NILIKIONA CHA MOTO URITHI WA
BABU 24
ILIPOISHIA
Macho ya watu wote
yakaelekea kwenye mwili huo. Polisi hao waliufungua uso wa marehemu
huyo. Ingawa ngozi yake ilikuwa nyeusi kwa sababu ya kukaa ndani ya kaburi kwa
muda mrefu haikuwa imeharibika.
Uso wake ulikuwa mwembamba na
uliosinyaa lakini haukunizuia kugundua kuwa ulikuwa na sura ya Ummy.
“Hebu mtazameni, huyu ndiye
maiti wenu?” Inapekta Amour akawauliza wazazi wa Ummy.
“Ndiye yeye” Mzee Nasri
akajibu haraka.
Polisi mmoja aliyekuwa na kamera ya kuchukua alama za
vidole alipiga picha alama za viganja vya Ummy. Polisi mwingine aliupiga picha
uso wake. Daktari naye aliuchunguza mwili huo na kukata kipande cha ngozi yake ya mkono.
Baada ya uchunguzi huo kumalizika,
mwili huo ulirudishwa kwenye kaburi na kufukiwa tena
Daktari akawambia watu kwamba
atakuwa na matokeo kamili ya uchunguzi wake baada ya saa sita. Polisi walioupiga picha mwili huo wakasema watakamilisha
uchunguzi wao baada ya saa tatu.
Tukaondoka.
SASA ENDELEA
Inspekta Amour alinirudisha nyumbani
kwangu akanitaka nifike kituo cha polisi asubuuhi ya kesho yake ili nionanne
naye.
Baada ya kuagana naye,
Inspekta huyo aliondoka. Niliridhika sana na hatua alizochukua. Alikuwa ni
miongoni mwa makachero wa polisi niliowakubali sana. Alikuwa akitambua wajibu
wake kama polisi mpelelezi.
Hata hivyo bado niliona kitu
kama ukungu katika uchunguzi huo wa polisi. Dalili kwamba huenda tukajikuta
tupo njia panda katika uchunguzi huo ni kule kukuta maiti ya iliyoonekana kuwa
ni ya Ummy kwenye kaburi lililofukuliwa.
Nilijiambia kama itathibitika
kuwa aliyezikwa ni Ummy Nasir, moja kwa moja yule msichana anayenipigia simu
atakuwa ni mzuka wa Ummy na ndio uliokwenda kusajili namba ya simu kwa ajili ya
kunipigia mimi.
Na kama itathibitika
kwamba yule si Ummy, basi Ummy atakuwa
yupo hai na ndiye aliyeuawa watu waliokuwa wakidaiwa na babu
yangu, na ndiye huyo huyo aliyekwenda kusajili namba ya simu.
Kwa vyovyote itakavyokuwa,
niliendelea kujiambia, huenda Ummy huyo asiwe na nia njema na mimi. Kama amedai
anaijua siri ya mali ya babu yangu huenda anataka kuniua ili aweze kumiliki
mali hizo.
Shaka hii ilinijia baada ya
kuona ameshaua watu waliokuwa wanadaiwa na babu yangu bila kueleweka dhamiri
yake ilikuwa nini.
Lakini kama utakuwa ni mzuka,
suala litakuwa zito zaidi.
Usiku wa siku ile sikupata
usingzi kwa kuwaza. Niliwaza mengi yaliyonikera moyo wangu lakini
hatimae kulikucha salama.
Saa tatu asubuhi nikawasili
kituo cha polisi cha Kinondoni na kuonana na Inspekta Amour.
Inspekta Amour alinikaribisha
kwenye kiti akaniuliza.
“Yule msichana hajakupigia
simu?”
“Hajanipigia”
“Tumeanza kupata utata kuhusu
suala lake. Tumefanya uchunguzi wa kutosha jana na leo lakini matokeo yamekuwa
ni ya kutia shaka”
“Kwanini?”
“Uchuguzi wa madaktari wa
Muhimbili kwa kutumia chembechembe za mwili wa marehemu na vielelezo vingine
umebaini kuwa ule ulikuwa mwili wa Ummy…”
Nilikuwa niimemkodolea macho
Inspekta huyo kumsikiliza. Akaendelea.
“Sasa utata unakuja kwa
sababuni hata uchunguzi tuliofanya sisi
unaonesha kuwa mtu anayekupigia simu ni Ummy huyo huyo ambaye ameshakufa. Alama
zake za vidole zilizoko katika usajili wake na alama tulizozichukua jana katika viganja vyake zinafanana. Hii inaonesha kuwa
ni Ummy huyo huyo!”
“Una maana kwamba alama za
vidole za watu hazifanani?”
Inspekta Amour akatikisa kichwa.
“Alama za vidole za binaadamu
hazifanani kabisa. Kila mtu ana alama zake”
“Hata kama watachunguzwa watu milioni moja, watakutwa na
alama za vidole tofauti?”
“Hata watu milioni kumi,
wanaweza kufanana sura tu lakini alama
zao za vidole hazifanani. Kila binaadamu anakuwa na alama zake mwenyewe”
“Hicho ni kitu cha ajabu
sana”
“Ndiyo maumbile yetu binaadamu. Na wataalamu waligundua
hilo. Ndiyo maana alama za vidole
zimekuwa kielelezo muhimu cha kumkamatisha mhalifu”
“Mungu ni muweza sana”
“Unaiona ile mistari ya pundamilia?”
“Ndiyo, niimeshawahi kuiona”
“Unaweza kuiona kama
inafanana lakini ile pia haifanani.
Kila punda milia ana aina yake ya mistari, hata wawepo pundamilia
milioni kumi, watakuwa na mistari tofauti”
“Hilo sijawahi kulisikia”
“Ndiyo nakueleza mimi ili uone maajabu ya Mungu, si katika
alama za vidole za binaadamu tu bali tofauti zipo hata katika alama za wanyama”
“Nimekuelewa Inspekta. Sasa
hili suala la Ummy unalifikiriaje?’
“Ndiyo nilikuwa nataka
kukueleza kwamba limekuwa suala lenye
utata. Mtu ambaye imethibitika kuwa amekufa na kuzikwa miaka mitano iliyopita
lakini kunakuwepo na ushahidi kuwa yuko hai. Hili jambo ni la ajabu sana”
“Niliwahi kukwambia kwamba
inawezekana kuwa ni mzuka wa Ummy”
“Suala hilo la kiimani hatuwezi
kuliingiza katika uchunguzi. Kazi yetu
haiamini kuwepo kwa mizuka”
“Sasa atakuwa ni nani yule?’
“Siwezi kusema ni nani kwa
sababu hatujamthibitisha ila wewe utakuwa ni nguzo muhimu katika uchunguzi wetu wa awamu ya pili. Nisikilize kwa makini”
“Ndiyo”
“Wakati wowote atakapokupigia
simu, kubali kukutana naye halafu tupigie simu ili tufike mahali hapo. Pale mtakapokutana tu
tunamkamata hapo hapo”
“Nafikiri hilo litakuwa wazo
zuri. Hapo mwanzo nilikuwa sitaki kukutana naye kwa sababu ya hofu lakini kama
polisi mtakuja nitaweza kukutana naye”
“Tutakuja. Muulize angependa mkutane wapi”
“Mara nyingi anapenda
tukutane mahotelini”
“Basi muache ataje yeye
hoteli ambayo angependa mkutane”
ITAENDELEA kesho hapa hapa tangakumekuchablog usikose uhondo huu mwanana
No comments:
Post a Comment