KISIWA CHA HARISHI (4)
ILIPOISHIA TOLEO LILILOPITA
Yasmin akajifuta machozi yake
kwa shuka aliyokuwa amejifunga kisha akainua uso wake na kututazama. Sasa macho
yake yalikuwa mekundu na uso wake ulikuwa umeiva.
“Wiki moja kabla ya harusi
yangu huko Comoro nilikiota hiki kisiwa. Nikamuota kichaa mmoja akiniambia siku
zako zimekaribia za kuja kukaa katika kisiwa hiki” Yasmin akaanza kutueleza.
Tukawa tunamsikiliza kwa makini.
Akaendelea. “Nikamwambia yule
kichaa, siwezi kuja kukaa hapa, mimi natarajia kufunga ndoa hivi karibuni.
Nitakwenda kukaa Ufaransa si hapa
“Yule kichaa akaniambia, ndoa
yangu nitafunga na yeye kwani yeye alinichunuka tangu nilipokuwa ninasoma na
hatakubali niolewe na mtu mwingine.
“Nilipoamka asubuhi nilipuuza
ile ndoto. Sikumuelezea mtu yeyote na kwa kweli nilifanya kosa kuipuuza,
pengine nisingekuwa hapa leo hii. Yaani mpaka leo hii ninajuta”
Msichana huyo akaendelea
kutuelea. “Ile siku ya harusi yangu ilipofika saa mbili usiku niliona
kizunguzungu. Macho yangu yakafunga kiza. Nikaona kama moyo wangu unanisokota
na ghafla nikapiga ukelele na kuanguka chini. Baada ya hapo sikujijua tena
“Nilizinduka asubuhi na
kujikuta nomo ndani ya jumba hili katika kisiwa hiki. Mbele yangu nikamuona
yule kichaa niliyemuota akiniambia kuwa nitakuja kukaa hapa”
SASA ENDELEA
“Yule mtu niliyemuota hakuwa
binaadamu bali alikuwa jinni aliyekuwa amenichunuka. Siku ile nilipomuota
nilimuona katika sura ya kibinaadamu kichaa lakini nilipozinduka nikiwa katika
jumba hili alikuwa katika sura na umbile la kijini” Yasmin aliendelea
kutueleza. Kisa chake kilikuwa kimetushangaza na kutuogopesha.
Akaendelea. “Huyo jinni
aliponiona nimeshituka aliniambia Yasmin usiogope umeshafika nyumbani kwako,
mimi ndio nitakuwa mume wako. Utaishi katika jumba hili na hutarudi tena kwenu.
“Akaniambia kwamba yeye ni
jini wa ukoo wa kisubiani makata. Jina lake ni
Harishi wa Harishn. Chakula chake ni damu ya binaadamu. Ameniambia wazi kuwa
yeye ni jini mbaya aliyelaaniwa na ameshaua watu wengi.
“Akanihadithia kisa cha
kisiwa hiki. Aliniambia kilikuwa kinaishi watu zamani na mfalme wao alikuwa
akiishi katika jumba hili. Lakini yeye harishi ndiye aliyewaua mmoja mmoja kwa
kuwafyonza damu hadi kukimaliza kisiwa chote.
“Watu wachache waliobaki
waliondoka na kikiacha kisiwa kikiwa kitupu. Ndiyo sababu mlikuta magofu matupu
na mifupa ya watu waliouliwa na Harishi. Siku za mwanzo mwannzo mji huu ulikuwa
haukaliki kwa harufu zilizotokana na maiti za watu. Kunguru wa Zanzibar walihamia hapa
kujipatia riziki zao. Sasa hivi iliyobaki ni mifupa mitupu.
“Kwa sasa kisiwa hiki
kinajulikana kama kisiwa cha mauti. Wavuvi
ambao hawajui habari za kisiwa hiki wakifika hapa kushona nyavu zao Harishi
aliwaua mmoja mmoja kwa kuwafyonza damu”
Maelezo ya Yasmin yalitufanya
tutazamane mara kwa mara huku nyuso zetu zikiwa zimepigwa na butwaa. Hatukuwahi
kusikia kisa cha ajabu kama kile.
“Mimi nilikuwa nikilia peke
yangu hadi sasa silii tena. Ni kama nimeshazoea kuishi na yule jinni” Yasmin
aliendelea kutueleza.
“Kila wiki ankuja mara moja.
Au kama nina dharura ninamuita, anakuja. Humu ndani mna kila kitu. Mna kila
aina ya vyakula. Huwa najipikia mwenyewe chakula ninachotaka. Vyakula
vikipungua ananilete vingine.
“Pia ananiletea nguo za
kifalme pamoja na dhahabu. Huwa anaiba nguo hizo katika kasri za wafalme na
marais. Kila kitu ninachotaka ananiletea lakini hainisaidii. Maisha ya upweke
yananifanya nijione kama nimo ndani ya kaburi”
Wakati Yasmin anatuhadithia
kile kisa, nilimuuliza. “Umetuambia huyo jini anafyonza damu za watu na kuwaua,
je wewe utaendelea kuwa salama kweli”
“Mimi nimeshakuwa mke wake.
Ameniambia damu yangu ni haramu kwake. Hawezi kuniua ila hatanirudisha tena
kwetu. Nitaendelea kuishi hapa hadi mauti yanikute” Yasmin alituambia.
Kwa kweli hayakuwa maneno ya
kuogopesha tu bali pia yalikuwa yanasikitisha sana.
Maisha ya Yasmin yalikuwa
yanasikitisha. Alionesha wazi kukata tama na pia niliona kwa vyovyote
itakavyokuwa maish yake yatakuwa mafupi.
“Kwa hiyo sisi hatutapona?”
Mwenzetu mmoja akamuuliza Yasmin
“Sipendi niwafiche, nawaeleza
ukweli ili mujue kuwasaa zenu zimekaribia sana”
“Je kama tutaondoka ndani ya
jumba hili na kwenda kujificha mahali pengine?”
“Mtajificha wapi ambapo
hafiki. Kisiwa chote hiki amekimiliki yeye. Halafu yeye ni jini, lazima
atawagundua tu”
“Sisi tuko watu saba. Kweli
ataweza kutuua sisi sote kwa pamoja?”
“Nyinyi atawaua mmoaja mmoja.
Leo akiua mmoja, kesho anarudi tena kuua mwingine hadi mtamalizika nyote.
Akishaua mtu anamtupa nje aliwe na kunguru”
Msichana akatikisa kichwa
peke yake kabla ya kuendelea.
“Halafu hataki kuona mtu humu
ndani. Wivu wake ni mkali sana.
Siku nyingine anakuja na hasira, anasema anasikia harufu ya mtu humu ndani,
basi hunipiga hadi nazimia kisha huenda zake”
Kila mmoja wetu aliguna na
kumtazama mwenzake.
“Unadhani atakuja lini tena?”
nikamuuliza.
Usipitwe na Uhondo huu kila siku na Kumekucha blog nitaendelea kukupa habari na mambo kemkem
ITAENDELEA KESHO
|
Sunday, December 7, 2014
Kisiwa cha Harishi
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment