Uchambuzi huu wa magazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha elimu cha Candle Education Centre Tanga, kituo kinaongoza kufaulisha wanafunzi kidato cha pili hadi cha sita na wanaojiendeleza kielimu. Kituo kinatoa kozi mbalimbali za kielimu na kiufundi zikiwemo za umeme na ufundi wa komputer. Kituo kipo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 772746
MTANZANIA
UMOJA wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wamemuonya Rais Jakaya Kikwete,
wakisema ndiye mwenye dhamana ya kulinda usalama wa wananchi na
akiendelea kutumia vibaya vyombo vya dola, Novemba mwaka huu watamburuza
Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) iliyopo The Hague,
Uholanzi.
Kauli hiyo ilitolewa jana mjini Zanzibar na viongozi wa Ukawa, katika
mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Kibanda Maiti wenye lengo la
kutafuta wadhamini kwa mgombea urais wa umoja huo kupitia Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa.
Akizungumza katika mkutano huo jana mjini hapa Katibu Mkuu wa CUF
ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalimu Seif Sharif
Hamad, alisema CCM wanahubiri amani wakiwa majukwaani lakini wakishuka
wao ndio wa kwanza kuivunja.
“Kama kuna watu wana nidhamu ni watu wa Ukawa, Mbeya, Arusha, watu
wawalikuwa wanasubiri kwa amani, polisi wanapiga mabomu, wao ndiyo
wanaleta tensheni katika nchi, siyo wafuasi wa Ukawa.
“Namwambia Kikwete (Rais), atimize wajibu wake, akifanya vinginevyo
watakwenda ICC, Kikwete ondoka kwenye nchi ikiwa salama kama
ulivyokabidhiwa ikiwa salama, wananchi wakukumbuke kuwa umeiacha
salama,” alisema Maalim Seif ambaye pia ni mgombea urais wa Zanzibar
kupitia umoja huo.
Mbatia
Akihutubia katika mkutano huo, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James
Mbatia, amewataka wanasheria wa Ukawa, kuanza kuandika matukio yote
yanayotokea nchini kwa sasa ili wayawasilishe katika Mahakama ya
Kimataifa ya Makosa ya Uhalifu (ICC).
“Tumeshawaagiza mawakili wetu waandike matendo yote maovu
yanayofanywa, waandikie ICC, wapeleke nakala kwa mabalozi wote ili Fatou
Bensouda (Mwendesha mashitaka Mkuu wa ICC) aje aanze kuangalia
yanayofanyika hapa.
“Tumechoka kudanganywa, tumechoka kuibiwa ushindi wetu, mwaka huu
tunasema, hapana, hapana. Walikuja kuandikisha watu wao hapa na baada
ya Ukawa kutangaza mgombea watu wao wote sasa wamehamia Ukawa,” alisema
Mbatia.
Alisema Watanzania kwa sasa wanataka mabadiliko kwa asilimia 99, na
jeshi la polisi likiendelea kuvunja amani, Novemba mwaka huu watakwenda
ICC.
Juma Duni
Naye Mgombea Mwenza wa Chadema, Juma Duni Haji, alisema ni bahati
mbaya sana watawala wanadhani kutumia mabavu kutawasaidia kubaki
madarakani jambo ambalo kwa sasa haliwezi kutokea.
Lowassa na Kingunge
Kwa upande wake Lowassa alisema kitendo cha CCM kumvua wadhifa wake
Kamanda wa UVCCM, Kingunge Ngombale Mwiru kwa sababu tu mwanasiasa huyo
mkongwe alitumia demokrasia kueleza hisia zake ni kuchuma laana.
Alisema Kingunge ambaye ni mmoja wa waasisi wa TANU na CCM, alikuwa
amebaki kama mfano ndani ya chama hicho kutokana na historia yake.
