Kumekucha blog
Tanga, CHAMA Cha Wananchi (CUF) Tanga
kimezindua kampeni yake ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa kuwataka viongozi
wa dini kuacha kuikingia kifua CCM na badala yake wahubiri amani na utulivu
vipindi vyote vya uchaguzi.
Akizungumza katika mkutano uliofanyika mtaa wa Ngamiani kati,
Diwani wa Ngamiani Kusini, Mussa Mbarouk aliwataka viongozi hao kuwahubiria
waumini wao amani na utulivu na kuacha kukishabikia cha cha Mapinduzi kwa madai
kuwa kimeshindwa kuwaboreshea wananchi maisha yao.
Alisema chama cha CCM kimeshindwa kutekeleza ahadi zake na kimekuwa kikiwakandamiza katika kodi
mbalimbali zikiwemo za mapango na za biashara na hivyo kuwataka viongozi hao
kuikumbusha Serikali hiyo ya CCM na kuacha kuikumbatia.
“Kuna baadhi ya viongozi wa madhehebu ya dini wamekuwa
wakiikingia kifua chama cha mapinduzi kwa kudhani kuwa kitawasaidia katika
mambo yao----ukweli ni kuwa imeshindwa kuboresha huduma na haina uwezo zaidi ya kuwakandamiza” alisema Mussa
Alisema CUF itafanya kampeni mfululizo mjini na vijijini
kueleza udhaifu wa CCM pamoja na ahadi ilizotoa ambazo hazijatekelezwa zikiwemo
za kuwapatia huduma ya umeme na maji
safi vijijini
Alisema wananchi wa vijijini wamekuwa wakiishi katika
mazingira magumu na wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita chama hicho
kiliwaahidi kuwapelekea huduma ya maji safi lakini hakuna kilichofanyika.
Akizungumza katika ufunguzi huo, Diwani wa Ngamiani kati,
Habib Mpa (CUF) aliwataka wananchi kukichagua chama hicho na kuacha kukichagua
chama cha Mapinduzi kwa madai kuwa hakina jipya.
Alisema viongozi wa chama cha CCM wameshindwa kutetea maslahi
ya wananchi na badala yake wamekuwa wakifanya kazi kwa mazoea na kushindwa
kukanyana jambo ambalo limekuwa likiwagharimu wananchi.
“Musikichagua cha cha CCM kwani viongozi wake wamekuwa
wakilindana hata mtu abainike kufanya ufisadi----hii imekuwa ikiwagharimu
nyinyi wanyonge” alisema Mpa
Alisema hakuna tofauti ya mwananchi wa mjini wala vijijini na
kila mtu analilia shida ambapo zamani maisha ya mjini yalikuwa nafuu na kila
mtu alikuwa ikikimbilia na kwa sasa kilio cha maisha magumu ni kila kona.
Alisema maisha ya mjini yameelemewa na kodi nyingi na
kuwalazimu baadhi ya wafanyabiashara kubadilisha aina ya biashara zao na hivyo
kuwataka wananchi kuutumia mtaji huo kuwaondoa viongozi wa CCM walioshikilia
nafasi za uongozi.

No comments:
Post a Comment