Monday, April 27, 2015

SOMA MAKUBWA YALIYOANDIKWA MAGAZETINI APRL 27 TZ

Uchambuzi huu wa magazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu Cha Candle Education Centre Tanga, Kituo kinaongoza kufaulisha wanafunzi kidato cha pili hadi cha sita. Kituo pia kinatoa kozi ya Kiingereza na Computer. Kituo kipo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 772746

ELE
NIPASHE
Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk.  Willibrod Slaa, amesema kuwa iwapo Watanzania watakipa  ridhaa  chama hicho  ili  kushika dola  katika uchaguzi wa mwaka huu, kitu cha  kwanza watakachoanza nacho  ni kuifuta Katiba inayopendekezwa sasa na kuanzisha mchakato wa Katiba yenye maslahi ya wananchi.
Dk.  Slaa alisema hayo wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika mjini hapa katika viwanja vya Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege,  Manispaa ya Morogoro na kuudhuriwa na umati mkubwa wa watu.
Alisema Katiba iliyopendekezwa na kupigiwa debe hivi sasa na Chama cha Mapinduzi (CCM) haina maslahi yoyote kwa  wananchi wa pande zote mbili za Muungano na kwamba ipo kwa ajili  ya kunufaisha viongozi wachache, hivyo wakiingia madarakani wataifuta mara moja.
Dk. Slaa alisema kuwa Katiba ya Wananchi wa pande zote mbili ambayo inagusa maslahi yao na kutetea haki zao ni rasimu  iliyopelekwa katika Bunge Maalum iliyoandaliwa na  aliyekuwa Mwenyekiti wa tume ya mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.
Sote tunamfahamu Jaji Warioba, alikuwa Waziri Mkuu wa nchi na ndiye aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya mabadiliko ya Katiba na katika tume yake alikusanya mapendekezo yenu nyinyi wananchi, lakini kwa maslahi yao hasa viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wakatoa maoni yenu na kuweka maslahi yao ,sasa nyie tuchagueni tuingie Ikulu tuwarudishie Katiba yenu,”  Dk. Slaa.
Alisema Jaji Warioba ni mmoja wa viongozi wachache wenye uchungu na nchi hii na ndio maana wakati wa kukusanya maoni alizingatia maslahi ya wananchi wote bila kuangalia rangi, kabila pamoja na itikadi ya vyama vya siasa.
Dk. Slaa alisema kuwa katika mchakato watakaounzisha endapo watapewa dola na Watanzania ni kuunganisha mapendekezo yote ya wananchi waliyotoa katika iliyokuwa tume ya Jaji Warioba ukiwamo muundo wa Serikali tatu ambao unakatiliwa na Serikali ya CCM.
NIPASHE
Wizara ya Kazi na Ajira, Mamlaka ya Usimamizi wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA) na Jeshi la Polisi, wataanza ukaguzi wa mikataba ya madereva wa mabasi na malori ambayo itatakiwa kubandikwa kwenye magari ikiwa na picha za dereva husika.
 Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk. Makongoro Mahanga , alisema kwa sasa kila dereva anatakiwa kubandika mkataba wake na mwajiri wenye picha kwenye kioo cha gari au kuwa nao ili ukaguzi unapofanyika uonyeshe picha halisi ya dereva anayeendesha gari lengo likiwa kuepusha magari kuendeshwa na madereva wasio na mikataba.
“Ukaguzi utaanza mara moja, tumeshakutana na waajiri na tutakutana nao kwa awamu nyingine, tunataka kila dereva awe na mkataba…mikataba ya awali ilikuwa mibovu sana,”Mahanga.
 Katika hatua nyingine, alisema suala la madereva kwenda kusoma lipo pale pale kwa kuwa ni jambo la kawaida kwa mtu kupata  mafunzo  kila  baada  ya  muda fulani.
