Saturday, August 29, 2015

SOMA HABARI KUBWA ZILIZOPEWA UZITO MAGAZETI YA LEO, AUG 29 TZ

Uchambuzi huu wa magazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu Cha Candle Education Centre Tanga, kituo kinaongoza kufaulisha wanafunzi kidato cha pili hadi cha sita na wanaojiendeleza kielimu. Kituo pia kinatoa kozi mbalimbali za kielimu na ufundi ukiwemo umeme na Compuetr. Kituo kipo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 772746
CLOUD
MWANANCHI
Mtu mmoja amefariki dunia na mwingine kujeruhiwa wakati watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi waliposimamisha daladala eneo la Jangwani na kuingia ndani kupora mkoba unaosadikiwa kuwa na fedha.
Watu hao, waliokuwa na pikipiki aina ya boxer, walikuwa wakifuatilia basi hilo linalofanya safari zake kati ya Kariakoo na Mwenge na kulisimamisha eneo la Jangwani saa 7.30 mchana na baadaye kuwaamuru abiria wote wainame kabla ya kuelekea kiti cha nyuma alikokuwa amekaa mtu huyo aliyekuwa amebeba mkoba.
Mmoja wa abiria wa daladala hilo, Rehema Michael alisema wakati basi lao likiwa linaenda taratibu, alimuona mtu aliyekuwa amepakizwa kwenye pikipiki akishuka na kumfuata dereva na kisha kumuelekezea bastola usoni, akimtaka asimamishe gari.
Alisema dereva wao alitaka kukunja kona kuelekea Jangwani, lakini akatii amri na ndipo dereva wa bodaboda alipokwenda nyuma ya daladala na kumtaka mmoja wa abiria aliyekuwa amekaa nyuma ya daladala kutoa begi, huku mwingine akipiga risasi hewani, lakini hakupewa mkoba huo.
“Baada ya kuona yule abiria anakaidi  agizo lao, mmoja wa majambazi hao alimpiga risasi ya kichwani na kifuani na kuanguka chini huku yule abiria mwenzake ambaye alipewa begi hilo alishike alilitupa chini na mmoja wa majambazi aliingia ndani ya daladala na kulichukua,Hashim Ally.
Shuhuda mwingine, Richard Urio alisema wakati uvamizi huo ukitokea abiria walikuwepo ndani ya daladala hiyo akiwemo konda walilazimika kulala chini baada ya kusikia milio ya risasi zilizokuwa zikipigwa hewani, na kwamba baada ya kuchukua lile begi walimpiga risasi abiria mwingine ambaye alikuwa karibu na marehemu baada kuhisi alikuwa akizuia begi lisitolewe.
“Siti ya nyuma walikuwa wamekaa abiria wanne, na wawili kati yao walikuwa wamasai ambao mmoja wapo alikuwa amevaa begi mgongoni ambalo lilichukuliwa na majambazi baada ya kumuua mmoja wa wamasai huku mwingine akijeruhiwa na bastola shavuni,”Urio.
Shuhuda mwingine, Regina Mateso alisema yeye alipanda daladala hiyo eneo la Shakilango  na kuwakuta wamasai hao ambao inasemakana walikuwa na fedha nyingi kutokana na maongezi yao.
“Wale wamasai walikuwa wanapigiana mahesabu na wapi kwa kwenda kubadilisha fedha. Yule aliyefariki alikuwa anamwambia mwenzake ukibadilisha hizi dola unapata Sh16 milioni, hivyo inawezekana wale abiria walikuwa na kiasi hicho cha fedha ambacho walikuwa wameweka katika begi la mgongoni,”  Mateso.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Polisi Ilala, Lucas Mkondya alisema tukio hilo limetokea na wanalifanyia  kazi .
“Na sisi polisi tumelipata sasa hivi ndio kwanza tunalifanyia kazi likikamilika tutatia taarifa,” Mkonya
MWANANCHI
Baba wa familia iliyoteketea kwa moto ndani ya nyumba walimokuwa wamelala, jijini Dar es Salaam, Masoud Mattar Masoud amesema kama angeona miili ya familia yake, naye angekufa.
Masoud alipoteza ndugu tisa baada ya nyumba yake kuteketea kwa moto, unaosadikiwa ulitokana na jiko la gesi.
Katika tukio hilo lililotokea eneo la Buguruni Malapa, usiku wa kuamkia juzi, jumla ya watu tisa walifariki dunia kwa kuungua moto ndani ya nyumba hiyo namba 40, baada ya juhudi za wananchi kuwaokoa kushindikana.
