Tuesday, August 18, 2015

HADITHI SEHEMU YA (12)

HADITHI hii inaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya Mkombozi Sanitarium Clinic. Mkombozi ni mabingwa wa magonjwa sugu na yaliyoshindikana. Mkombozi wako na mashine za kisasa za kugundua magonjwa na kutoa tiba ya uhakika. Mkombozi wapo Tanga eneo la Chuda mkabala na Raha Leo, simu 0654 361333
 
NILIJUA NIMEUA
 
ILIPOISHIA
 
Nilipomtazama vizuri nikamgundua. Alikuwa ni Rita, dada yake marehemu mke wangu. Udugu wao ulikuwa ni wa shangazi kwa mjomba.
 
Nilipooana na Halima yeye ndiye aliyekuwa mstari wa mbele kusimamia harusi yetu.
 
“Oh kumbe ni wewe shemeji!” nikamwambia na kumuuliza “Umekuja saa ngapi?”
 
“Nimekuja sasa hivi, nikakuta mlango upo wazi. Naingia ndani sikuti mtu”
 
“Ah nilikuwa nimetoka mara moja, nilisahau kufunga mlango”
 
“Huogopi waizi?”
 
“Nilisahau tu, si unajua mambo ni mengi kichwani”
 
“Eh shauri yenu, mtakuja lia kilio cha m’bwa!. Yuko wapi mwenzako?”
 
SASA ENDELEA
 
Jibu nilikuwa ninalo.
 
“Amekwenda Pongwe” nilimjibu haraka.
 
“Amekwenda saa ngapi? Si amenipigia simu nikitoka Habours Club nije hapa”
 
Rita akanikwamisha.
 
“Amekupigia simu saa ngapi?”
 
“Kama saa moja hivi. Nikamwambia nitakwenda Habours Club, jahazi wanapiga leo. Akaniambia nikitoka huko nimfuate”
 
“Alikwambia anakuitia nini?”
 
“Sikumuuliza, nilimwambia tu nitakuja”
 
“Basi aliondoka muda huo huo kwenda Pongwe, labda alitaka akuage”
 
“Sasa kwanini hakuniambia kama anaondoka”
 
“Labda alisahau, si unamjua mdogo wako kwa wahaka!”
 
“Akili gani! Wewe unajua kuwa unasafari halafu unaniambia nije kwako? Ameniudhi kweli”
 
“Basi msamehe mdogo wako”
 
“Tena ngoja nimpigie nimwambie nimeshakuja hapa”
 
“Saa hizi atakuwa amelala, anaweza kuzima simu. Mpigie kesho”
 
Nilimwambia hivyo Rita kwa sababu simu ya Halima ilikuwa pale pale kwenye kochi alipokuwa ameketi. Kama ataipiga ingeita palepale na Rita angeniona mimi ni muongo.
 
Rita hata hakunisikiliza. Alitoa simu yake kwenye mkoba akapiga na kuiweka simu sikioni.
 
“Kama kazima simu nitampigia kesho” akajisemea huku akiisikiliza.
 
Nikawa nimemtumbulia macho nikimuangalia.
 
“Inaita!” akasema.
 
Ghafla simu ya Halima iliyokuwa kwenye kochi ikaanza kuita.
 
Halima akageuza macho na kuitazma
 
“Siumu yake si ile pale?”
 
Nikajifanya nashituka.
 
“Ah! Ameisahau…”
 
“Yaani amekwenda bila simu?”
 
“Yule msichana ana wahaka sana, ameisahau. Na mimi ndio naiona sasa hivi”
 
Rita akakata simu na kuirudisha mkobani.
 
“Basi naenda zangu, nipeleke”
 
“Sawa. Nitakupeleka” nilimkubalia haraka ili aondoke.
 
Ghafla akaliona shati langu.
 
“Mbona shati lako lina damu hivi?” akaniuliza kwa mshangao.
 
Nikagutuka na kulitazama shati langu. Kweli lilikuwa limeingia matone makubwa ya damu ya mke wangu. Sikuwa nimeyaona tangu mwanzo kwa sababu ya wahaka wa kuiondoa ile maiti.
 
Jinsi nilivyogutuka moyo ukawa unanienda mbio.
 
“Hiyo damu inatoka wapi?” Rita akaniuliza tena, sasa akiwa amekunja uso.
 
“Nilichinja kuku usiku huu akanitia damu. Nilisahau kubadili shati” nikasema uongo.
 
“Ulimchinja wapi kuku huyo?”
 
“Huko uani”
 
“Pia nimekuta damu nyingi huko uani, nikashangaa”
 
Moyo wangu ukalipuka.
 
“Ni damu ya kuku niliyemchinja. Nilimchinja hapo hapo”
 
“Ni damu  ya kuku ile? Mbona ni nyingi sana, imenishitua”
 
“Kuku mwenyewe alikuwa jogoo mkubwa. Ngoja nikupeleke nije nipige deki”
 
Kumbe ningechelewa kidogo tu ile maiti ingekutwa humu ndani, nikawaza huku nikielekea chumbani kubadili lile shati.
 
“Sasa unaenda wapi tena?” Rita akaniuliza.
 
“Nabadili hili shati mara moja”
 
“Mimi nakusubiri kwenye gari”
 
“Sawa nisubiri”
 
ITAENDELEA kesho na usikose nini kitatokea hapaha tangakumekuchablog

No comments:

Post a Comment