“Walichokosea Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) ni kutangaza mpango wa kwenda kusoma bila kuhakikisha kanuni zimekamilika, kwenda ‘refresh course’ (mafunzo ya muda mfupi) ya miezi mitatu ni muhimu sana,” alisema na kuongeza:
Teknolojia inakua na kubadilika kila siku na magari wanayoendesha, yapo mapya yanakuja ili wamudu kuyaendesha vizuri ni vyema wakapata mafunzo mafupi kila baada ya miezi mitatu.”  
 Alisema kwa siku zijazo katika uchumi wa gesi, barabara kuu zinapaswa kuwa njia nne ili kuepusha magari kukutana.
NIPASHE
Siku 51 baada Mnikulu, Shaban Gurumo, kukiri mbele ya Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma kupokea mgawo wa zaidi ya Sh. milioni 80.8 kutoka kwa mmiliki wa kampuni ya VIP Engineering and Marketing, James Rugemalira, hadi leo anaendelea kukalia ofisi ya umma bila kuchukuliwa hatua.
Fedha hizo ni sehemu ya zaidi ya Sh. bilioni 200 zilizochotwa kifisadi katika akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Mamlaka za juu serikalini ikiwamo Ikulu zimeshindwa kueleza sababu za kutomchukulia hatua za kinidhamu, ikiwamo ya kumsimamisha kazi.
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue , lakini alisema Gurumo hayumo katika mamlaka yake ya nidhamu, bali Katibu Mkuu Ikulu ndiye anayeweza kuulizwa.
Gurumo ambaye alikiri mbele ya Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma iliyokuwa inaongozwa na Jaji Hamisi Msumi, alidai  kuwa Rugemalira ni rafiki yake takriban miaka 10 sasa, na ndiye aliyemshauri kufungua akaunti kwenye Benki ya Biashara ya Mkombozi, tawi la St. Joseph, jijini Dar es Salaam, kabla ya kumuingizia Sh. 80, 850,000 katika akaunti hiyo.
Kutokana na hali hiyo,  Baraza lilieleza kuwa Gurumo alikiuka sheria ya maadili ya viongozi wa umma inayokataza kiongozi wa serikali kupokea zawadi zaidi ya zawadi ndogondogo na ukarimu wa kawaida.
Pia, inakataza kiongozi wa umma kudai, kuomba au kupokea maslahi ya kiuchumi zaidi ya ukarimu wa kawaida au zawadi ndogondogo.
Hata hivyo, Gurumo aliliambia Baraza kuwa hakutambua kusudio la Rugemalira kumuwekea fedha hizo kwenye akaunti hiyo.
Alidai anahisi pengine Rugemalira alifanya hivyo kwa kuwa kipindi hicho alikuwa ana mgonjwa anayesumbuliwa na maradhi ya saratani.
MWANANCHI
Katika kile kinachoonekana kuendelea kujiimarisha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) vimegawana maeneo mbalimbali nchini vikifanya mikutano ya hadhara na mafunzo kwa viongozi wake ikiwa ni utekelezaji wa mkakati wa ushindi.
Ukawa unaundwa na vyama vya Chadema, NLD, NCCR-Mageuzi na CUF.
Chadema kilianza ziara zake mikoani wiki zilizopita baada ya kuzindua mkakati wake uitwao ‘Hakuna kulala, Hakuna kula, Mpaka Kieleweke’ nchi nzima wakati timu ya NCCR-Mageuzi ikiweka kambi mkoani Kigoma kwa kile ilichokiita kuimarisha majimbo ya kimkakati.
Sanjari na vyama hivyo, CUF tangu juzi kiliingia katika moja ya ngome zake, mkoani Mtwara pamoja na mipango mengine ya kiushindi, kinahamasisha wananchi kujitokeza kujiandikisha kupiga kura.
Jitihada za Ukawa kuzunguka mikoani zinakuja ikiwa ni majuma kadhaa tangu Chama cha Mapinduzi (CCM) kikiongozwa na Katibu Mkuu wake Abdulrahman Kinana kilipomaliza ziara ya kujiimarisha na kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2010.
Pia, ziara hizo ziligongana na zile za Chama cha ACT – Wazalendo zilizosababisha Chadema na chama hicho kipya kugongana Butiama.