“Nianze kwa kueleza masikitiko yangu kwa hatua aliyochukuliwa mzee
Kingune jana (juzi), mzee huyu alibaki kama kielelezo cha TANU, yote
yaliyomfika ni kutokana na kutoa maoni yake, hatua waliyochukua ni
laana… laana ya Kingunge itawapata,” alisema Lowassa.
Lowassa alisema amefika Zanzibar kuomba wadhamini kwa sababu anataka kupambana na umaskini na anauchukia.
“Nilivyoona sipewi nafasi ya kupambana nao huko CCM nikaondoka,
niliondoka kwa maneno ya Mwalimu Nyerere (Baba wa Taifa) kwamba
Watanzania wanataka mabadiliko, wasipoyatapa ndani ya CCM watayapata
nje ya CCM, naifahamu Tanzania,” alisema Lowassa.
Akizungumzia kuhusu Katiba mpya, alisema tangu wakati wa G55 alikuwa
ni muumini wa Serikali tatu na kwamba hata kwenye Tume ya Jaji Wairioba
alisema hilo.
“Nilisema nataka Serikali tatu lakini Muungano ubaki, muungano huu
siyo wa uongozi ni wa watu. Nataka Muungano imara ndani ya watu imara,
Serikali tatu inayozingatia mahitaji ya watu sawa ya watu wa Zanzibar
na wale wa Bara,” alisema.
MTANZANIA
WANANCHI na wagombea udiwani wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) katika Kata nane za Manispaa ya Morogoro wamevamia
ofisi za chama hicho wakitaka ufafanuzi wa majina ya wagombea wa
udiwani waliokatwa wakiwa wameshinda katika kura za maoni.
Ghasia hizo zilizuka saa 9.00 mchana baada ya makundi ya
wagombea kutoka katika Kata za Kionda, Kichangani, Kilakala, Lukobe,
Mlimani, Boma, Mjimpya na Kiwanja cha Ndege kuvamia ofisi hiyo
kupata ufafanuzi wa sababu za majina yao kukatwa wakati wakiwa
wameshinda katika kura za maoni.
Wanachama walivamia gari la mwenyekiti wa Chadema wa wilaya na
kumzuia asiondoke hadi atakapotoa ufafanuzi wa madai hayo.
Mmoja wa wagombea aliyekatwa jina lake huku akiwa ameongoza
katika mchakato wa kura za maoni, Mwanahenzi Shaha alisema
ameshangazwa na hatua hiyo.
“Mimi katika Kata ya Mlimani nimeshinda kura za maoni lakini
nashangaa leo naambiwa jina langu hakuna na tayari ameteuliwa mtu
mwingine hii ni rushwa,” alisema huyo kwa hasira.
Mmmoja wa wanachama aliyekuwapo katika msafara huo
aliyejitambulisha kwa jina la Fiderik Boniface, alidai kitendo
cha viongozi wa wilaya na mkoa kukata baadhi ya wagombea kitaleta
madhara makubwa katika chama.
Juhudi za kuwapata viongozi wa Chadema ngazi ya wilaya na mkoa hazikuzaa matunda baada ya simu zao kutokuwa hewani jana.
MTANZANIA
LICHA ya Chama Cha Mpinduzi (CCM) kuamuru kurudiwa uchaguzi katika
baadhi ya majimbo yakiwamo yaliyokuwa yanaongozwa na mawaziri wa Rais
Jakaya Kikwete, hatimaye chama hicho kimewatosa rasmi.
Kutoswa kwa mawaziri hao kunatokana na kushindwa kwao kwenye kura za
maoni za marudio ambako pia wana CCM wamebwaga katika mchakato huo na
kusubiri hatima ya Kamati Kuu ya chama hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu wa
NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alisema baada ya kurudiwa uchaguzi
katika majimbo kadhaa hatimaye Kamati Kuu imefanya uteuzi wa mwisho huku
ikiwaweka kando mawaziri hao.
