Tanga, MKUU wa Mkoa wa Tanga, Martin
Shighella, ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania Tanesco Tanga, kuzikatia umeme
taasisi zote na mashirika ambayo yamelimbikiza madeni ya umeme.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana,
Shighela alisema agizo la Rais Magufuli la kuzikatia umeme mashirika na Taasisi
za Serikali linapaswa kuheshimiwa hivyo kulitaka Shirika hilo kuanza mchakato
wa ukataji kwa wadaiwa sugu.
Alisema kuna baadhi ya Mashirika na Taasisi zimekuwa
zikilimbikiza madeni ya umeme ilhali zimekuwa na bajeti ya umeme hivyo ili
kujua umuhimu wa nishati hivyo ni kuzikatia.
“Natoa agizo kwa taasisi za Serikali na Mashirika ya umma
kuhakikisha wanalipa umeme kwa wakati na
kuepuka aibu ya kukatiwa, agizo
la Rais linapaswa kuheshimiwa” alisema Shighella na kuongeza
“Rais ametoa agizo la kila mtumiaji wa nishati ya umeme
kulipa kwa wakati na yoyote ambaye analimbikiza madeni kukatiwa, sisi ni
watendaji kuhakikisha maagizo yake yatekelezwe” alisema
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Tanesco Tanga, Cesilia
Msangi, amewataka watumiaji wa umeme Tanga kuhakikisha wanalipa Ankara zao kwa
wakati ili kuepuka kukatiwa umeme.
Alisema kwa sasa Shirika hilo linafanya msako wa nyumba moja
baada ya nyengine ikiwemo kuwabaini watu waliojiunganishia umeme kwa njia za
udanganyifu.
Alisema watu ambao watabainika kujipatia umeme kwa njia za
hila watafikishwa mahakamani wakiwemo mafundi vishoka ambao wamekuwa
wakilihujumu shirika hilo.
“Kuna baadhi ya watu wamekuwa wakirubuniwa na wafundi vishoka
kwa kuwaunganishia umeme, kwa hili hatutakuwa na msamaha zaidi ya kuwafikisha
mahakamani” alisema
Aliwataka watumiaji wa umeme kuwa na ada ya kulipa kwa wakati
bili zao ili kuepuka malimbikizi ambayo unafika wakati hushindwa kulipa na
mwisho wake ni kukatiwa.
Kwa upande wake Meneja Mkuu wa kiwanda cha Maziwa (Tanga
Fresh) Michael Karata, amelitaka Shirika hilo kuwapunguzia gharama za umeme kwa
watu wenye viwanda.
Alisema gharama ya umeme ni kubwa hivyo kulitaka kuwaangalia
wawekezaji na wenye viwanda jambo ambalo litaweza kuongeza ufanisi na
uzalishaji wa bidhaa.
Mwisho
No comments:
Post a Comment