Walioteketea katika tukio hilo ni mama wa familia hiyo, Samira Juma Ibrahim (42) maarufu kwa jina la mama Aisha na watoto wake wanne; wavulana watatu na msichana mmoja. Watoto hao ni Ahmed Masoud (15), aliyekuwa mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari ya Msimbazi na Aisha Masoud (13), aliyekuwa mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Alfurqan.
Watoto wengine wa familia hiyo ni Abdillah Masoud (10), ambaye pia alikuwa mwanafunzi wa darasa la tatu katika Shule ya Msingi Alfurqan, pamoja na Ashraf Masoud (5).
Mbali na watoto wa familia hiyo, wengine waliofariki katika tuki hilo ni mama yake Samira, yaani bibi wa familia hiyo, Bimdogo Masoud (72); mtoto wa dada yake Samira, Wadhati Saleh (27) na mtoto wake Fahir Fesal (mwaka mmoja na nusu) pamoja Samira Haroun (17).
Wadhati ambaye alikuwa akiishi Magomeni, alikuwa mgeni katika nyumba hiyo na alifika nyumbani hapo asubuhi ya siku ya tukio hilo yeye na mtoto wake pamoja na Samira ambaye ni binti aliyekuwa akiishi naye.
Mashuhuda wa tukio hilo walisema baada ya kusikia kelele za vilio, waliizunguka nyumba hiyo kwa lengo la kutaka kuwaokoa, lakini ilishindikana baada ya milango kutofunguka na moto kuwa mkali kiasi cha kushindwa kuingia.
“Katika namna ya kujaribu kujiokoa, Ahmed alijaribu hata kurusha nje funguo ili waweze kufunguliwa mlango, lakini ilishindikana. Hivyo alirudi chumbani wakashikana pamoja kusubiri kifo,Suleiman Bashraf, ambaye ni kaka wa Samira.
Bashraf, anayeishi Mikocheni na ambaye anasema alifika eneo la tukio wakati dada yake na watoto wake wakiwa wameshafariki, alibainisha kuwa baba wa familia hiyo, alikuwa kazini wakati wa tukio hilo
Jana katika mahojiano na Mwananchi akiwa Kigogo CCM yaliko matanga kwa ndugu wa mkewe Masoud, ambaye ni baba wa familia hiyo iliyoteketea alisema, “Ninaushukru uongozi wa msikiti wa Gulam kunizuia kufika eneo la tukio na pengine hata mimi ningekufa palepale.”
“Siku ya tukio mimi sikuwapo nyumbani, nilikuwa kazini na kwamba nilipata taarifa za tukio hilo kutoka Pemba kwa mjomba,” anaeleza.
Masoud ambaye ni mfanyakazi wa kampuni ya Kimataifa ya Huduma za Kontena (TICTS) inayofanya kazi kwenye Bandari ya Dar es Salaam, anasema anapokuwa zamu ya usiku huwa anaondoka nyumbani saa 10 jioni na kupitia msikitini kufanya ibada na baada ya hapo anakwenda kazini.
Masoud, huku akibubujikwa machozi kwa huzuni na kujifuta mara kwa mara anasimulia: “Siku ya tukio hilo kulikuwa na ugeni nyumbani kwangu kwani kulikuwa na mtoto wa dada wa mke wangu aitwaye Wadhati Saleh, huwa ana kawaida ya kuja karibu kila wiki kumsalimia bibi yake. Wadhati alifika asubuhi ya siku hiyo akiwa na mtoto wake pamoja na binti mmoja aliyekuwa akiishi naye aitwaye Samira.
“Mtu pekee ambaye hakuwapo nyumbani wakati naondoka kwenda kazini alikuwa Ahmed ambaye alikuwa shuleni.
“Kwa kawaida wakati ninapoondoka nyumbani mara nyingi huwa nataniana na mke wangu. Yeye huwa ananitania kuwa mbona unaondoka mapema hivyo nami huwa namjibu kuwa napitia msikitini kwanza. Hata siku hiyo wakati naondoka mke wangu ambaye alikuwa amekaa nje na mtoto wa dada yake (Samira) alinitania kama kawaida yake ‘mbona mapema hivi’, nami kama kawaida nilimjibu kuwa ‘napitia msikitini’.
Basi mtoto wa Wadhati alinifuata, nikamchukua na nikamrudisha kwa mama yake halafu nikamuaga kuwa ningerudi kumchukua. Niliagana na familia yangu na nikaiacha ikiwa yenye furaha. Niliondoka hadi msikitini ambako nilifanya ibada kama kawaida na baada ya ibada nilikwenda kituoni ambako nilipanda daladala na kwenda kazini. Kule kazini nilizima simu na kuiweka kwenye chaji. Majira ya saa 10 alfajiri nilikwenda msikitini kwa ajili ya ibada ya alfajiri na kwamba baada ya kutoka msikitini, nilirudi kuchukua simu.