Alisema kikao kilichofanyika jana chini ya Mwenyekiti wa CCM, Rais
Jakaya Kikwete, kimefanya uteuzi huo kutokana na matokeo ya kura za
maoni.
Katika matokeo hayo ya kura za maoni, mawaziri waliojikuta
wakiangukia pua ni pamoja na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif
Rashid, Waziri wa Uvuvi na Maendeleo ya Mifugo, Dk. Titus Kamani na
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk. Binilith
Mahenge.
Nape alisema katika kikao hicho cha CC pamoja na mambo mengine,
kilikuwa na ajenda ya kupitisha majina ya wagombea katika majimbo
yaliyorudia uchaguzi pamoja na Uchaguzi Mkuu
“Tumepitisha majina ya wagombea katika majimbo tisa tuweze
kusimamisha wagombea kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba
mwaka huu,” alisema Nape.
Aliwataja wagombea waliopitishwa katika majimbo hayo kuwa ni
aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry (Ukonga), Edward Mwalongo
(Njombe Kusini) na Venance Mwamoto (Kilolo).
Wengine ni Profesa Norman Sigala (Makete), Dk. Raphael Chegeni
(Busega), Edwin Ngonyani (Namtumbo), Martin Msuha (Chilonwa), Joel
Makanyanga (Mbinga Vijijini) na Mohamed Mchengerwa (Rufiji).
Akizungumzia wanachama wa chama hicho wanaoendelea kulalamikia
matokeo ya kura za maoni, Nape alisema wagombea hao walipaswa kuandika
barua ya malalamiko yao kwa kamati kuu iweze kupitiwa na kutolewa
uamuzi.
“Hakuna malalamiko yaliyowasilishwa kwenye kamati hii ambayo
hayajafanyiwa kazi jambo ambalo lilisaidia baadhi ya majimbo kurudiwa
uchaguzi, hivyo basi wanachama wao wanapaswa kuacha malalamiko nje ya
vikao.
“Kama wanaona chama hakijawatendea haki na kwamba CCM haiwezi
kuwaletea maendeleo wanaweza kufanya uamuzi mgumu wa kujiunga na vyama
vya upinzani ambako wanaamini wanaweza kutendewa haki.
“Ikiwa kuna mwanachama ambaye anaona haki anaweza kuipata akiwa
upinzani na siyo CCM basi anaweza kwenda kutafuta hiyo haki, lakini kama
CCM hatushughuliki na malalamiko ya nje bali tunashughulika na matatizo
ya wananchi na malalamiko ya ndani ya vikao,” alisema.
NIPASHE
Aliyewahi Mbunge wa Mbinga Mashariki, Gaudence Kayombo (pichani),
ambaye aligombea Jimbo la Mbinga Vijijini mkoani Ruvuma, kupitia tiketi
ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kura za maoni, anadaiwa kudai
arudishiwe vifa vyake alivyokipatia Chama kwa ajili ya kampeni.
Kayombo alikwenda ofisi za CCM wilayani humo Agosti 14 na kutaka
arudishiwe vifaa vya matangazo, baada ya kushindwa kwenye kura za maoni
Agosti Mosi 2, mwaka huu.
Mmoja wa makada alisema Kayombo alichukua hatua hiyo akisema viongozi wa Chama wilaya hawamtaki.
Katibu wa CCM wilaya ya Mbinga, Zainabu Chinowa, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba wamesikitishwa na kitendo hicho.
“Tunajua kitendo cha kutunyang’anya vipaza sauti ni hasira baada ya
kushindwa, kwenye uchaguzi wa kura za maoni,” alisema Chinowa.
Alipotafutwa Kayombo, alisema kuwa madai hayo siyo ya kweli na
kueleza kuwa Chama kimekuwa kikiviazima vifaa vyake mara kwa mara kwa
kuwa yeye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec).
