Saturday, December 20, 2014
AISHA MADINDA ALIZIKWA JANA JIONI KIBADA,KIGAMBONI
Mwili wa Aisha Madinda ukitolewa kwenye gari la kubebea maiti mara baada ya kuwasili nyumbani kwao,Kigamboni jana jioni.
Mwili wa Aisha Madinda ukiwasili nyumbani kwa ajili ya kuswaliwa kabla ya mazishi yaliyofanyika katika makaburi ya Kibada, Kigamboni jijini Dar es salaam jana jioni
Mwili wa Aisha Madinda ukiswaliwa kabla ya maziko huko Kigamboni jijini Dar.
WAKURUGENZI
wa bendi hasimu za dansi Tanzania, African Stars, Asha Baraka na Extra
Bongo, Ali Choki, jana wameongoza mamia ya waombolezaji kumzika aliyekuwa
mnenguaji wa zamani wa bendi hizo, Aisha Mohamed Mbegu ‘Aisha Madinda’.
Mazishi
ya Aisha Madinda yamefanyika jana kwenye Makaburi ya Kijiji cha Mikwambe,
Kigamboni jijini Dar es Salaam, baada ya kukwama kufanyika jana
kutokana na zuio la Jeshi la Polisi, kupisha uchunguzi wa sababu za kifo
cha ghafla cha mnenguaji huyo.
Baada ya
uchunguzi huo kufanyika na ripoti kukabidhiwa kwa Jeshi la Polisi na
familia, mazishi hayo yakafanyika leo jioni yakihudhuriwa na Asha Baraka
na Choki, pamoja na Makamu wa Rais wa Shirikisho la Muziki Tanzania,
Salim Omari Mwinyi.
Akizungumza
katika mazishi hayo, Asha Baraka ambaye ni Mkurugenzi wa African Stars
Entertainment inayoimiliki Bendi ya African Stars ‘Twanga Pepeta’,
alimuelezea Aisha kuwa ni sawa na mwanaye kutokana na muda mwingi
aliotumia akiwa Twanga.
Baraka
aliongeza kuwa licha ya kutokuwa na Aisha katika siku za karibuni, bado
Twanga Pepeta inatambua na kuthamini mchango wa mkali huyo wa jukwaa na
kwamba pengo lake halitasahaulika kirahisi ndani ya bendi hiyo kongwe.
Kwa
upande wake Choki alisema daima atakumbuka uwajibikaji, usikivu na
upendo wa Aisha akiwa na Extra Bongo ‘Wazee wa Kizigo,’ na kwamba kwake
yeye marehemu ni sawa na dada yake, huku akimtaja kama mtumishi mwema.
“Alikuwa
na Extra Bongo kwa muda mfupi, lakini aina yake ya utumishi utabaki
katika kumbukumbu zetu daima. Huu ni mwaka wa taabu kwangu, kwani siku
ya arobaini ya marehemu mke wangu, alifariki pia mzee wangu Shem
Karenga,” alisikitika Choki.
Choki
alienda mbali zaidi kwa kulalama kuwa, siku moja baada ya kumzika Shem
Karenga, ndio siku aliyofariki Aisha Madinda, hivyo kuendeleza mfululizo
wa majonzi kwake na wadau wa tasnia nzima ya muziki wa dansi nchini.
Kwa
upande wake, mtoto wa dada wa marehemu, Sheikh Mohamed Mussa, ambaye
aliongoza mazishi upande wa familia, aliwashukuru Watanzania kwa
ushirikiano walioutoa katika kufanikisha mazishi hayo, huku akiwataka
kuuendelea kumuombea.
No comments:
Post a Comment