ZULIA LA FAKI
NILIKIONA CHA MOTO URITHI WA
BABU 28
ILIPOISHIA
Kwa kweli nilishangaa kuona
polisi wamenigeuka na kunifungulia mashitaka. Maelezo yalikuwa yamegeuzwa. Badala
yake nimeshitakiwa kwa kuendesha kwa uzembe wakati hapakuwa na uzembe wowote. Kilichotokea
kilikuwa miujiza tu.
Kadhalika nilikuwa nimemgonga Ummy na polisi wamekwenda
kampuni ya simu na kuthibitisha kuwa Ummy alinipigia simu na alikuwa mbele ya gari langu lakini hakutajwa kuwa nilimgonga.
Inspekata Amour sikumuona
tena. Kweli polisi hana rafiki. Anakuwa rafiki yako pale anapotaka lake.
Baada ya kusomewa mashitaka
hayo na kuyakana, upande wa
mashitaka ulisisitiza kuwa nisipewe dhamana kwa sababu ninaweza kuingilia na
kuharibu uchunguzi wao kwani uchunguzi wa tukio hilo ulikuwa bado unaendelea.
Nikapelekwa rumande.
Ile kesi iliendelea kuunguruma kwa miezi minne.
Wakati wote huo nilikuwa nimewekwa mahabusi.
Japokuwa uchunguzi wa polisi ulikuwa umekamilika, nilinyimwa dhamna kwa
madai kuwa hasara niliyoisababisha ni kubwa na ningeweza kutoroka kama nitaachiwa
kwa dhamana.
SASA ENDELEA
Inspekta Amour alikuwa ndiye
shahidi wa kwanza aliyekuja kutoa ushahidi dhidi yangu. Aliieleza mahakama kuwa
alinifahamu nilipokwenda katika kituo cha polisi anachofanyia kazi na kuripoti
kuhusu msichana anayeitwa Ummy ambaye alikuwa ananisumbua.
Alieleza kuhusu uchunguzi
wake na jinsi alivyogundua kuwa msichana huyo alikuwa ameshakufa lakini
kulikuwa na vielelezo na ushahidi kuwa alikuwa hai.
“Kwa vile tulitaka kumkamata tulimwambia mshitakiwa kuwa
atakapopigiwa simu na msichana huyo apange naye mahali pa kukutana na atuarifu
ili twende tukamkamate” Alieleza Inspekata Amour.
Huku akiongozwa na Mwendesha
Mashitaka, Amour aliendelea kueleza jinsi nilivyowaarifu kuwa Ummy alinipigia
simu na nilipanga kukutana naye katika goteli ya Lux saa nne asubuuhi ambapo
Amour aliandaa mtego wa kumkamata msichana huyo.
Lakini wakati polisi
wanajiandaa kwenda hukohoteli ya Lux ndipo walipopata taarifa ya ajali ya gari
iliyogonga nguzo ya umeme na kusababisha moto mkubwa kuwaka.
“Tulipofika hapo hoteli
tulikuta aliyesababisha ajali hiyo alikuwa mshitakiwa. Tulikuta gari lake
likiwa pembeni mwa nguzo zilizokuwa zinawaka huku mwenyewe akiwa amezirai. Tukafanya jitihada za
kuokoa maisha yake” Inspekta Amour
alisema.
Aliendelea kueleza kuwa baada
ya kufanikiwa kunitoa kwenye gari na
kunipakia kwenye gari la hospitali, kikosi cha zima moto kiliendelea na
jitihada ya kuuzima moto huku
wafanyakazi wa shirika la umeme wakiwa wameingia kazini kuzima umeme
katika eneo hilo.
“Uchunguzi wetu umeonesha kuwa
ajali ile ilitokana na uendeshaji wa kizembe wa mshitakiwa ambaye bila kuwa
muangalifu na kujali sheria za usalama barabarani aligonga nguzo za umeme
zilizokuwa zimebeba transfoma na kusababisha mlipuko wa moto” Inspekta Amour
alimalizia hivyo maelezo yake.
Baada ya inspekta Amour,
alikuja polisi wa usalama barabarani ambaye alionesha vipimo vya jinsi ajali
ilivyotokea na kueleza kwamba niliacha njia sahihi na kwenda kugonga nguzo za
umeme.
Shahidi mwingine alikuwa
afisa mmoja wa shirika la umeme ambaye alieleza kuwa kugongwa kwa nguzo za
umeme kulisababisha transfoma ya shirika hilo kulipuka na
kuwaka moto.