“Siku za kwanza za kampeni hawakuvitumia vipaza sauti vyangu,
walisema vimeharibika. Baadaye walinunua vipya na wakavipeleka majimbo
ya Mbinga Mjini na Vijijini,” alisema Kayombo na kuongeza:
“Majuzi nilikwenda nikakuta havijatunzwa vizuri , nikawaambia wanirudishie vifaa vyangu.”
Kadhalika, Kayombo alisema hakushindwa kura za maoni kwa kuwa matokeo ya kata mbili hayajajumuishwa.
Katibu wa CCM wa mkoa wa Ruvuma, Vellena Shumbusho, alisema amelazimika Chinowa kumkabidhi haraka Kayombo vifaa vyake anavyodai.
Alisema Kayombo alikuwa amevinunua na kuvikabidhi kwenye Chama kwa
ajili ya kusaidia matangazo wakati wa kampeni za kura za maoni Jimbo la
Mbinga Vijijini lilikuwa na wagombea ubunge nane waliochuana katika
kura za maoni.
Martin Msuha aliyeongoza kwa kura 13,354, Kayombo (12,068), Deodatus
Ndunguru (7,060), Humprey Kisika (545) na Dk. Silverius Komba (3,941).
NIPASHE
Hali ya hewa ndani ya Chama cha ACT- Wazalendo ambacho kinaongozwa na
Zitto Kabwe, imechafuka, baada ya Kamati Kuu kumpitisha na kumchukulia
fomu ya urais, Prof. Kitila Mkumbo, huku mwenyewe akisita kulipokea
jukumu hilo.
Kufuatia hatua hiyo, Prof. Kitila ameandika katika mtandao wa kijamii
kuwa hajaandaliwa kisaikolojia kupeperusha bendera ya chama hicho
katika nafasi ya urais na jukumu hilo wapewe viongozi wengine
waandamizi.
Tofauti na ilivyozoeleka kwa wagombea kwenda na wafuasi wao Tume ya
Taifa ya Uchaguzi (Nec) kuchukua fomu za kugombea urais, kwa upande wa
ACT – Wazalendo, Katibu Mkuu, Samson Mwigamba, jana alikwenda Nec
kumchukulia fomu Prof. Kitila ambaye inadaiwa viongozi wakuu wa chama
hicho wamekutana naye kwa mazungumzo ya kumshawishi akubali kupeperusha
bendera ya chama hicho kuelekea Ikulu.
Mapema asubuhi jana Prof. Kitila alifika ofisi za chama hicho
Kijitonyama na kuondoka na majira ya saa 5:00 asubuhi wafuasi zaidi ya
100 wakiwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali walivamia ofisi hiyo na
kumbana Mwigamba kuwaeleza kwanini chama hicho kinachelewa kuweka wazi
mchakato wa mgombea wake wa urais.
Habari zinasema kuwa licha ya Prof. Kitila kutokuwapo kwenye kikao
cha Kamati Kuu (CC) kilichopitisha uamuzi wa kumtaka apeperushe bendera
ya chama hicho katika nafasi ya urais, lakini ulipitishwa uamuzi wa
kwamba abebe jukumu hilo zito.
Wakati Kamati Kuu kiamua hivyo, hadi jana alasiri hapakuwapo na
makubaliano na Prof. Kitila, lakini viongozi wakuu wa chama walikuwa
kwenye mazungumzo naye.
Akizungumza na Nipashe jana, Mwigamba alisema alichukua fomu hiyo saa
4:00 asubuhi, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Kamati Kuu iliyokutana
Agosti 15, mwaka huu.
Alisema pamoja na azimio hilo, Kamati Kuu ilipitisha majina ya
wagombea ubunge nchi nzima, wagombea udiwani na kupokea ripoti ya
wataalamu washauri juu ya ushiriki katika harakati za uchaguzi wa rais.
