KISIWA CHA HARISH
FAKI A FAKI
Sikuwahi kuona sherehe kubwa
ya harusi kama ile niliyoiona katika visiwa
vya Ngazija nchini Comoro mwaka mmoja uliopita.
Ilikuwa harusi ya binti wa
Rais wa Moroco Yasmini binti Sharif Abdilatif aliyekuwa akolewa na mwana wa
mkuu wa majeshi ya ulinzi wa Moroco Abubakar
Mustafa Al- Shiraz aliyekuwa akiishi Ufaransa.
Sisi tulikuwa tumetoka Zanzibar. Mke wa mkuu wa
majeshi ya Comoro Kulthum alikuwa Mzanzibari tena Mkojani wa Pemba, ndiye
aliyetoa mwaliko kwa ndugu zake walioko Zanzibar.
Zilitolewa kadi kumi za
mwaliko kwa watu kumi. Kwa vile na mimi nilikuwa na nasaba na Kulthum nikapata
kadi moja na tikiti ya ndege ya kwenda Ngazija.
Wakati ule nilikuwa na umri
wa miaka ishirini na mine. Nilikuwa bado kijana na shughuli zangu zilikuwa ni
uvuvi. Nilikuwa sijaoa bado lakini nilikuwa katika maandalizi ya kutafuta mchumba.
Ndege tuliyosafiri nayo
ilifika Comoro saa kumi jioni. Ndoa ilikuwa inafungwa saa mbili usiku baada ya
swala ya isha katika msikiti wa Riadha, msikiti mkuu wa ijumaa nchini humo.
Nyumbani kwa bwana harusi kulikuwa kumejaa shamra shamra. Kadhalika nyumbani
kwa Rais Sharif Abdulatif nako kulikuwa hakutoshi.
Kulikuwa na hoteli mbili
kubwa zilizokodishwa siku ile kwa ajili ya sherehe za harusi. Na kulikuwa na
hoteli nyingine kadhaa zilizokodiwa kwa ajili ya wageni walioalikwa kutoka nchi
mbalimbali.
Sisi tulifikia katika hoteli
ya Zaharani. Jina la hoteli hiyo lilifanana na jina langu. Jina langu ni
Zaharani Shazume. Hoteli hiyo ilikuwa jirani na msikiti wa Riadha mahali ambapo
ndoa ya Yasmin na Abubakar ingefungwa usiku ule.
Kwa kawaida msikiti wa ijumaa
hujaa watu siku za ijumaa lakini siku ile kwa mara ya kwanza ulijaa watu katika
swala ya isha.
Kulikuwa na ulinzi mkali wa
polisi na maafisa usalama waliokuwa na kazi ya kuhakikisha usalama unakuwepo
katika eneo hilo.
Nilijitahidi sana nipate safu ya mbele
lakini sikuweza. Safu hiyo ilikuwa imejaa masheikh na maafisa usalama.
Nilibahatika kupata safu ya tatu yake.
Baadaya swala ya isha Rais wa
Comoro Sharif Abdulatif alitakiwa kutoa idhini ya kumuozesha mwanawe.
Wakati anatoa idhini alipokea
simu hapo hapo iliyomtambulisha kuwa binti yake Yasmin alikuwa ameanguka
nyumbani na alikuwa akitokwa na povu mdomoni.
Shughuli ya ufungishaji ndoa
ikasimama. Hapo hapo Rais Abdulatif na wasaidizi wake pamoja na maafisa usalama
walitoka kwenda nyumbani.
Habari iliyopatikana baadaye
ilieleza kuwa Yasmini alikuwa ameanguka na kupoteza fahamu huku akitokwa na
povu midomoni. Baba yake alipofika na kumuona aliamrisha apelekwe hospitali haraka.
Gari la hospitali lilikuwa
limeshafika. Yasmin alipakiwa na kukimbizwa hospitali. Gari hilo la hospitali lilifuatana na gari la
maafisa usalama na gari la rais mwenyewe.
