Wednesday, May 24, 2017

SIMULIZI, NILIKIONA CHA MOTO URITHI WA BABU SEHEMU YA 31

ZULIA LA FAKI
 
NILIKIONA CHA MOTO URITHI WA BABU 31
 
ILIPOISHIA
 
Nikatega masikio yangu kusikiliza vizuri ili nijiridhishe kuwa mlango wa nje  ulikuwa unabishwa. Mlango huo ukabishwa tena.
 
“Hodi! Hodi!” Sauti ya mwanamke ikasikika.
 
Nikanyamza kimya huku nikijiuliza ni nani abishaye mlango usiku ule. Ile sauti iliporudia  tena kupiga hodi nikaigundua kuwa ilikuwa sauti ya Ummy.
 
Nikashituka. Ummy ameamua kunifuata nyumbani usiku?
 
Wakati najiuliza hivyo nikasikia mlango wa nje unafunguliwa. Nikasikia kama viatu vya Ummy vikitembea ukumbini hadi kwenye mlango wa chumba changu. Kitendo hicho kilinishangaza kwa sababu sikujua ule mlango uliwezaje kufunguka wakati hakukuwa na mtu aliyeufungua.
 
Ndani ya ile nyumba nilikuwa ninaishi peke  yangu.
 
Sasa mlango wa chumbani mwangu nao ukaanza kubishwa!
 
Nikaisikia sauti ya Ummy ikipiga hodi.
 
“Hodi! Hodi!”
 
Hapo ndipo nilipoanza kutetemeka nikijua kuwa sasa Ummy ananiingilia chumbani mwangu.
 
SASA ENDELEA
 
Nilikuwa nimejifinika shuka shuka gubigubi huku nimetega masikio yangu kwenye mlango. Jinsi nilivyokuwa nikitetemeka sikutofautiana na mgonjwa wa homa ya baridi aliyekuwa amefinikwa shuka.
 
Licha ya kuisikia waziwazi sauti ya Ummy ikipiga hodi kwenye mlango wa chumbani kwangu sikuthubutu kujibu chochote.
 
Nilijua kuwa maana ya Ummy kuopiga hodi ni kutaka nimkaribishe chumbani mwangu lakini wakati huo huo alishaingia ndani ya nyumba yangu bila  kumkaribisha.
 
Nikajiambia hata kama sitamfungulia mlango wa chumbani, ataingia mwenyewe kama alivyoingia ukumbini.
 
Kunyamza kimya kwangu  kusingesaidia kumzuia msichana huyo asiyeeleweka kuniingilia chumbani.
 
Nikajikuta nikijuta kwa kutotimiza ile ahadi tuliyowekeana ya kukutana saa kumi na moja jioni kwenye bustani ya Mnazi Mmoja. Kama tungekutana, Ummy asingekuja nyumbani kwangu usiku huo. Nilijua kuja kwake kulitokana na mimi  kutotimiza ahadi yangu.
 
“Hodi! Hodi!”  Sauti ya Ummy iliendelea kusikika mbele ya mlango.
 
Alipoona simjibu aliniambia.
 
“Kama hunijibu, naingia chummbani mwako!”
 
Maneno hayo ndiyo yaliyonipasua moyo wangu, nikawa nahema kama niliyemuona Ziraili akiniambia amekuja kuitoa roho yangu.
 
Mara ile ile nikausikia mlango wa chumbani mwangu ukitoa mlio wa kufunguliwa.
 
Nikafungua shuka kwenye usawa wa macho yangu na kuchungulia. Nikamuona Ummy Nasri akiingia chumbani. Alikuwa amevaa viatu vya mchcumio vilivyokuwa vikitoa mlio wakati akitembea.
 
Alipoingia chumbani kwangu macho yake yalikwenda kwenye kitanda nilichokuwa nimelala.  Akawa anakisogelea kitanda hicho huku akinitazma jinsi nilivyokuwa nimejifinika shuka. Ili asione kuwa niko macho nilifumba macho yangu niikajifanya nimelala.
 
Ummy alitembea kwa mwendo wa taratibu akafika kando ya kitanda  changu. Akasimama na kukitupia macho chumba changu kisha akakaa kwenye pembe ya kitanda changu ambapo palikuwa na nafasi ndogo.
 