ACT – Wazalendo kinachoongozwa na Zitto Kabwe kilihitimisha ziara yake ya kimkakati katika mikoa tisa inayoonekana kuwa ngome ya CCM, wiki iliyopita wilayani Bariadi, Shinyanga na kuvuna wanachama zaidi 6,000 katika mikoa hiyo.
Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe alisema jana kuwa Ukawa ina mikakati inayofanana ndani ya vyama vyao ya kuhakikisha inajiimarisha kisiasa nchi nzima ili ishinde Uchaguzi Mkuu.
Alisema siku 10 zilizopita, timu ya NCCR ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti – Zanzibar, Haji Hamis Hamad ilianza ziara Kigoma kuhakikisha majimbo ya mkoa huo yanaendelea kuwa ngome yake.
“Katika kikosi hicho, pia wamo Katibu Mwenezi, David Kafulila, Katibu Mkuu Mstaafu, Samuel Ruhuza na Kamishna wa Kagera, Peterson Mshenyela na wengineo,”Nyambabe.
MWANANCHI
Katibu mtendaji wa iliyokuwa Kamati ya Ukombozi Kusini mwa Afrika, Brigedia Jenerali Hashim Mbita , amefariki dunia jana saa tatu asubuhi katika Hospitali ya Jeshi, Lugalo, Dar es Salaam.
Mbita amekuwa akisumbuliwa na maradhi ya moyo katika kipindi cha miezi minane iliyopita.
Mtoto wa marehemu, Iddi Mbita alisema jana nyumbani kwa marehemu Chang’ombe, Dar es Salaam kuwa afya ya baba yake imekuwa ikibadilika mara kwa mara.
Alisema siku tatu zilizopita, hali yake ilikuwa mbaya kiasi cha kulazimika kuwekewa mipira ya kumsaidia kula.
Jana mzee aliamka vizuri asubuhi, lakini muda mfupi baadaye hali yake ikabadilika na kufariki dunia,” alisema.
Kuhusu mazishi, alisema yatafanyika keshokutwa saa 10 alasiri katika Makaburi ya Kisutu baada ibada ya kumuaga kwenye Msikiti wa Mtoro, Kariakoo.
Msiba utakuwa hapahapa nyumbani kwake, Chang’ombe. Upande wa familia tutakuwa na taratibu zetu, lakini upande wa Serikali na jeshi pia watakuwa na utaratibu wao wa mazishi,”
Rais Jakaya Kikwete ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya marehemu kutokana na kifo hicho.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu iliiagiza Serikali na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kushirikiana na familia katika kuandaa mazishi hadi maziko ya kiongozi huyo.
MWANANCHI
Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima ameliombea Taifa ili liepukane na ajali za barabarani, akisema nyingi zinasababishwa na kafara zinazofanywa na baadhi ya watu aliowaita wabaya.
Akitoa mahubiri kwa mamia ya waumini wa kanisa hilo jana, Gwajima alisema ajali nyingi si za kawaida, bali ni makafara yanayotolewa na baadhi ya watu na kutaka kila mmoja kuliombea Taifa ili kuondokana na tatizo hilo.
Gwajima ambaye anatuhumiwa kwa kuachia silaha katika mikono isiyo salama pamoja na kumkashifu, Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, alisema takwimu za Kikosi cha Usalama Barabarani zinaonyesha kwamba tangu Januari hadi Machi, mwaka huu, watu 866 walikufa kwa ajali za barabarani na wengine 2,370 kujeruhiwa.
“Ni lazima tujiulize ni kwa nini watu wengi wamekufa kwa ajali mwaka huu, haya ni makafara yanayotolewa na watu, naomba makafara yawarudie wenyewe waliyoyatengeneza,” alisema bila kutaja majina.
Alisema idadi ya watu waliokufa ni ya kuishia Machi na kwamba idadi ya Aprili ikiongezwa, itaongezeka karibu mara mbili.
Gwajima alisema kuna sababu nyingi ambazo zimekuwa zikitolewa kuwa zinasababisha ajali za barabarani na kwamba Serikali inatakiwa kutafakari kwa kina.
