Friday, August 28, 2015

SOMA HABARI KUBWA ZILIZOPEWA UZITO MAGAZETI YA LEO, AUG 28 TZ

Uchambuzi huu wa magazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha elimu cha Candle Education Centre Tanga, kituo kinaongoza kufaulisha wanafunzi kidato cha pili hadi cha sita na wanaojiendeleza kielimu. Kituo pia kinatoa kozi mbalimbali za kielimu na Ufundi. Wapo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 772746

wite
NIPASHE
Benki ya Dunia (WB), imeipatia Serikali ya Tanzania mkopo wa Dola milioni 200 za Marekani (sawa na Sh. bilioni 422) kwa ajili ya kusaidia uboreshaji wa huduma za afya kwa wajawazito na watoto wachanga.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Sebastian Likwelile, alisema serikali itahakikisha fedha hizo zinazaa matunda kwa wakati.
“Kwanza niishukuru Benki ya Dunia kwa kutupa mkopo wenye riba ndogo na ya muda mrefu kwa ajili ya kusaidia uboreshaji wa huduma za afya kwa mama na mtoto kutokana na kundi hili kukabiliwa na changamoto nyingi,” Likwelile.
Aidha, alisema pamoja na kuwapo kwa mikakati mbalimbali ya kupambana na changamoto hizo, bado kuna kazi kubwa kuhakikisha huduma za afya zinaboreshwa ili kupunguza vifo ambavyo si vya lazima kwa wajawazito na watoto wachanga.
“Serikali imekuwa ikipambana kupunguza tatizo hili na kufanikiwa kwa kiwango kidogo kutokana na upungufu wa vifaa ambapo mwaka 2010 wajawazito 454 kati ya 100,000 walifariki dunia,”.
Aliongeza kuwa watoto 26 kati ya 1,000  wenye umri wa kati ya miaka mitano, hufariki dunia kutokana na magonjwa mbalimbali na wengine wakati wa kuzaliwa.
Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Bernad Konga, aliishukuru WB kwa mkopo huo na kusema kuwa utasaidia kwa kiwango kikubwa kuimarisha huduma za afya.
“Tunaahidi kuwa fedha hizo zitatumika kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuhakikisha vifo vya watoto wachanga na wanawake wakati wa kujifungua vinapungua,” Konga.
“Sekta ya afya inakabiliwa na changamoto nyingi lakini kwa kutumia fedha hizi, tutahakikisha zinatatuliwa kwa kiwango kikubwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo,”.
NIPASHE
Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amesema hana deni la kulipa kwa mtu yeyote akichaguliwa kushika wadhifa huo kwa kuwa hakutoa rushwa wakati wa uteuzi ndani ya chama hicho.
Magufuli alitoa kauli hiyo jana wakati akijinadi yeye na wagombea udiwani na ubunge wa CCM mkoani hapa ili wachaguliwe katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Dk. Magufuli alikuwa akijinadi na wagombea hao kwa nyakati tofauti katika mji wa Mbalizi na wilayani Songwe eneo la Mkwajuni, Makongolosi wilaya ya Chunya.
Magufuli ambaye jana alikuwa katika  siku ya nne ya kujinadi kwa wananchi na kuomba kura tangu kufunguliwa kwa pazia la kampeni mikoani, alisema tangu kuanza kwa mchakato wa kumpata mgombea wa CCM wa urais ndani ya chama hicho, hakutumia fedha bali alikwenda kimya kimya makao yao makuu kuchukua fomu na kuzirejesha.
Alisema kwa mantiki hiyo,  hana cha kulipa kwa sababu hadaiwi na mtu yeyote.
Magufuli alisisitiza kuwa anachofahamu ni kwamba deni kubwa alilonalo ni kuwatumikia Watazania na kuwaletea maendeleo ili wazidi kuwa na maisha bora.
“Nilichukua fomu kimya kimya na kurudisha kimya kimya, natembea na barabara ili shida zenu ziwe shida zangu, ili nikiingia Ikulu nizishughulikie kwa haraka,” alisema.
Magufuli alisema anaamini kuwa kuteuliwa kwake na CCM kupeperusha bendera ya chama hicho katika kinyang’anyiro hicho kuna makusudi ya Mwenyezi  Mungu ili afanye kazi.
Sikutoa rushwa kwa kuwa ni dhambi na adui wa haki… niliacha mchakato huo wa kumpata rais ndani ya CCM ufanywe na Mungu,” alisema.
Dk. Magufuli alisema wale wanaosalimia kwa kutumia salamu na kauli mbiu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Peoples Power, wampe ‘power’ aende Ikulu kuharakisha maendeleo ya watanzania.
“Nipeni wabunge na madiwani wa CCM nikafanye kazi, tutafanyakazi bila kinyongo, hatutawabagua, hapa ni kazi tu,” aliahidi.
Alisema maendeleo hayana chama, kabila wala rangi, hivyo amepanga kufanya kazi na makundi yote bila kubagua na kuomba kura kwa wananchi wote bila ya kujali vyama vyao vya siasa.
“Hakuna anayezaliwa kutoka tumboni mwa mama yake akiwa na kadi ya chama fulani, bali wanavikuta, hivyo msidangaywe na vyama, kinachotakiwa ni maendeleo,” .
Akizungumzia kuhusu madai ya walimu nchini, alisema kada hiyo siyo wito bali ni kazi, fedha na kuwafundisha wanafunzi kwenye shule walizopangiwa na serikali.
Alisema baada ya kuingia Ikulu, kazi yake ya kwanza itakuwa ni kuwalipa madeni wanaoyoidai serikali.
Magufuli aliwataka walimu kuwa wavumilivu na kuwaomba kumchagua kwa kura nyingi katika uchaguzi huo.
MTANZANIA
Chama cha Wanasheria cha Tanganyika (TLS), kimelaani kitendo cha mwanachama wake ambaye amewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Lawrence Masha, kunyimwa dhamana mahakamani.
Katika taarifa yake iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari, TLS imesema mahakama imekuwa na tabia ya kunyima watu haki yao hiyo kwa kisingizio cha kuhakiki nyaraka za dhamana.
Kutokana na hali hiyo, chama hicho kimesema kitaunda tume maalumu ya kuchunguza uvunjwaji wa taratibu za mahakama unaosababisha watu kukosa haki za dhamana.
Masha ambaye pia ni wakili, alikamatwa hivi karibuni Kituo cha Polisi Oysterbay, Kinondoni, jijini Dar es Salaam, alipokwenda kuwawekea dhamana vijana waliokamatwa kwa kosa la kukusanyika kinyume cha sheria.
Inadaiwa kuwa Masha alitoa lugha ya matusi kwa askari aliowakuta katika kituo hicho, hivyo naye akakamatwa na kuwekwa mahabusu kabla ya kufikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambako alinyimwa dhamana na kupelekwa gereza la Segerea.
Rais wa TLS, Charles Rwechungura, alisema katika taarifa hiyo kuwa kumekuwa na tabia ya mashtaka huchukua muda mrefu kushughulikiwa na mshtakiwa anatakiwa abaki rumande akiwa na dhamana yake mfukoni.
“Tunalazimika kueleza hisia zetu kama wanachama wa kundi hili kutokana na tukio la hivi karibuni la kuomba dhamana kwa mmoja wa wanachama wetu. TLS inalaani bila kujuta na bila kuomba radhi kwa tabia hiyo ya aibu ambapo mwanachama wetu Lawrence Masha (Wakili) alifanyiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu,”  Rwechungura.
“Kosa alilokuwa akishtakiwa Masha la kutoa lugha chafu kinyume cha Kifungu cha 89(1) (a) cha Kanuni ya Adhabu [Cap 16 R.E.2002] linaangukia katika kundi la makosa madogo yanayotolewa dhamana,” aliongeza Rwechungura katika tamko hilo.
Alisema kutokana na ukiukwaji huo wa taratibu za mahakama, TLS itaunda tume maalumu ya kukusanya taarifa ili kukomesha tabia hiyo.
