Thursday, December 18, 2014

Wazee kufunga safari kumuona Waziri Hawa Ghassia



Kumekucha blog
Tanga,UTARATIBU , wa Serikali kuwapatia wazee huduma ya matibabu bure umechukua sura mpya baada ya wazee Tanga kuadhimia kufunga safari ya kumuona Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa (Tamisemi) Hawa Ghassia kumjulisha kuwa  huduma hiyo kwao hakuna.
Kikundi cha wazee waliofika katika ofisi za kumekucha blog,  walisema  ahadi iliyotolewa na Serikali ya kuwapatia vitambulisho vya matibabu limekuwa ndoto na hivyo kwa sasa ni vyema wakafikisha kilio chao kwa Waziri Ghasia.
Wamesema kuna baadhi ya hospitali wameweka madirisha ya wazee kama ushahidi na kutokuwepo kwa huduma yoyote na hivyo kuona ni vyema kumuonaWaziri na kumueleza kero ambayo wamekuwa wakikabiliana nayo.
“Kwanza walisema watatupatia vitambulisho vya matibabu hadi leo hakuna lolote---tuendapo hospitali tunapaga foleni kama watu wengine” alisema Shaban Mkarama
“Alikuja naibu waziri hapa na kutupa matumaini ya kumalizika kwa ukiritimba wa upatikanaji wa huduma ya matibabu kwa wazee na sasa hakuna hata dalili za kusema tuwe na matumaini”alisema
Mkarama amemtaka Waziri Hawa Ghassia kulishughulikia kero hiyo kwani wamekuwa wakiteseka kwa kupanga foleni katika vyumba vya matibabu na madirisha ya dawa kitu ambacho kwao hakitakiwi kuwepo.
Alisema kwa muda mrefu wamekuwa wakipewa matumaini ya vitambulisho jambo ambalo halijatekelezwa na hivyo kupata shida wakati wa kuhitaji matibabu na kusababisha migongano na vijana na wazee wenzao.
Kwa upande wake, mkazi wa Ngamiani, Suleiman Madebe, ameitaka Wizara ya Afya na Ustawi wa jamii kuwaingiza wazee kwenye utaratibu wa matibabu katika mifuko ya jamii ili kwao kuwa rahisi kupata huduma tofauti na hivi sasa.
Alisema kuingizwa katika mifuko ya afya ya jamii itakuwa rahisi kupata huduma na matibabu bora zaidi na kuhudumiwa kwa wepesi tofauti na mfumo uliopo wa vitambulisho ambavyo pia upatikanaji wake ni mgumu.
“Ni vyema Wizara ya Afya na ustawi wa jamii kutuingiza katika mfumo wa matibabu wa mifuko ya jamii----huku tuliko sasa ni matatizo na ukiritimba” alisema
Alisema ni vyema Wizara ya afya ikalichukulia suala hilo ilio kuondoa manung’uniko kwa baadhi ya wazee na kuwepo kwa utaratibu wa matibabu kwa mfumo wa bimaya afya.
                                                         Mwisho

No comments:

Post a Comment