Tuesday, August 18, 2015

DC AOMBA AMANI WAKATI WA UCHAGUZI

Tangakumekuchablog

Korogwe, MKUU wa Wilaya ya Korogwe Mkoani Tanga, Hafsa Mtassiwa, ameitaka jamii kuitunza amani na mshikamano uliopo hasa kipindi hiki cha kuelekea  uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi October.

Akizungumza na Umoja wa Waandishi wa habari Wanawake Mkoa wa Tanga (TWMO) Wilayani hapa , Mtassiwa alisema kuelekea uchaguzi mkuu ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha amani na utulivu unaimarishwa.

Alisema utofauti wa vyama isiwe chanzo cha  kuharibika kwa amani na utulivu uliopo na hivyo kuwataka kushirikiana kwa kila jambo bila ushabiki wa kisiasa na kuwataka kushiriki kikamilifu katika zoezi la upigaji kura na kuwachagua viongozi bora.

“Leo nimefarijika sana kuzungumza na watu muhimu ambao ndio watoaji wa taarifa na kusambaza kila kinachotokea kwa wakati na muda huo huo-----kupitia kwenu niwaombe kuwatangazia wananchi kuilinda amani iliyopo” alisema Hafsa na kuongeza

“Sote tunatambua kuwa tunaelekea uchaguzi mkuu ambao kimsingi ni kuwachagua viongozi watakaoshika gurudumu la maendeleo kwa miaka mitano zaidi-----hivyo tukumbuke amani na utulivu uliopo ” alisema

Alisema utamaduni wa Watanzania umejengeka katika misingi ya kuvumiliana jambo ambalo limekuwa likizidi kuiletea sifa Taifa na nche nyengine kuiga hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuwa mlinzi wa amani kwa mwenzake.

Awali akizungumza katika kongamano hilo, Mwenyekiti wa Chama Cha Waandishi Wanawake Mkoa wa Tanga, Betha Mwambela, alisema mbali ya changamoto ambazo chama inakumbana nazo lakini wameweza kuwasukuma wanawake katika kazi za maendeleo.

Alisema Chama hicho kimeweza kuwavuta wanawake wengine katika kazi za ujasiriamali zikiwemo za mikono na kuunda Saccos ambazo zimekuwa mkombozi kwa mwanamke.

“Chama chetu kimekuwa katika changamoto mbalimbali ila jambo ambalo tunafarijika ni kuwa tunahamasishana kujitokeza katika kila palipo na fursa ya mwanamke kufanya au kugombea katika nafasi za kuongoza” alisema Mwambela  na kuongeza

“Sisi kama waandishi wanawake tumepiga hatua kubwa za kushika nafasi za kuongoza katika chama cha waandishi wa habari ambapo hapo awali tulikuwahakuna hata mwanamke mmoja” alisema

Ameitaka jamii kukiangalia chama hicho kwa kukipa misaada na mafunzo mbalimbali yahusuyio mwanamke  ili kuweza kufikia malengo kusimama na kutetea haki za wanawake mwenzao .

                                                            Mwisho

No comments:

Post a Comment