Akaniita kwa kulitaja jina langu. Nikanyamaza kimya.
 
“Mimi  najua kuwa uko macho na umesikia wakati naingia ndani ya nyumba  hii” akaniambia lakini  mimi niliendelea kunyamza.
 
“Umenyamza lakini mwili wako unatetemeka, inaonesha kuwa uko macho na umeshaniona” Ummy aliendelea kuniambia kwa kunisuta.
 
Mtetemeko ulikuwa umeniumbua lakini sikuwa na namna ya kujizuia nisitetemeke.
 
“Inuka  tafadhali”
 
Nikaitenga shuka na kuinuka, nikakaa kitandani.
 
“Mimi ni Ummy Nasri” Ummy akaniambia mara tu alipoona  nimeketi kitandani.
 
“Nimeamua kuja nyumbani kwako baada ya kuona  umekuwa ukinikwepa  sana. Kama ungejua usingenikwepa kwani nina habari zenye manufaa kwako wewe” Ummy aliendelea kuniambia.
 
Ummy akanyamaza kidogo na kunitazama kisha akaendelea.
 
“Nataka kukupa hadithi fupi kuhusu marehemu babu yako. Babu yako alimpenda sana Ummy Nasri mpaka alimuachia mali zake, lakini Ummy hakumtaka  babu yako zaidi ya kutaka kumla pesa zake kwa sababu babu yako alikuwa mzee”
 
Ummy aliendelea kuniambia.
 
“Kuna mwanamke wa kijini  ambaye alimchunuka babu yako. Mwanamke huyo alitaka aolewe na babu yako na aliahidi kumpa utajiri. Alimfuata babu yako mara kadhaa lakini babu yako hakuwa tayari kukubaliana na jini huyo na sababu kubwa ni kuwa moyo  wa babu yako ulikuwa kwa Ummy Nasri.
 
“Huyo jini akachukua uamuzi wa kumuua Ummy Nasri kisha akavaa sura ya Ummy na hapo akamfuata babu yako na kumwambia yeye ni Ummy anataka waoane. Ndipo babu yako alipooana na jini huyo akijua ameoana na Ummy Nasri. Babu yako akapata utajiri mkubwa sana.
 
“Jini huyo alimuonesha babu yako mahali ambapo angepata madini ya Tanzanite ambayo aliyauza nje ya nchi na kumpatia pesa nyingi”
 
Maneno  ya Ummy sasa yakaanza kuniingia vizuri kichwani mwangu kwani ni kweli babu yangu alikuwa akiuza madini hayo nje  ya nchi  na mara kadhaa  niliwahi kujiuliza babu yangu alikuwa akiyapata wapi madini hayo.
 
Ummy aliendelea kuniambia.
 
“Jini huyo aliendelea kuishi na babu yako. Babu yako  alipokufa yule jini alichukua mali yote aliyompa na ndiyo  maana wewe hukupata mali yote ya babu yako na umekuwa ukijiuliza utajiri wa babu yako umekwenda wapi”
 
Maneno hayo sasa yalianza kuzindua akili yangu. Sasa nikaanza kufahamu asili ya utajiri wa babu yangu na jinsi utajiri huo ulivyotoweka mara tu mwenyewe alipokufa.
 
“Umekuwa ukinidhania kuwa mimi ni mzuka  wa Ummy. Ukweli ni kwamba mimi ndiye huyo jini niliyevaa sura ya Ummy ambaye nilikuwa mke wa babu yako. Mimi ndiye niliyempa utajiri babu  yako na mimi ndiye niliyeupoteza utajiri huo mara tu baada ya babu yako kufa” Ummy aliendelea kuniambia.
 
Nikainua yangu  yangu na kumtazama mwanamke huyo usoni.
 
“Niangalie vizuri. Mimi ni mwanamke wa kijini” Mwanamke huyo akaniambia na kuongeza.
 
“Jina langu ninaitwa Maimun. Usilinganishe na Maimuna. Mimi ni Maimun binti Hashhash”
 
 
 ITAENDELEA kesho usikode uhondo huu

No comments:

Post a Comment