HADITHI hii inaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Tiba cha Mkombozi Sanitarium Clinic, Mabingwa wa magonjwa yaliyoshindikana na yaliyojificha. Mkombozi wako na mashine ya kisasa ya ugunduzi wa magonjwa yaliyofichikana na kutoa tiba ya kupona haraka. Wapo Chuda Tanga mkabala na kampuni ya mabasi ya Raha Leo, simu 0654 361333
NILIJUA NIMEUA (9)
ILIPOISHIA
Niliisikia waziwazi sauti
yake ikihitimisha hukumu yangu kwa maneno yasemayo.
“Nimeridhika na ushahidi
uliotolewa kwamba wewe mshitakiwa umemuua mke wako kikatili kwa kumkatakata na
panga. Kwa sababu hiyo mahakama hii imekutia hatiani. Adhabu yako ni kunyongwa
kwa kitanzi hadi ufe!”
Yale maneno “Utanyongwa kwa
kitanzi hadi ufe” yalizindua akili yangu, nikazinduka kama
mtu aliyetoka kwenye ndoto. Nikashusha pumzi ndefu na kuikazia macho maiti ya
mke wangu.
Nisipobuni maarifa ya
kufanya, nilijiambia, picha iliyonijia akilini nikihukumiwa kunyongwa itakuwa
kweli!.
Nitatumia akili gani kuokoa
maisha yangu? Nikajiuliza bila kupata jibu.
Nikaendelea kujiuliza,
itakuwa sahihi kweli mke wangu afe na mimi ninyongwe?
Hapo hapo nikapata wazo.
Nilitoka nje nikaiwasha teksi yangu kisha nikafungua mlango wa nyuma wa teksi
na kuuacha wazi. Nilirudi ndani nikazima taa ya nje, nikaenda uani na kuibeba
maiti ya Halima. Nikaenda nayo hadi mlango wa mbele ambao sikuwa nimeufunga
kabisa.
SASA ENDELEA
Niliufungua kwa mguu
nikachungulia nje. Barazani kwangu kulikuwa giza baada ya kuzima taa. Na hakukuwa na mtu
yeyote aliyekuwa akipita barabarani usiku huo.
Nikatoka haraka na maiti ya
Halima na kuipakia kwenye teksi kwa kutumia mlango wa nyuma niliouacha wazi.
Niliilaza ile maiti kwenye siti kisha nikafunga mlango wa teksi na kurudi
ndani.
Nilikwenda chumbani
nikachukua tochi yangu ya mawe sita, nikatoka chumbani na kwenda stoo kuchukua
shepe.
Nikiwa nimeshika shepe na
tochi nilitoka nje nikafungua boneti la nyuma la teksi yangu na kuliweka lile
shepe pamoja na tochi kisha nikalifunga boneti.
Nilikwenda kwenye mlango wa
dereva nikajipakia na kuiondoa teksi.
Eneo la makaburi halikuwa
mbali sana na
mtaa niliokuwa ninaishi pale Msambweni. Nikaiendesha teksi taratibu hadi katika
eneo hilo la
makaburi. Niliingiza teksi ndani kabisa ili isionekane mahali hapo. Nilikuwa
nimezima taa za mbele na za nyuma.
Nilipofika mahali
nilipopataka niliisimamisha teksi nikafungua mlango na kushuka. Nilikwenda
nyuma ya teksi nikafungua boneti na kutoa shepe pamoja na tochi. Nikawwa natafuta
mahali pa kuchimba kaburi ili niizike ile maiti ya Halima nipoteze ushahidi.
Baada ya kumulikamulika tochi
nilipata sehemu nzuri ambayo haikuwa na kaburi. Nikatazama huku na huku,
nilipoona kulikuwa kimya nikaanza kuchimba.
Mchanga ulikuwa mgumu lakini
nilijitahidi hivyohivyo, jasho likawa linanitoka. Nilipochoka nilipumzika
kwenye gari kisha nikarudi tena kuendelea kuchimba. Nilichimba hadi nikapata
shimo la kutosha. Nikaliweka shepe chini nikaenda kwenye teksi na kuutoa mwili
wa Halima.
Sikuwa na nguvu za kuubeba
kwa vile nguvu nyingi nilizitumia kuchimba kaburi hilo. Niliuweka chini kisha nikauburuza
kuelekea kwenye lile kaburi. Nilipolifikia nikausukumia ndani ya kaburi hilo.
