ZULIA LA FAKI 0655 340572
NILIKIONA CHA MTO URITHI WA
BABU 20
ILIPOISHIA
Niliendelea kujiambia kama
msichana huyo amekiri kuwa ni mzuka, atakuwa ni muuaji tu. Pengine alikuwa na
kisasi na babu yangu ambaye niliambiwa
alikuwa mwanamke wake.
Nitakutanaje na kuzungumza na
mzuka? Nilijiuliza huku nikifikiria niende Mwananyamala nikamjulishe mzee Nasri
kuhusu yale maelezo ya Ummy.
Hata hivyo upande mmoja wa
akili yangu ulinikataza kwenda Mwananyamala kwa vile nilijua yule mzee atapuuza
maelezo yangu kwa ile imani yake kuwa Ummy alishakufa na aliyekufa hawezi
kurudi tena duniani.
Sasa nifanye nini, huyu
msichana ataendelea kuniandama?”
nikajiuliza
Sikuweza kupata jibu la
haraka kwa vile akili yangu ilikuwa imetaharuki. Nilijiambia nitakapotulia na
kurudi katika hali ya kawaida, huenda nitajua nitafanya nini.
Wakati nazungumza na Ummy
nilikuwa nimesimama kwa kutaharuki, nikakaa kwenye kochi na kuendelea kuwaza.
SASA ENDELEA
Hisia zangu tangu nianze
kumfahamu Ummy sasa zilikuwa zimebadilika. Mwanzo nilikuwa nikihisi kuwa Ummy
alikuwa binaadamu anayetumia miujiza kuua watu. Nilijua hivyo tangu nilipoanza kumuona
kule Botswana.
Na hata pale nilipomkimbia
katika chumba cha hoteli aliponiita, nilimkimbia kwa hofu kuwa alitaka kuniua kama alivyowaua wale
wadeni wa marehemu babu.
Lakini sasa mtazamo haukuwa
huo. Hisia zangu zilikuwa upande mwingine kwamba Ummy hakuwa muuaji mwenye
miujiza kama nilivyokuwa nikidhani bali alikuwa mzuka wa mtu aliyekwisha kufa miaka mitano iliyopita.
Kama Ummy aliyekufa alikuwa
binadamu, huyu Ummy wa sasa si binaadamu tena. Huu ni mzuka kama alivyoniambia
wenyewe. Hauna akili ya kibinaadamu. Mara nyingi mzuka unapotokea unakuja kuua watu halafu unapotea.
Niliwaza kwamba mimi pia nilikuwa katika orodha ya kuuawa na mzuka huo
kwani wale waliouawa kwanza walikuwa wako pamoja na mzuka huo kiurafiki
wakidhani alikuwa binaadamu mwenzao. Na wote waliuawa katika mazingira ya kimapenzi.
Sasa kama mzuka huo wa Ummy
umeanza kuniambia kuwa umenipenda, ndio unataka kunitia kamba ili uniue
kirahisi.
Lakini wakati nawaza hivyo
suala la mali za babu lilikuwa likitikisa kichwa changu. Kwanini mzuka huo
aliniambia unazijua siri za mali ya babu yangu?.
Ilikuwa ni muhimu nikutane
naye lakini niliogopa. Huenda hapo tutakapokutana ndio nikauawa hapo hapo.
Nikajiuliza niende nikaripoti
polisi ili Ummy akamatwe na kuhojiwa? Au, niliendelea kujiuliza, niende kwa
mganga ili anieleze ukweli kuhusu kiumbe huyu na nia yake kwangu?
Wazo la kwenda polisi
sikuafikiana nalo. Nilijiambia polisi hawashughulikii masuala ya mizuka.
Ningeweza kudai kuwa huyu msichana anadaiwa kuwa alikufa miaka mitano iliyopita
lakini ninamuona na ananipigia simu kutaka nikutane naye.
Madai hayo yanaweza kuwavutia
polisi wamuandalie mtego na kumkamata.