“Wanasema ajali zinasababishwa na madereva walevi, kwani miaka iliyopita hakukuwa na walevi, wanasema madereva hawana mikataba ya ajira, mwaka jana walikuwa nayo hiyo mikataba, tujiulize kwa nini sasa?” alisema.
Alisema pamoja na lawama nyingi kuwaendea madareva, lakini na wao wanakufa na kujeruhiwa kwenye ajali hizo.
Askofu huyo alisema kwa vile na wao wanakufa kwenye ajali hizo, inaonyesha kwamba tatizo hilo liko nje ya uwezo wao na kwamba unahitajika mjadala wa kitaifa ili kukabiliana nalo.
MTANZANIA
Jeshi la Polisi mkoani Mbeya linawashikilia watu wawili wanaodaiwa kuwa makada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambao ni vijana wa kikosi cha ulinzi cha chama hicho (Red Brigade), wakidaiwa kuwa na sare za jeshi na silaha zikiwamo za jadi.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi, alisema vijana hao walikamatwa juzi jioni katika eneo la Sogea wilayani Momba, baada ya kutolewa taarifa na raia wema.
Kamanda Msangi aliwataha vijana hao waliotiwa mbaroni kuwa ni Mathayo Mwafongo na Salehe Sichalwe, ambao kwa pamoja walikutwa na visu, manati, mawe ya kurushwa kwa kutumia manati, sare za jeshi na simu tatu za mkononi.
Vijana hao pia walikuwa na fulana ya Chadema, kilemba na barua tatu za kuwatambulisha kuwa wao ni wafuasi wa Chadema waliokuwa wakienda Kata ya Chitete, Msangano na Kamsamba wilayani Momba, kutoa mafunzo kwa vijana wa chama hicho.
Kamanda Msangi alisema kutokana na kushamiri kwa matukio ya ugaidi katika maeneo mbalimbali, jeshi la polisi limeweka ulinzi kudhibiti matukio hayo katika kila kona ya nchi.
“Kwa hiyo wakati askari wakiwa katika doria, walipata taarifa juu ya watu hao na kuzifanyia kazi,”  Msangi.
Alisema askari wa doria kwa kushirikiana na wananchi, waliweza kuwakamata vijana hao saa tatu asubuhi wakiwa kwenye pikipiki.
Kamanda alisema vijana hao walikamtwa eneo la Sogea, Tunduma wakiwa wamevaa mavazi meusi, wamebeba mikoba mgongoni na wakiwa wamefunika nyuso zao.
“Raia wema walifika kituoni na kutoa taarifa juu ya hofu yao kwa watu hawa ambao walikuwa wamevaa mavazi tofauti na muonekana wa watu wengine…tulivyowafuatilia tuliwakamata na walipopekuliwa walikutwa na silaha na sare za jeshi.
Kamanda wa Ulinzi Chadema Nyanda za Juu Kusini, Aron Siwale alikiri kumtambua mtuhumiwa Mathayo Mwafongo huku akimkana Salehe na kusema kuwa ni dereva wa bodaboda.
Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, amedai chama chake kinawindwa na polisi kila kona.
Polisi wamekuwa na kazi kubwa ya kuhakikisha kikosi cha ulinzi cha Red Bregade hakifanikishi malengo yake.
“Tunawindwa kila kona ya nchi hii, polisi hawalali kwa ajili yetu sisi…nawaambia tutakufa nao katika hili, haturudi nyuma,”  Mbowe.
MTANZANIA
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo , Freeman Mbowe, amesema hawatamruhusu Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, kujiunga na Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).
Kauli ya Mbowe imetolewa siku chache baada ya Zitto kutangaza kuwa ACT ipo tayari kujiunga na Ukawa kama wanavyotaka Watanzania wakiwamo baadhi ya viongozi wa umoja huo.
Mbowe alisema kuwa hawamwamini tena Zitto kwa madai kuwa akiingia Ukawa atakuwa akivujisha siri za umoja huo kwenda Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Hatuwezi kumruhusu Zitto na chama chake kiwe miongoni mwa Ukawa. Tukiruhusu Zitto awepo siri zote zitakuwa zikiwafikia CCM,” alisema Mbowe.
Aprili 15 mwaka huu, Chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT-Wazalendo), kilitangaza kuwa kipo tayari kushirikiana na vyama vingine vya siasa kwa lengo la kuleta mapinduzi ya uchumi na kubomoa mfumo unaowanyonya wananchi.
Zitto alisema hivi sasa taifa limekuwa na shauku ya ACT kushirikiana na vyama vingine kama njia ya kufanikisha malengo ya kukitoa CCM madarakani.
MTANZANIA
Rais Jakaya Kikwete ametoa msamaha kwa wafungwa 4,129 ambako 400 wataachiwa huru na wengine 3,729 watapunguziwa vifungo vyao.
Alitoa msamaha huo katika kuadhimisha miaka 51 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, kwa kutumia madaraka yake aliyopewa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na kusainiwa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Mbarak Abdulwakil, wafungwa waliopunguziwa vifungo watabaki gerezani wakitumikia sehemu ya kifungo kilichobaki.
Ni mategemeo ya Serikali kwamba wafungwa watakaoachiwa huru watarejea katika jamii kushirikiana na wananchi wenzao katika ujenzi wa taifa na watajiepusha kutenda makosa ili wasirejee tena gerezani,”ilisema taarifa hiyo.
Katika msamaha huo wafungwa wote watapunguziwa moja ya sita ya vifungo vyao zaidi ya punguzo la kawaida linalotolewa chini ya kifungu namba 49(1) cha Sheria ya Magereza sura ya 58, isipokuwa wafungwa wenye makosa yasiyo na msamaha.
Wafungwa waliosamehewa ni wenye magonjwa kama Ukimwi, kifua kikuu na saratani, wafungwa wazee wenye umri wa miaka 70 au zaidi na wafungwa wa kike walioingia na mimba gerezani na wale walioingia na watoto wanaonyonya na wasionyonya.
Wengine ni wafungwa wenye ulemavu wa mwili na akili. Wote waliosamehewa wanatakiwa kuthibitishwa na jopo la waganga chini ya uenyekiti wa mganga mkuu wa mkoa ama mganga mkuu wa wilaya.
JAMBOLEO
NI sherehe tu! Timu ya Yanga imepanga kufungua champagne endapo watapata pointi tatu dhidi ya Polisi Morogoro leo, zitakazowafanya kutangazwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom msimu huu.
Yanga itashuka kwenye Uwanja wa Taifa jijini hapa ikisaka pointi tatu dhidi ya Polisi Moro zitakazowafanya kufikisha pointi 55 ambazo hazitaweza kufikiwa na mabingwa watetezi Azam FC wenye pointi 45 katika nafasi ya pili.
Katibu Mkuu wa Yanga, Dk. Jonas Tiboroha, alisema kuwa wameandaa champagne na jezi za kutosha kwa ajili ya kusherehesha ubingwa huo kama watautwaa leo.
Tunajua umuhimu wa mchezo huo (Polisi Moro) ambao utakuwa mgumu kutokana na wapinzani wetu kuwa kwenye hatari ya kushuka daraja, lakini sisi lengo letu ni ushindi ili kutangaza ubingwa mapema.”
Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van Pluijm, naye alisema: “Mechi ya kesho (leo) ni muhimu sana mbali ya kuwa ya ubingwa, nimepanga kuitumia kukisoma kikosi nitakachokipanga kwenye mchezo wa marudiano dhidi ya Etoile du Sahel.”
Wakati Yanga ikitamba hivyo, kocha wa timu ya Polisi Morogoro, John Tamba amedai kuwa hawatakubali kuwa ngazi ya Yanga kutangaza ubingwa, wamejipanga kushinda ili kujinasua kwenye janga la kushuka daraja.
Tumeshakamilisha maandalizi yetu na tumejiandaa kwa ajili ya kuzoa pointi tatu ili tuendelee kupanda juu na sio kushuka daraja,” alisema.
Yanga itakuwa na kibarua kigumu kupata pointi hizo kutokana na Polisi Moro kuwa kwenye vita ya kuwania kutokushuka daraja, hivyo Polisi wataingia uwanjani kwa lengo la kushinda na kutoka katika nafasi ya 12 wakiwa na pointi 25.
Hata hivyo, kwenye mchezo wa kwanza baina ya timu hizo uliofanyika Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, Yanga ilishinda kwa mbinde bao 1-0 lililofungwa na Danny Mrwanda wakati huo Polisi Moro ilikuwa ikinolewa na kocha Adolph Rishard aliyetimuliwa mwezi uliopita.
Yanga inatarajia kuondoka na msafara wa watu 70 keshokutwa kuelekea Tunisia kwa ajili ya mchezo wao wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Etoile utakaofanyika jijini Sousse nchini humo Jumamosi hii.
“Ndege tutakayotumia itakuwa na watu 68, wawili tutawapitia Afrika Kusini na kufanya idadi ya watu 70, lakini kuna wengine wanne watatokea Ubelgiji kuja kuisapoti Yanga Tunisia. Katika idadi yote hiyo watu 29 ni wachezaji, benchi la ufundi pamoja na sisi viongozi, waliobakia wote watakuwa mashabiki (45),”  Tibohora.
HABARILEO
Miezi imeanza kuhesabika kabla ya huduma ya usafiri kupitia mradi wa mabasi yaendayo haraka jijini Dar es Salaam kuanza, baada ya mkataba kusainiwa kati ya serikali na wamiliki wa daladala kwa ajili ya kuendesha katika kipindi cha mpito.
Serikali kupitia Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) imetia saini makubaliano ya uendeshaji na Kampuni ya Uda Rapid Transit kuendesha huduma ya usafiri huo katika kipindi cha mpito.
Kampuni ya Uda Rapid Transit imeundwa kwa pamoja baina ya Kampuni ya Usafiri Dar es Salaam (Uda) na wamiliki wa daladala. Kusainiwa kwa makubaliano hayo, kumeelezwa na serikali kuwa ni tukio la kihistoria katika mchakato wa mfumo wa mabasi yaendayo haraka.
 Katika mkataba huo wa miaka miwili, kampuni hiyo itatakiwa kununua mabasi 76 yenye urefu wa meta 12 na 18 kuanza kutoa huduma hiyo katika barabara za mradi jijini Dar es Salaam miezi minne kuanzia sasa.
Wakati Dart ikiwakilishwa na Mtendaji Mkuu wake, Asteria Mlambo, Kampuni ya Uda Rapid Transport iliwakilishwa na Robert Kisena na Sabri Mabruki.
Walioshuhudia utiaji saini huo ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Hawa Ghasia na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki na viongozi wengine.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini jijini Dar es Salaam, Ghasia alisema tukio hilo ni la kihistoria katika mchakato wa mfumo wa mabasi yaendayo haraka.
“Tumefikia hatua nzuri kwa nchi yetu kuwa serikali imeweza kushirikiana vyema na wadau binafsi wa usafiri kupata kampuni ya kuendesha huduma ya usafiri kipindi cha mpito,” alisema.
Alisema pamoja na kwamba mradi mzima haujakamilika, serikali imeamua kuanza na huduma ya mpito katika barabara ya Kimara hadi Kivukoni ambayo imekamilika kwa asilimia 90 na kuwa sasa kazi inayofanyika ni ya kuweka taa za barabarani.
Alifafanua kuwa usafiri katika barabara hiyo utakuwa wa uhakika na wa kisasa kwa vile basi moja la urefu wa meta 18 litakuwa na uwezo wa kubeba watu 150 wakati ya meta 12 yatakuwa na uwezo wa kubeba abiria 80 kila moja.
Mwakilishi wa Uda Rapid Transit ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Daladala (DARCOBOA), Mabruki alisema wamejipanga kutoa huduma nzuri ya usafiri katika kipindi cha mpito.
Hautopitwa na stori yoyote inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia www.tangakumekucha.blogspot.com

No comments:

Post a Comment