Ulivyoangukia ndivyo hivyo
hivyo nilivyoufukia. Sikuwa na muda wa kuingia ndani ya kaburi hilo na kuuweka sawa.
Nilipomaliza kufukia
nilisawazisha mchanga na kuushindiliankwa miguu. Wakati nafanya hivyo
niliona kama kulikuwa na mtu nyuma ya mti uliokuwa ubavuni kwangu
akinichungulia. Nikashituka!.
Niliinama chini nikaichukua
ile tochi na kumulika pale kwenye mti. Ule uso uliokuwa ukinichungulia ulipoona
mwanga ulijificha nyuma ya mti.
Nikapata hofu na wasiwasi kwa
sababu sikujua mtu yule alikuwa nani na kama
alikuwa akinifuatilia mimi.
Nilijiambia kama mtu huyo
alikuwa ananifuatilia mimi atakuwa ameshgundua siri yangu na ilikuwa si siri
tena.
Dukuduku la kutaka kumjua
likanipata. Nilitaka nijue kama ni mtu
niliyekuwa namfahamu au yeye ananifahamu mimi.
Nikalishika lile shepe kama silaha yangu na kunyemelea kunako ule mti huku
nikiendelea kumulika tochi.
Nilinyemelea kuuzunguka ule
mti nikiuambaa kwa mbali kwa kuhofia kushambuliwa ghafla kwani sikuwa nikijua
aliyekuwa nyuma ya mti huo alikuwa nani.
Nilipozunguka nusu tu ya mti
huo nikamuona mtu amechutama chini ya mti huo. Nikammulika kwa tochi ili niweze
kumuona vizuri. Nilimuona alikuwa msichana na alikuwa uchi wa mnyama! Nguo zake
alikuwa amezishika mkononi akikinga uso wake usimulikwe.
Kitendo cha kumuona msichana
yule mahali pale na usiku ule tena akiwa uchi, kwa kweli kilinitisha. Maswali
mawili yakanijia.
Alikuwa nani?
Alikuwa akinichunguza mimi au
alikuwa na lake?
Sikutosheka kujiuliza peke
yangu kwa sababu nisingepata jibu, nikaikaza sauti yangu na kumuuliza.
“Wewe nani?”
“Zima tochi kwanza!”
akaniambia. Sauti yake ilikuwa ya chini lakini ilikuwa ya ukali.
Nikazima ile tochi lakini
mwanga wa mbalamwezi ulitosha kuyafanya macho yangu yamuone.
Alipoona nimezima tochi
alisimama akavaa nguo zake haraka haraka huku akiniambia “Subiri hapo hapo”
Alipomaliza kuvaa akaniambia.
“Samahani kaka yangu, mimi
nilikuwa na ishu yangu hapa ndiyo nikakuona wewe unafukia hilo kaburi. Nadhani wewe pia ulikuwa na ishu
yako. Sote ni wachawi, tusidhuriane”
Sote ni wachawi? Ina maana
yeye ni mchawi? Nikajiuliza.
“Ulikuwa na ishu yako ipi?”
“Kaka usiwe na wasiwasi na
mimi. Mimi nilikuja kuzika vitu vyangu kwenye kaburi”
“Vitu?”
“Ndiyo vitu”
“Vitu gani?”
“Ni vitu vya uganga. Nilipewa
na mganga wangu. Aliniambia nije nivizike usiku kwenye kaburi”
“Wewe ni mchawi?”
“Hapana, si mchawi”
“Mbona umeniambia sote ni
wachawi tusidhuriane”
“Nimekwambia hivyo kwa maana
tunavyovifanya hapa ni vitendo vya kichawi vya kufukua makaburi usiku”
“Hivyo vitu ulivyozika
vinahusu nini?”
“Ni mambo yangu binafsi”
“Kwa hiyo huna tatizo jingine?’
Msichana akabetua mabega.
“Mimi sina tatizo, ni
wasiwasi wako tu”
Nikamsogelea karibu na
kumuuliza.
“Hivyo vitu umevizika kwenye
kaburi gani?”
Akanionesha kaburi lililokuwa
upande wa pili pembeni mwa ule mti.
Wakati nalitazama hilo kaburi aliniuliza.
Je alimuuliza nini n nini
kitatokea? Usikose kuendelea na hadithi hii kesho.
No comments:
Post a Comment