Wednesday, August 26, 2015

SOMA HABARI KUBWA ZILIZOPEWA UZITO MAGAZETI YA LEO, AUG 26 TZ

Uchambuzi huu wa magazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha elimu cha Candle Education Centre Tanga, kituo kinaongoza kufaulisha wanafunzi kidato cha pili hadi cha sita na wanaojiendeleza kielimu. Kituo kinatoa kozi mbalimbali za kielimu na kiufundi ukiwemo Umeme na Computer. Wapo Tanga mkabala na bank ya CRDB simu 0715 772746

leoleo
MWANANCHI
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limemtahadharisha mgombea wa urais kwa tiketi ya Chadema Edward Lowassa kuwa kampeni alizoanza kwa kuyatembelea makundi kadhaa zinaweza kutumiwa na maadui wa kisiasa kumdhuru.
Hata hivyo, wanasiasa wametakiwa kufuata ratiba ya kampeni kwa kuzingatia mwongozo wa Tume ya Uchaguzi (NEC) ili kulisaidia jeshi hilo kukabiliana na vitendo viovu.
Onyo hilo limetolewa ikiwa ni siku ya pili tangu Lowassa na mgombea mwenza Juma Duni Haji walipoanza kuwatembelea wananchi huku wakitumia usafiri wa umma.
Kwa kutumia staili hiyo, leo Lowassa akiwa na Duni Haji wametembelea maeneo ya Tandika, Tandale na Kariakoo jijini Dar.
Akizungumza na wanahabari leo jijini Dar, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, Suleiman Kova amesema ziara iliyofanywa leo maeneo ya Swahili, Kariakoo zimesababisha mikusanyiko isiyo ya lazima na kusimamisha shughuli za maendeleo.
Baada ya CCM kuzindua kampeni zake mwishoni mwa juma lililopita viwanja vya Jangwani, jijini Dar es Salaam, Chadema nacho kinajiandaa kufanya hivyo Agosti 29 maeneo hayohayo.
HABARILEO
WATU nane wamethibitishwa kufariki kwa ugonjwa wa kipindupindu na wengine 262 wameambukizwa maradhi hayo katika mkoa wa Dar es Salaam na Morogoro. Waziri wa Afya na Usatwi wa Jamii, Dk Seif Rashid akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mwenendo wa maradhi ya ugonjwa huo uliozuka hivi karibuni alisema hadi kufikia jana, kwa mkoa wa Dar es Salaam, watu saba wamefariki na wengine wapatao 230 tayari wameambukizwa ugonjwa huo.
“Tangu ugonjwa huu uanze Agosti 15 mwaka huu, idadi ya wagonjwa walioripotiwa kwa mkoa wa Dar es Salaam ni 230 na vifo vya watu saba,” alisema Dk Rashid. Kwa mujibu wa Dk Rashid, maeneo yalioathirika zaidi na ugonjwa huu kwa mkoa wa Dar es salaam ni pamoja na maeneo ya Makumbusho, Kimara, Tandale, Manzese, Saranga na Magomeni.
Maeneo mengine ni Mwananyamala, Kibamba, Kigogo, Goba, Mburahati, Kinondoni na Kijitonyama kwa manispaa ya Kinondoni. Kwa upande wa manispaa ya Ilala, maeneo yaliyoathirika ni pamoja na Buguruni, Majohe, Chanika, Sharifu Shamba na Tabata, wakati katika manispaa ya Temeke, maeneo yalioathirika ni Mtoni kwa Azizi Ally, Keko na Yombo Vituka.
Katika mkoa wa Morogoro, Dk Rashid alisema ugonjwa huo ulianza mkoani hapo Agosti 17 mwaka huu na hadi kufikia Agosti 24, mtu mmoja amefariki dunia na wengine 32 wameambukizwa.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dk Rufaro Chatora amepongeza hatua zilizochukuliwa na serikali lakini amesema haina budi kuchukua hatua zaidi ili kudhibiti maambukizi yasiongezeke.
NIPASHE
Aliyekuwa Waziri na Mambo ya Ndani na Mbunge wa Jimbo la Nyamagana, jijini Mwanza, Lawrence Masha, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, akikabiliwa na shitaka la kutoa lugha ya matusi dhidi ya maofisa wa Jeshi la Polisi na kisha kupelekwa selo katika gereza la Segerea.

