Kada wa Vijana Chadema Dar auawa kwa risasi
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa
Vijana Chadema Tawi la Luis, Mbezi Luis, Dar es Salaam, Dennis Kasanga
ameuawa kwa kupigwa risasi shingoni usiku wa kuamkia jana, huku taarifa
zilizotolewa na polisi zikitofautiana na mashuhuda wa tukio hilo.
Kasanga,
mkazi wa Mbezi Luis alipigwa risasi na watu wanaodaiwa kuwa majambazi
waliovamia baa inayojulikana kwa jina la Mtauli iliyopo njiapanda ya
Barabara ya Goba na Makabe saa saba usiku. Hata hivyo, polisi wamesema
tukio hilo halihusiani na ujambazi na wala halikutokea muda huo.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Camillius Wambura alisema jana
kuwa tukio hilo lilitokea saa 10 alfajiri kuamkia jana.
Alisema
tukio hilo lilitokea Barabara ya Goba baada ya watu wanne waliokuwa
wakisukuma gari bovu kuvamiwa na watu wengine wanne na kuibuka mzozo
kati yao.
“Baada ya mzozo, ghafla mmoja aliibuka na
kuanza kuwafyatulia risasi iliyowajeruhi watu wawili na kuua mmoja
aliyepigwa risasi shingoni,” alisema Kamanda Wambura.
Kamanda
Wambura alisema tukio hilo halihusiani na ujambazi kama watu
wanavyodai. “Siyo kila mtu anayefyatua risasi ni jambazi, subiri kwanza
tunaendelea na uchunguzi wa tukio.”
Hata hivyo,
mashuhuda wa tukio hilo walidai kuwa marehemu aliuawa kwa kupigwa risasi
na majambazi, ambao pia waliwajeruhi watu wengine wawili akiwamo mlinzi
wa baa hiyo.
Mbali na kujeruhi, watu waliokuwa na
bastola, mapanga na marungu pia waliwapora simu na fedha wateja wachache
waliokuwapo kwenye baa hiyo.
Kati ya waliojeruhiwa,
mmoja ni mlinzi aliyepigwa rungu usoni na mwingine aitwaye Erasmo
Basheja, mkazi wa eneo la Basondole aliyepigwa risasi begani.
Mhudumu
mmoja wa baa hiyo aliyekataa kutaja jina lake, aliliambia gazeti hili
jana kuwa watu kati ya sita au saba walifika kwenye baa hiyo saa saba
usiku wakijifanya wateja waliotaka kuhudumiwa vinywaji.
Alisema
wakati wakifika, baa ilishafungwa ila kulikuwa na wateja wachache nje
na yeye muda huo alikuwa ndani. “Baa ilishafungwa zamani, ila kulikuwa
na wateja wachache nje wakimalizia vinywaji,” alisema shuhuda huyo.
Alisema
baada ya watu hao kuelezwa kuwa baa imeshafungwa, ghafla walibadilika
na kuwataka watu waliokuwa hapo kulala chini na wakaanza kuwapekua
mifukoni na kupora simu zao.
“Nilisikia mlio wa risasi
na haraka haraka nilifunga mlango wa kuingia kaunta ya vinywaji kisha
nikalala uvunguni kwenye chumba kinachotumia mlango mmoja na kaunta,”
alisema shuhuda huyo.
Aliongeza: “Niliwasikia wale
majambazi wakisema, ‘hawa wanawake wameshafunga geti.’ Nilikaa kimya
nikiwa nimejilaza chini ya godoro.”
Alisema majambazi
hao wanaijua fika baa hiyo, kwani baada ya kuwalaza watu chini
walizunguka nyuma, ambako ndiko kwenye geti la kuingia kaunta na vyumba
vya ndani.
Mlinzi wa baa hiyo, ambaye amejeruhiwa usoni
kwa kupigwa na rungu aliiambia gazeti hili kuwa majambazi hao walifika
kwenye baa hiyo saa saba usiku wakati tayari pameshafungwa.
Alisema
alikuwa amekaa kaunta pamoja na marehemu na mtu mwingine ambaye
hakumbuki jina lake, ndipo aliposikia mlio wa risasi na wakati
akitaharuki, alivamiwa na mmoja wa watu hao na kupigwa rungu usoni huku
akisema: “Usiniangalie usoni.”
“Nilidondoka chini na
wakaanza kunisachi mifukoni huku wakinitaka kutoa simu na fedha,
niliwajibu sina kitu na baada ya kunipiga niliamua kutoa simu na
kuwapa,” alisema mlinzi huyo.
Alisema marehemu alipigwa
risasi wakati akiondoka alipoketi na kwenda sehemu ambayo alisikia mlio
wa risasi. “Alikuwa kaunta na baada ya mlio wa risasi alinyanyuka na
kwenda sehemu ya nje ya baa huko ndiko alikopigwa risasi na kufariki
dunia papo hapo,” alisema.
Kifo cha kiongozi huyo wa vijana Chadema pia kimethibitishwa na mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Luis, Finna Massawe.
Majirani
wa eneo ilipo baa hiyo walidai kuwa baa hiyo imekuwa ikivamiwa na
majambazi, mara kwa mara, na kwamba ingawa tukio la kuuawa mtu ni mara
ya kwanza kutokea, lakini tayari uhalifu wa kuvamiwa baa hiyo
ulishafanyika mara mbili.CHANZO MWANANCHI
Ungana nami kwa habari, matukio na michezo hapa hapa tangakumekuchablog
Ungana nami kwa habari, matukio na michezo hapa hapa tangakumekuchablog
No comments:
Post a Comment