Sunday, August 23, 2015

SOMA HABARI KUBWA ZILIZOPEWA UZITO MAGAZETI YA LEO AUG 23 TZ

Uchambuzi huu wa magazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha elimu cha Candle Education Centre Tanga. Kituo kinaongoza kufaulsha wanafunzi kidato cha pili hadi cha sita na wanaojiendeleza kielimu. Kituo kinatoa kozi mbalimbli za kielimu na kiufundi ukiwemo umeme na Computer. Wapo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 772746
SUND
MWANANCHI
Miezi kadhaa baada ya treni ya kubeba abiria jijini Dar es salaam kusitisha safari zake kutokana na ubovu, imeelezwa kuwa hali hiyo inatokana na uchakavu wa injini.
Mkuu wa masoko wa kampuni ya Reli Tanzania Charles Ndenge alisema treni hiyo imekua ikiharibika mara kwa mara kutokana na injini zake kutumika kwa muda mrefu huku ikifanya kazi tofauti na ilivyoundwa.
“Treni hii ilitengenezwa kwa safari za mbali, hata hivyo imefanya kazi kwa muda mrefu na injini zake zimechoka ndio maana zinafanyiwa marekebisho, niwahakikishie watumiaji huduma ya usafiri itarejea kama kawaida” Ndenge.
Alifafanua mpaka sasa matengenezo yamefikia hatua nzuri na wiki mbili zijazo huduma hiyo itaanza kufanya kazi tena.
HABARILEO
Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Sumbawanga imewatia hatiani watu sita na kuwahukumu kunyongwa hadi kufa kwa kosa la kuua kwa kukusudia. Waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa ni Oden Msongela , Philibert Majaliwa , Edwin Simba , Sabas Alfred,Wenseslaus Kakwale na Maiko Simfukwe. Hukumu hiyo imetolewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mwakipombe Sango.
Watu hao wamepatikana na hatia ya kumuua kwa kukusudia kwa kumpasua fuvu mkazi wa kijiji cha Lusaka, wilayani Sumbawanga, mkoani Rukwa, Maiko Hussein (56).
Baada ya Jaji Sambo kusikiliza ushahidi aliwahukumu washitakiwa sita kifo huku wengine wawili wakiachiwa huru.
Walioachiwa huru ni Gilbert Mwanandenje  na Meresi Namazali . Waliachiwa huru baada ya upande wa mashtaka kushindwa kutoa ushahidi usiotia shaka mahakamani hapo.
“Mahakama hii imewatia hatiani washtakiwa hawa sita kwa kosa la kuua kwa kukusudia baada ya kujiridhisha na aina ya silaha zilizotumika zikiwemo nondo, mashoka , panga na marungu , pia nguvu kubwa iliyotumika kushambulia na madhara yaliyosababishwa na kipigo,” alisema.
Jaji Sambo alisema mashahidi wote sita walioitwa mahakamani na upande wa mashtaka wametoa ushahidi, ambao haukuwa na mashaka yoyote, hivyo kuwatia hatiani watu hao sita kwa kosa la mauaji.
“Ushahidi uliotolewa wa utambuzi wa washtakiwa ulikidhi viwango vinavyohitajika katika mashauri ya jinai… hakika ulikuwa umeenea, hivyo nawahukumu kunyongwa mpaka kufa,” alisema Jaji Sambo wakati akisoma hukumu hiyo.
Upande wa mashitaka uliongozwa na Mwanasheria wa Serikali, Scholastica Lugongo huku washtakiwa hao wakitetewa na wakili wa kujitegemea , Mathias Budodi. Awali kabla ya hukumu hiyo, ushahidi uliotolewa mahakamani hapo ulieleza kuwa Hussein alitendewa unyama huo Mei 13 , 2012 katika kijiji cha Lusaka, wilaya ya Sumbawanga kati ya saa tatu na saa nne usiku.
Inadaiwa kuwa Hussein usiku huo alikuwa na mkewe Winfrida ambapo washtakiwa hao walibisha mlango na walipofunguliwa waliingia ndani na kumkamata marehemu na kumtoa nje ya nyumba yake na kuanza kumpiga.
Ushahidi huo unaeleza kuwa Hussein alifanikiwa kuwachomoka washtakiwa hao na kuanza kutimua mbio lakini walimfukuza hadi wakamkamata na kuanza kumshambulia kwa silaha za jadi kisha mmoja wao akampiga kwa panga kichwani na kumpasua fuvu lake .
