Friday, July 17, 2015

SOMA HABARI KUBWA ZILIZOPEWA UZITO MAGAZETI YA LEO JULY 17 TZ

Uchambuzi huu wa magazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha elimu cha Candle Education Centre Tanga. Kituo kinaongoza kufaulisha wanafunzi kidato cha pili hadi cha sita na wanaojiendeleza kielimu. Kituo kinatoa kozi mbalimbali za kitaaluma ikiwemo ya Umeme. Wapo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 772746

theMWANANCHI
Wakati mchakato wa kumtafuta mgombea wa urais kwa tiketi ya CCM ukiwa umekamilika, ni dhahiri kwamba baadhi ya vigogo waliokuwa na matumaini makubwa ya kuukwaa, sasa wanaugulia maumivu huku wengine wakiwa wameshautangazia umma kutoendelea na ubunge.
Licha ya kuwa siasa ni pata potea, kwa wanasiasa vijana huenda mchakato huo ukawa ni mwanzo wa safari ya kuelekea kwenye kilele cha mafanikio na kwa baadhi ya vigogo huenda ukawa ndiyo mwanzo wa kuelekea kustaafu siasa.
Edward Lowassa, Frederick Sumaye, Dk Mohammed Gharib Bilal, Stephen Wasira, Mizengo Pinda, Samuel Sitta na Profesa Mark Mwandosya ni makada waliojitokeza kujaribu bahati yao ya kuteuliwa kugombea urais, lakini ni dhahiri kuwa sasa watakuwa wanaanza kujiwekea mazingira ya kuachana na siasa.
Wote hawakumudu kuingia kwenye orodha ya wagombea watano waliopelekwa kwenye Halmashauri Kuu kwa ajili ya kuchujwa hadi kubakia watatu ambao hupelekwa kwenye Mkutano Mkuu kwa ajili ya kumpata mgombea urais wa CCM.
Kwa mujibu wa utaratibu wa CCM wa kumuachia mteule agombee kwa vipindi viwili iwapo anashinda uchaguzi wa Rais, makada hao sasa watalazimika kusubiri hadi mwaka 2025 ili kujaribu tena bahati yao, jambo ambalo linaonekana halitakuwa rahisi.
“Nyakati za kisiasa zinabadilika haraka sana. Miaka 10 ijayo siyo mchezo,” alisema Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), Hamad Salim alipohojiwa na Mwananchi kuhusu mustakabali wa makada waliokosa nafasi ya kupeperusha bendera ya CCM kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25.
“Kwa kipindi hicho, mambo mengi yatabadilika, wanasiasa waliogombea kipindi hiki hawawezi kuwa kwenye umaarufu wa sasa, wanaweza kupanda chati au kushuka.
 “Pia, kuna suala la umri wazee kama Dk Bilal au Sumaye miaka 10 ijayo kupanda jukwaani na kushuka mara kwa mara itakuwa shida kidogo. Wanasiasa wengi waliokuwamo kwenye kinyang’anyiro hicho ni wazee na ule siyo umri wa kushinda majukwaani.”
Licha ya sifa za mgombea kutozungumzia umri wa juu bali wa chini ambao ni kuanzia miaka 40, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Richard Mbunda alishauri baadhi ya vigogo walioshindwa kupumzika kupisha damu changa za mabadiliko.
Alisema: “Siasa nchini hazitabiriki na ni za kipekee kwani unaweza ukawa maarufu usichagulike na siku zinavyokwenda ukapoteza umaarufu huo.
“Kwa hali ya sasa, Bilal, Pinda, Lowassa, Sitta tayari walishakamata nafasi za juu nchini na umri wao umeshasogea. Bila shaka ni muda muafaka kupisha wengine… wameshaitumikia nchi vya kutosha na wana marupurupu ya kutosha baada ya kustaafu. Ni bora wawaachie vijana walete mabadiliko,”  Mbunda.
Alisema makada hao ni washauri wazuri iwapo wataachana na siasa za kushindana. Alisema hata kwa wale ambao umri unawaruhusu, haitakuwa vizuri kuwapa vyeo vidogo kama vya ubalozi na kwa maana hiyo alisema safari yao kisiasa, imefikia ukingoni.
