Kumekucha blog
Tanga,WAZAZI na walezi Tanga wamelalamikia
hali ngumu ya maisha baada ya bidhaa nyingi kuwa bei juu vikiwemo vifaa vya
shule kwa wanafunzi na hivyo kuitaka Serikali kupunguza wingi wa kodi ili
kupata unafuu kwa baadhi ya mambo.
Wakizungumza wakati wa soko la Jumanne uwanja wa
Tangamano, baadhi ya wazazi hao walisema kukithiri wingi wa kodi imekuwa chanzo
cha maisha kuwa magumu na kuwapa kichwa wafanyabiashara kupandisha bidhaa zao.
Walisema kipindi hiki cha kuelekea shule kufunguliwa
wamedai vitu vingi viko bei juu jambo ambalo
kwa wazazi wenye vipato vya chini kushindwa kumudu mahitaji ya watoto wao
ikiwemo vifaa vya shule na ada.
“Kipindi hiki ni cha heka heka kuelekea sikukuu ya krismass
na kufunguliwa shule---hapa kila ukionacho hakinunuliki na hii ni sababu ya
kuwepo kwa utitiri wa kodi” alisema Abdalla Zubeir
“Ukizihesabu kodi za nchi yetu utachoka nijuavyo kuna
kodi moja tu ndio iliyoondolewa ambayo ilikuwa ikijulikana kama kodi ya
kichwa---mfanyabiashara analipa kodi hadi nyengine anazisahau” alisema
Alishauri Serikali kuwapatia maisha bora Watanzania
kwa kupunguza wingi wa kodi hizo kwa kuamini kuwa kupanda kwa bidhaa madukani
na masokoni na maisha kuwa magumu inatokana na kodi kuwaelemea wafanyabiashara.
Kwa upande wake mzazi mkazi wa Mikanjuni, Fatma
Athuman, ameishauri Serikali kudhibiti mfumo wa bei madukani kwani kitu
kinachofanyika kwa sasa ni ulanguzi na hivyo kutaka kuweko kwa utaratibu wa bei
moja.
Alisema kutokuwepo udhibiti wa bei imekuwa chanzo cha
kila mfanyabiashara kuwa na bei yake jambo ambalo limekuwa likiwaumiza wananchi
hasa masikini na kushindwa kukamilisha kwa baadhi ya mambo.
Alisema uhuru walionao wafanyabiashara umekuwa
ukiwaumiza wananchi masikini hasa vipindi vya sikukuu na kuelekea kufunguliwa
kwa shule na hivyo kuitaka Serikali kuchukua hatua madhubuti.
“Kila mfanyabiashara yuko na bei yake kitu ni kilekile
iweje huyu yuko na bei hii na yule yuko
na bei ile-----huku ni ukandamizaji na kudidimizana katika dimbwi la umasikini
jamani” alisema Fatma
Kuelekea vipindi vya sikukuu na ufunguaji wa shule,
mzazi huyo amewataka wafanyabiashara kuacha kupandisha bidhaa zao kwa tamaa ya
kujipatia pesa kwa njia za kiulanguzi jambo ambalo ni kosa na dhambi.
No comments:
Post a Comment