SIMULIZI
KISIWA CHA HARISHI (5)
ILIPOISHIA TOLEO LILILOPITA
“Sasa unamuitaje?”
“Alinipa chupa. Mnaiona ile
chupa iliyopo juu ya kabati? Chupa ile iko wazi. Kifiniko chake kipo pembeni.
Ameniambia nisiifunge. Anapotaka kuja ile chupa inajaa moshi halafu inavuma.
Ule moshi ukishajaa unatoka kwenye mdomo wa ile chupa na kuundaumbile la jinni
halafu anakuwa jinni kabisa.
“Sasa nikitaka kumuita
nachukua ile chupa naiweka naiweka karibu na mdomo wangu kisha nataja jina lake
mara tatu, hazitapita dakika mbili chupa itajaa moshi. Moshi ule utatoka kwenye
mdomo wa chupa na kugeuka Harishi”
“Sasa kama anakuja kila wiki
tutapata muda wa kuishi na pengine tunaweza kupata msaada kwani tutakwenda
kukaa fukweni kusubiri vyombo vinavyopita” nikamwambia Yasmin
“Jaribuni hahati yenu.
Nawaombe Mungu awasalimishe” Yasmin alituambia kwa ungonge.
Nikawambia wenzangu. “Jamani
maneno mmeyasikia. Hapa hapakaliki”
“Sasa tuondoke” Mtu mmoja
akauliza.
“Inabidi tuondoke tusalimishe
maisha yetu”
“Sasa tutakwenda wapi?”
Mwingine akauliza.
“Twende ufukweni tuangalie
vyombo vinavyopita, tunaweza kupata msaada”
“Sasa huyu msichana naye tumchukue?” Mtu mwingine naye akauliza.
SASA ENDELEA
“Itakuwa ni jambo zuri
tukimchukua kama mwenyewe atakubali” nikawambia wenzangu kish nikamtazama Yasmin.
“Bibie unaonaje kama tutakuchukua ili tukunusuru?” nikamuuliza yasmin.
“Kunichukua mimi hakutakuwa
nusura kwangu wala kwenu kwa sababu mpaka sasa hamna uhakika wa usalama wenu
hata kama mtakwenda ufukweni mwa bahari
kusuiri vyombo vinavyopita” Yasmin akatuambia.
“Kwanini unatuambia hivyo?”
nikamuuliza.
“Kwa sababu Harishi anaweza
kututoke hapa hapa na kutuua sote kwa hasira’
Sote tukagunana kutazamana.
Yasmin aliendelea kutuambia.
“kwanza akija hapa nyumbani
hata kama mtakuwa mmeshaondoka atasema
anasikia harufu ya binaadamu na atataka kujua ni nani aliyeingia humu na
itakuwa ni balaa kubwa”
“Sasa unatushauri nini?” nikamuuliza Yasmin katika hali ya kukata
tama.
“Nawashauri muondoke ndani ya
jumba hili. Mwende popote mtakapoona mtaweza kujiokoa. Mimi niacheni hapa hapa”
“Sawa. Basi sisi tunondoka”
Yule msichana kwa kuonesha
wema na ukarimu alituambia tumpishe mle chumbani avae nguo. Tukatoka ukumbini.
Yasmin alipovaa alitoka akaenda jikoni. Akachukua vyakula na kututilia ndani ya
mfuko.
“Sasa nendeni, msikae karibu
kabisa” akatuambia.
Tukamuaga na kutoka. Tukaanza
kutembea haraka haraka kwa kufuata ile njia tuliokwendea.
Kisiwa kilikuwa kimya na
kilichokuwa kinatisha. Kelele zilizosikika zilikuwa ni za kunguru waliokuwa
wakilialia na kurukaruka kwenye miti kama
waliokuwa wakiambizana “Hao! Hao! Hao!”
Tulikuwa tukiangalia huku na
huku kwa hofu ya kutokewa na Harishi. Kuwa na silaha katika mazingira yale
ilikuwa muhimu. Mimi nilikuwa na sime
niliyokuwa nimeichomeka kiunoni. Wenzangu wawili walikuwa na mapanga. Wenzetu
wengine walikuwa mikono mitupu.
Kwa sababu ya hofu
iliyosababishwa na kelele za wale kunguru nilitoa sime yangu na kuishika
mkononi. Sasa nikawa tayari kukabiliana na chochote kitakachotokea.