Ilielezwa kuwa baada ya kufanya mauaji hayo washtakiwa hao waliufunika mwili huo kwa nyasi kisha wakauteketeza kwa moto . Watuhumiwa hao pia wanadaiwa kuteketeza nyumba hiyo ya marehemu na nyumba nyingine tano katika kijiji hicho cha Lusaka wakiwatuhumu wenye nyumba hizo kuwa ni wachawi.
HABARILEO
Mkazi wa Gogoni kata ya Dunda wilayani Bagamoyo mkoani Pwani Ramadhan Mlala anatuhumiwa kumuua mke wake Angelina Pius kwa kumchoma na kisu sehemu mbalimbali za mwili wake kutokana na wivu wa mapenzi, akiwa katika ofisi za Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA).
Baada ya tukio hilo mtuhumiwa huyo naye kwa kutumia kisu hicho alijichoma tumboni na kutaka kujiua na kusababisha utumbo wake kutoka nje.
Kamanda wa Polisi mkoani Pwani Jafar Ibrahim alisema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 21 mwaka huu majira ya saa tatu asubuhi eneo la Gogoni, kata ya Dunda ambapo chanzo cha mauaji hayo ni wivu wa mapenzi.
“Mtuhumiwa alimshambulia mke wake akiwa mlangoni kwenye ofisi za Bakwata alikokwenda kupeleka malalamiko yake ndipo alipomvamia na kumchoma kisu sehemu mbalimbali za mwili wake hadi kufa,” alisema Kamanda Ibrahim.
Kamanda Ibrahim alisema kuwa kabla ya mkasa huo kutokea, wanandoa hao walikuwa na mgogoro wa ndoa wa muda mrefu huku Angelina akidai talaka mara kwa mara baada ya kuona hakuna suluhu zaidi ya kuachana na mumewe huyo.
Kamanda Ibrahim alisema mtuhumiwa huyo kwa sasa anapatiwa matibabu chini ya uangalizi wa jeshi hilo ili akipona ajibu tuhuma zinazomkabili za mauaji ya kukusudia na kuwa kisu alichofanyia mauaji hayo kimepatikana.
HABARILEO
Chama Cha Mapinduzi (CCM), kinatarajiwa kuzindua kampeni zake za urais, ubunge na udiwani nchi nzima katika viwanja vya Jangwani leo, katika mkutano utakaorushwa moja kwa moja na televisheni na redio mbalimbali nchi nzima.
Katika uzinduzi huo, CCM pia inatarajiwa kuweka ilani yake ya uchaguzi hadharani, itakayonadiwa na mgombea urais wake, Dk John Magufuli na wagombea wengine wa ubunge na udiwani nchi nzima.
Moja ya mambo ambayo CCM inatarajiwa kufafanua ni matumaini makubwa ya uwezo wa mgombea wake katika kusimamia utekelezaji wa ilani hiyo, kutokana na historia yake ya utendaji ndani ya Serikali katika nafasi mbalimbali alizokabidhiwa, ikiwemo Waziri wa Ujenzi.
Wageni mbalimbali pia wamealikwa kuhudhuria uzinduzi huo vikiwemo pia vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Msemaji wa CCM Mkoa, Juma Simba vile vile wanatarajia wageni kutoka ndani na nje ya jiji la Dar es Salaam kuhudhuria mkutano huo leo. “Tumetuma mialiko ya mkutano wa kesho (leo) sio tu kwa wana CCM wenzetu bali pia kwa vyama vingine vya siasa ikiwa ni pamoja na kwa vyama vya ‘Ukawa’,” alisema.
Simba alisema mkutano huo utakuwa mkubwa na wa aina yake ambapo viongozi mbalimbali wa chama wanatarajiwa kushiriki na kwamba mkutano huo ratiba yake itaanza asubuhi saa tatu kwa burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali na wananchi kuendelea kuwasili uwanjani.
Sifa za Magufuli Mgombea huyo amekuwa akitajwa kuwa na sifa ya mchapakazi, makini, asiyependa uvivu, ambapo Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete alimpachika jina “Tingatinga”.
Rais Kikwete alimpachika Magufuli jina hilo, baada ya kutangazwa kuwashinda makada wengine wawili waliokuwa wakiwania kuteuliwa kuwania urais kupitia chama hicho katika Mkutano Mkuu wa chama hicho uliofanyika Dodoma. “Kila mtu anaitwa jembe lakini huyu ni zaidi ya jembe.
Ni tingatinga… Magufuli ni bulldozer. Magufuli havumilii ujinga, ni mtu ambaye anataka kuona kazi zake zinafanyika kama alivyoagiza,” alikaririwa akisema.