“Tanganyika Law Society itaunda tume maalumu ya kukusanya taarifa za kutosha iwezekanavyo kwa uvunjifu wa taratibu za mahakama katika utoaji wa dhamana, ili kuushirikisha mhimili wa mahakama kurejesha hali ya kawaida,” Rwechungura.
Hata hivyo, alisema TLS haihoji kukamatwa kwa Masha na kama ni mkosaji au kosa aliloshitakiwa litachukuliwa kwa uzito gani na mahakama, bali wanacholalamikia ni kitendo chama mahakama kusababisha Masha kukosa haki yake ya dhamana.
“Wala TLS haihoji masharti ya dhamana yaliyowekwa na mahakama kwa sababu kwa maoni yetu kwa masharti hayo yangesaidia. Tunacholalamikia na kukosoa ni uhalali na umakini wa mahakama kuacha jukumu lake na kusababisha Masha kukosa haki yake ya dhamana,” .
Alisema wakati wote TLS imekuwa ikikemea kupitia matukio mbalimbali vitendo vya wazi vya kudharau mahakama na hasa pale mahakama inajikuta kwenye mazingira kama hayo.
MTANZANIA
Mke wa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Regina, amesema anashindwa kuelewa ni kwanini watu wanatunga uongo kuhusu mumewe.
Akizungumza katika mkutano na wanawake kutoka vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), Regina alisema yeye ni mtu pekee anayemfahamu mumewe kuliko  mwingine yeyote.
“Huyu ni mume wangu, namfahamu kulikoni mtu mwingine yeyote… ni mchapakazi, ni mtu anayethamini utu, mpenda maendeleo, asiyependa unyanyasaji. Nashindwa kuelewa kwanini watu wamtungie uongo badala ya kuja kwangu kuniuliza,”.
Akizungumza huku akishangiliwa na wanawake waliohudhuria mkutano huo na kulazimu mshereheshaji muda wote kuingilia kati kuwaomba kunyamaza, Regina alisema kila mmoja afanye mabadiliko pamoja na kufika viwanja vya Jangwani kesho ambapo uzinduzi wa kampeni za Ukawa utafanyika.
Regina alisema kuwa amefarijika kuzungumza na wanawake na mabinti wa Tanzania kwa kuwa wao ndio chimbuko la maendeleo.
“Taifa linapaswa kufanya mabadiliko ya kweli ili kufikia maendeleo, na yatafanywa na wanawake… Kuna sheria nyingi ambazo zinamnyima mwanamke nguvu kama vile sheria ya kumiliki mali, wakati umefika wa kufanya mabadiliko. Ni wakati wa mabinti kuacha kudhalilishwa, wakati umefika kina mama kumiliki mali, huduma bora za jamii,  afya, elimu nk,”.
Alisema wanawake ambao wanazalisha zaidi kuliko wanaume hawana manufaa na mazao wanayoyapata kutokana na kushindwa kuwezeshwa.
“Nadhani kuna umuhimu wa kubadilisha sera za kilimo, ufugaji na hilo litasaidia mabadiliko, sensa inaonyesha wanawake ni wengi na hivyo ni jeshi kubwa tukiamua kuleta mabadiliko tunaweza,” alisema.
Akihutubia umati huo wa wanawake, Lowassa alisema anadeka  kutokana na mafuriko ya wanawake ndani na nje ya ukumbi huo ambayo yalisababisha rafiki yake kutoka Zanzibar kumweleza kuwa si mapenzi bali ni mahaba.
“Nadeka, hizi ni baraka za mwenyezi Mungu na sio mkono wa mtu, rafiki yangu wa Zanzibar aliwahi kuniambia haya si mapenzi bali ni mahaba. Sasa nawapeni kazi, nimekuwa mbunge kwa miaka 30, wanawake ni waaminifu,  wakisema wanakupa kura wanakupa, naomba mnitafutie kura, nataka kura za kutosha kuwashangaza Watanzania, sio kura yako tu bali pia ya mume, watoto na mtu mwingine,” alisema.
Lowassa ambaye muda wote alikuwa akishangiliwa, alisema kuna ambao wanaona kuwa ameingia kwenye mchezo kwa kucheza, na kwamba watashangazwa na sanduku la kura Oktoba 25.
