HADITHI
KISIWA CHA HARISHI (2)
Hapo ndipo tulipoanza
kufadhaika. Hatukuwa na la kufanya, tukawa tunatazamana!.
Tulikuwa tumepelekwa mbali sana kiasi kwamba
hatukuweza kuona vyombo vyovyote ambavyo vingeweza kutusaidia. Tukakata tama
kabisa.
Injini ya boti inapozima boti
inakuwa kwenye hatari ya kupigwa na dharuba na kupinduka. Kama hilo lingetokea ungekuwa
ndio mwisho wetu!
Hata hivyo bahari ilikuwa
tulivu. Tatizo letu ni kuwa safari yetu haikuwa na mwisho wala muelekeo
maalumu. Boti yetu ilikuwa inakokotwa kufuata upepo unakokwenda.
Mpaka jua linakuchwa hatukuwa
tumetokea kwenye nchi yoyote wala kisiwa chochote. Ndani ya boti tulikuwa na
vyakula vya akiba lakini hakukuwa na yeyote miongoni mwetu aliyesikia njaa.
Usiku ukapita kwa taabu huku
tukiendelea kupelekwa. Asubuhi tuliendelea tena na jitihada ya kuiwasha injini
lakini injini ilikataa katakata kuwaka. Tukaendelea kukokotwa hadi jioni. Hapo
tukatoa vyakula vyetu na maji tukala kidogo tu.
Tulilala tena kwenye boti
hadi siku ya tatu na ya nne. Vyakula vikatuishia licha ya kwamba tulikuwa
hatuli sana.
Tulibakisha maji kidogo tu.
Sasa tukahisi kwamba kama hatutakufa maji tutakufa kwa njaa kwani kwa siku
hizo nne tulizokuwa baharini tulikuwa tumekonda.
Alfajiri ya kuamkia siku ya
tano ndipo tulipotokea kwenye kisiwa. Sote tukashukuru ingawa hatukujua
kilikuwa kisiwa gani na kilikuwa katika eneo gani.
Kilikuwa kisiwa kikubwa
ingawa hakikuwa kikubwa sana.
Kwa vile tulikitokea wakati wa usiku hatukukiona kwa sababu ya giza. Tulikiona kulipoanza
kucha. Wakati tunakiona tulikuwa tumekikaribia sana. Sote tukapata furaha na matumaini ya
kuokoka.
Mawimbi yaliendelea
kutusukuma kidogodogo na kutufikisha kwenye maji madogo kabisa.
Suala kwamba kisiwa hicho
kilikuwa kisiwa gani na kipo wapi halikuwa na umuhimu kwetu. Kilichokuwa muhimu
ni kuwa tumefika mahali ambapo tungeweza kuyasalimisha maisha yetu nap engine
kupata msaada wa kutuwezesha kurudi kwetu.
Tulishusha nanga na kushuka
kwenye boti. Maji yalikuwa yakitufikia kwenye magoti. Tukaliacha boti na
kutembea kwa miguu kwa kuyasukuma maji hadi tukafika ufukweni mwa bahari.
Mahali tulipotokea hapakuwa na muinuko mkubwa. Tukapanda kwenye nchi kavu na
kuanza kutembea kwemye vichaka huku tukiangaza macho huku na huku.
Kulikuwa na kunguru wengi
waliokuwa wakiruka ruka kwenye miti. Jinsi walivyokuwa wakipiga kelele walikuwa
kama wanaotukaribisha katika kisiwa hicho
kilichokuwa kimya.
Tukaendelea kutembea
tukiingia ndani zaidi ya kisiwa. Mtarajio yetu yalikuwa kupata mji au kijiji
kilichokuwa kinakaa watu ili tuweze kusaidiwa.
Baada ya mwendo wa kama nusu saa tulianza kuona vibanda vilivyokuwa
vimebomoka. Tukapata matumaini kuwa kulikuwa na watu waliokuwa wanaishi katika
kisiwa hicho. Pia tulikuta visima viwili vya maji ambavyo vilikuwa vimekauka.
