NILIKIONA CHA MOTO URITHI WA
BABU 32
ILIPOISHIA
Nikainamisha uso wangu na
kuanza kuwaza kwamba kumbe yule mwanamke aliyekuwa akitusumbua alikuwa jinni na
si mzuka wa Ummy.
“Nilikuelekeza uende nyumbani
kwa kina Ummy uniulizie, lengo langu ni kutaka kukuonesha miujiza. Baada ya Miujiza
ile nilitaka tukutane nikueleze ukweli lakini ulikuwa
ukinikwepa hadi hii leo nilipofanya uamuzi wa kukufuata nyumbani kwako” Maimun
aliniambia.
Akaendelea. “Najua
kilichokutisha ni jinsi nilivyowaua wale
watu kule Botswana, Zimbabwe na Afrika kusini. Wale watu baada ya kugundua
kuwa aliyewapa mali alikuwa amekufa walipanga njama za kukuua. Ndipo
nilipochukua uamuzi wa kuwaua wao mmoja baada ya mwingine. Wewe hujui tu lakini
mimi nipo na wewe tangu babu yako alipofariki”
Wakati wote huo nilikuwa
kimya nikimsikiliza kwa makini mwanamke huyo.
“Nilikwambia kuwa ninaijua siri ya mali ya babu yako, siri yake
ndiyo hiyo. Utajiri wa babu yako ninao
mimi na ninakusudia kukupa wewe. Lakini nisingekupa mpaka nikutane na wewe kama
tulivyokutana hii leo na unirithi mimi”
SASA ENDELEA
Nikainua uso wangu na kumtazama
mwanamke huyo huku nikimfananisha na jini. Hakuonesha ishara yoyote ya kuwa jini
zaidi ya ile miujiza yake alionionesha siku ile katika eneo la hoteli ya Lux.
Ile miujiza pekee ilitosha kunipa imani
kuwa alikuwa jini kweli.
“Nikurithi kivipi?”
nikamuuliza.
“Unirithi kama mke wa babu
yako na uendelee kuishi na mimi kama mke wako”
“Mimi sijui mlikuwa mnaishi
namna gani?”
“Tulikuwa tunaishi kama mke
na mume. Tofauti ilikuwa mimi ni jini, yeye ni binaadamu”
Nilijaribu kuwaza kwamba
ninaishi na mwanamke ambaye ni jini nikaona jambo hilo haliwezekani.
Nikatikisa kichwa.
“Naona kama haiwezekani
kuishi na mwanamke ambaye ni jini”
“Inawezekana. Mbona babu yako
aliweza”
“Sijui alikuwa akitumia mbinu
gani kuishi na wewe”
“Haihitaji mbinu. Tunaishi tu
kama mke na mume. Vile ambavyo utamtumia mke wako ndivyo ambavyo utanitumia
mimi. Na vile ambavyo mimi nitamtumia mume wangu ndivyo ambavyo nitakutumia
wewe”
“Unaweza kunipa muda wa
kufikiria jambo hilo na kunipa muda wa
kujiandaa”
“Ninaweza. Niambie
nikupe muda wa siku ngapi?”
“Nipe muda wa wiki moja tu”
“Sawa. Nitakupa muda wa wiki moja. Lakini nitakuwa na
masharti yangu ambayo ni lazima uyafuate”
“Masharti gani?”
“Kwanza sitataka ujihusishe
kimapenzi na mwanamke mwingine. Pili kila jambo ambalo utalifanya ni lazima
utake ruhusa kutoka kwangu. Na mimi kila jambo ambalo nitalifanya ni lazima nitake
ruhusa kutoka kwako”
“Sawa. Na kuhusu huo utajiri
nitaupataje?”
“Utaupata wakati tutakapokuwa
tumekubalina kuwa wanandoa”
“Sawa”
Pakapita ukimya wa karibu
sekunde kumi. Maimun alikuwa akikikodolea macho chumaba changu.
“Sasa mimi nakwenda zangu”
akaniambia baada ya sekunde hizo.
“Sawa, tutawasiliana”
Maimun akainuka kutoka
kitandani na kuniambia.
“Kwaheri”
“Karibu sana”
Akageuka na kuelekea kwenye
mlango. Alifungua mlango akatoka. Nikainuka na kumfuatia ukumbini. Sikumuona
tena. Nilikwenda kwenye mlango wa mbele
nikaukuta umefungwa kwa ndani.
Sikuweza kujua alitoka vipi. Nikarudi chumbani mwangu na kufunga mlango.
Nilijitupa kitandani na
kuanza kuwaza. Kile kitendawili cha Ummy alikuwa nani, kilikuwa kimeshateguka.
Sasa nilikuwa nikifahamu kuwa Ummy ni jini na siye yule Ummy tuliyekuwa
tukimdhania aliyekuwa amezikwa kaburini.
Kile kitendo cha kuvaa sura
ya Ummy ndicho ambacho kilinichanganya na kumdhania alikuwa mzuka wa Ummy.
Sasa suala la Ummy ni nani
lilikuwa limeshapata jibu. Ummy ni jini na jina lake ni Maimun binti Hashhash.
Suala sasa ni la kufikiria kuishi na mwanamke huyo kama mke na mume.
Awali sikuwa nikijua kama babu
yangu alikuwa na mke wa kijini. Kwa vile
nilikuwa nikiishi Morogoro sikuwahi kumuona
hata siku moja na babu yangu hakuwahi kuniambia. Jambo hilo
alilifanya kuwa siri yake.
Sasa babu ameshakufa,
nilijiambia, jini huyo amenifuata mimi na ametaka nimrithi.
Amenipa siku saba za kufikiria ama kumkubalia ama kumkatalia.
Nikajiuliza endapo nitakubali
kumrithi Maimun na kuwa mke wangu faida yake itakuwa ni nini?
Jibu nililipata mara
moja. Faida yake ni
moja tu, kupata utajiri ambao kila mwanaadamu katika ulimwengu huu
anauwania.
Nikimrithi Maimun nitakuwa
tajiri. Nitaishi katika jumba la
kifahari na nitakuwa na gari kama sio magari ya gharama. Vile vile nitaishi
maisha ya hali ya juu.
Na je kama sitataka kumrihi
athari yake itakuwa nini? Nilijiuliza.
Jibu hilo lilipaswa litolewe
na Maimun mwenyewe lakini nililijibu mimi kwamba endapo sitamrithi Maimun
sitapata utajiri. Nitendelea kuishi katika umasikini. Hilo ndilo jibu la haraka haraka nililolipata.
Usiku ule nilikesha macho
nikiwaza hadi asubuhi. Wazo ambalo niliamka nalo ni la kwenda kwa yule mganga
wa marehemu babu aliyeko Chanika ili anipe
ushauri wake.
Ilipofika saa nne nikaliwasha gari na kwenda Chanika kwa yule mganga.
Nilipofika nyumbani kwake
nilimkuta akikatakata vipande vya mzizi.
“Habari za siku nyingi?”
akaniuliza.
“Nzuri. Habari za hapa?”
“Hapa ni kwema. Karibu sana”
“Asante. Niimekuja nina tatizo moja. Nataka kupata ushauri wako”
“Tatizo gani hilo?”
Nikamueleza kuhusu yule jini
aliyekuwa mke wa babu yangu.
Baada ya kumpa maelezo yangu
mganga alishituka na kushngaa. Akaacha
kukatakata vipande vya mizizi.
ITAENDELEA ksho usikose
No comments:
Post a Comment