MWANANCHI
Baada ya tetesi za muda mrefu, hatimaye Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi ), Moses Machali amejiunga na Chama cha ACT – Wazalendo.
Naibu Katibu Mkuu wa ACT – Wazalendo, Msafiri Mtemelwa alisema hayo jana alipokuwa akimtambulisha kwa waandishi wa habari, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kitengo cha Vijana wa NCCR  – Mageuzi, Deo Meck ambaye naye amejiunga na chama hicho.
Machali ambaye hakuwapo kwenye utambulisho huo, alithibitisha kwa simu jana kujiunga na chama hicho kipya kinachoongozwa na aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe na kusema atatoa ya moyoni Julai 21 katika mkutano utakaofanyika kwenye Uwanja wa Kiganamo, Kasulu Mjini.
“Nitakuwa na Zitto na wabunge wengine ambao siwataji kwa sasa,” alisema Machali. awali, Mtemelwa alisema Machali amejiunga na chama hicho na kwamba kinachosubiriwa ni utaratibu maalumu wa kumtambulisha kwa wananchi.
“Siyo Machali pekee ambaye amekuwa akihusishwa kuhamia katika chama hiki, bado kuna wabunge kama wanne, nao wakati wowote watatambulishwa kwa wananchi. Staili yetu kwa hawa wabunge ni kuwapokea na kuwatambulisha  katika majimbo yao, mbele ya wapigakura,”Mtemelwa.
Alisema kuhamia katika chama hicho kwa wabunge na vijana wengi kutoka upinzani ni mwendelezo wake wa kupokea wananchi wa sehemu mbalimbali wanaotaka demokrasia ya kweli.
Meck ambaye alikabidhiwa kadi ya uanachama jana hiyohiyo, alisema ameamua kuhamia ACT kwa sababu vyama alivyopita havikuwa na demokrasia na mabadiliko ya kweli.
Alisema baadhi ya vyama vya siasa havijajikita katika kutoa elimu kwa wanachama wake na kwamba ACT imedhamiria  kuirudisha nchi katika misingi iliyowekwa na waasisi  wa Taifa.
“ACT kipo tofauti na vyama vingine, leo (jana ) nimejiunga na nimepewa vielelezo ambavyo ni kama mwongozo kwa kile kinachofanywa,” alisema Meck.
Mbali na mwanachama huyo, pia aliyewahi kuwa mlinzi wa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Khalid Kagenzi naye alionekana katika ofisi hizo.
NIPASHE
Ofisa Mwandamizi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Kigoma, Conrad Mtega , amefariki dunia baada ya gari alilokuwa akisafiria na Meneja Kampeni wake kwenda kuchukua fomu ya kuomba kuwania ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Songwe Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya kupinduka.
Kampeni Meneja wake aliyeaga dunia katika ajali hiyo ni Nyawili Kalenga.
Majeruhi katika ajali hiyo ambao wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Iringa ni Baraka Zachayo na Rebeca Mtega.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Pudensiana Protace, alisema ajali hiyo ilitokea juzi eneo la Tanangozi saa 8:30 mchana katika barabara kuu ya Iringa-Mbeya.
Alisema ajali hiyo ilitokea baada ya gari lenye namba za usajili T 291 BNK aina ya Nissan Patrol iliyokuwa ikiendeshwa na Ofisa huyo wa Takukuru kugongana uso kwa uso na lori lenye namba za usajili T 738 ATQ lililokuwa likiendeshwa na Henry Lulandala, likitoka Mbeya kwenda Dar es Salaam.
Kamanda Pudensiana alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa dereva wa Nissan Patrol ambaye aliyumba na kupoteza mwelekeo na kisha kugongana na lori hilo na kusababisha vifo na majeruhi hao.
Ofisa Uhusiano wa Takukuru, Doreen Kapwani, alithibitisha kupokea taarifa za kifo cha mfanyakazi huyo na kufafanua kwamba alikuwa Mkaguzi wa Kanda Takukuru.
Mbunge wa Songwe (CCM), Philip Mulugo, alisema amepokea kwa masikitiko makubwa tukio la kifo cha watu hao ambao walikuwa wanakwenda jimboni kwake kuchukua fomu ya kuwania ubunge.