Wakati tunaendelea kwenda
ghafla tuliona tumetokea kwenye barabara pana ya changarawe. Tukaifuata ile
barabara mpaka tukatokea katikati ya mji. Ulikuwa mji mzuri uliokuwa na
barabara na majumba. Lakini nyumba zote zilikuwa zimechakaa na kubomoka. Baadhi
yake zilionekana kama mahame.
Jambo ambalo lilitushangaza
ni kuwa hatukuona mtu hata mmoja. Mji wote ulikuwa kimya kabisa. Tulikuwa ni
sisi peke yetu tu. Tulikatiza mtaa hadi mtaa kutafuta wenyeji wa kisiwa hicho
lakini hatukuona mtu.
Udadisi ukatufanya tuanze
kuingia katika zile nyumba. Tuliingia katika
nyumba ya kwanza. Tukakuta vitu vya ndani vilivyochakaa na kukongoroka.
Vilikuwa kama vitu vya zamani visivyotumika tena. Katika kutafiti tafiti
tulishituka tulipokuta mafumvu na mifupa ya binaadamu. Kuna iliyokuwa imelala
kwenye kitanda na mengine ilisambaa ovyo.
Tukatoka haraka katika nyumba
ile na kuingia katika nyumba nyingine, nako tulikuta vitu mbalimbali vya ndani
ya nyumba vilivyokuwa vimechakaa na mifupa ya binaadamu.
Tukawa tunatazamana kwa hofu.
Kila mmoja wetu alikuwa akijiuliza moyoni mwake, kulikoni? Lakini hatukupata
jibu.
Katika mitaa mengine tulikuta
mafuvu na mifupa ya binaadamu ikiwa barazani mwa nyumba na kando kando ya
barabara. Tulivyozidi tena kwenda mbele tulikuta mifupa ya mikono nay a miguu
ya binaadamu ikining’nia kwenye miti. Tukawa tunazidi kuitazama ile mifupa huku
tunazidi kwenda.
Ghafla tukatokea kwenye jumba
moja kubwa. Jumba hilo
ndilo lililokuwa kubwa na zuri kuliko jumba lolote katika kisiwa hicho.
Mbele ya jumba hilo kulikuwa na bustani ya maua na miti ya vivuli. Kutokana na uzuri wa
jumba hilo
tukaona tuingie ndani ili tuangalie lilivyo.
Tulipoingia tu pua zetu
zilikaribishwa na harufu nzuri ya manukato yaliyokuwa yananukia humo ndani.
Tulitembea katika sakafu ya marumaru iliyonakishiwa maua ya kupendeza.
Tulikuwa tumeingia katika
ukumbi mpana uliokuwa na madirisha na
mapazia ya hariri. Tulikuta meza, viti na makabati. Zilikuwa fanicha za
kifahari sana.
Baada ya kuupita ukumbi huo
tulitokea katika kumbi nyingine ndogondogo zilizokuwa na vyumba vipana. Tukawa
tunaingia kila chumba kuchunguza.
Katika chumba cha kwanza
tulikuta kitanda kilichotandikwa vizurii. Pia tulikuta makabati ya vioo
yaliyokuwa yanapendeza.
“Inaelekea kuna watu wanaoishi
ndani ya jumba hili” Mwenzetu mmoja akasema.
“Lakini mbona hatuwaoni hao
watu?” Mwingine akauliza.
“Ndiyo hatuelewi sasa”
aliyesema mwanzo akamjibu.
Je wavuvi hao wametokea
kwenye kisiwa gani hicho na ni kitu gani kitakachowatokea? Endelea kufuatilia
hadithi hii katika blogy hii kesho.
Unaweza kutuma maoni yako kuhusu
hadithi hii kwa kutumia blogy au kwa kutuma ujumbe mfupi kwa namba 0655 902929.
|
Tuesday, December 2, 2014
Soma hadithi ya kusisimua na Kumekucha blog
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment