Thursday, August 20, 2015

KIWANDA CHA SARUJI CHA SIMBA CEMENT CHATOA MSAADA WA MIFUKO 110 KITUO YA YATIMA, TANGA



Tangakumekuchablog
Tanga, KIWANDA cha Saruji cha Simba Cement cha Tanga, kimetoa msaada wa mifuko ya saruji 110 yenye thamani zaidi ya shilingi milioni moja laki mbili kwa kituo cha watoto yatima kukamilisha ujenzi wa vyumba na kisima cha maji kilichopo Kilapula Tanga.
Akizungumza wakati wa makabidhiano jana, Injinia wa kiwanda hicho, Benedict Lema, alisema msaada huo umekuja kutokana na umuhimu wa watoto hao kupata makazi mazuri na salama baada ya kuondokewa na wazazi wao.
Alisema jamii imejisahau kuwangalia watoto wanaoishi katika mazingira magumu na badala yake wamekuwa wakijishughulisha na mambo mengine na hivyo kuitaka kutoa misaada ili nao kuweza kuishi kama watoto wengine.
“Uongozi wa kiwanda cha saruji umeguswa na kituo hiki cha nyumba ya furaha kwani kimeona jitihada zao katika kuhakikisha watoto wote wanapata malezi na elimu bora kama ilivyo kwa wengine” alisema Lema na kuongeza
“Kwa maana hiyo kiwanda kinatoa mifuko mia na kumi ikiwa ni kuendeleza kituo katika mambo mbalimbali yakiwemo ya vyumba na vyoo vya kisasa kwani ndani ya watoto hao kuna walemavu na wa mazingira tofautitofauti” alisema
Alisema kituo hicho kinatakiwa kuangalia katika mazingira tofautitofauti kuhakikisha watoto wote wanapata elimu na huduma zote za kijamii ili nao waweze kuishi kama watoto wengine.
Kwa upande wake, mwangalizi wa watoto kituo cha watoto cha Casa Della Giola Ophanage (Jumba la Furaha), Consolata Mgamba, alikishukuru kiwanda cha Saruji cha Simba Cementi na kusema kuwa mifuko hiyo ya saruji itatumika kama ilivyokusudiwa.
Alisema kwa msaada huo ameitaka jamii na watu wenye uwezo kukisaidia kituo hicho katika mambo mbalimbali ya kielimu na afya na kuweza kuyafikia malengo ya kila mtoto kupata huduma mzuri na pamoja na elimu bora.
“Kwa niaba ya uongozi wa jumba la furaha tunakishukuru kiwanda cha saruji cha Simba kwa kuwa na moyo wa huruma------tunakiomba tena kuwa walezi wetu na kila ambapo wataona kuna fursa ya kutoa msaada tutashukuru” alisema Mgamba
Ameitaka jamii kuiga kutoka kiwanda hicho kwani kituo kinakabiliwa na changamoto mbalimbali na hivyo kuitaka kufika kujionea kazi na huduma ambazo wamekuwa wakizitoa.
                                                      Mwisho



,Injinia wa kiwanda cha Saruji cha Simba Cement, Benedict Lema (kulia) akimkabidhi mifuko ya saruji 110 yenye thamani zaidi ya shilingi milioni moja na laki mbili , mwangalizi wa watoto kituo cha watoto wanaoishi maisha hatarishi, Consolata Mgamba, ikiwa ni ujenzi wa kisima cha maji, vyumba na vyoo kituo kilicho  Kilapula nje kidogo ya jiji la Tanga.



 Meneja Rasilimali watu kiwanda cha Saruji cha Simba Cement, Diana Malambugi, akimkabidhi mifuko ya saruji 110 yenye thamani zaidi ya shilingi milioni moja na laki mbili mwangalizi wa kituo cha watoto yatima cha Casa Della Giola ikiwa ni ujenzi wa kisima cha maji, vyumba pamoja na vyoo kituo kilichopo Kilapula nje kidogo ya jiji la Tanga.

No comments:

Post a Comment