Nilipoiwasha tu nilisikia milio kuashiria kuwa kuna simu nilikuwa nimepigiwa lakini sikupatikana. Punde kidogo nilipigiwa simu na mjomba wangu Suleiman Salim, kutoka Pemba. Aliniuliza kuwa niko wapi maana napigiwa simu sipatikani, nami nikamjibu kuwa niko kazini na simu yangu niliizima nikaiweka kwenye chaji. Kisha aliniambia niende haraka nyumbani kuna moto.
Aliponiambia hivyo niliomba gari kazini likanipeleka nyumbani. Wakati tukiwa njiani nilipigiwa tena simu nyingine na mkwe wangu, Ali Saidi, mume wa mtoto wa dada. Alinitaka pia niende haraka nyumbani. Nilimuuliza kama kuna usalama lakini yeye akasisitiza tu kuwa niende haraka.
Nilihisi kuna tatizo kubwa na pale pale akili yangu ikaanza kuchanganyikiwa. Nilipofika katika msikiti wa Masjid Gulam, nikasimamishwa na maimamu na waumini wengine waliokuwapo pale msikitini, wakaniambia nisiende huko nyumbani.
Walifungua mlango wa gari wakanishusha na wakanichukua na kunipeleka hadi msikitini. Huko wakaniambia nipumzike humo kwanza huku wakinitaka niwe mstahimilivu. Imam Said na waumini wengine walinizunguka. Nikawaambia wanieleze nini kinaendelea kwa kuwa mimi ni mtu mzima, lakini waliendelea kunipa maneno ya kunifariji.
Ndipo wakaniambia kuwa hawakutoa hata mtu mmoja katika ajali hiyo. Nadhani wakati ule waliponizuia kwenda kule nyumbani kwangu ndio wakati Polisi walikuwa wakizipakia maiti kwenye gari kuzipeleka hospitalini. Hali yangu ilibadilika sana na pengine kama ningeziona maiti nami ningekufa palepale.
Nilikaa msikitini humo hadi asubuhi kwenye saa nne kasoro hivi nilipochukuliwa kupelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ambako miili ya marehemu ilikuwa imehifadhiwa kwa ajili ya taratibu za mazishi. Hata huko Muhimbili sikuruhusiwa kuiona miili ile na hata mimi sikutaka kuiona kwani nilikuwa nikiteseka sana kutokana na matatizo ya shinikizo la damu.
Mke wangu alikuwa ndiyo dira yangu. Alikuwa mdogo lakini kaniongoza na kanistahimili kwa mambo mengi. Mke wangu alikuwa kiongozi wangu mambo mengi yeye ndiye alikuwa akiyafanya.
Wakati mahojiano yakiendelea alifika Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) inayoendeshwa kwa mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), Seif Sharrif Hamad.
Maalim Seif aliwasili msibani hapo saa 5.46 asubuhi  na akatoa salamu za rambirambi akiwataka wafiwa kumtumaini Mungu na kuwaombea dua waliofariki. “Huyu (Masoud) siku yake ilikuwa haijafika ndiyo maana wakati haya yakitokea hakuwapo. Lakini hawa siku yao ilikuwa imefika. Hivyo tuwaombee dua kwa Mwenyezi Mungu.”
HABARILEO
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge, iliyochunguza sakata la upewaji zabuni ya mabilioni ya kufua umeme kwa kampuni ya Richmond, Dk Harrison Mwakyembe ameibua upya suala hilo.
Mwakyembe aliyasema hayo mbele ya maelfu waliojitokeza katika mkutano wa hadhara wa mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli katika viwanja vya Luandanzovwe jijini Mbeya, jana.
Akizungumzia madai ya kwa nini baadhi ya wahusika hawakupelekwa mahakamani kama kuna ushahidi, mhadhiri huyo wa sheria alisema kosa la jinai, halina ukomo na wakati wowote linaweza kufunguliwa mashitaka, huku akiapa kuwa anaweza kumfungulia mtu mashitaka hata kesho.
Alionya viongozi na makada wa Chadema na vyama vinavyowaunga mkono katika umoja wa Ukawa wanaozindua kampeni zao leo jijini Dar es Salaam, kwamba wasithubutu kujibu hoja zake.
