nilieleza kwamba nilizungumza na msichana huyo na akanitaka niende kwao Mwananyamala ili nikutane naye kwa mazungumzo zaidi.
 
Nikaeleza kuwa nilipofika Mwananyamala katika nyumba aliyonielekeza, nilitaja jina lake lakini watu walioniambia kuwa ni wazazi wake waliniambia kuwa Ummy alikuwa ameshakufa miaka mitano iliyopita..
 
Nilimwambia Inspekta huyo kwamba wazazi hao wa Ummy walinionesha picha zake na nikathibitisha kuwa Ummy niliyemuona alikuwa ni yeye lakini la kushangaza ni kuambiwa kuwa alishakufa miaka  mitano iliyopita.
 
Nikaendelea kueleza kuwa baba yake alinipeleka katika kaburi aliloniambia kuwa ni la Ummy  na hakutaka kukubaliana na mimi kwamba Ummy yuko  hai..
 
“Lakini namba yake ya simu waliikubali. Mdogo wake Ummy aliniambia namba niliyowaonesha ilikuwa ya Ummy kweli” nikaeleza.
 
“Huyo  msichana alinipigia tena simu akakubali kuwa yeye alikufa na kwamba ni mzuka uliokuwa unataka kunipa taarifa ya mali za babu yangu na la kunishangaza zaidi ameniambia kuwa ananipenda na anataka niwe mume wake. Haya mambo yameitia wasiwasi sana” nikamaliza.
 
ITAENDELEA kesho hapa hapa tangakumekuchablog

No comments:

Post a Comment