Kikwete aliendelea kummwagia sifa Dk Magufuli kuhusu utendaji wake akisema kuwa alipokuwa akifuatilia makandarasi kwenye miradi ya ujenzi, alidiriki kuwatimua pale alipobaini walikuwa wakifanya kazi kinyume na makubaliano.
Baadhi ya watu waliofanya naye kazi wamekaririwa wakisema iwapo atachaguliwa kuwa rais basi wavivu wajitayarishe kukimbia kwani Waziri huyo ni mchapa kazi wa hali ya juu.
Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mussa Iyombe, aliyefanya kazi na Dk Magufuli kwa zaidi ya miaka 10, alikaririwa akisema kwa kipindi alichofanya kazi na Magufuli ameshuhudia kuwa hataki mchezo katika kazi, hana mzaha na mwenye umakini mkubwa kwa kila anachofanya.
Msemaji wa Wizara ya Ujenzi, Segolena Francis alikaririwa akimsifu Magufuli kuwa ni mtu anayejali muda, anayependa kazi yake na asiyetaka mtu legelege.
“Nimejifunza mambo mengi kwake na nina tumaini kuwa kama atakuwa Rais, basi taifa litakuwa limepata mchapakazi. Anafuatilia kila kitu yeye mwenyewe, hana makundi, hana ukabila wala udini,” alikaririwa akisema.
Katika mkutano huo wa leo , CCM pia inatarajiwa kufafanua mafanikio yake katika miaka 10 iliyopita, ikiwemo kuongeza mapato ya serikali.
Taarifa za serikali zinaonesha kuwa mapato ya serikali yameongezeka kutoka Sh bilioni 177.1 mwaka 2005 kwa mwezi, hadi takribani Sh bilioni 850 na kuwezesha bajeti ya serikali kukua kutoka trilioni 4.13 mwaka 2005/2006 hadi trilioni 22.49 mwaka 2015/2016.
Mafanikio hayo ya makusanyo yamewezesha serikali kutekeleza kazi zake na miradi ya maendeleo, huku ikipunguza misaada na mikopo ya washirika wa maendeleo, kutoka asilimia 42 ya Bajeti ya serikali mwaka 2005 hadi asilimia 15 mwaka 2014/2015 na kushusha zaidi hadi asilimia 8 mwaka huu wa fedha wa 2015/2016.
Barabara Ujenzi wa barabara ni matunda ya ongezeko la mapato ya serikali na udhibiti katika matumizi ya fedha za umma uliofanyika katika uongozi wa Awamu ya Nne.

NIPASHE
Wakati mchakato wa uteuzi wa wagombea wa nafasi za udiwani na ubunge katika vyama mbalimbali vya siasa ukielekea ukingoni, wananchama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Jimbo la Songea Mjini, wamerushiana makonde na kusababisha mtafuruku.
Hatua hiyo imesababisha Mwenyekiti wa chama hicho wilaya ya Songea, John Mwankina na mgombea udiwani kata ya Tanga, Musa Ndomba, kupigwa na baadhi ya wafuasi.
Habari zilizothibitishwa na Mwankina zimeeleza kuwa vurugu hizo zilianza Agosti 21, saa 2:30 na kudumu hadi saa 4 usiku kwenye ofisi ya chama hicho baada Ndomba kudai  kuwepo makundi ndani ya chama na kusababisha kushindwa kwenye uchaguzi mkuu.
Taarifa zaidi za tukio hilo zimeeleza kuwa muda mfupi baada ya kumaliza mchakato wa kura za maoni ya udiwani na ubunge kwa baadhi ya wagombea ambao walishindwa, waliamua kukata rufaa kupinga matokeo hayo kwenye kata za  Majengo, Tanga, Msamala na Matarawe na kuwa rufaa hizo zilipelekwa moja kwenye ngazi ya mkoa ambako baraza la wazee wa chama hicho lilipokea na kuzifanyia kazi.
Taarifa zilidai kuwa baadae baraza la wazee lilitoa mapendekezo kwa kamati ya utendaji ya chama ya wilaya ya Songea kuwa maamuzi yatakayotolewa na kamati ya utendaji yafuatwe na kuzingatia ushauri uliotolewa na baraza hilo.
Mgogoro huo ulifikia hatua ya kuanza kupigana na kumfungia ndani ya ofisi katibu wa chama wa wilaya hiyo, Olais Cheenga, ambaye baadae alilazimika kumpigia simu Mwenyekiti wa Chadema wa wilaya, aliyekuwa mbali na eneo hilo ambaye alifika na kukuta kikundi cha ulinzi cha chama hicho cha Red brigade kikiwa kimezingira eneo hilo.