“Kila mwanamke anayenisikiliza naomba anipatie kura na tukimaliza kazi ya kura tutakutana Arusha Ngurdoto Desemba kama tulivyo. Halima na Mbowe tumezungumza jambo hilo, tukae mahali tujadili mabadiliko maana yake nini, nataka kupeleka maendeleo kwa kasi ya ajabu,” Lowassa.
Alisema mabadiliko nchini hayaepukiki, kwani mwaka 1995 Nyerere aliuambia mkutano wa Chama Cha Mapinduzi kuwa Watanzania wanataka mabadiliko na wasipoyapata ndani ya CCM watayatafuta nje.
MTANZANIA
Aliyekuwa Mbunge wa Longido, Michael Lekule Laizer, amemweleza mgombea mwenza wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, kwamba kitendo cha Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuhama chama hicho, kimegawa wananchi wa jimbo hilo.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Namanga mkoani Arusha, Laizer alisema baada ya jina la Lowassa kuenguliwa kwenye wagombea wa CCM na kuamua kuhamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), baadhi ya wananchi wamemfuata kwenye chama hicho licha ya kujaribu kuwaelimisha sababu zilizofanya kada huyo aenguliwe.
Alisema mbali na kundi linalomuunga mkono Lowassa, wengine wamebaki CCM wakisema kiongozi huyo hajawahi kuwasaidia kitu.
“Wananchi wa Longido wamegawanyika kwa kitendo cha Lowassa kukatwa kwenye nafasi ya urais na kuhamia Chadema, jambo ambalo limewafanya wengine kumfuata,” Laizer.
Alisema wananchi wa jimbo hilo hawana matatizo na CCM wala madiwani wa chama hicho, bali wana matatizo na mchakato mzima wa uteuzi wa majina ya wagombea ulivyofanyika kwa sababu hawajui utaratibu gani unaotumika uliosababisha kukatwa kwa jina la Lowassa.
Laizer aliwaambia wananchi hao kuwa, Kamati Kuu ya CCM ndiyo yenye jukumu la kupitisha jina la mgombea wa urais wa chama hicho.
Viongozi wa juu wa CCM, wakiwamo Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilali pia ni miongoni mwa waliondolewa.
Laizer alisema baada ya kuwaambia wananchi hao, baadhi yao walimwelewa, lakini wengine hawakumwelewa, hali iliyosababisha kujitokeza kwa mgawanyiko huo.
Alisema mtu anaamua kuondoka kwa uamuzi wake, lakini shughuli za chama zitabaki kama ilivyokuwa, hivyo basi aliwataka wananchi hao kuwa na umoja ili kuhakikisha CCM inapata ushindi, jambo ambalo linaweza kuwasaidia kupata maendeleo.
“Maendeleo hayawezi kuletwa na upinzani bali yanaletwa na wananchi kupitia CCM, hivyo basi tunapaswa kuungana na kuhakikisha mgombea ubunge wa jimbo hilo kupitia CCM anapata ushindi ili aweze kuleta maendeleo,” alisema.
Alisema katika kipindi hiki ambacho ameamua kupumzika, atashirikiana na mgombea huyo pamoja na wana CCM wenzake kuhakikisha ushindi unapatikana.
Kwa upande wake mgombea mwenza wa CCM, Samia Suluhu Hassan, alimtaka Laizer kuwaelimisha wananchi wa jimbo hilo ili waweze kukichagua chama hicho katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Alisema mkakati wa Serikali ni kujenga hospitali ya wilaya katika jimbo hilo ili wananchi waweze kupata huduma ya afya.
Alimshukuru Laizer kutoa ofisi ya mbunge na kugeuza mahakama ya mwanzo na wilaya ili watendaji wa mahakama waweze kutimiza majukumu yao.
MWANANCHI
Watu tisa wa familia moja wameteketea kwa moto baada ya nyumba yao kuungua usiku wa kuamkia jana jijini Dar es Salaam, huku mashuhuda wakisema walikuta miili yao ikiwa imeshikana.