“Baada ya kupokea taarifa na mapendekezo yao tukajiridhisha kwa
mustakabali wa taifa, chama kinahitaji kusimamisha mgombea urais, ndipo
nilipoagizwa kwenda kuchukua kwa sababu muda unaenda zianze kujazwa ili
Ijumaa ambayo ndiyo siku ya mwisho zirudishwe,” alisema Mwigamba.
Alisema Kamati Kuu imeamua hivyo kwa kuwa Prof. Kitila ni mwadilifu,
mzalendo wa kweli, anaweka mbele maslahi ya Taifa na kwamba ana sifa
zote za kuliongoza taifa na mgombea mwenza atakuwa ni Mwandishi wa
habari mkongwe, Hawra Shamte.
Hata hivyo, Hawra, alipoulizwa kuhusu maamuzi hayo ya Kamati Kuu,
alisema hana taarifa zozote na kwamba hadi jana jioni hakuarifiwa
chochote.
Alisema wakati mgombea huyo anakutana na viongozi wakuu wa chama
hicho, fomu hiyo itaendelea kusambazwa mikoani ili kusaka wadhamini na
kwamba walianza kufanya hivyo jana.
“Tofauti yetu na wengine hatutakuwa na ziara kwenye kusaka wadhamini,
nimeenda na wanachama wengine watatu kuchukua fomu na sikuwa na msururu
wa watu na hivyo hivyo kwenye kusaka wadhamini itakuwa kimya kimya,”
alisema Mwigamba.
Alipoulizwa juu ya utayari wa Prof. Kitila kupeperusha bendera hiyo,
alisema: “Hatuna wasiwasi, tunaamini atakubali uamuzi wa Kamati Kuu,
anajua ni wajibu kubeba jukumu chama kinapomuhitaji.”
Aidha, Mwigamba alisema kama itashindikana kwa Prof. Kitila, ni
lazima chama hicho kisimamishe mgombea mwingine katika nafasi hiyo.
KITILA: SINA MAANDALIZI
Katika kundi la mtandao wa kijamii la chama hicho la Whatsaap,
lijulikanalo kama ACT Taasisi Imara, Prof. Kitila aliandika taarifa ya
kuwashukuru wanachama na viongozi kwa imani yao kwake, lakini alisema
hawezi kubeba jukumu hilo.
“Naomba niwashukuru nyote kwa imani kubwa mliyonayo juu yangu katika
kukiwakilisha chama katika nafasi ya urais, naishukuru Kamati Kuu kwa
imani yake kwangu hata kufikia hatua ya kupitisha azimio la kuniomba
kugombea urais kwa chama chetu. Jana CC (Kamati Kuu) ilituma ujumbe
maalum nyumbani kwangu kwa ajili ya kuzungumza na familia na jamaa zangu
juu ya ombi hilo,” alisema katika andiko hilo na kuongeza:
“Nimekuwa nikitafakari tangu Alhamisi nilipoombwa rasmi kutafakari
uwezekano wa mimi kugombea baada ya juhudi zetu za kutafuta mgombea
kushindikana. Nimefanya mawasiliano mapana ndani ya familia, chama,
chuoni ninapofanyia kazi, kanisani kwangu na kwa watu na taasisi
mbalimbali ninazohusiana nazo.”
Alisema baada ya tafakari na mawasiliano mapana (consultations),
ameona hana utayari na maandalizi ya maana ya kisaikolojia, kifamilia na
kisiasa kumuwezesha kugombea nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu ujao.
“Najua nimewaangusha sana katika uamuzi wangu huu, lakini naamini
kwamba mtaheshimu uamuzi wangu na kwamba hamtaacha kuthamini mchango
wangu katika chama kwa sababu ya kukataa kugombea urais,” alisema na
kuongeza:
“Nasikitika kwa tuhuma ambazo baadhi ya wanachama wetu wanarusha
katika mitandao ya kijamii na sehemu nyingine. Nathamini na kuheshimu
haki ya wanachama kuonyesha hasira kwa jambo wasilolipenda…nawasihi
wanachama wajizuie kuzusha mambo yatakayochochea chuki ndani ya chama na
kukatishana tamaa.”