“Marehemu (Mtega) alipata ajali wakati akija jimboni kwangu kuchukua fomu na alishatangaza nia ya kugombea ubunge Jimbo la Songwe siku nyingi,  Mulugo.
NIPASHE
Wasichana watatu waliofanya vizuri masomo ya Sayansi katika mtihani wa taifa wa kidato cha Sita mwaka jana, wameeleza siri ya mafanikio yao kuwa ni kusoma kwa bidii, kujituma na kujiepusha na mambo yasiyo ya msingi kwenye masomo.
Wahitimu hao, wametoa ushauri kwa watoto wa kike na wazazi kuwawezesha kufanya vizuri kimasomo, kimaisha na kusimama wenyewe.
Hunayza Salim Mohammed, ni mtahiniwa wa kwanza msichana kwenye kumi bora kwa masomo ya sayansi kitaifa na watatu katika idadi hiyo, kutoka shule ya sekondari ya Feza Girl’s jijini Dar es Salaam, katika masomo ya Fizikia, Kemia na Hisabati (PCM).
Hunayza alisema Mungu ndiye aliyemuwezesha kufanya vizuri zaidi katika mtihani huo kutokana na kumjalia kuwa na uwezo wa akili.
Hunayza  ambaye ni mtoto wa pili kuzaliwa kati ya watoto saba katika familia yao, alisema jingine ni kushirikiana na wenzake kusoma na kusaidiana.
Alisema anatambua kuwa wazazi wake walihangaika ili apate elimu tangu akiwa shule ya awali kwani walijinyima na kuhakikish anasoma shule yenye mazingira bora na walimu wa kutosha.
Mwanafunzi mwingine, Rosemary Osian Chengula , ni msichana wa tatu kati ya watahiniwa 10 bora wa masomo ya Sayansi kitaifa na wa pili kati ya wasichana watato waliochomoza kwenye kundi hilo, alisoma masomo ya Fizikia, Kemia na Hisabati (PCM).
Kwa sasa yupo Jeshi la Kujenga taifa (JKT), kwa ajili ya mafunzo ya muda mfupi kwa mujibu wa sheria za nchi.
Baba mzazi wa Rosemary, Osian Chengula, ambaye ni mfanyabiashara wa viungo vya pilau na mboga katika soko kuu la Makambako, alisema siri ya mafanikio ya binti yake ni uwezo wake,  amezaliwa na kipaji na ni mwepesi wa kufuata ushauri wa wazazi na jamii anayoishi.
Msichana Meghna Vipul Solanki , ni mhitimu wa shule ya sekondari ya Shaaban Robert, jijini Dar es Salaam, katika masomo ya Fiziki, Kemia na Baolojia (PCB).
Binti huyo ni kutoka familia ya kipato cha chini na kutokana na jitihada zake kimasomo alipata ufadhili unaotolewa na shule hiyo kupitia mfumo maalum kuanzia kidato cha pili hadi cha sita.
 Meghna anasema muda mwingi alikuwa anajisomea baada ya kupanga ratiba yake kwa yale aliyokuwa anafundishwa darasani na walimu wake.
Anasema siku za mapumziko ya juma na likizo, husoma hadi saa saba usiku, muda mchache wa ushiriki michezo mbalimbali na hana muda wa kwenda disco au kuongea mambo ambayo hayamsaidii katika maisha yake.
“Sijawahi kusoma masomo ya ziada, zaidi ya ninavyofundishwa shuleni, nimeona wazazi wangu wanavyohangaika huku na kule kuhakikisha na mdogo wangu tunapata elimu,”
Mkuu wa shule hiyo, Suryakant Ramji, anasema anapenda kuoa watoto wa kike wanafanya vizuri na ndiyo maaa wametoa motisha kwa wanafunzi wote wanaofanya vizuri lakini zaidi hususan watoto wa kike.
Mama mzazi wa Meghna, Bina Solanki, anasema mafanikio ya mtoto wake ni Baraka za Mungu kwa sababu si wa kusukumwa kwa jambo lolote.
NIPASHE
Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimemtaka mwanasiasa mkongwe, Kingunge-Ngombale Mwiru kufanya anachotaka kufanya.
Juzi Kingunge alijitokeza hadharani na kuzungumzia na waandishi wa habari huku akiwaambia kwamba kilichofanywa na CCM katika kumpata mgombea wa urais, Dk. John Magufuli ni haramu.
Dalili ya CCM kupasuka vipande zimeanza kuonekana dhahiri, baada ya Kingunge kujitokeza hadharani kupingana na maamuzi yote yaliyofanywa hususani kukata jina la Edward Lowassa katika hatua za mwanzo za kuteua mgombea urais.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye  jana alisema kuhusu tuhuma zilitolewa na Kingunge ambaye kadi yake ya uanachama ni namba nane, alijibu kwa kifupi kwamba afanye anachotaka kufanya na kwamba hana maoni zaidi.
“Sina Comment (maoni) wewe unataka niseme nini? kaandike hivyo nilivyosema kwa sababu na mimi ni mwandishi na nilishawahi kuwa mhariri kwa hiyo najua,” alisema na kukata simu.
Chama hicho tawala kilimteua Dk. John Magufuli na Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea wake mwenza kupeperusha bendera yake katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwakani.
Jumla ya watia nia 38 majina yao yaliingia katika vikao vya awali, lakini waliovuta kuingia tano bora ni Magufuli, Dk. Asha-Rose Migiro, Balozi Amina Salum Ali, Januari Makamba na Bernard Membe.
Hata hivyo, Halmashauri Kuu (NEC) iliwachuja Makamba na Membe na kuwabakiza Magufuli, Amina na Migiro kisha Magufuli kuibuka mshindi.
NIPASHE
Kasi ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuomba nafasi za udiwani na ubunge katika Jimbo la Monduli, inasuasua na tayari chama hicho kimeitisha kikao cha dharura cha Kamati ya Siasa kitakachokutana leo kukuna vichwa kutafuta ufumbuzi wa hali hiyo.
Katibu wa CCM Wilaya ya Monduli, Elisante Kimaro, alisema jana kuwa kusuasua kwa wanachama kuchukua fomu za kuomba kugombea nafasi hizo kunatokana na kushuka kwa morali ya wanachama baada ya Mbunge wa zamani, Edward Lowassa, aliyekuwa akiwania kuteuliwa na chama chake kugombea urais, kukatwa jina lake.
“Zoezi la uchukuaji wa fomu za udiwani linasuasua, lilianza juzi na siku ya mwisho ni Julai 19, mwaka huu saa 10 jioni.
“Zoezi hili ni gumu sana, hata hivyo bado ni mapema sana kutoa taarifa, lakini morali ya wanachama kuchukua fomu za kuomba kugombea imepungua,” alisema.
Alisema ameitisha kikao cha dharura cha Kamati ya Siasa chenye wajumbe 16 kuzungumzia suala hilo ili kwa pamoja wahamasishe wanachama kugombea.
“Tunawahimiza wanachama wajitokeze kuchukua fomu za kugombea nafasi hizo,” alisema na kuongeza: “Hili jimbo ni ngome ya CCM na wala sina shaka na hilo.”
Alisema kusuasua huko kunatokana na baadhi ya madiwani waliomaliza muda wao kufanya propaganda ya kuwazuia wanachama kwenda kuchukua fomu kwa madai kwamba wasubiri kwanza kauli ya mbunge wao.
“Baadhi ya madiwani wa zamani wanatengeneza propaganda, hawa ni madiwani wale ambao hawakubaliki katika kata zao…wanawahamasisha watu wasichukue fomu kwa kigezo kwamba wasubiri kauli ya Mbunge Lowassa, jambo ambalo siyo kweli,” alisema.
Aliongeza: “Lowassa hajawahi kufanya kitu kama hicho cha kuwaambia wanachama wasichukue fomu hadi atakapotoa kauli yake…jana (juzi), alikuja hapa Monduli kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, hakutamka lolote, alisema tu hana la kusema.” 
Alisema watu hao wanatumia mgongo wa Lowassa kueneza propaganda.