Juhudi za kuwaokoa watu hao waliofariki dunia wakiwa kwenye moja ya vyumba vya nyumba hiyo namba 40 iliyoko katika Mtaa wa Ulam, Buguruni Malapa wilayani Ilala, zilishindikana na chanzo cha moto huo hakijajulikana ingawa mashuhuda wanasema mtungi wa gesi ulilipuka baada ya moto kuwaka kwa muda mrefu.
Walioteketea katika tukio hilo ni mama wa familia hiyo, Samira Juma Ibrahim (42), maarufu kwa jina la Mama Aisha na watoto wake wanne, Ahmed Masoud (15) aliyekuwa mwanafunzi wa kidato cha kwanza, Aisha Masoud (17), aliyekuwa mwanafunzi wa darasa la sita, Abdillah Masoud (10) na Ashraf Masoud (5).
Wengine ni Bimdogo Masoud (72), ambaye alikuwa mgonjwa na mama wa Samira, pamoja na wadogo zake wawili wa kike, Samira Harood (17) na Wahat Saleh (27), ambaye alitokea Unguja, pamoja na Fahir Fesal mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu.
Mashuhuda wa tukio hilo walisema baada ya kusikia kelele za vilio, waliizunguka nyumba hiyo kwa lengo la kutaka kuwaokoa, lakini ilishindikana baada ya milango kutofunguka na moto kuwa mkali kiasi cha kushindwa kuingia.
“Katika namna ya kujaribu kujiokoa, Ahmed alijaribu hata kurusha nje funguo ili waweze kufunguliwa mlango, lakini ilishindikana. Hivyo alirudi chumbani wakashikana pamoja kusubiri kifo,”  Suleiman Bashraf ambaye ni kaka wa Samira.
Bashraf, anayeishi Mikocheni na ambaye anasema alifika eneo la tukio wakati dada yake na watoto wake wakiwa wameshafariki, alibainisha kuwa baba wa familia hiyo, Masoud Materu ambaye ni mfanyakazi wa kampuni ya Kimataifa ya Huduma za Kontena (TICTS) inayofanya kazi kwenye Bandari ya Dar es Salaam, alikuwa kazini wakati wa tukio hilo.
Alisema alipopigiwa simu hakuelezwa kuhusu tukio hilo, badala yake wafanyakazi wenzake walimsindikiza hadi Msikiti wa Ulam na baadaye saa tatu asubuhi alipelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambako maiti za waliofariki zimehifadhiwa.
Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema wamepokea taarifa ya tukio hilo na jeshi hilo linaendelea na uchunguzi.
Shuhuda mmoja wa tukio hilo, Hassan Banda alisema ingawa alifika eneo hilo mapema, walishindwa kuingia ndani kuwa mlango wa nondo haukuweza kufunguka.
Alisema baadaye, mmoja wao aliruka ukuta lakini alikuta hali ni mbaya kwani mlango wa nyuma wa kutokea jikoni ndiko moto ulikuwa umeanzia na ulikuwa mkali sana, hivyo akalazimika kurudi upande wa mbele.
“Kuna kijana mmoja (marehemu Ahmed) ndiye tulikuwa tukiwasiliana naye tukimpa maelekezo akiwa ndani ya nyumba. Tulimwambia alete chuma cha kuvunjia, lakini akaleta funguo na kuurusha nje. Kwa kuwa kitasa kilishapata moto ilishindikana kufungua,” alisema.
“Baadaye akasema anakwenda chumbani kwa bibi yao. Waliendelea kulia wakihitaji msaada, lakini baadaye kukawa kimya na hapakuwa na mawasiliano tena.”
Shuhuda huyo alisema muda mfupi baadaye walisikia kishindo kikubwa cha kulipuka kwa mtungi wa gesi na kisha paa la nyumba likashuka chini, lakini akasema wakati huo tayari watu wote walishafariki dunia.
Marehemu walizikwa jana kwenye Makaburi ya Kisutu baada ya ibada iliyofanyika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
MWANANCHI
Baada ya kushambulia mikoa ya Dar es Salaam na Morogoro, ugonjwa wa kipindupindu sasa umepiga hodi katika Mkoa wa Pwani na tayari watu tisa wameonekana kuwa na dalili za ugonjwa huo.