Aidha, alishauri wanachama wengine waandamizi waombwe wachukue jukumu
hilo na kuwataja kuwa ni Mwenyekiti wa ACT – Wazalendo na Katibu Mkuu,
Mwigamba na kwamba wakati hayo yakitafakariwa wasisahau malengo mapana
ya chama waliyojiwekea katika uchaguzi huo.
Alisema mafanikio waliyofikia ni kuweka wagombea ubunge na udiwani kata na majimbo mengi nchini.
Mwigamba alipoulizwa juu ya taarifa hiyo, alijibu: “Sina simu ya
whatsaap ila naenda kwenye kikao hadi leo (kesho) nitawapa taarifa.”
WAFUASI WAKUSANYIKA
Baadhi ya mabango yaliyokuwa yamebebwa na wanachama na wafuasi wa
ACT-Wazalendo yalikuwa na ujumbe wa ‘wamenunuliwa’ na mgombea wa
Chadema, Edward Lowassa ili wasisimamishe mgombea urais.
Wafuasi hao walikaa kwa saa nne nje ya ofisi hizo wakiimba nyimbo mbalimbali.
HABARILEO
MKAZI wa Chuo, tarafa ya Shimbi Kwandele wilayani Rombo, Kilimanjaro,
Fidensia Salvatory (27) anashikiliwa na Polisi mkoani hapa kwa tuhuma
za kumuua kwa kumnywesha sumu mwanawe wa miezi sita kwa madai ya kukerwa
na wakwe zake.
Mwanamke huyo anadaiwa kumnywesha sumu ya panya mwanawe huyo kama
sehemu ya kupunguza hasira zake baada ya kukerwa na manyanyaso kutoka
ukweni anakoishi na mumewe.
Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Fulgence Ngonyani alisema tukio
hilo limetokea Agosti 15 mwaka huu majira ya saa 8.30 mchana nyumbani
kwa wazazi wa mtoto huyo.
Akielezea tukio hilo Kamanda Ngonyani alisema siku ya tukio baba
mzazi wa mtoto huyo, Salvatory Baltazary alifika nyumbani kwake majira
ya mchana na kukuta mwanawe akiwa amelala kitandani akiwa anatokwa na
povu mdomoni na puani hali iliyoashiria kupata madhara.
Alisema baada ya kuona hali hiyo alitoa taarifa Polisi ambao walifika
nyumbani hapo na kumpeleka mtoto hospitali huku wakiokota baadhi ya
vitu vilivyokuwa vimehifadhi sumu hiyo.
Kamanda Ngonyani alisema askari hao walikuta pakiti iliyokuwa na unga unaodhaniwa sumu ya panya iliyotumika kumuua mtoto huyo.
Alisema Polisi ilimkamata mtuhumiwa na baada ya mahojiano alikiri
kumpa sumu mtoto wake kwa madai ya kuchoshwa na manyanyaso kutoka kwa
wakwe zake.
HABARILEO
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesisitiza kuwa kitashinda Uchaguzi Mkuu
mwaka huu kwa sababu kina mtandao mkubwa wa wanachama kuanzia ngazi ya
chini na kwamba kufurika kwa wananchi katika mikutano ya Mgombea Urais
wa Chadema, Edward Lowassa sio ushindi, kikisema kura ni mahesabu.
Aidha, kimesema kuwa mgombea huyo wa Chadema na umoja wa vyama vinne
vya upinzani (Ukawa), amedanganywa na wapambe wake kuihama CCM na
kumkejeli ikisema gari la wagonjwa linapaswa kuwekwa nyumbani kwake siku
ya uchaguzi kwani CCM itapata ushindi wa uhakika asubuhi.
