HADITHI hii inaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Tiba Asilia (Mkombozi Sanitarium Clinic) mabingwa wa tiba na magonjwa yaliyoshindikana. Kituo kiko na mashine za kupima mwili mzima na kugundua magonjwa yaliyofichikana. Kituo kipo Chuda Tanga mkabala na Raha Leo Transport, simu 0654 361333
NILIJUA NIMEUA (7)
ILIPOISHIA
Baada ya kupelekwa wodini Dk
Kweka aliniita, nikaenda wodini na kumuona mke wangu. Hali aliyokuwa nayo
wakati anapelekwa kufanyiwa usafishwaji, siyo aliyokuwa nayo wakati ametolewa.
Alikuwa na afadhali sana.
Nikamshukuru Dk Kweka nay eye
akanishukuru pia.
“Unaweza kurudi naye
nyumbani” akaniambia.
“Tatizo lake limekwisha
kabisa?” nikamuuliza.
“Limekwisha isipokuwa kila
wiki umlete kuangalia maendeleo yake”
“Lilikuwa ni tatizo gani?”
“Mimba ilikuwa haikushika
sawa sawa. Ana udhaifu kwenye kizazi chake. Katika hali kama
hiyo anapopata mshituko, hofu au fadhaa, mara moja mimba inaweza kutoka”
Nikahisi ile ndoto aliyoota
ndiyo iliyomshitua na kusababisha mimba hiyo kuporomoka.
“Asante dokta, sasa unatushauri
nini?”
“Kama
nilivyokwambia kila wiki mlete hapa hospitali, nione maendeleo yake”
“Sawa dokta, nitafanya hivyo”
SASA ENDELEA
Baada ya hapo niliondoka na
mke wangu tukarudi nyumbani. Kila wiki nikawa nampeleka hospitali kufanyiwa
uchunguzi na Dk Kweka. Wiki nyingine ambazo sikuwa na nafasi alikuwa akienda
mwenyewe.
Zoezi hilo lilichukua wiki sita ndipo tukaacha
kwenda hospitali. Dk Kweka akanihakikishia kuwa tatizo la mke wangu halikuwepo
tena.
“Kama
unataka mimba nyingine kazi kwako” Dk Kweka akaniambia kwa utani.
“Asante
sana. Kwa kweli
ninakushukuru kwa msaada wako” nikamwambia.
Siku moja ambayo sitaisahau
maishani mwangu nilikuwa kwenye kiwanja cha ndege cha Tanga. Kulikuwa na ndege
ya abiria iliyotua kutoka Zanzibar.
Nikapata abiria mmoja ambaye
alivutia sana
hisia zangu. Alikuwa ni kijana ambaye nilisoma naye katika shule ya sekondari
ya Usagara. Mimi nilikomea kidato cha nne, yeye alifanikiwa kuendelea kidato
cha tano na cha sita. Alikuwa anaitwa Zacharia.
Tangu tulipoondoka shule
hatukukutana tena hadi siku ile. Miaka minane ilikuwa imeshapita. Mbali ya
kufurahi kumuona pia alinishitua, kwanza kumuona akishuka kwenye ndege na kwa
jinsi alivyokuwa amevaa na kupendeza.
Alikuwa amevaa suti nyeusi.
Koti lake alikuwa amelivua na kulipachika begani.
Ndani ya suti kulikuwa na shati jeupe na tai yangi nyekundu. Uso wake uliokuwa
umenawiri ulionesha mwenzangu alitoka kwenye neema
Kukutana kwangu na Zacharia
baada ya kufarakana kwa karibu miaka minane kulikuwa ndio mwanzo wa masahibu
niliyokutana nayo amabayo sitayasahau kamwe.
“Oh Machawi! Habari za siku?’
Hivyo ndivyo Zacharia alivyonisalimia huku akinipa mkono mara tu aliponiona
ndani ya jengo la kiwanja cha ndege.
Machawi lilikuwa jina langu
la utani ambalo vijana wenzangu walikuwa wakiniita shuleni. Walianza kuniita
mchawi kwa sababu nilikuwa na tabia ya kutoroka toroka shule. Naweza kuonekana
msitarini lakini wanafunzi wakiingia darasani hawanioni! Nimeshatoroka.
Nikaitwa mchawi. Baadaye jina hilo
likabadilika likawa Machawi.
“Nzuri Zacharia. Kumbe
unaishi Zanzibar?”
“Nilienda kwa muda, niko Dar”
“Kikazi uko wapi?”
“Baada ya kuchukua shahada
yangu ya sheria niliajiriwa na Wizara ya mambo ya nje”
“Nimefurahi kukuona, karibu
tena Tanga”
“Asante. Nahitaji teksi ya
kunipeleka mjini”
“Mimi pia ni dereva wa teksi.
Hapa nimefuata abiria”
“Kumbe unaendesha teksi!
Vizuri sana.
Basi twenzetu”
Nikatoka naye. Mara tu baada
ya kujipakia kwenye teksi mazungumzo yakaanza.
“Ajira zimekuwa ngumu sana. Nimeangukia kwenye udereva”
nilimwambia Zacharia wakati nikiiwasha teksi.
“Kwa sasa hivi sekta binafsi
ndio kimbilio la watu wengi. Hata mimi kuna uwezekano mkubwa nikaacha kazi na
kujiajiri mwenyewe”
“Wewe mwenzetu una shahada
yako ya sheria, unaweza kujiajiri mwenyewe. Taabu ni kwetu sisi tulioishia
sekondari”
“Hapana. Ajira ni ajira tu.
Hata kuendesha teksi ni ajira, ilimradi tu unapata riziki yako na maisha
yanakwenda. Kwani teksi ni ya kwako mwenyewe?”
“Hapana si yangu”
“Lakini masilahi yapo”
“Nashukuru, si sawa na kukosa
kabisa”
“Mimi nataka kuwa wakili wa
kujitegemea. Nitakuja kufanya kazi zangu hapa Tanga”
“Itakuwa vizuri sana. Huduma ya uwakili
inahitajika sana na katika mkoa wetu tuna mawakili wachache sana”
“Pengine mwakani nitakuwa
nimeshapata leseni”
“Nakuombea mafanikio.
Unakwenda wapi?”
“Mtendele Hotel”
“Pale Chuda?”
“Ndiyo Chuda. Nitakuwa pale
kwa wiki moja hivi”
“Zanzibar ulifuata nini?”
“Nilienda kikazi”
‘Tulifika Mtendele Hotel.
Wakati anashuka alinikaribisha. Na mimi nikashuka na kumfuata.
“Hatuwezi kuachana haraka.
Hatujakutana miaka mingi” aliniambia wakati tunapenya katika lango la hoteli
hiyo mpya.
Wakati anaandikisha chumba
aliniambia nikae kwenye kiti, akaniagizia bia.
Alipopatiwa chumba alirudi
tukaakaa sote. Na yeye akaagiza bia. Tulikunywa huku tunazungumza hadi nikakata
chupa nne. Baada ya kulipia bia tulizokunywa alinipa shilingi laki mbili.
“Chukua hizo rafiki yangu”
akaniambia. Nikamshukuru sana.
“Nipatie namba yako ya simu
ili kama nitahitaji teksi nikuite” akaniambia.
“Sawa”
Nikampa namba yangu na yeye
akanipa yake. Tukaagana na nikamuacha hapo hoteli.
Usiptwe na uhondo huu kesho nini kitatokea ni hapahapa tangakumekuchablog
No comments:
Post a Comment