Kumekucha blog
Pangani,WAKAZI Wilayani Pangani Mkoani Tanga,
wamewataka wagombea nafasi za Serikali za mitaa kuikumbusha Serikali kuanza mchakato wa ujenzi wa ukuta wa maji Mto Pangani vyenginevyo wataususia uchaguzi
mkuu mwakani 2015.
Wakizungumza mara baada ya kumalizika mkutano wa kampeni wa
CCM kata ya Bushiri jana, wakazi hao wamesema kwa muda mrefu kumekuwa
kukitolewa ahadi lakini hadi kufikia
sasa hakuna dalili zozote za kuanza mchakato huo.
Walisema ukuta huo kwa
muda mrefu umeanguka na kutishia maji kuingia katika makazi ya watu na viongozi
wa wa juu wa Serikali na wa vyama wamekuwa wakitoa ahadi za matumaini kisha wakipotea jambo ambalo limekuwa likiwatia
hofu.
“Kupitia uchaguzi wa
Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwakani tunataka wagombea kusimama kidete
kuzungumzia ukuta wa mto Pangani----ambaye hatauzungumzia atakuwa hana
uzalendo” alisema Bakar Saleh
“Kama hatutaona wagombea wakishikia kidedea ukuta tunasema
tutaususia uchaguzi huu na wa mwakani---na hii itatupa ishara kuwa viongozi
wetu hawana uzalendo na badala yake wako kwa maslahi binafsi” alisema Saleh
Alisema viongozi wa Serikali Wilayani humo wamekuwa
wakilifumbia macho tatizo hilo jambo ambalo limekuwa likizidisha hofu kwa wananchi na hivyo kuwaeleza kuwa
vipimo vyao ni kipindi hiki cha kampeni za Serikali za mitaa.
Kwa upande wake mkazi wa Mikoroshoni, Mrisho Khalfan,
amewataka wagombea wa vyama vya siasa kuzungumzia sera za kufanya jamb gani
wakati wakishinda katika uchaguzi huo na kuacha kutupiana vijembe ambavyo
havijengi.
Alisema wananchi wa Pangani wako na kero nyingi zikiwemo
za masoko ya kuuzia mazao yao ambapo kwa
sasa wamekuwa wakiuza kwa walanguzi na kpata hasara na hivyo badala ya kusonga
mbele wanarudi nyuma.
Alisema kutokuwepo kwa masoko ya kuuzia bidhaa zao
kumewafanya kuwa masikini wa kila siku na baadhi ya matajiri kuwatishia kuwa
bidhaa hizo hazina masoko nje ya Wilaya hiyo.
“Kwa vile sisi ni walalahoi matajiri wamekuwa wakija kwetu na
kututishia vitisho kibao vikiwemo vya kutokuwa na kleseni za biashara na
kukamatwa na mamlaka ya mapatop---hili kwetu ni kitisho kikubwa na huwa
tunaamini” alisema Khalfan
Alisema ili kuondosha kero hiyo na baadhi ya wakulima na
wafanyabiashara kuuza mazao yao kwa uhakika ni vyema Serikali ikawajengea soko
la kuuzia mazao yao na kuepuka kulanguliwa.
No comments:
Post a Comment