Masha ambaye ni wakili wa kujitegemea alikamatwa juzi na kulala selo katika Kituo cha Polisi Oysterbay, alifikishwa mahakamani hapo jana saa 4:20 asubuhi akiwa amevaa fulana la rangi nyeusi, suruali ya jinsi ya rangi ya bluu mpauko na sendozi za rangi nyeusi.

Alifikishwa mahakamani hapo na msafara wa magari saba ya jeshi hilo likiwamo la maji ya kuwasha akiwa pamoja na  washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi mbalimbali.

SHITAKA LINALOMKABILI
Saa 8:40 asubuhi alisomewa shitaka moja linalomkabili mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Warialwande Lema.

Akisoma hati ya mashitaka, Wakili wa Serikali Wankyo Simon alidai kuwa, Agosti 24, mwaka huu katika Kituo cha Polisi Oysterbay, mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, jijini Dar es Salaam, mshitakiwa huyo alitoa lugha ya matusi dhidi ya Inspekta Msaidizi wa Polisi Juma Mshana na wenzake kituoni hapo.

Alidai Masha aliwatolea lugha ya matusi maofisa hao wa polisi, akinukuu maneno hayo: ‘Polisi ni washenzi, waonevu hamna shukrani, huruma wala dini’ na kusababisha uvunjifu wa amani.

Mshitakiwa Masha alikana shitaka hilo. Upande wa Jamhuri ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na haukuwa na pingamizi la dhamana dhidi ya mshtakiwa.

AENDA SEGEREA
Baada ya kusikiliza mashitaka hayo, Hakimu Lema alisema mshtakiwa atakuwa nje kwa dhamana kwa kuwa na wadhamini wawili wanaotoka kwenye taasisi zinazotambulika ambao watatakiwa kusaini hati ya dhamana ya Sh. milioni moja kila mmoja.

Baada ya hakimu kuweka wazi dhamana kwa mshitakiwa, upande wa Jamhuri uliomba muda wa kuhakiki nyaraka za wadhamini wawili waliojitokeza kumdhamini, ombi ambalo lilikubaliwa na hakimu na kuahirisha kesi hiyo hadi Septemba 7, mwaka huu.

Hata hivyo, ilipofika saa  9:40 alasiri Masha aliondolewa mahakamani hapo chini ya ulinzi makali wa polisi na kupelekwa katika mahabusu ya Gereza la Segerea kutokana na muda wa mahakama kufanyakazi kumalizika huku taratibu za dhamana zikiwa hazijakamilika.

ALIVYOKAMATWA
Masha alikamatwa juzi kwa kile kilichoelezwa na Jeshi la Polisi kuwa alifanyia vurugu pamoja na kuwaporomoshea matusi ya nguoni askari waliokuwa zamu katika Pituo cha Polisi cha Oysterbay.

Akizungumza na Nipashe jana jijini Dar es Salaam, Kamanda  wa Polisi  Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura,  alisema majira ya saa 10 jioni eneo la Moroko kulikuwa na kundi kubwa la vijana kati ya 70 hadi 100 ambao walikusanyika.

Alisema kundi hilo lilianza na watu 10, 20,30 na baadaye kufikia idadi hiyo hali ambayo iliwashtua kuwa kulikuwa na jambo lisilo la kawaida katika mkusanyiko usiokuwa halali na ndipo askari walipoamua kuwakamata.
Kamanda Wambura alisema katika kundi hilo walifanikiwa kuwakamata vijana 19 na wengine walikimbia lakini walikuwa wamevalia tisheti nyeupe zenye maandishi ya “Team mabadiliko yasipoyapata ndani ya CCM watayapata nje ya CCM.”

Alisema ilipofika saa 1:45 usiku, Masha alifika kituoni hapo akihitaji kuonana na vijana hao na kujulishwa wanahojiwa.

Alidai baada ya kujulishwa kuwa wanahojiwa hakuwa mstaarabu alianza kutoa maneno ya kashfa, lugha chafu, kutoa matusi ya nguoni pamoja na kupiga meza ya kaunta kwa kutumia mikomo yake.

Kamanda Wambura alisema walimhoji usiku huo na kumuandalia jalada lake pamoja na la vijana 19 na kupelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ili kuandaliwa mashtaka.