Taarifa zinaeleza kuwa mwenyekiti huyo alijikuta akipigwa na kikundi hicho cha ulinzi kisha kumfuata Ndomba aliyekuwa amesimamisha gari karibu na eneo hilo na kumpiga yeye na dereva wake.
Ndomba aliwaambia waandishi wa habari  aliamua kuandika barua kujiengua kugombea udiwani baada ya kuona kundi la mgombea ubunge linakikuka kanuni na taratibu za ndani ya chama.
Naye mgombea ubunge Jimbo la Songea mjini kupitia chama hicho, Joseph Fuime, alipoulizwa kuhusiana sintofahamu hiyo ndani ya chama alikanusha kuhusika na mgogoro huo.
Kamanda wa polisi wa mkoa wa Ruvuma Mihayo Msikhela, amesema polisi halijapokea taarifa za tukio hilo licha ya kupata kupitia vyombo vingine.
NIPASHE
Mgombea Ubunge Jimbo la Kasulu Mjini kupitia chama cha ACT-Wazalendo, Moses Machali, ameweka pingamizi la uteuzi wa mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Daniel Nsanzugwanko, kwa madai kuwa hafai kuwa mgombea baada ya kujaza fomu kuwa amezaliwa tarehe 15/08/2015.
Tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 10 jioni baada ya wagombea wengine kuona fomu yake kwenye ubao matangazo wa Halmashauri ya Mji wa Kasulu.
Machali alitoa pingamizi hilo jana kwa Msimamizi wa uchaguzi ambaye ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kasulu, Fatina Hussein, kwa madai kuwa kutokana na mgombea wa ubunge kupitia CCM, Nsanzugwanko kujaza fomu kuwa alizaliwa tarehe hiyo, mwaka huu, hafai kuwa mgombea.
Kwa mujibu wa Machali, kisheria ni kosa kwa mtu mwenye umri chini ya miaka 21 kugombea nafasi ya ubunge, lakini pia kwa kosa hilo ambalo ni la kisheria ni wazi msimamizi wa uchaguzi anapaswa kutomteua mgombea huyo wa CCM ambaye kwa mujibu wa Machali,  Nsanzugwanko ameapa kiapo kinachoonesha umri wake ni siku sita.
Alisema katika mazingira hayo amepoteza sifa za kuteuliwa kuwa mgombea na suala hilo halihitaji mjadala.
Hata hivyo, katika hatua iliyowashangaza  wananchi ni pale Mkurugenzi huyo kutaka kubandua fomu hiyo ili abandike nyingine.
Akifafanua kuhusu hatua hiyo, Hussein alisema, juzi majira ya saa 10 jioni alibandika fomu kwenye ubao kama sheria inavyosema na ilionekana Nsanzugwanko alijaza fomu kuwa alizaliwa mwaka 2015.
Fatina alisema baada ya wagombea kubaini kuwa fomu ya mgombea wa CCM imekosewa aliwaambia wachukue fomu za pingamizi.
Mkurugenzi huyo aliwataka wagombea kuwa na amani na utulivu na kwamba fomu zitalindwa na uchaguzi utafanyika kwa haki.
Kwa upande wake CCM Nsanzugwanko  alipoulizwa kuhusu tarehe hiyo ya kuzaliwa alijibu kwa kifupi: “ Je wewe unaamini, kwa heri.”
NIPASHE
Rais Jakaya Kikwete ameiasa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) kuonyesha usawa katika kushughulikia masuala ya viongozi wa Afrika na Ulaya.
Kikwete alitoa msimamo huo jana jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wa 16 wa Chama cha Wanasheria kutoka nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Aliilaumu kazi ya ICC huku akipendekeza mahakama hiyo iache kuwashtaki viongozi wa kiafrika kama ilivyokuwa kwa kesi ya hivi karibuni ya Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta.
Alisema katika kesi mbalimbali viongozi wa kiafrika wamekuwa walengwa wakuu ambao hupelekwa kwenye mahakama hiyo kwa kesi ambazo ni sawa na zile zinazofanywa na viongozi kutoka bara la Ulaya.
“Kuna viongozi wengi waliotenda jinai kubwa ambazo zinaathiri jumuiya ya kimataifa lakini hawajawahi hata kuhojiwa,” alisema.
Kwa mujibu wa Rais Kikwete, haiwezekani iwe tu kwa mataifa dhaifu kuingia kwenye mkondo wakushtakiwa bali hata wale wa mataifa makubwa wanatakiwa kufanyiwa hivyo.