Lakini nikajiuliza kama Ummy ni mzuka kweli, anaweza kukamatika au ninajidanganya?
Wazo zuri, niliendelea
kujiambia, ni la kwenda kwa mganga. Mganga anaweza kunitegulia kitendawili hiki.
Baadaya kuwaza hivyo nikaamua
niende kwa mganga mmoja wakati ule alikuwa akikaa Chanika. Alikuwa mzigua wa Handeni.
Alikuwa akifahamiana na babu na kuna
siku niliwahi kwenda kwake nikiwa na babu.
Babu yangu licha ya utajiri aliokuwa
nae alikuwa mshirikina sana.
Siku ambayo nilikwenda naye kwa
mganga huyo alikwenda kumroga mfanyabiashara mwenzake ambaye naye alikuwa na
vituo vya mafuta. Walikuwa wakishindana kibiashara na babu akaamua kuingiza na
uchawi.
Siku hiyo nakumbuka, mganga
alizika mbuzi watatu wakiwa hai kwenye kaburi la mwanamke aliyekufa zamani. Juu
ya kaburi pakamwagwa mchanga wa alama za viatu za mfanyabiashara aliyekuwa
akishindana na babu yangu.
Babu alikuwa ametuma watu
kuzitafuta alama za viatu za
mfanyabiashara huyo kwa dau la shilingi
milioni tatu kwa mtu atakayefanikisha kuzipata. Watu hao wakawa wanamuandama
mfanyabiashara huyo usiku na mchana mpaka wakafanikiwa kupata alama zake.
Alama hizo walizipata
aliposhuka kwenye gari na kukanyaga mchanga kabla ya kwenda kulikagua eneo
ambalo alitaka kulinunua pale Ubungo.
Baada ya mchanga huo kumwagwa
juu ya kaburi hilo palikutwa kibao kilichokuwa na jina lake. Baada ya siku saba
mfanyabiashara huyo aliaga dunia baada ya gari lake kugongwa na lori la mafuta!
Babu akafurahi.
Mganga huyo alikuwa mzigua
aliyetoka Handeni. Wenyeji wa Chanika walimpa jina la “mashine ya kuua”
Tangu kipindi hicho miaka
mingi ilikuwa imepita na sikuwahi kwenda kwake tena kwa vile sikuwa na tabia za
kwenda kwa waganga wa kienyeji. Hiyo tabia alikuwa nayo babu yangu.
Nikaona niende nikamueleze
matatizo yangu nikiamiini kuwa anaweza kunipatia ufumbuzi.
Nikaenda kwa gari langu
Nilipofika niliikuta ile
nyumba yake ambayo wakati ule ilikuwa ikiendelea kujengwa, ilikuwa
imeshakamilika. Lakini nilikuta msururu wa watu.
Ikabidi na mimi nipange msitari. Hadi nafanikiwa
kuingia katika chumba chake cha uganga ilikuwa karibu saa kumi na moja jioni.
Nilikuwa na matumaini madogo sana kama angelishughulikia suala langu kwa
vile muda ulikuwa umekwenda sana.
Mganga mwenyewe alikuwa
amenisahau, nikamkumbusha. Mara moja akamkumbuka babu yangu lakini mimi
hakunikumbuka.
“Wewe ni mjukuu wa yule mzee?”
akaniuliza.
“Ni mimi lakini babu mwenyewe
alishakufa”
Mganga akashituka.
“Kumbe mzee Limbunga alikufa?”
“Alikufa”
“Alikufa mwaka gani?”
“Alikufa mwaka huu”
“Kwa hiyo wewe ndiye umesimamia
shughuli zake?”
“Ni mimi lakini kuna matatizo
yamejitokeza”
“Matatizo gani?”
“Wewe unajua kuwa mzee
Limbunga alikuwa tajiri lakini alipokufa mali zake hazikuonekana”
“Kwanini?”
“Sijui”
ITAENDELEA kesho usikose uhundo huu
No comments:
Post a Comment