Mpaka tunatokea kule ufukweni
mwa bahari tulizungukazunguka sana
kwani tulikuwa tunapotea njia mara kwa mara. Kulikuwa na mti mkubwa ulioota
kando ya bahari. Tukakaa chini ya ule mti.
Tulitoa vyakula tulivyopewa
na Yasmin na kuanza kula. Vilikuwa vhyakula vizuri vikiwa mchanganyiko wa
mikate ya mayai, keki, sambusa na biriani.
Wakati tunakula mawazo yangu
yalikuwa kwa yule msichana. Kwa kweli nilimuhurumia sana kwa kuishi maisha ya peke yake katika
kisiwa kile cha kutisha. Laiti ningekuwa na uwezo wa kumuokoa ningemuokoa
lakini ndio hivyo hatukuwa na uwezo na bado sisi wenyewe pia hatukuwa na
uhakika wa maisha yetu.
Hata hivyo nilimsifu kwa kuwa
na moyo wa kijasiri na wa kiume kwani asingeweza kuishi na kuendelea kuwa hai
hadi leo wakati yuko kwenye jinamizi la mauti. Kuishi na jini anayeua watu peke
yake lilikuwa ni jinamizi la mauti mbali ya kule kuishi peke yake katika kisiwa
kile kinachotisha!.
Nikajiambia kama chombo chetu
kingekuwa kizima tungeondoka naye hata kama
angekataa.
Baada ya kula kile chakula
tulipata akili tukaanza kujadiliana.
“Sasa tufanye nini jamani?”
Mwenzetu mmoja akauliza.
“Tuijaribu tena ile boti,
inaweza kukubali” nikatoa wazo ambalo lilikubaliwa na wenzangu.
Tukaenda kwenye chombo chetu
tukajaribu kukiwasha lakini chombo hakikuwaka. Kila mmoja wetu alijaribu
kukiwasha kwa mkono wake. Hakukuwa na yeyote aliyefanikiwa.
Tukaamua kujitia ufundi
kuanza kuichokoresha mashine ya boti. Kila mmoja alitia ufundi wake lakini pia
hatukufanikiwa. Mimi nilijitupa chini kwenye mchanga nikawaacha wenzangu
wakiendelea kushindana nayo.
Yalipita karibu masaa mawili.
Hatimaye niliona wenzangu mmoja mmoja akiondoka kwenye boti na kutafuta mahali
pa kukaa. Wote walikuwa wamekata tama kama
nilivyokata mimi.
Mawazo yangu yakarudi kwa
Harishi. Kama alivyotwambia Yasmin Harishi anaweza kutokea na kutumaliza kama alivyowamaliza watu wa kisiwa hicho.
Kwa muda sote tulikuwa kimya.
Kila mmoja alikuwa akiwaza lake. Tulipokitokea kisiwa kile tuliona tuliona
tumeokoka tukafurahi. Kumbe tumeepuka kufa maji, tumekwenda kwa muuaji mwingine
anayefyonza damu.
Tuliendelea kukaa pale
tukiangalia baharini hadi jua likaanza kuchwa. Hatukuona chombo chochote
kilichopita karibu. Tulichokiona ni mawingu yaliyoonekana kama
yanazama upeoni mwa macho yetu.
Wakati giza linaingia hatukujua tungejisitiri mahali
gani usiku huo kwani kwa vyovyote vile tusingeweza kuupitisha usiku mahali hapo
kutokana na baridi. Pia usalama wetu ulikuwa mdogo. Lolote lingeweza kutokea
wakati wa usiku. Kuna vitu kama majoka na
wanyama wakali ambao hujificha wakati wa mchana na kujitokeza wakati wa usiku.
Baada ya kuufikiria usalama
wetu tulishauriana turudi tena katika lile jumba la yule msichana. Kuna
waliopinga wakataka tupande juu ya mti ule tuupitishe usiku.
Lakini upepo mkali ulioanza
kuvuma pamoja na ngurumo za radi ndio uliofanya tukubaliane kwa pamoja kurudi
katika lile jumba kwani tulijua muda si mrefu mvua kali ingenyesha na kututosa.
ITAENDELEA KESHO.
Usipitwe na hadithi hii ya kusisimua hapo kesho na Kumekucha blog
![]() |
No comments:
Post a Comment