NILIKIONA CHA MTO URITHI WA
BABU 29
ILIPOISHIA
Akaja kwenye
ushahidi wa polisi wa usalama
barabarani ulioonesha jinsi ajali
ilivyotokea. Akaeleza kuwa pia amekubaliana na
ushahidi huo uliokuwa na vipimo vya polisi ambao walipima ajali hiyo.
Ushahidi wa afisa wa shirika
la umeme uliotaja tathmini ya hasara
iliyotokea nao ulichambuliwa na
kukubaliwa.
Wakati wote niliokuwa
nikisikiliza hukumu hiyo, moyo wangu ulikuwa ukienda mbio
kama saa. Na mara moja moja miguu
yangu ilikuwa ikitetemeka.
Hakimu alipomaliza kuuchambua ushahidi wa mashahidi wote alisema
kuwa mashitaka yote matatu
niliyoshitakiwa yalikuwa yamethibitishwa bila kuacha
shaka yoyote.
“Kutokana na ushidi huo,
mahakama hii inakutia hatiani kwa makosa
yote matatu.…”Hakimu aliniambia huku akinitazama.
SASA ENDELEA
Ingawa nilijua kuwa ningetiwa
hatiani, nilishituka. Uso wangu ulionesha wazi kupigwa na butwaa.
Sasa hapo ilikuwa ni kutiwa
hatiani tu, bado adhabu. sikujua ningekula miaka mingapi. Nikapatwa na kihoro
kilichofanya nimkodolee macho hakimu.
“Adhabu” Hakimu alisema baada
ya kuyageuza macho yake kutoka usoni kwangu na kulitazama jalada alilokuwa
akilisoma.
“Baada ya kukutia hatiani
ninakuhukumu adhabu ya kulipa faini ya shilingi laki tatu au kifungo cha miezi
mitatu kwa kosa la kwanza ambalo ni la kuendesha kwa uzembe”
Hakimu alipenua ukurasa
mwingine akaendelea kusoma.
“Pia ninakuhukumu kifungo cha
miaka miwili kwa kosa la kugonga nguzo za umeme au ulipe faini ya shilingi
milioni kumi”
Hakimu alisita akanitazama
kabla ya kuendelea.
“Kwa kosa la tatu ambalo ni
kulitia hasara ya shilingi milioni hamsini shirika la umeme, ninakuhukumu
kifungo cha miaka mitatu jela au ulipe faini ya shilingi milioni kumi na tano
pamoja na fidia ya shilingi milioni hamsini ambayo unatakiwa uwalipe shirika la
umeme” Hakimu alimaliza kupigilia
msumari kwenye moyo wangu. Msumari huo ulikuwa umenimaliza kabisa.
Ilikuwa hukumu ambayo
sikuitarajia kabisa. Nilijiuliza.
“Nitapata wapi pesa hizo za
kulipia faini pamoja na fidia ya shilingi milioni hamsini?
Hapo ilikuwa ni kukubali tu
kufungwa, hakukuwa na jingine.
“Kama utaweza kulipa faini na
kulipa fidia utakuwa umeepukana na adhabu ya kifungo” Hakimu aliendelea
kunifahamisha.
“Na kama utatumikia kifungo
bado utalazimika kulipa fidia baada ya kifungo chako” hakimu alimaliza hukumu yake.
Nilihisi kijasho chembamba
kikinitiririka kwenye uti wa mgongo wangu. Yalikuwa ni matokeo ya joto lililofumka
ghafla mwilini mwangu.
Baada ya kusomewa hukumu hiyo nilikuwa kama niliyepatwa na
wazimu. Nilikuwa nikisema peke yangu huku nikiwalaumu polisi hususan Inspekta
Amour..
“Mshitakiwa utalipa faini na
fidia au utatumikia kifungo ambapo utakapomaliza kifungo chako utalazimika
kulipa fidia ya shilingi milioni hamsini” Hakimu akaniuliza baada ya kimya
kifupi.
Sikuwa na jibu. Akili yangu ilikuwa imeruka.
Pakapita ukimya wa karibu sekunde tatu
kabla ya kuisikia sauti ya mwanamke
ikisema.
“Mheshimiwa nitamlipia fainii
pamoja na fidia ili asitumikie kifungo”
Maneno hayo yalinishitua,
nikageuza uso wangu kuelekea upande sauti hiyo ilikotokea.
Ilitokea kwenye safu za watu
waliokuwa wakisikiliza ile kesi. Kulikuwa na msichana mmoja aliyekuwa amesimama
akimtazama hakimu. Nikahisi yeye ndiye aliyesema atanilipia faini pamoja
na fidia.
“Hebu tokea hapa mbele”
hakimu alimwambia.
Msichana huyo alitoka na
kusimama karibu na meza ya mwendesha mashitaka. Nilipomtazama vizuri nilishituka
nilipogundua kuwa alikuwa Ummy!
Alikuwa amevaa wigi lililompendeza
na alipachika begani mkoba wa ngozi ya pindamilia uliokuwa umeendana na vazi
allilokuwa amevaa.
“Hebu rudia ulichosema”
hakimu akamwambia.
“Nimesema kwamba nitalipa
faini na fidia aliyotozwa mshitakiwa”
“Umeisikiliza kesi vizuri?”
hakimu akamuuliza.
“Ndiyo, nimeisikiliza”
“Umeisikia na hukumu
niliyoitoa hapa?”
“Nimeisikia”
“Utamlipia faini ya kiasi
gani na fidia ya kiasi gani?”
“Kiasi chote
kitakachohitajika”
“Fidia peke yake ni shilingi
milioni hamsini!”
“Ninajua mheshimiwa”
“Haya nenda kalipe”
Hakimu akamtaka polisi aliyekuwa
akinilinda kufuatana na Ummy pamoja na
mimi kwenda kulipa faini na fidia.
Sikuamini na sikujua kama Ummy
angeweza kulipa kiasi cha pesa kilichohitajika. Lakini katika hali ya
kushangaza Ummy alitoa katika mkoba wake
maburungutu ya noti nyekundu ambayo aliyakabidhi kwa karani wa mahakama.
Taratibu za kulipa faini na
fidia pamoja na kuachiwa huru zilichukua karibu saa moja. Wakati ule Ummy
akinilipia pesa hizo nilijikuta
nikimheshimu na kumchukulia kama mkombozi wangu ingawa ndiye yeye aliyekuwa ameniangamiza.
Nilipoachiwa huru na kutoka nje
ya mahakama nikakutana na Imspekta Amour, akanipa mkono na kunisalimia.
“Pole sana na hongera”
akaniambia kwa uso mkavu usio na aibu.
ITAENDELEA kesho hapahapa usikose
No comments:
Post a Comment