Alisema kwa upande wa ubunge hadi sasa amejitokeza mwanachama mmoja tu, Mbayani Tayayi, aliyechukua fomu yake jana saa 4:00 asubuhi, wakati kwa upande wa udiwani waliochukua fomu ni mwanachama mmoja mmoja katika kata za Mswakini, Lepurko na Engutoto.
Pamoja na kusuasua huko, Kimaro alisema atahakikisha kata zote 20 zinapata wagombea wa udiwani na kumpata mgombea ubunge.
Alizitaja kata hizo kuwa Engaruka, Engutoto, Esilalei, Lepurko, Loksale, Majengo, Makuyuni, Meserani, Nalalani, Lemooti, Moita, Monduli Juu, Monduli Mjini, Mfereji, Mswakini, Mto wa Mbu, Migungani, Selela, Sepeko na Lashaini.
Alisema tangu kumalizika kwa mchakato kupata mgombea ndani ya chama hicho Julai 12, mwaka huu, mjini Dodoma ambapo jina la Lowassa lilikatwa katika mazingira ya kutatanisha, kumekuwa na maneno mengi yakisambaa kwenye mitandano ya kijamii kwamba Lowassa anakihama chama hicho.
“Hizi habari si za kweli, bado tuna imani na Lowassa,” alisema.
Alisema mchakato wa kumpata mgombea ndani ya chama hicho tayari umemalizika kwa kumpata mgombea wake, Dk. John Magufuli.
Baadhi ya wakazi mjini Monduli walisema kitendo cha kuenguliwa kwa mbunge wake katika kinyang’anyiro cha urais, kimewavunja moyo kwa maelezo kuwa utaratibu haukufanyika kwa haki.
JAMBOLEO
Aliyekuwa Mkurugenzi  Mtendaji wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade), Ramadhan Khalfan, na wenzake wawili, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashitaka matano ikiwamo matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia serikali hasara ya Sh. milioni 49.145.
Mbali na Khalifan, washtakiwa wengine ni, Mkurugenzi  wa Utafiti na Mipango, Samuel Mvingira na Kaimu Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, Judith Msuya. 
Washtakiwa hao walisomewa mashitaka yao mbele ya Hakimu Mkazi, Wilfred Dyansobera.
Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Maghela Ndimbo, alidai kuwa mshtakiwa wa kwanza ni mgonjwa hajafikishwa mahakamani hapo.
Hata hivyo, washtakiwa  Samuel na Judith walisomewa mashitaka yao kwamba kati ya Septemba 2007 na Julai 2008 huko Temeke, Dar es Salaam, walitumia madaraka yao vibaya  kwa kufanya manunuzi  ya gari chakavu    kinyume cha kanuni, taratibu na sheria  ya manunuzi ya umma namba 58(3)  kitu ambacho kiiwezesha kampuni ya  Al Hamad Motors TZD kupata faida ya Sh. 34,895,400.
Katika shtaka la pili, Ndimbo alidai kuwa katika kipindi  cha Septemba 2007 na Julai 2008, Samuel na Judith wakiwa watumishi wa Tantrade kwa kudhamiria walitumia madaraka yao vibaya kwa kununua gari chakavu lenye namba za usajili SU 37332  kitu ambacho kiliiwezesha kampuni ya Humera Stars Used Cars FZCO kupata faida ya Sh. 32,773,475.
Katika shtaka la tatu  wanadaiwa kutumia madaraka yao  vibaya kinyume cha kifungu cha 31 cha sheria ya Takukuru namba 11 ya mwaka 2007 katika kutekeleza majukumu yao.
Alidai kuwa washtakiwa hapo  pasipo kufuata utaratibu za ushindani wa zabuni walinunua gari chakavu lenye namba za usajili  37332 na kuiwezesha kampuni ya AL Hamad Motors FZD kupata faida ya Sh. 34,895,400.
Katika shtaka la nne, ilidaiwa katika kipindi hicho hicho washtakiwa hao pasipo kufuata taratibu za ushindani wa zabuni walinunua gari  chakavu lenye namba SU 37332 na kuiwezesha kampuni ya Humera Stars Used Cars FZCO kupata faidia ya Sh. 32,773,475.