WENGINE 19 KIZIMBANI
Wakati huohuo, watu 19 wakiwamo wanafunzi wamefikishwa mahakamani hapo wakikabiliwa na mashitaka mawili ya kula njama na kufanya mkusanyiko kwa lengo la kuandamana isivyo halali.
Washtakiwa hao walisomewa mashitaka yao jana mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi, Mwandamizi, Emmilius Mchauru.

Wakili wa Serikali, Paul Kadushi, aliwataja washtakiwa hao kuwa ni, Rwegasira  Alex (23), Yusuph  Adamu (22), Sia Kimambo (21), Mariam Michael (20), Michael Litanda (25) ,Vivian  Nchimbi (25), Scolastica Masanja (29), Jackline Michael (25), Pradius Kaiza (29), Edwin Kaiza (25) na Godfrey Mhando(25).

Wengine ni,  Dickson Congress (25), Mary  Malick (28), Abdallah  Hamisi (20), Fortune Francis (28), Jumanne Mvuma (22),  Baraka  Athuman (22), Francis Mbwilo (22) na  Said  Katora (30).

Katika hati ya mashitaka ilidaiwa kuwa, washitakiwa wote kwa pamoja Agosti 24,  mwaka huu, eneo la Morocco, jijini Dar es Salaam, walikula njama ya kufanya kosa la jinai.

Kadushi alidai katika shitaka la pili, tarehe hiyohiyo katika barabara ya Ali Hassan Mwinyi, Kinondoni, jijini Dar es Salaam, washtakiwa walifanya mkusanyiko kwa lengo la kufanya maandamano isivyo halali.

Washtakiwa wote kwa nyakati tofauti walikana mashitaka hayo.

Hakimu Mchauru alisema washtakiwa watakuwa nje kwa dhamana kwa kuwa na wadhamini wawili kila mmoja wanaotoka kwenye taasisi zinazotambulika na watatakiwa kusaini hati ya dhamana ya Sh. 800,000 kila mmoja na hawata hawataruhusiwi kutoka nje ya mkoa wa Dar es Salaam bila kibali cha mahakama.

Hata hivyo, washitakiwa hao walishindwa kutimiza masharti hayo na walipelekwa mahabusu hadi Septemba 7, mwaka huu kesi yao itakapotajwa tena.
NIPASHE
Serikali imesema zaidi ya Sh. bilioni 230 zimepotea katika kipindi cha mwaka uliopita kutokana na ajali za barabarani nchi nzima.

Akizungumza katika ufunguzi wa semina ya madereva wa magari makubwa, mabasi ya masafa marefu na daladala jijini Mwanza juzi, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Baraka Konisaga (pichani), alisema kiasi cha Sh. bilioni 230 zilipotea katika ajali zilizotokea kipindi hicho licha ya baadhi ya ajali hizo zingeweza kuepukika.

Katika semina hiyo ya kuwaelimisha madereva juu ya makosa ya kibinadamu yanavyochangia kwa kiasi kikubwa ajali za barabarani, Konisaga alisema uzembe, ulevi, uchakavu wa barabara, ubovu wa magari ni miongoni mwa sababu hizo.

“Katika kipindi cha mwaka jana pekee Sh. bilioni 230 zilipotea kutokana na matukio mbalimbali ya ajali za barabarani ambazo nyingi zimesababishwa na makosa ya binadamu,” alisema.

Awali akizungumza katika semina hiyo, Meneja wa Usalama Barabarani  na Mazingira wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchikavu (Sumatra), Geofrey Silanda, alisema tafiti mbalimbali zilizofanywa nchini zinaonyesha asilimia 75 za ajali za barabarani zinatokana na makosa ya kibinadamu.

“Lakini pia asilimia 50 ya makosa hayo ya barabarani yanayohusiana na mambo ya kibinadamu yanafanywa na madereva,” alisema Silanda.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Madereva wa Mabasi Mkoani Mwanza (Uwamata), Shabani Wandiba, aliitupia lawama serikali kuwa ndiyo inayochangia kwa kiasi kikubwa kusababisha ajali za barabarani kutokana na kupanga muda wa magari kusafiri bila ya kuangalia umbali.

