Sunday, December 7, 2014

Wananchi wenye hasira kali wauwa majambazi wawili

Kumekucha blog

Tanga,WATU wawili wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wameuwawa na wananchi wenye hasira kali baada ya jaribio lao la kutaka kupora fedha ofisi ndani ya kiwanda cha chokaa cha Meelkh Limited kilichopo Amboni Tanga kushindikana.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kaimu kamanda wa polisi Mkoa wa Tanga, Juma Ndaki alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 3 asubuhi baada ya walinzi wa kiwanda hicho kurushiana risasi ndani ya kiwanda.

Akiwataja majambazi hao waliuwawa kuwa ni, Timoth Chales (36) na Mwinyimkuu  Hamis(46) wote wakiwa ni wakazi wa Kinondoni Dar es Salaam na maiti zao kuhifadhiwa hospitali ya Rufaa ya Bombo.

Kwa mujibu wa maelezo yake Ndaki, alisema majambazi watatu walifanikiwa kutoroka kwa kuruka ukuta ambao ulikuwa umekuzungushiwa waya na wananchi kushindwa kuwakamata baada ya kutokomea porini.

“Kukamatwa kwa majambazi hao haikuwa kazi nyepesi kwani kulikuwa na kurushiana risasi zaidi ya nusu saa----kwa kushirikiana na wananchi majambazi wawili waliwakamata” alisema Ndaki na kuongeza

“Baada ya majambazi watatu kutoroka wananchi wenye hasira kali waliwashambulia kwa mawe na marungu na kufa wakati wakipelekwa hospitali ya Bombo” alisema Ndaki

Ndaki alisema majambazi hao waliingia ndani ya kiwanda hicho na kujitambulisha kwa walinzi kuwa wao ni wateja wa chokaa kutoka Dar es Salaam hivyo kuomba kuonyeshwa ofisi ya mhasibu kwa kufanya malipo.

Alisema baada ya kufika kwa mhasibu majambazi hao walimlazimisha kuonyeshwa sanduku la pesa na kumtishia kumkata shingo kama hatoweza kutoa ushirikiano na kuzipata pesa hizo na  kumtaka asipige kelele.

Alisema wakati  majambazi hao wakiwa ndani mlinzi wa geti aliewaruhusu kuingia ndani alipatwa na mashaka na ndipo alipowafuatilia nyendo zao na wakati akiingia ndani alisikia kelele za mwizi na ndipo alipotoa taarifa kwa wafanyakazi wa kiwanda hicho.

Alisema wafanyakazi na wananchi waliokuwa nje ya kiwanda hicho waliingia ndani na kuanza kurushiana mawe na marungu na wajambazi watu kufanikiwa kutoroka jambo lililowakasirisha na kuanza kuwapiga mfululizo.

“Polisi walipofika waliwachukua majambazi yale na wakati wakiwa njiani kuelekea hospitali ya Bombo wote walishakufa----kipigo walichokipata kilikuwa kikubwa kwani wote miili yao iliharibiwa vibaya” alisema Ndaki

Akitoa wito kwa wananchi, kaimu kamanda huyo aliwataka kuacha kujichukulia sheria mikononi na badala yake wavitaarifu vyombo vya usalama kufanya kazi zake kwani kufanya  hivyo amedai kuwa ni makosa.

                                    Mwisho

No comments:

Post a Comment