Dk Mwakyembe alisema ikilazimika kusema ukweli, ataweka hadharani uchafu wote uliofanyika, ambao alisema bungeni kuwa asingeuanika na kuifanya Richmond hoja ya kila siku mpaka Watanzania waelewe kilichofanyika.
“Tunao ushahidi. Hawa walitakiwa kuwa jela badala ya kuimba nyimbo za ajabu,” alisema Dk Mwakyembe katika mkutano huo uliorushwa moja kwa moja nchi nzima na kuongeza kuwa Dk Magufuli akiingia madarakani, anakwenda kuanzisha Mahakama ya Ufisadi.
Alisema yeye na wenzake walipewa kazi ya Bunge kuchunguza ilikuwaje viongozi waandamizi wakaamua kuipa kampuni hewa zabuni ya mabilioni ya fedha, ambayo imesababisha mpaka leo kuna shida ya umeme nchini.
Dk Mwakyembe alikumbusha kuwa walikwenda mpaka Marekani kuchunguza uwepo wa kampuni hiyo iliyodaiwa kutoka katika nchi hiyo, na kukutana na kampuni ya kuchapisha kadi za harusi.
Kwa mujibu wa Dk Mwakyembe, baada ya kubaini ubadhirifu huo, aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, alishinikizwa kujiuzulu na kumaliza suala hilo na hivyo hatua ya kiongozi huyo kutaka kwenda Ikulu, wazalendo hawawezi kuikubali.
“Hatutaruhusu watumie demokrasia kuingia Ikulu na hiyo ndiyo shida ya kuazima wagombea,” alisema Dk Mwakyembe akimaanisha kuwa chama cha Chadema, kimeazima mgombea bila kumfahamu. Dk Mwakyembe alisema suala hilo lilishafungwa bungeni, lakini anashangaa kusikia linarejeshwa kinyemela.
Naye Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Mwigulu Nchemba, alisema mgombea wa Ukawa, Lowassa, tangu akiwa kijana alikuwa ‘mpiga-dili’.
Kwa mujibu wa Mwigulu, Rais Kikwete alipoingia madarakani, alidhani kuwa Lowassa alikuwa ameonewa, akamteua kuwa Waziri Mkuu, lakini kabla ya kumaliza miaka miwili, akaendeleza tabia yake ya ‘kupigadili’.
Mwigulu alionya kuwa, Watanzania wakimpeleka ‘mpiga-dili’ Ikulu, shida yake na wenzake si changamoto za watu wa Mbeya wapate maji, huduma bora za afya na nyingine bora za umma, bali kurejesha fedha walizotumia wakati wa kutafuta urais.

HABARILEO
Umoja wa Ulaya (EU) utatuma timu ya waangalizi yenye wajumbe 128 nchi nzima kwa ajili ya kushiriki katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 25, 2015.
Hayo yalibainishwa wakati wa uwekaji saini wa makubaliano ya awali ya kuruhusu timu hiyo kuja nchini kulikofanywa jana baina ya EU na Serikali ya Tanzania katika Ofisi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Uwekaji saini huo umefanywa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje, Balozi Liberata Mulamula kwa niaba ya serikali na Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania Filiberto Ceriani Sebregondi kwa niaba ya EU.
Akizungumza baada ya uwekaji saini wa makubaliano hayo, Balozi Sebregondi alisema kuwa EU imekuwa ikituma timu hiyo kwa nchi washirika ambazo zina historia nzuri ya demokrasia na kwamba nchi hizo zina dhamira ya dhati ya kukuza mahusiano na EU kwa kuruhusu waangalizi wafanye majukumu yao katika hatua zote za uchaguzi kwa madhumuni ya kuhakikisha kuwa uchaguzi unakuwa wa haki na huru.
HABARILEO
Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk John Magufuli, amesema nchi inapopata neema, wabaya nao huingia.
Akizungumza na wananchi katika maeneo ya Makongorosi na Chunya katika mkoa mpya wa Songwe juzi, Dk Magufulia alifafanua kuwa Tanzania ina rasilimali nyingi kuanzia madini, hifadhi za taifa na gesi, ambazo zinatakiwa zitumiwe kwa manufaa ya wote.
Aliwaonya wananchi kuwa makini na wagombea wanaotoa fedha, akikumbushia mchakato wa kumpata mgombea ndani ya CCM, ulivyogubikwa na baadhi ya wagombea kumwaga fedha.
Alisema mgombea anayetoa fedha, maana yake anawanunua wapiga kura na kuonya kuwa kama akipata madaraka kwa kununua watu, iko siku atawauza.
“Mimi nilijitokeza kimyakimya, nikatafuta wadhamini kimyakimya na kurejesha fomu kimyakimya… Sikutaka kutoa fedha kwa kuwa ni dhambi kwa Mungu,” alisema Dk Magufuli.