Katika shtaka la tano, ilidaiwa kuwa Septemba 2007 na Julai 2008 waliisababishia hasara mamlaka hiyo ya Sh. 49,145,855.5.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, washtakiwa walikana.
HABARILEO
Siku moja baada ya kufunguliwa kwa pazia la mbio za ubunge kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa baadaye mwaka huu, mchakato huo umeonekana kuvutia wengi, wakiwemo watumishi wa umma wenye nyadhifa za juu serikalini.
Katika orodha ya makada wa CCM waliochukua fomu za kuwania ubunge katika majimbo mbalimbali nchini, ukiachilia mbali mawaziri ambao kimsingi ni wanasiasa ni pamoja na vigogo serikalini kutoka ofisi nyeti kama Ikulu, makatibu tawala wa mikoa, wakuu wa mikoa na wilaya.
Katika jimbo la Morogoro Kusini, Katibu wa Rais Jakaya Kikwete, Prosper Mbena amejitosa kuwania ubunge kuchuana na Innocent Kalogeries, mbunge anayemaliza muda wake, lakini akiwa amechukua fomu ya kuomba ridhaa ya kuendelea kuliongoza jimbo hilo.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro naye amejitosa kwa mara nyingine kusaka ubunge katika Jimbo la Kalenga, mkoani Iringa.
Aidha, Katibu Mkuu wa zamani wa Wizara ya Uchukuzi ambaye kwa sasa ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Omar Chambo, naye amejitosa kwenye ubunge katika Jimbo la Handeni Vijijini.
Mbio za ubunge zimewavutia pia wakuu wa wilaya mbalimbali nchini. Kufikia jana, Mkuu wa Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma, Toima Kiroye alichukua fomu kuwania ubunge wa Jimbo la Simanjiro ambalo kwa sasa linaongozwa na Christopher Ole Sendeka.
Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe, Frederick Mwakalebela pia anatarajia kuchukua fomu kesho kuwania ubunge Jimbo la Iringa Mjini, kama ilivyo kwa Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma, Anthony Mavunde anayeingiza kete yake katika Jimbo la Dodoma Mjini.
Mwingine ni Festo Kiswaga, Mkuu wa Wilaya ya Misenyi mkoani Kagera naye amejitosa kuchukua fomu katika Jimbo la Isimani, Iringa ambalo tangu kuanzishwa kwake mwaka 1995 limekuwa likiongozwa na Waziri wa sasa wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi.
Mkuu mwingine wa wilaya anayeusaka ubunge ni Venance Mwamoto wa Kaliua mkoani Tabora ambaye anarudi Kilolo baada ya kukaa nje ya ulingo huo wa siasa kwa tabrikani miaka kumi.
Atachuana na makada kadhaa, akiwemo mbunge wa sasa na waziri wa zamani, Profesa Peter Msolla. Mboni Mhita, Mkuu wa Wilaya ya Mufundi ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM nchini (UVCCM), ametangaza nia kuwania ubunge katika Jimbo la Handeni Vijijini.
Habari zilizotufikia wakati tunakwenda mitamboni zinasema aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, amejitosa kuwania ubunge katika Jimbo jipya la Butiama, mkoani Mara.
Muhongo aliyejaribu kuwania Urais kwa tiketi ya CCM akiwa miongoni mwa makada 42, hii itakuwa mara yake ya kwanza kujaribu siasa za majimbo, kwani alipata uwaziri baada ya kuteuliwa kuwa mbunge na Rais Jakaya Kikwete.
HABARILEO
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana imetoa hati ya kukamatwa kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Simon Group, Robert Kisena na mwenzake kwa kuwa hawajafika mahakamani kusomewa mashitaka yanayowakabili.
Hakimu Mkazi Thomas Simba alitoa hati hiyo baada ya kukubali ombi lililowasilishwa na upande wa Jamhuri wakati kesi hiyo ilipotajwa.
Akiwasilisha ombi hilo, Wakili wa Serikali, Vitalis Peter alidai kesi hiyo inawakabili washitakiwa watatu, lakini mshitakiwa Venance Matondo, ambaye ni Mhasibu wa kampuni ya Simon Group ndiye aliyefika mahakamani hapo.
