ZULIA LA FAKI
NILIKIONA CHA MTO URITHI WA
BABU 22
ILIPOISHIA
“Sasa ulitaka tukusaidieje?”
Inspekta huyo akaniuliza baada ya kumaliza maelezo yangu.
“Ninaiomba polisi ichunguze
kuhusu huyu msichana na ikiwezekana akamatwe ili ajieleze ni nani. Nimepatwa na
wasiwasi sana hasa baada ya kuambiwa kuwa alishakufa”
“Kazi ya jeshi la polisi nni kulinda usalama wa raia na mali zao. Vile vile
tunashughulikia masuala ya jinai. Kwa vile suala hilo linahusu usalama
wako na linaweza kuingia pia katika jinai, tutakusaidia kufanya uchunguzi”
“Nitashukuru sana”
“Nipatie namba ya huyo msichana”
Nikampatia kachero huyo namba
ambayo Ummy amekuwa akinipigia simu.
Nilipompa namba ya Ummy
aliipiga na kuitega simu sikioni. Baada ya kusubiri kwa sekunde kadhaa
aliniambia.
“Namba inaita lakini haipokelewi”
Akaiondoa simu sikioni na
kuniambia.
“Twende huko nyumbani kwao”
SASA ENDELEA
Dakika chache baadaye,
kachero huyo aliyeonekana kuipenda na kuithamini kazi yake alikuwa amenipakia
kwenye gari la polisi tukielekea Mwananyamala.
Alilisimamisha gari mbele ya
nyumba niliyomuonesha. Mzee Nasri alikuwa amekaa barazani kwenye kiti cha
uvivu akisoma gazeti la lugha ya Kiingeza.
Tulishuka kwenye gari hilo
tukamsalimia mzee huyo.
Baada ya salamu Inspeketab
Amour alijitambulisha kwake kabla ya kumuuliza kama alikuwa anafahamu Ummy
Nasri.
“Namfahamu. Ni mwanagu lakini
alishakufa” Mzee akamjibu.
“Alikufa lini?”
“Alikufa miaka mitano
iliyopita”
Inspekta Amour alinitazama kisha
akayarudisha macho yake kwa yule mzee.
“Unamfahamu huyu kijana?”
akamuuliza.
“Huyu kijana aliwahi kuja
juzi akatuambia kuwa alionana na marehemu lakini hilo jambo tulilipinga
sana kwa sababu marehemu alishakufa”
“Ana uhakika
kwamba alikutana na binti yako unayedai kuwa amekufa na amekuja kutoa
ripoti kituo cha polisi hii leo. Amedai kuwa huyo msichana anamsumbua na
kumsababishia hofu kwani kila mara anampigia simu. Hiyo ndiyo sababu
tumekuja kwako ili tupate ukweli”
“Ukweli ndio huo niliokueleza kwamba huyo
binti alishakufa. Sasa sijui huyo
anayemsumbua yeye ni nani”
“Huyo msichana amemwambia
kuwa yeye ni mzuka wa Ummy”
Mzee akatikisa kichwa.
“Hakuna kitu kama hicho”
“Namba ya simu anayotumia
huyo msichana umewahi kuiona?” Inspekta alimuuliza mzee huyo.
“Alituonesha juzi. Binti
yangu alikubali kwamba ilikuwa namba ya marehemu lakini tangu alipokufa hadi leo ni miaka mitano. Mtu
mwingine anaweza kupewa namba hiyo”
“Una picha za huyo
marehemu??”
“Picha zipo”
“Ningeomba nizione”
Mzee akainuka na kuingia
ndani.
Baada ya muda kidogo alitoka
akiwa na mke wake pamoja na mdogo wake Ummy.
Mke wake na mdogo
wa Ummy walitusalimia wakati yule
mzee akituonesha picha za Ummy.
“Ummy mwenyewe ndiye huyu?”
Inspekta akauliza.
“Ndiye yeye. Picha zote hizi ni yeye”
“Na mna uhakika kwamba
alikufa??”
“Alikufa, naweza hata kwenda
kukuonesha kaburi lake”
“Kwanza ningeomba unipatie
picha mojawapo kwa ajili ya uchunguzi”
“Unahitaji ipi?”
Inspekata alichagua picha aliyoitaka.
Mzee akaichomoa kwenye albamu na kumpa.
“Sasa nipeleke nikalione hilo kaburi lake”
Mzee akatupeleka. Baada ya
Inspekata Amour kuliuona kaburi la Ummy alimwambia mzee Nasri.
“Kaburi nimeshaliona, sasa turudi nyumbani”
Tukarudi. Mke wa Mzee Nasri
pamoja na binti yao walikuwa
wakitusubiri barazani.
“Baba kuna mazingara
yanafanyika siku hizi. Unaweza kuambiwa
mtu fulani amekufa kumbe yuko hai. Sisi
tulikwenda kwa mganga tukaambiwa Ummy
yuko hai amechukuliwa msukule lakini baba yake amekataa jambo hilo” Mke wa mzee Nasri akatuambia.
“Tukiingiza imani kama hizo
tutaharibu uchunguzi. Lakini vyovyote vitakavyokuwa ukweli utabainika muda si
mrefu kwamba Ummy amekufa au amechukuliwa msukule. Tutajua tu….” Ispekta alimwambia.
“Huo uchunguzi utakuwa ni muhimu
sana kwa sababu hilo jambo limeshaanza kututia wasiwasi” Mke wa mzee Nasri alisisitiza.
“Sawa. Hivi sasa
tunakwenda katika kampuni ya simu ili
tujue ni nani anayetumia hii namba ya
Ummy”
“Naamini utampata mtu
aliyezusha huu utata” Mzee Nasri
akatuambia kabla ya kuagana naye.
Tuliondoka na Inspekta Amour
hadi katika ofisi ya kampuni ya simu
inayomiliki namba ambayo Ummy amekuwa akinipigia.
Baada ya Amour kujitambulisha aliomba aoneshwe usajili
wa namba hiyo.
Sekunde chache tu kompyuta ya
kampuni hiyo iliutoa usajili wa namba ya Ummy pamoja na picha yake. Kitu
ambacho kiliniacha hoi na pengine kilimuacha hoi Inspekta Amour ni kuona kuwa usajili
huo ulikuwa na jina la Ummy Nasri na picha ya kitambulisho pia ilikuwa ya Ummy.
Ndipo maswali yalipoanza.
“Hii namba ilisajiliwa lini?” Inspekta Amour akauliza.
“Kwa mara ya kwanza namba hii
ilisajiliwa miaka sita iliyopita. Baada ya kutumika kwa mwaka mmoja iliacha
kutumiwa kwa karibu miaka mitano, tukaifuta”
“Baada ya kuifuta nani alikuja
kuirudisha?”
“Ni mhusika huyo huyo,
alikuja mwezi uliopita akaitaka namba
yake. Kwa vile hatukuwa tumeiuza kwa mtu mwingine tukampatia na hivyo alifanya usajili upya”
“Huyo huyo Ummy Nasir ndiye
aliyefanya usajili upya?”
“Ndiye huyo huyo kama ambavyo picha yake inaonekana”
ITAENDELEA kesho usikose uhondo huu mtamu na mwanana hapo kesho asubuhi na mapema
No comments:
Post a Comment