“Ratiba inapangwa bila kuangalia umbali, mwendo kulingana na alama za barabarani, mfano mwendo wa kilomita 80, 50, 20 kwa saa pamoja na muda wa chakula yote hayo ni miongoni mwa vyanzo vya ajali,” alisema Wandiba.

Naye Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Mwanza, Mrakibu wa Polisi Mohamed Likwata, alisema ajali nyingi zinasababishwa na madereva ambao wanashindwa kufuata sheria na alama za usalama barabarani kikamilifu.

Kuhusu muda, kamanda huyo alisema atashauriana na Sumatra kuangalia muda wa chakula wa dakika 10 ili uweze kuongezwa kutokana na mabasi yenye uwezo wa kuchukua abiria 60 kutoweza kutimiza sheria hiyo ambayo inawabana madereva.

NIPASHE
Walimu zaidi ya 2,000 mkoani Mwanza wanaidai serikali malimbikizo ya mishahara pamoja na gharama za upandishwaji madaraja.

Aidha, baadhi ya walimu wanaidai serikali fedha za likizo na matibabu na wengine wakisubiri kupandishwa madaraja.

Akizungumza na NIPASHE juzi mjini hapa,  Mwenyekiti wa Chama cha Walimu (CWT) mkoani Mwanza, Sibora Kisheri, alisema wanaungana na Rais wa chama hicho taifa, Gratian Mkoba (pichani), kuitaka serikali kuwalipa madeni yao kabla ya Septemba mwaka huu.

Hata hivyo, Kisheria hakutaja kiasi cha fedha ambacho walimu wanaidai serikali mkoani humo.

Alisema wanaunga mkono kauli ya Mkoba ya kuitaka serikali kulipwa madeni yao kabla ya Septemba, mwaka huu pamoja na kwamba Rais Jakaya Kikwete alishaahidi kuwalipa wakati mkutano mkuu wa CWT uliofanyika mkoani Arusha.

“Mwanza tupo tayari kupokea maelekezo yoyote ya CWT makao makuu na kuyaunga mkono, tunataka haki yetu ilipwe kwa wakati maana walimu tunaathirika na tunafanya kazi katika mazingira magumu,” alisema Kisheri.

Naye Katibu wa CWT Mkoa wa Mwanza, Said Mselem, aliiomba serikali wakati wa kupanga bajeti, walimu wawe wanahusishwa ili inapopitishwa waelewe kilichopitishwa.

alisema wakati wa kupitisha bajeti wamekuwa hawahusishwi hivyo kuwawia vigumu kujua kipi kilichopitishwa ili utekelezaji usipofanyika waweze kufuatilia jambo ambalo hata katika sheria zao zinaeleza hivyo.

Mselem alisema CWT mkoa wa Mwanza hawatakubali kuona mwalimu yeyote mkoani humo anahamishwa na kupelekwa eneo jingine bila kulipwa gharama za uhamisho.

NIPASHE
Rais Jakaya Kikwete amesema Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimempitisha, Dk. John Magufuli (pichani), kugombea urais kupitia chama hicho kwa kumuamini kuwa atasimamia vizuri rasilimali za nchi ikiwamo gesi na madini kwa manufaa ya taifa na Watanzania.

Akizungumza jijini Arusha juzi wakati akifungua mkutano wa nne kati ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-Tamisemi), Bodi ya Mfuko wa Barabara na wadau wa barabara, Rais Kikwete alisema ana amini endapo Magufuli atachaguliwa kuwa Rais wa Tanzania waKati wa uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu, atasimamia vizuri rasilimali hizo kutokana na kuwa msomi mzuri na kuwa na uchungu wa maendeleo ya taifa lake na watu wake.

“Huyu Magufuli siwezi kujilinganisha naye, mwenzangu ana PhD ya kusomea na ameifanyia utafiti kwenye ganda la korosho jinsi ya kutumia mafuta yake kunufaisha nchi kwenye maendeleo ya taifa, ila mimi nina PhD ya heshima, hatuwezikuwa sawa, hivyo nina imani naye sana,” alisema.

Rais Kikwete alisema CCM imemchagua kwa makusudi Dk. Magufuli kwa ajili ya kuhakikisha nchi inaneemeka na rasilimali ya gesi ambayo hadi sasa uwekezaji wake umegharimu dola za Marekani bilioni 20 hadi 30 mpaka kuanza uvunaji wake.