Peter aliomba hati ya kukamatwa kwa Kisena ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Usafiri Dar es Salaam (UDA) na Ofisa Msimamizi na Mchunguzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo Tanzania (TIB), Adam Yusuph, kwa kuwa waliwapelekea hati za kuitwa mahakamani lakini hawajafika.
Aidha, Wakili wa Serikali Joseph Kiula alidai, Kisena alipelekewa hati ya wito akasaini, na walipokuwa wanampigia simu alikuwa anasema atakuja kesho, lakini hati ilimtaka afike mahakamani jana.
Yusuph alipelekewa hati na ilisainiwa na mke wake, lakini hakufika na simu yake haipatikani.
Awali, Kiula akimsomea mashitaka Matondo, alidai kuwa Oktoba 18, 2009, yeye na Kisena walighushi hati ya malipo kwa lengo la kuonesha kuwa Chama cha Ushirika Shinyanga 84 Ltd kilisambaza tani 1000 za mbegu za pamba zenye thamani ya Sh milioni 145, jambo ambalo si kweli.
Mshitakiwa alikana mashitaka na kuachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya kuwa na wadhamini wawili waliosaini hati ya Sh milioni 10 kila mmoja. Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 28 mwaka huu kwaajili ya kutajwa.
Pia alitoa hati ya kukamatwa kwa washitakiwa hao kwa kuwa upande wa Jamhuri, umethibitisha kuwa walipelekewa hati za wito, lakini hawajafika mahakamani.
MTANZANIA
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimelazimika kupangua ratiba ya awali ya uchukuaji fomu za ubunge na udiwani kwa wanachama wake, baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutangaza majimbo mapya 26 ya uchaguzi hivi karibuni.
Aidha, kimeruhusu wanachama wote wenye sifa kuchukua na kurejesha fomu za kuwania uteuzi wa ndani ya chama katika nafasi za udiwani na ubunge katika majimbo yote ya uchaguzi nchi nzima.
Kupitia Waraka wa Katibu Mkuu Namba 5 wa mwaka 2015 uliosainiwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa, wananchi wenye nia na sifa za kuchukua fomu za ubunge kwenye majimbo yote yakiwemo mapya wanaruhusiwa kufanya hivyo hadi keshokutwa Jumapili.
Kwa mujibu wa Dk Slaa, kwa nafasi za udiwani, uchukuaji na urejeshaji wa fomu katika kata zote nchi nzima limeongezwa muda hadi Julai 29.
Alisema awali Chadema ilitoa ratiba yake ya uteuzi wa ndani ambapo ilionesha kuwa uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kuwania udiwani na ubunge katika kata na majimbo yenye madiwani au wabunge wa chama hicho ulitakiwa kusubiri hadi halmashauri zitakapokoma.
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimelazimika kupangua ratiba ya awali ya uchukuaji fomu za ubunge na udiwani kwa wanachama wake, baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutangaza majimbo mapya 26 ya uchaguzi hivi karibuni.
Aidha, kimeruhusu wanachama wote wenye sifa kuchukua na kurejesha fomu za kuwania uteuzi wa ndani ya chama katika nafasi za udiwani na ubunge katika majimbo yote ya uchaguzi nchi nzima.
Kupitia Waraka wa Katibu Mkuu Namba 5 wa mwaka 2015 uliosainiwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa, wananchi wenye nia na sifa za kuchukua fomu za ubunge kwenye majimbo yote yakiwemo mapya wanaruhusiwa kufanya hivyo hadi keshokutwa Jumapili.
Kwa mujibu wa Dk Slaa, kwa nafasi za udiwani, uchukuaji na urejeshaji wa fomu katika kata zote nchi nzima limeongezwa muda hadi Julai 29.
Alisema awali Chadema ilitoa ratiba yake ya uteuzi wa ndani ambapo ilionesha kuwa uchukuaji na urejeshaji wa fomu za kuwania udiwani na ubunge katika kata na majimbo yenye madiwani au wabunge wa chama hicho ulitakiwa kusubiri hadi halmashauri zitakapokoma.
Kwa habari, matukio na michezo ni hapa hapa tangakumekuchablog

No comments:

Post a Comment