Tuesday, December 2, 2014

Walemavu watakiwa kujitokeza kugombea nafasi Serikali za Mitaa

Kumekucha blog

Tanga, JAMII ya Walemavu Tanga  imetakiwa kujitokeza kwa wingi katika nafasi za kugombea na kuitaka  kuhakikisha inawachagua viongozi ambao wataweza kutetea haki zao katika vyombo vya kutunga sheria.

Akizungumza na watoto wenye ulemavu wa viungo wakati wa kutoa zawadi za Krismass jana, Mratibu wa kituo cha walemavu Tanga (YDPC), Hendry William, aliwataka walemavu  kujitokeza katika chaguzi za Serikali za mitaa zilizoanza kampeni zake juzi.

Aliwataka kuutumia vyema uchaguzi wa Serikali za mitaa kwa kujitokeza kwa wingi katika kugombea nafasi za kuongoza pamoja na kuwachagua viongozi ambao watatetea maslahi yao.

“Leo ni siku ya furaha kuona kituo cha watoto wenye ulemavu wa viungo wanazawadiwa zawadi ya Krismass wakiwa na wazazi na walezi wao---kupitia hadhara hii nawaomba kuzitumia chaguzi za Serikali za mitaa kwa kujitokeza kugombea” alisema na kuongeza

“Chaguzi hizi ni kipimo kwenu cha kuwatambua viongozi wanaofaa--- hii ni pamoja na ninyi kujitokeza na kuwa wamoja kuhakikisha munashika nafasi za kuongoza” alisema Hendry

Aliitaka jamii hiyo ya walemavu pamoja na ndugu na jamaa wa watoto wenye ulemavu kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi katika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwakani na kuchagua viongozi wanaowapenda.

Akitoa nasaha zake wakati wa sherehe hiyo ya kuwagawia zawadi za Krismass na mwaka mpya, Padri wa Kanisa la Magomeni, Ayoub Kuminambili,ameyataka makampuni na taasisi za Serikali na watu binafsi kuweka kitengo maalumu cha watu wenye ulemavu.

Alisema kufanya hivyo kutawawezesha jamii ya walemavu kuona wanatambuliwa na hivyo mahitaji yao kushughulikiwa kwa haraka tofauti na sasa ambapo taasisi nyingi hazina vitengo kwa walemavu na hivyo kuwa kero.

“Kupitia siku ya leo na waandishi wa habari tunayaomba makapuni na taasisi za uma kuweka vitengo kwa walemavu---hii itawasaidia kuharakisha kupatiwa huduma” alisema Kuminambili

Aliyakumbusha makambuni ya ujenzi wa majengo kukumbuka kuweka miundombinu ya walemavu ikiwemo njia ili kuzifikia huduma na kumaliza malalamiko ya walemavu kushindwa kufika kuliko na mahitaji.

                                                 Mwisho

No comments:

Post a Comment