“Naomba tusifanye mchezo na rasilimali hii, ndiyo sababu  mimi nimehakikisha tunakuwa na sheria nzuri ya kusimamia vizuri rasilimali hii isije ikatupeleka kubaya, japo baadhi ya watu walisema naharakisha ya nini, ila najua kuna nchi walipata mafuta ila watu wakubwa wakakopa kwa kujivunia mafuta hayo na matokeo yake hadi sasa wanalipa madeni na nchi, mimi sikutaka hayo,” alisema.

Alisema ni vizuri rasilimali kama hizo zikawekewa utaratibu wa kuzilinda kabla ya kuanza uvunaji wake na kwamba baada ya miaka michache ana amini Tanzania itakuwa nchi tajiri kwa kuuza gesi nje kwenye masoko makubwa.

Rais Kikwete alisema Dk. Magufuli kutokana na usomi na uchapakazi wake, kila wizara aliyowekwa aliongoza vizuri na kupatikana mafanikio makubwa, hivyo akiwa Rais atafanya mambo mengi makubwa zaidi kwa manufaa ya taifa na wananchi wote.

MTANZANIA
MGOMBEA urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli amesema ikiwa atachaguliwa kuongoza Serikali ya awamu ya tano atahakikisha anapambana na watendaji wala rushwa serikalini.
Amesema watendaji hao ndiyo wamekuwa wakikwamisha juhudi za Serikali kupeleka maendeleo kwa wananchi hali inayosababisha malalamiko ya wananchi.
Kauli hiyo aliitoa jana kwa nyakati tofauti alipohutubia wananchi katika mikutano ya kampeni  katika mikoa ya Katavi na Rukwa.
Dk. Magufuli pia aliahidi kufuta utaratibu wa wakulima kukopwa mazao yao na serikali.
Alisema utaratibu huo umekuwa hauleti tija kwa wananchi na badala yake wamekuwa wakirudi nyuma kwa maendeleo badala ya kusonga mbele.
“Hakuna jambo linaloniudhi kama wakulima kukopwa mazao yao, ninajua mikoa ya Katavi hasa Majimoto   na Nkasi ni wakulima wazuri wa mahindi na mpunga ila nimekuwa siridhiki na namna watu wanavyokopwa mazao yao.
Mgombea huyo wa urais aliwaahidi wananchi kuwa ikiwa atafanikiwa kuchaguliwa kuwa rais wa awamu wa tano, kuanzia Februari mwaka kesho elimu ya msingi hadi sekondari itakuwa bure kwa watoto wote.
“Fedha zipo lakini kuna wala rushwa wachache ambao wamekuwa wakikwamisha juhudi za serikali, mimi ninasema nichagueni nikapambane na watendaji wabovu ambao hawafai kwa sasa.
“Ninajua wazi kero kubwa ni barabara na ninachopenda kuwaambia wakandarasi waliposikia nimeteuliwa kuwania urais hivi sasa wote wamerudi kazini licha ya wengine hawaidai serikali, na ni lazima barabara ya Nkasi-Mpanda ikamilike kwa wakati.
“Kubwa ninachowaomba mniamini ndugu zangu na mnichague mimi   na wabunge, madiwani wa CCM,” alisema.
Dk. Magufuli alisema ingawa Serikali ya awamu ya nne imefanya kazi kubwa  changamoto zimebaki na akaahidi kuzikamilisha kwa wakati.
“Ninashangazwa sana leo tuna kero ya maji sasa inafanyika wiki ya maji wakati maji yenyewe hayapo, wiki ya Ukimwi dawa hakuna, wiki ya maziwa lakini viwanda na maziwa hakuna, kwangu ninataka kurekebisha hili kwa vitendo,” alisema.
Alisema moja ya ahadi yake kupitia ilani ni kuhakikisha ujenzi wa zahanati na huduma ya umeme kwa kila kijiji katika kipindi cha miaka mitano ya utawala wake.
“Ilikuwa awamu ya kwanza ya Mwalimu Nyerere (Julius), mzee Mwinyi, Mkapa, Rais Kikwete na awamu ya tano ninawaomba mnikabidhi mimi kwani
ni zamu yangu kuwatumikia Watanzania,” alisema.
Kwa habari, matukio na michezo ni hapahapa tangakumekuchablog

No comments:

Post a Comment