Hadithi hii inaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Tiba cha Mkombozi Sanitarium Clinic, Mkombozi ni mabingwa wa magonjwa sugu na yaliyoshindikana. Mkombozi wako na mashine za kisasa zenye uwezo wa kugundua magonjwa yaliyojificha. Wapo Chuda Tanga mkabala na Raha Leo, simu 0654 361333
NILIJUA NIMEUA(14)
ILIPOISHIA
Nilikumbuka kuna siku moja
ambayo nilikwenda kwa mganga mmoja wa kienyeji akaniambia kama
nataka kupata pesa kwa wingi nikubali kuzini na maiti. Aliponiambia hivyo
niling’aka kisha niliondoka bila kumuaga.
Katika kipindi kile pia
kulikuwa na taarifa nyingi kwenye duru za habari juu ya watu wanaokamatwa na viungo vya maiti.
Kwa hiyo dhana ya ushirikina
imetawala katika hisia za watu hivyo vitendo vya kuzini na maiti au kuwakata
viungo maiti vilikuwa ya kawaida.
Nilijiambia kama maiti ya mke
wangu hakupelekwa kuziniwa, imekwenda kukatwa viungo ili vitumike katika mambo
ya kishirikina.
Nilimuhurumia sana Halima. Matukio
mawili mabaya yamemkuta katika usiku mmoja. Kwanza
nimemtoa roho yake kikatili kwa panga na pili mwili wake umechukuliwa kwenda
kuziniwa au kukatwa viungo.
Viumbe hawa katili sana! Nilijiambia na kutikisa
kichwa.
Sikuwa na jingine la kufanya
zaidi ya kuondoka mahali hapo huku nikiendelea kusikitika kwa huzuni na
majonzi.
SASA ENDELEA
Nilijipakia kwenye gari na
kuondoka. Wakati naendesha ghafla nikamkumbuka yule msichana niliyemkuta jana
usiku pale makaburini. Nilipata wasiwasi sana
kwamba huenda akahusika na kuchukuliwa kwa maiti ya mke wangu.
Nikajiambia huenda jana
nilipomuona alikuwa akinichunguza mimi. Alikuwa akingoja nimfukie marehemu ili
awambie wenzake waje wamfukue.
Vile alivyoniambia kuwa
alitumwa na mganga azike vitu ulikuwa ni uongo mtupu!
Bila shaka nilipomfikisha
nyumbani aliwambia wenzake, ndio wakarudi tena kule makaburini na kuufukua
mwili wa marehemu.
Baada ya kuwaza hivyo
niliamua kumfuata ili nimuulize. Nyumba niliyomteremsha usiku uliopita nilikuwa
naikumbuka vizuri. Nilipofika kwenye ule mtaa nilizitupia macho nyumba
zilizokuwa mwanzo mwanzo. Nikaiona ile nyumba. Kulikuwa na msichana aliyekuwa
anatoka nikamdhani alikuwa ni yeye. Hapo hapo nikasimamisha gari.
Nilifungua mlango wa gari na
kushuka. Nilipomuangalia vizuri yule msichana nikaona hakuwa yule
niliyemdhania. Na yeye alipoona teksi akasimama ingawa alionesha alikuwa
anatoka.
“Habari ya saa hizi?”
nikamsalimia.
“Nzuri” akanijibu huku
akinitazama kwa udadisi. Bila shaka alinigundua kuwa nilikuwa nataka kumuuliza
mtu.
“Samahani. Unaishi humu
ndani?”
“Ndiyo naishi humu”
“Kuna msichana mmoja
namuulizia”
“Anaitwa nani?”
Tatizo lilikuwa jina lake.
Jina lake nilikuwa silijui. Nilipokuwa naye jana
sikuwahi kumuuliza anaitwa nani. Lakini sikujilaumu kwa kutomuuliza jina lake kwani
sikuwa na sababu ya kumuuliza jina na hata yeye hakuniuliza jina langu.
Kwanza sikufikiria kabisa kwamba nitahitaji kukutana naye
tena. Nilichojua ni kwamba ile jana ungekuwa ndio mwisho wetu wa kukutana,
labda tuje tukutane kwa bahati mbaya.
“Anaitwa nani?” Msichana huyo
akaniuliza tena alipoona nimeduwaa.
“Kwa kweli jina lake silifahamu.
Lakini jana usiku nilimleta hapa kwa teksi”
“Sasa nitamjuaje kama hufahamu jina lake, kwani mlikutana wapi?”
Sikuweza kumwambia kama tulikutana makaburini, badala yake nikamuuliza.
“Kwani hakuna msichana
mwingine anayeishi humu ndani?”
“Tuko wasichana watatu lakini
siwezi kujua ni yupi”
“Huyo ni mrefu na mweusi. Kama nilimtazama vizuri ana mwanya wa juu”
“Ni Mwajuma!”
“Nafikiri atakuwa ni huyo
huyo. Ninamuhitaji”
“Mwajuma, muda huu huwezi
kumpata. Yuko kazini kwake. Mpaka jioni ndio anarudi”
“Anafanya kazi wapi?”
“Barabara ya tisa”
Nilitaka kujua kama Mwajuma alikuwa na mume ili nitengeze hoja kwamba mmoja
wa wale watu niliowaona jana usiku alikuwa ni mume wake. Nikamuuliza kwa hila.
“Naweza kumpata mume wake?’
“Hana mume” Msichana
akanijibu.
“Hapa ni kwao au
amepangisha?”
“Amepangisha chumba”
“Umesema anarudi jioni saa
ngapi?”
“Saa kumi na mbili jioni”
Niliona kusubiri hadi saa
kumi na mbili jioni ilikuwa mbali sana.
Nikaamua nimfuate huko huko kazini kwake.
“Anafanya kazi gain huko
barabara ya tisa?”
“Anauza duka la nguo”
“Tafadhali nielekeze hilo duka lilipo”
“Lipo barabara ya tisa kwa
barabara ya Jamaa. Upande wa kulia kuna jengo la ghorofa mbili limeandikwa KHADIJA MANSION. Lina maduka mengi lakini duka
la kwanza ndilo analouza yeye”
“Nimeshapaelewa. Acha
nimfuate, nina shida naye muhimu sana.
Asante”
Ungana nami hapo kesho hapa hapa tangakumekuchablog ujue nini kitajitokeza katika hadithi hii ya kusisimua .
No comments:
Post a Comment