Akitoa taarifa kuhusu kikao cha Kamati Kuu kilichofanyika jana katika
Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Mtaa wa Lumumba, Dar es Salaam,
Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alisisitiza kuwa ushindi wa
chama hicho tawala na kikongwe hauna shaka kutokana na mtandao wake
kuanzia ngazi ya chini.
Akijibu swali kuhusu kufurika kwa wananchi katika mikutano ya mgombea
huyo wa Chadema, Nape alisema: “Kwa walioanza siasa jana ndio
watashituka. Mwaka 2010 Slaa (Dk Willibrod) katika mkutano wake wa
mwisho wa kampeni Mbeya alipata watu wengi kuliko wale aliopata Edward.
Lakini kura alizopata Mbeya utashangaa. “Kupata watu wengi mkutanoni
hakutushangazi kwani kura ni mahesabu, hawa (Chadema na mgombea wao)
wanatoka pointi moja kwenda nyingine. CCM ina mtandao, ukiondoka mjumbe
wa nyumba kumi anapitia watu wake anasafisha nyayo zenu,” alisema
kiongozi huyo.
Nape aliongeza kuwa wapinzani wote wametoka ndani ya CCM kuanzia kwa
Augustino Mrema mwaka 1995 na hadi katika chaguzi nyingine zilizofuta na
zote wapinzani walishindwa, na hata safari hii CCM itashinda.
Akimgeukia Lowassa, Nape alisema Waziri Mkuu huyo aliyejiuzulu kwa
kashfa ya zabuni ya kampuni ya kufua umeme ya Richmond, amedanganywa na
wapambe wake na kuondoka chama tawala, na kwamba licha ya kuhamia huko,
CCM itamshinda asubuhi na kuwataka wanaotishia kukihama kufanya hivyo na
si kuleta shinikizo.
“Katika mchakato wa uchaguzi si wote watakaoridhika na matokeo kwa
sababu kuna wengi wanajiandaa kushinda na sio kushindwa, na matokeo
yanapokuwa hivyo, wanakuwa hawaridhiki na hapo ndipo wanazungumzia
kwenda upande wa pili, na hasa kwa shinikizo la wapambe.
“Hili limetokea kwa Edward, amekwenda upande wa pili, amedanganywa na
watu, tutampiga. Ushindi wa CCM ni wa uhakika, sio wa matumaini.
Matumaini yapo Angaza, CCM ni ya uhakika. Tutashinda asubuhi. Tumesema
ni mpambano kati ya wagombea na makapi,” alisema Nape na kuongeza: “Zipo
mechi ambazo unajua hii utashinda. Yanga na Lipuli ya Iringa unajua
matokeo yake.
Tunataka mgombea mwenzetu apelekewe ambulance (gari la wagonjwa)
nyumbani kwake, kwani ushindi kwetu ni uhakika.” Kuhusu wanaolalamika na
kutishia kuhama, alisema malalamiko hayawezi kutolewa barabarani kwani
chama hicho kina utaratibu wake na yale yote yaliyolalamikiwa yakiwamo
ya udiwani, yamefanyiwa kazi. “Tulisema wakati ule wa mchakato wa
kutafuta mgombea wa urais kuwa hatutafanya kazi kwa shinikizo.
Tunajua uimara wa chama chetu, kama kuna watu wanataka kwenda upande
wa pili waende. Lakini CCM haiwezi kufanya kazi kwa vitisho na
shinikizo. Tatizo ni kwamba kunatokea wagombea 12, halafu unasema lazima
uwe wewe. Kuna watu (wanaotaka kuhama) wanafanya hivyo kwa shinikizo la
viroba na hela,” alisema Nape.
HABARILEO
MUIMBAJI maarufu hapa nchini wa nyimbo za Injili, Rose Muhando
anatafutwa na waandaaji wa tamasha la Injili wilayani Simanjiro mkoani
Manyara kwa madai ya kutoonekana kutumbuiza kama jinsi walivyokubaliana.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Zephania Simoni ambaye ni
Mjumbe wa Kamati ya Uratibu alisema wameingia hasara ya Sh milioni 4.3
kutokana na tamasha hilo kuvurugika baada ya kutapeliwa na Muhando.