Hali hiyo imeulazimu uongozi wa idara ya afya mkoani Pwani kutenga maeneo ya kuwalaza kwa ajili ya vipimo na tiba huku katika Mkoa wa Dar es Salaam ugonjwa huo umewakumba watu 348 na vifo 10. Juzi, Mkoa wa Morogoro uliripotiwa kuwa na wagonjwa 32 huku mmoja akiwa tayari amepoteza maisha.
Wakati wagonjwa katika mikoa hiyo wakizidi kuongezeka, Ofisa Afya wa Mkoa wa Pwani, Simon Malulu alisema mtu mmoja amethibitika kuugua kipindupindu huku wengine wanane wakilazwa kwa kuwa na dalili za ugonjwa huo.
Alisema Agosti 18, kulikuwa na wagonjwa wawili kutoka Bagamoyo na wamekuwa wakiongezeka kutoka Mkuranga, Kibaha Vijijini na Kibaha Mjini.
Alisema mara ya mwisho, ugonjwa huo uliikumba Pwani mwaka 2005.
Wakati huohuo; Manispaa ya Kinondoni imetumia polisi kuwakamata baba na mama lishe wanaokiuka agizo la kutokufanya biashara ya chakula kipindi hiki cha mlipuko wa kipindupindu.
Ofisa afya manispaa hiyo, Mathias Kapizo alisema wamelazimika kuchukua hatua hiyo baada ya kuona idadi ya watu wagonjwa inaongezeka. Alisema wamepokea wagonjwa wapya 35 na kufanya idadi yao kufikia 52.
Waandishi wetu waliotembelea Soko la Mapinduzi, Mwananyamala waliwakuta mama lishe wakiendelea na biashara hiyo.
Mwenyekiti wa soko hilo, Hamis Marande alisema maofisa wa afya hawajawapa taarifa yoyote na hawajasikia tangazo linalokataza kuuza chakula badala yake maofisa wanapita kudai Sh5,000 kwa ajili ya kupima afya.
Katika hatua nyingine, Manispaa ya Ilala imewatoza faini ya Sh50,000 wafanyabiashara waliokaidi agizo la kuuza chakula katika mazingira machafu.
Mganga mkuu wa manispaa hiyo, Victorina Ludovick alisema: “Hatutatumia nguvu kubwa lakini eneo hili lina watu wakorofi ndiyo maana tumeongozana na mgambo.” Alisema juzi, walipokea wagonjwa wapya wanne na walioko kambini ni 14 na kufanya idadi ya watu waliougua ugonjwa huo kufikia 60 katika manispaa hiyo.
HABARILEO
Raia wa China, Jianfeng Wu amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashitaka ya kukutwa na meno ya simba yenye thamani ya Sh milioni 10.1.
Baada ya kusomewa mashitaka, mshitakiwa hakuruhusiwa kujibu mashitaka kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo ya uhujumu uchumi isipokuwa Mahakama Kuu.
Awali, wakili wa Serikali, Paul Kadushi alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha kuwa ilikuwa Agosti 18, mwaka huu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Wu alipokamatwa akiwa na meno matatu ya simba.
Hakimu Mkeha aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 10, mwaka huu itakapokuja tena mahakamani hapo kwa hatua nyingine.
HABARILEO
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Kailima Kombwey amemkabidhi Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) majina 52,078 ya watu ambao wamejiandikisha zaidi ya mara moja kwenye daftari la kudumu la wapiga kura.
Orodha hiyo imepokelewa na Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Benedict Wakulyamba aliyemwakilisha IGP. Orodha hiyo imekabidhiwa ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya watu hao ambao wamevunja sheria ya uandikishaji wa BVR.
Alisema wamebaini majina hayo baada ya kuingiza taarifa za wapiga kura na mitambo kubaini alama za vidole.
Kombwey alisema miongoni mwa watu hao, wapo waliojiandikisha mara mbili na wengine wamejiandikisha mara saba kwa kutumia majina tofauti.