Afisa huyo aliendelea kueleza
kuwa hasara waliyoipata kutoka na tukio hilo ilifikia shilling milioni hamsini.
Wakati mashahidi hao wakitoa
ushahidi wao, kichwa kilikuwa kinaniuma na kilikuwa kizito kwa mawazo yaliyochnaganyika na fadhaa hasa nilipowaza kwamba kesi
ile ingenifunga miaka mingi.
Baada ya mashahidi
hao kutoa ushahidi wao, kesi
iliahirishwa na kupangiwa tarehe
nyingine ya usikilizaji.
Nilirudishwa mahabusi
ambako niliendelea kusota na kuwazia
maisha yangu ambayo niliona
yalikuwa yameshafikia kikomo kwani nilijjua kuwa nitafia jela.
Tarehe ya kuendelea kwa kesi
hiyo ilipowadia nilipelekwa mahakamani nikiwa
na hali mbaya ya kiafya kwani nilikuwa nimekonda. Kule mahabusi nilikuwa sili chakula vizuri
kutokana na fadhaa.
Vile vile nilikuwa nikimlaani
Inspekta Amour aliyekuwa amenigeuka ili kulinda kazi yake. Amour alifahamu
fika kuwa ajali ile ilitokea kimiujiza na si mimi
niliyeisababisha lakini alitoa maelezo
ya kunitia katika hatia.
Kesi iliendelea kwa mashahidi
mbalimbali kuja kutoa ushaidi wao. Katika kipindi chote wakati ushahidi unatolewa nilipewa nafasi ya
kuuliza maswali kama kulikuwa na kitu
sikubaliani nacho. Lakini ukweli ni kwamba nilishindwa kuuliza chochote.
Nilishindwa kwa sababu ya
kutojua sheria na pia kupatawa na hofu.
Pale nilielewa ni kwanini
hata wanasheria wanapokabiliwa na kesi wanaweka mawakili wa kuwatetea. Ni kwa
sababu wao wenyewe licha ya kujua sheria wasingeweza kujitetea vizuri kwa
sababu ya hofu.
Baada ya upande wa mashitaka
kumaliza kuleta mashahidi wake, hakimu alisoma muhutasari wa kesi na kueleza
kuwa nina kesi ya kujibu, kwa hiyo
nilitakiwa nijitetee.
Niliulizwa kama
nilikuwa na mashahidi, nikajibu kuwa sikuwa na shahidi yeyote.
Baada ya kujibu hivyo nilitakiwa niandae utetezi wangu ili
kesi itakapoitishwa tena niweze kujitetea.
Baada ya hapo kesi
ikaahirishwa na kupangiwa tarehe nyingine.
Siku hiyo ilipofika
nilipelekwa tena mahakamani ambako nilijitetea kwa kuieleza mahakama
kuwa tukio lile la ajali lilitokea kimiiujiza na kwamba ajali ile
sikuisababisha mimi.
Hakimu aliandika maelezo
yangu na kupanga tarehe ya kutoa hukumu.
Usiku wa siku ile ya kutolewa
hukumu niliota ndoto mbaya sana. Niliota
ninahukumiwa kifungo cha miaka thelathini jela na kutakiwa nililipe shirika la umeme
shilingi milioni hamsini.
Nilikuwa sina pesa hizo nikajikuta
nimetupwa jela. Baada ya kusota jela kwa
mika thelathini, eti nikaona ninatoka jela nikiwa mzeee ninayetembea kwa
mkongojo!
Ndoto ile ilinishitua sana
nikajua ndio mambo yatakavyokuwa.
Asubuhi nilipelekwa mahakamani
kwenda kusikiliza hukumu yangu.
Jalada langu
lilipoitishwa nilipanda kizimbani na
hakimu akanisomea hukumu aliyokuwa ameniandalia.
Alianza kuyataja mashitaka yaliyokuwa yananikabili na akaeleza kuwa niliyakana mashitaka yote niliyosomewa.
Baada ya hapo akaanza
kuuchambua ushahidi uliokuwa umetolewa na upande wa mashitaka. Alianza kuuchambua ushahidi wa Inspekta Amour.
Akaeleza kuwa ushidi huo
anaukubali kwa vile mimi kama mshitakiwa nilishindwa kumhoji shahdi huyo
chochote ikimaanisha kuwa nilikubaliana
nao.
ITAENDELEA kesho hapahapa Usikose
No comments:
Post a Comment