Akifafanua kauli ya wabaya kuivizia neema ya nchi, Dk Magufuli aliwataka Watanzania kutazama mfano wa nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Kwa mujibu wa Dk Magufuli, nchi hiyo jirani ina kila aina ya rasilimali zenye thamani kubwa duniani, lakini mpaka sasa ina mtandao wa barabara za lami wenye urefu wa kilometa 1,500 tu.
Hali hiyo ya DRC ni tofauti na Tanzania ambapo Dk Magufuli alisema kwa sasa imefanikiwa kujenga karibu kilometa 20,000 za barabara. Pamoja na mafanikio hayo, Dk Magufuli alisema bado Watanzania wamekuwa wakikosa huduma muhimu wakati Serikali ina fedha za kutosha.
Alisema Watanzania wamefikia mahali pa kuichukia Serikali yao, huku wakisema ni ya mafisadi na kuwasihi wananchi wasitoe hukumu ya jumla, kwa kuwa wabadhirifu ni wachache.
Dk Magufuli alisema Watanzania sasa wanahitaji mabadiliko yenye tija, kama yaliyotokea nchini China ambayo sasa ni nchi ya dunia ya kwanza na si mabadiliko yasiyo na tija kama yaliyotokea nchini Libya.
Akifafanua kauli hiyo, Dk Magufuli alisema China inayoongozwa na chama cha kikomunisti, baada ya kupata uzoefu, ilifanya mabadiliko kwa kutumia chama hicho hicho na leo hata Marekani inaishangaa.
Lakini Libya kwa mujibu wa Dk Magufuli, ilikuwa na Rais Muammar Gadafi ambaye alitumia vizuri rasilimali za nchi hiyo hasa mafuta, kunufaisha jamii kiasi cha kufikia hatua ya kuwapa fedha na nyumba vijana waliokuwa wakioa.
Alisema Walibya walipata raha wakati wa Gadafi, lakini wakalewa neema na amani, wakamuua na baada ya hapo wamejikuta wakivurugana, huku wengine wakikimbia nchi yao na wengine wakitamani Gadafi arudi lakini ndio hawawezi kumrudisha.
Naye Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Mbeya na Rungwe, Godfrey Zambi, alisema chama hicho kimempata Magufuli kuwa mgombea wa urais ambaye ni mwadilifu kiasi kwamba hata wapinzani hawawezi kumyooshea vidole.

Naye Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM na Mjumbe wa Kamati Kuu (CC) ya chama hicho, William Lukuvi, alisema ndani ya Serikali kuna magugu mengi na Dk Magufuli, ndiye tingatinga la kung’oa magugu hayo.
Lukuvi alisema Dk Magufuli amekuja kusafisha maovu yote serikalini na katika jamii ya Watanzania, kwa kuwa kuna kero nyingi, ambazo kwa uchapakazi wake atazitatua.
Kwa mujibu wa Lukuvi, ndani ya CCM walijiangalia na kujipima kutafuta mtu anayeweza kurejesha imani ya watu katika Serikali, kusimamia nidhamu ya matumizi ya Serikali na kutenda haki, wakamuona Dk Magufuli.

JAMBOLEO
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imepewa msaada wa vitu mbalimbali zikiwemo dawa zenye thamani ya Sh milioni 42.2 pamoja na fedha taslimu milioni 160 kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) ili kusaidia mapambano dhidi ya ugonjwa wa kipindupindu.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Dk Donan Mmbando alisema shirika hilo limetoa katoni 1,000 za dawa ya kutibu maji (Water guard) na lita 100 za dawa za kudhibiti mazingira (Cresol Saponated Liquid).
Mbali na kuishukuru WHO kwa msaada huo, alisema watahakikisha vitu hivyo vinawafikia walengwa na kuhakikisha vinatumika ipasavyo ili kusaidia kudhibiti ugonjwa huo.
Alisema Watanzania wanapaswa kuelewa kwamba bado ugonjwa huo unaendelea kuwakumba wananchi na ni hatari hivyo wanapaswa kuhakikisha wanajiepusha na mambo yanayoweza kusababisha wakaupata.
“Nimesikitika sana ugonjwa haujadhibitiwa Mkoa wa Pwani sasa una wagonjwa; Kibaha kuna wagonjwa sita na kifo kimoja, Mkuranga mgonjwa mmoja. Ni jambo la kusikitisha sana,”Mmbando.
Kwa habari , matukio na michezo ni hapahapa tangakumekuchablog

No comments:

Post a Comment