Akipokea majina hayo, Wakulyamba alisema watayafanyia kazi haraka iwezekanavyo ili wahusika waweze kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
“Leo naomba kumkabidhi IGP wa Polisi majina ya watu ambao wamejiandikisha zaidi ya mara moja ili wasakwe na wachukuliwe hatua za kisheria,” alisema Kombwey na kuongeza kuwa miongoni mwa watu ambao wamejiandikisha zaidi ya mara moja wamo wanasiasa ambao wanagombea nafasi mbalimbali za kisiasa katika uchaguzi mkuu ujao.
Alisema mitambo ya EMC V Block inayotumika ina uwezo wa kulinganisha alama milioni 16 kwa dakika moja.
Katika hafla hiyo waandishi walioneshwa watu ambao wamejiandikisha wengine wakibadilisha mifumo ya nywele, wengine nguo walizovaa pamoja na majina.
Mkurugenzi huyo alisema hadi sasa kesi 12 zimeshafunguliwa mahakamani na baadhi zimeshaisha na wahusika wamehukumiwa kati ya kifungo cha miezi sita hadi miaka miwili jela pamoja na kupigwa faini.
Alionya kuwa mtu ambaye atahukumiwa kifungo cha kuanzia miezi sita huyo hatakuwa na sifa ya kupiga kura na ataondolewa kwenye daftari hilo.
Pia alisema hatua inayofuata kwa sasa ni kubaini watu ambao wamejiandikisha wakati siyo raia wa Tanzania na amesema watafanikisha hatua hiyo baada ya kushirikiana na Idara ya Uhamiaji.
Alisema pia watu ambao watakuwa hawajafikisha miaka 18 siku ya kupiga kura ambayo ni Oktoba 25 pia watawekwa pembeni.
Hata hivyo hakuweza kutoa takwimu za raia wa kigeni mbao wamebainika kujiandikisha kwenye daftari hilo. Pia hakutoa takwimu za watu ambao watakuwa hawajafikisha miaka 18 siku ya kupita kura. Hata hivyo alisema kwamba Tume inaendelea kufanya uchambuzi na itakapokuwa tayari itatoa taarifa.
Aidha waandishi wa habari wamehakikishiwa kuwa hakuna mwananchi ambaye amejiandikisha jina lake litakosekana kwenye daftari la kudumu la wapiga kura.
Naibu Katibu wa Mkurugenzi wa NEC anayeshughulikia Tehama, Dk Sisti Cariah alisema kwamba taarifa za watu zimetunzwa katika maeneo sita.
Maeneo hayo ni fomu aliyojaza mpiga kura wakati anaenda kujiandikisha, flash, kwenye kompyuta mpakato iliyoko kwenye mashine ya BVR pamoja na kadi ya kuweka kumbukumbu (SD Card).
Alisema kwamba kama kuna taarifa za mtu zimekosewa wakati wa uandikishaji wana mfumo wa kutafuta fomu za mtu mmoja ndani ya dakika tatu ili kupata usahihi wa taarifa ya mpiga kura kama jina, jinsia na mengineyo.
Dk Cariah aliwahakikishia wananchi kuwa kumbukumbu zao ziko salama na hata kama litatokea janga la asili, kumbukumbu zote za wapiga kura zimehifadhiwa sehemu tatu tofauti jambo ambalo litafanya kazi za tume hiyo kuendelea hata kama kutatokea janga.
Hata hivyo aliwataka wananchi waendelee kuhakiki taarifa zao kwa kutumia namba za simu na pale watakapokuta taarifa zao sio sahihi waende kwa Mkurugenzi wa Wilaya ili taarifa ziweze kufikishwa Tume.
Alikanusha uvumi kuwa utaratibu wa kutumia simu wa kuhakiki taarifa za mtu utamfanya mtu apige kura na kusisitiza kuwa upigaji kura utafanyika kwa mtu kwenda kituo cha kupigia kura na kuchukua karatasi ya kupigia kura na kupiga kura kisha kuitumbukiza kwenye sanduku.
Kwa habari, matukio na michezo ni hapaha tangakumekuchablog

No comments:

Post a Comment