KISIWA CHA HARISHI (14)
ILIPOISHIA TOLEO LILILOPITA
“Acha nifurahishe moyo wangu
nisife na kinyongo”
“Sikuwa nikijua kuwa
umchangamfu kiasi hicho”
“Mimi ni mchangamfu sana, sema hili jinni
ndilo limeniharibia maisha yangu. Ningeweza kuliua ningeliua”
“Hata ukiliua utaondoka vipi
hapa kisiwani?”
“Hayo yatakuwa masuala
mengine, bora nimeshaliua”
“Kama boti yetu ingekuwa
nzima tungekutorosha tukaenda Zanzibar”
“Halafu ungenioa huko huko”
“Upendavyo”
“Mimi ningependa unioe Zanzibar. Gharama zote
angetoa baba yangu”
“Mimi nisingekuwa na amri
zaidi ya kukusikiliza wewe”
Nilipomwambia hivyo Yasmin
alifurahi sana.
Chakula kilipokuwa tayari alikipekua sehemu mbili. Sehemu moja ilikuwa yetu
mimi nay eye. Sehemu ya pili ilikuwa ya wenzetu.
“Sasa wapelekee halafu urudi
tuje tule” Yasmin akaniambia.
Alinitilia chakula kwenye
kapu nikaondoka. Wakati nakaribia kufka kwenye mlango wa kutokea, nikawaona
wenzangu wamenifuata.
“Tumeona unachelewa, tukapata
wasiwasi” Masudi akaniambia.
SASA ENDELEA
“Nilikuwa nasubiri chakula na
ndicho hiki ninawaletea” nikamwambia Masudi.
“Sasa na sisi tumeshakuja.
Kuna haja ya kwenda tena kule”
“Tunaweza kula hapa hapa”
Masudi akawatazama wenzake.
“Jamani tuleni hapa hapa, au
mnasemaje?’ akawauliza.
“Popote tu tunaweza kula”
Nikarudi ndani na kuliweka
lile kapu la chakula.
Yasmin alikuwa amesikia sauti
zetu akatufuata.
“Jamani mmekuja huku huku?”
akawauliza.
“Tuliona mwenzetu anachelewa
tukapata wasiwasi. Tulidhani labda ameshikwa na Harishi” Masudi akamjibu.
“Hapana. Alikuwa anasubiri
chakula, lakini mnaweza kula hapa hapa”
Yasmin akaandaa kile chakula
kwenye mswala. Kwa vile wenzetu walikuwa wamekuja, tuliona tule pamoja. Yasmin
akaleta na kile chakula kingine.
Tulipomaliza kula tuliendelea
kuzungumza pale pale tukiwa pamoja na Yasmin.
Masudi alikuwa akimtania sana Yasmin huku akimsifia
kwa uzuri. Yasmin alikuwa akichekacheka tu na kuficha uso wake uliokuwa umejaa
aibu.
Masudi akaeleza kisa ambacho
nilihisi kilikuwa cha uongo kwamba zamani alipokuwa anakaa Mombasa alipendana na msichana mmoja wa
Kilamu.
“Msichana. Alikuwa mzuri
huyo. Alinipenda na mimi nilimpenda lakini wanawake wa Mombasa hawaoleki bwana!”
“Kwanini?” nikamuuliza.
Wana gharama sana. Huyo msichana wangu
alikuwa anaitwa Nargisi. Kila siku alikuwa amechorwa piku, utadhania mwari wa
harusi”
“Sasa huyo atapata kweli muda
wa kupika ukimuoa?” nikamuuliza.
“Ndio maana nilishindwa
kumuoa. Nilikuwa nikijiambia huyu msichana sijamuoa yuko hivi, je nikimuoa
atakuwaje, piku kila siku…safari haziishi”
“Mapenzi ya kweli yana
gharama” Yasmin akamwambia.
“Ni kweli lakini gharama ya
mwanamke wa Mombasa
ni kubwa. Kwanza kunai le gharama ya miraa.
Kila siku ni lazima umnunulie kilo moja ya miraa, tena ile miraa safi ya bei ghali”
“Wacha we!” Yasmin alimwambia
kumtia jazba.
“Halafu wkati wa kula ile
miraa ni lazima apate kokakola na chupa
ya maji safi
pamoja na mfuko mzima wa Big G. Zote ni pesa” Masudi aliendelea kueleza.
“Na wewe ulikuwa unakula?”
nikamuuliza.
“Mimi nilikuwa nakula lakini
si sana.
Simalizi hata nusu lakini mwenzangu anaua kilo nzima. Akianza saa tisa hadi saa
nne usiku hakuna kitu”
“Sasa akishakula hiyo miraa
itamsaidia nini?” Yasmin akauliza.
“Anapata handasi” Masudi
akamjibu.
“Handasi ni kitu gani?”
“Handasi ni kileo cha miraa.
Wengine wanakiongezea na kungumanga. Wanasaga kungumanga, ule unga wake
wanachanganya na kahawa. Ashiki yake ni hatari!”
Sote tukacheka. Yasmin ndio
alicheka sana.
“Yaani mwanamke akitoka hapo
ni lazima apate bwana!” Masudi aliendelea.
“Asipopata bwana inakuwaje?”
Yasmin akamuuliza.
“Yaani anapokula miraa na
kuchanganya na kahawa ya kungumanga tayari anakuwa na ahadi ya bwana”
“Kwa hiyo huyo mpenzi wako
akishakula ndio mnakutana?’ Yasmin aliendelea kumuuliza. Maneno yalikuwa
yamemkolea.
“Ndiyo maana yake”
“Unaonaje mapenzi yake?”
“Ni mapenzi adhimu. Sijapata
kuona na sitamsahau yule msichana” Masudi kwa kutaka sifa aliongeza. “Na yeye
pia hatanisahau kwani nilikuwa…mh!...hata havisemeki”
“Sema tu ulikuwaje?” Yasmin
akamsisitizia.
“Mwenyewe alikuwa akiniambia
penzi nililokuwa nikimpa hajalipata kwa mwanaume yeyote”
Hapo tulicheka tena. Lakini
mimi nilicheka kwa kujua kuwa Masudi alikuwa akisema uongo kumfurahisha Yasmin.
Na kwa kweli nilihisi alitaka kujipependekeza naye ili apendwe yeye.
“Sasa ilikuwaje mkaachana?’
nikamuuliza.
“Tuliachana baada ya mimi
kurudi Unguja. Mama yangu aliniambia nirudi kwa sababu alikuwa akiishi peke
yake”
“Baba yako alikuwa yuko
wapi?” Yasmin akamuuliza.
“Alikuwa ameshakufa”
“Nani ambaye hajaoa katika
nyinyi?”
ITAENDELEA KESHO NA USIKOSE NA NINI KITATOKEA
No comments:
Post a Comment