Lakini gari alilopakiwa
Yasmin likapata ajali kabla ya kufika hospitali. Tairi lake la mbele la upande
wa kulia lilipasuka na kusababisha gari hilo
kuyumba na kuligonga gari jingine kabla ya kupindukia kwenye mtaro uliokuwa
kando ya barabara.
Heka heka ikawa kubwa!.
Magari ya maafisa usalama yakasimama. Maafisa hao wakashuka na kukimbilia kutoa
msaada. Dereva wa gari la hospitali alipotolewa alikutwa akiwa ameshakufa.
Yasmin mwenyewe hakuonekana. Wauguzi wawili waliokuwa naye walikutwa wamezirai.
Tukio hilo
lilizua taharuki kubwa.
Rais Abdulatif hakuamini
macho yake, akawa anauliza kwa ukali “Binti yangu yuko wapi?”
Lakini hakukuwa na aliyejua.
Yasmin alikuwa ametoweka ghafla. Kila aliyeshuhudia alishangaa.
Harusi ikavunjika. Badala ya
furaha sasa ikawa huzuni. Bwana harusi na mke wa Rais Sharif Abdullatif Bi
Kulthum walikuwa wanalia kutokana na
muujiza huo.
Usiku ule ule Rais Abdullatif
aliita masheikh ikulu na kuwauliza kama
walikuwa wanajua kilichomtokea binti yake.
Kila sheikh alisema lake.
Wako waliomwambia kuwa binti yake alikuwa amechukuliwa na wachawi. Wako
waliomwambia kuwa haikuwa muafaka kwa binti yake kuolewa na Abubakar ndiyo
sababu tukio hilo
limetokea. Na wako waliomwambia kuwa Yasimin alikuwa amechukuliwa na jini
aliyekuwa amemchunuka.
Rais Abdullatif hakujua
ashike kauli ya sheikh yupi. Kwa vile lilikuwa limeshamfika alikubaliana na
mashikh wote na kuwataka mashikh hao kutumia elimu zao kumrudisha binti yake.
Aliahidi mamilioni ya shilingi za ki Comoro kwa sheikh yeyote atakayefanikiwa
kumrudisha Yasmin.
Licha ya Rais Abdullatif
kusubiri kwa zaidi ya miezi mitatu. Hakukuwa na sheikh yeyote aliyefanikiwa
kumrudisha Yasmin! Yasmin akabaki kuwa historia kwani hakupatikana tena.
Ulikuwa msiba ambao kila mkazi wa Comro alihisi kuwa hautasahaulika.
Hivi sasa mwaka mmoja
umeshapita tangu tukio hilo
la kuhuzunisha litokee. Tangu wakati ule sikuwahi tena kurudi Moroco. Nilikuwa
Unguja nikiendelea na shughuli zangu za uvuvi.
Sasa siku moja ambayo
sitaisahau maishani mwangu tulikuwa kwenye boti letu tukielekea maji makuu
kuvua samaki. Ndani ya boti hilo
tulikuwa wavuvi saba.
Ilipofika saa nne asubuhi
tulikuwa mbali sana.
Boti yetu ilipigwa na dharuba kali. Mashine ya boti ikazima ghafla. Tilijaribu
kuiwasha lakini boti haikuwaka. Ikawa inakokotwa na maji.
Tulipumzika kidogo kisha
tulijaribu kuiwasha tena na tena lakini hatukufanikiwa kuiwasha Mashine
ilitugomea kabisa. Hatukujua ilikuwa imepatwa na hitilafu gani.
Je nini kitawatokea wavuvi
hao? Endelea kufuatilia hadithi hii katika blogy hii kesho.
Hadithi hii imetungwa na mtunzi maarufu wa hadithi hapa nchini na Afrika Mashariki, Faki A Faki
No comments:
Post a Comment