Rais Kikwete alisema kwamba, ICC imekuwa mstari wa mbele kuwashtaki viongozi wa kiafrika kama ilivyokuwa kwa Rais wa Sudan Omar Bashir ambaye alikimbia kutoka Afrika Kusini kutokana na  hati ya kumkamata kwa mashtaka ya kuasisi mauaji ya kimbari nchini kwake katika jimbo la Darfur.
Alikihasa chama cha wanasheria cha SADC kuwa na ushujaa bila ya kuogopa wakati  wakilipigania suala hilo.
Kuhusiana na kusitishwa kwa mahakama ya kimataifa maalumu kwa ajili ya Rwanda, Kikwete alisema SADC inahitaji kuona uwezekano wa kulifanyia kazi suala hilo kwa sababu si tu la kisheria bali pia ni la kisiasa.
Alisema kuna njia nzuri la kulifanyia kazi suala hilo badala ya kulipeleka mahakamani.
Kwa upande mwingine, Rais wa chama hicho, Gilberto Caldeira, alisema kuna umuhimu wa kutambua haki za binadamu bila ya woga kwa kuwa na sheria ambazo zinaweza kuziba pengo kati ya watawala na wananchi.
Hata hivyo, alikubaliana na wasiwasi wa mahakama hiyo akisema kuwa uhuru wa kushughulikia mashtaka ya jinai ni mdogo.
Aliituhumu Zimbabwe kwa ushawishi wa kusitishwa kwa mahakama hiyo akisema uhuru wa mahakama umeminywa.
Aliweka matarajio yake kuwa, uchaguzi ujao utatumika kama mfano kwa mataifa mengine yaliyotumia mbinu chafu ili kuendelea kubakia madarakani.
Hii sio mara ya kwanza kwa mataifa ya kiafrika kuilaumu ICC.hivi karibuni kwenye sherehe za siku za uhuru wa Kenya iliyofanyika Desemba mwaka jana, Rais Yoweri Mseveni wa Uganda alisema kwamba alikuwa akipanga kuzishawishi nchi za kiafrika kujitoa ICC kwenye mkutano ujao wa umoja wa Afrika kwa kuwa wanaweza kughulikia masuala ya nchi zao.
NIPASHE
Aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa. Sospeter Mohongo, ambaye anagombea ubunge jimbo la Musoma Vijijini kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) amewekewa pingamizi kwa kudaiwa kuanza kampeni kabla ya muda.
Amewekewa pingamizi hilo jana na mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)  Zakaria Chirangwile, katika ofisi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Mosoma mjini jana.
Alisema Profesa Muhongo amepoteza sifa ya kuwa mgombea baada ya kukiuka kanuni kwa kuanza kampeni kabla ya muda uliopangwa na tume.
Alisema amekusanya ushahidi ikiwamo vipeperushi, fulana na kofia zilizochapishwa sura yake na kuvaliwa na wanachama wa chama chake.
Chirangwile aliitupia NEC lawama kwa kushindwa kufuatilia nyendo za wagombea na kuwachukulia hatua watu wanaokiuka kanuni za uchaguzi.
Alisema kuwa mgombea huyo wa CCM ametawaliwa na  wasiwasi kutokana na wananchi wa jimbo hilo kukata tamaa na chama hicho na kumlazimu kukiuka sheria.
“Mimi nitawashangaa sana watanzania na wana-CCM ambao watampigia kura yao Muhongo, hivi watu wa aina yake ambao wanatuhumiwa kwa wizi wa zaidi ya billioni 300, halafu ukapange msitari unampigia kura, wanapaswa kuondoa wazo hilo kama lipo kichwani kwao.
Hata hivyo, alisema kitendo cha Muhongo kupita mtaani na kuanza kujitangaza kwamba yeye ndiye amesababisha na kutumia fedha zake kusambaza umeme katika jimbo hilo, umeonesha ni namna gani alivyo muongo  kwani fedha zinazosambaza umeme ni za walipa kodi na misaada kutoka nje.
Mkurugenzi Mtendaji wa  Halmashauri ya Musoma Vijini, Fiderica Miyovela, alipotafutwa kuzungumzia suala hilo alikiri kuwepo suala hilo na kwamba Ofisi yake inasubiri mlalamikiwa huyo kupewa taarifa za kuanza kampeni kabla ya wakati uliopangwa na NEC.
Hata hivyo Mwandishi wa habari hizi alipomtafuta, Prof. Sospeter  Muhongo kujibu tuhuma hizo kupitia simu yake haikuwa hewani hadi taarifa hizi zinachapishwa.
Kwa habari , matukio na micheze ni hapa hapa tangakumekuchablog

No comments:

Post a Comment