Thursday, August 27, 2015

VIZIWI TANGA WATAKA MKALIMANI KAMPENI ZA UCHAGUZI



Tanga,CHAMA cha Viziwi Mkoa wa Tanga (Chavita), imeitaka Tume ya  Taifa ya Uchaguzi  , kuweka  wakalimani wa lugha za alama katika mikutano ya kampeni ya wagombea Urais na Ubunge ili kujua sera za wagombea.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu wa Chavita Mkoa wa Tanga, Ali Nassour, alisema viziwi kipindi hiki cha kampeni za wagombea kundi hilo liko katika wakati mgumu na kukosa fursa za kusikiliza  sera za wagombea.

Alisema viziwi wanashindwa kwenda katika mikutano ya hadhara kusikiliza sera za wagombea kutokana na kukosekana wakalimani na hivyo kipindi cha kupiga kura kupiga kwa kubahatisha.

“Kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi tunaiomba tume ya uchaguzi kuweka wakalimani wa lugha za alama katika mikutano ya wagombea urais na ubunge-----hii itatusaidia kujua sera za wagombea” alisema Nassour na kuongeza

“Mimi binafsi nimeshuhudia mkutano pale tangamano na msambweni kwa vyama tofauti lakini nitaenda kusikiliza nini-----ukweli ni kuwa viziwi wako katika wakati mgumu” alisema

Kwa upande wake, Mshauri na mtetezi wa watoto wenye ulemavu kituo cha (YDCP) Prisca Joshua, ameitaka Serikali kuwawekea mazingira mazuri walemavu katika mikutano ya hadhara ya vyama ili itokeapo vurugu kuweza kulindwa.

Alisema walemavu hupata wakati mgumu vipindi vya kampeni za uchaguzi kutokana na kutowekewa ulinzi na hivyo kukumbana na misuguano ya wafuasi wa vyama hasa wakati wa kuisha kwa mkutano.

“Walemavu vipindi vya kampeni wako katika wakati mgumu kutokana na kutowekewa ulinzi na mazingira mazuri hasa baada ya kumalizika mkutano mara nyingi ndipo kunapotokea vurugu” alisem Joshua na kuongeza

“Vurugu hutokea pale mikutano inapoisha na wafuasi wa vyama kukumbana wakitoka katika mkutano-----mara nyingi hurushiana mawe na kukimbizana hapo ndipo walemavu wanakuwa na wakati mgumu” alisema

Akizungumzia changamoto za walemavu, Kaimu Mkurugenzi wa jiji la Tanga, Alpha Shemahonge, alisema ni  vyema vyama vya kisiasa kujiwekea utaratibu wa kuwa na wakalimani wao wakati wa kampeni ili kuweza kuvuna wapiga kura.

Alisema ili vyama kuweza kupata wapiga kura wengi ni kujiwekea utaratibu wa kuwa na wakalimani jambo ambalo litawavutia viziwi na kujua sera zao na kuwa rahisi wakati wa kupiga kura.

“Ili vyama kuvuna wapiga kura ni wajibu wao kuwa na mbinu tofauti zikiwemo za kuwa na wakalimani na kuweza kuwavuta viziwi na makundi mengine ya walemavu” alisema Shemahonge

Alisema Serikali imeweza kufanya jitihada kuweka wakalimani wakati wa matukio na taarifa za habari katika TV ya Taifa na hivyo kutambua kundi hilo changamoto inazokabiliana nazo na jitihada za kuzitatua  zinafanywa.

                                                  Mwisho







  Katibu wa Chama Cha Viziwi Mkoa wa Tanga (Chavita) Ali Nassour, akizungumza na waandishi wa habari Tanga kuitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi  kuweka wakalimani wa lugha za alama katika mikutano ya wagombea Urais na Wabunge.




No comments:

Post a Comment