Alifafanua kuwa tayari walikuwa wameishamkabidhi kiasi cha Sh
1,700,000 muimbaji huyo na ameshindwa kufika na hivyo kuonesha wazi kuwa
amewatapeli.
Alisema wameamua kuripoti tukio hilo kituo cha Polisi cha wilayani
humo na kupewa RB namba ORK/RB 395/2015 kwa Rose na kuanza kumsaka
popote alipo ili kukabiliana na kesi hiyo wilayani Simanjiro.
Wameshangazwa kwa mtumishi huyo wa Mungu kujiingiza katika masuala ya
kutapeli na ndio maana wameamua kuchukua hatua za kisheria.
Awali, alisema siku ya tamasha wakati wakiwa wanamsubiri siku moja
kabla ya tamasha alisema yupo njiani anakuja majira ya mchana mtu mmoja
aliyejitambulisha kwa jina la Lucas alitupigia simu na kutuambia Rose
hatakuja yupo kwa mgombea Urais anasaini mikataba ya kumnusuru katika
kusaidia kampeni, “ alisema Simon.
Akafafanua kuwa baada ya kupata taarifa hiyo na kuingia shaka
walianza kumtafuta Muhando bila mafanikio kupitia simu yake ya kiganjani
siku nzima hadi anatoa taarifa hii hawajawahi kuwasiliana naye.
Akionesha vielelezo vya makubaliano na jinsi fedha zilivyotumwa kwa
Rose, inaonesha kwa nyakati tofauti kuanzia Aprili 4 amekuwa akitumiwa
fedha hizo kwa ajili ya tamasha na hatimaye mkataba aliosaini Rose
Muhando Julai 7 mkoani Dodoma kuthibitisha kuchukua Sh milioni 1.5 kwa
ajili ya tamasha hilo na baadaye kutumiwa Sh 200, 000 kwa ajili ya
kwenda Simanjiro.
Hata hivyo, Muhando alipopigiwa simu na mwandishi wa habari hizi ili
kuthibitisha madai hayo simu yake iliita na wakati mwingine ilikuwa
‘busy’ na baadaye kwa mara ya nne ilipokelewa na mtu aliyejitambulisha
kuwa ni mdogo wake, lakini hakutaka kujitambulisha na alipoulizwa juu ya
madai haya alisema Rose ni dada yake hivyo akija atamwambia apige simu.
“Rose ni dada yangu na haya madai ndio tunayasikia na siwezi
kuzungumzia suala hili kwa sasa kwani mimi ni mdogo wake, lakini
nimesikia ila akija ntamwambia akupigie kisha akakata simu lakini sauti
ilisikika kama ya Rose mwenyewe”.
Hivi karibuni mwanamuziki huyo alikuwa akidaiwa Sh 6,000,000 na
alilipiwa na promota mashuhuri wa nyimbo za Injili Alex Msama ambaye
mara nyingi wamekuwa wakifanyakazi pamoja.
MAJIRA
UGONJWA wa kipindupindu umeripotiwa katika Jiji la Dar es Salaam na
watu wawili wamethibitika kufa. Wengine zaidi ya 30 wamelazwa katika
hospitali za Mwananyamala na Sinza zilizopo Manispaa ya Kinondoni.
Kutokana na tishio la ugonjwa huo, shughuli za kampeni za kisiasa za
uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu wa Rais, wabunge na madiwani, zilizo
kuwa zianze mwishoni mwa wiki hii, zimesogezwa mbele. Mkuu wa Mkoa wa
Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki alithibitisha hayo jana alipokuwa
akitoa taarifa ya ugonjwa huo kupitia Kituo cha Televisheni ya Taifa
(TBC 1).
Alisema watu hao wawili waliofariki, mmoja ni mwanamume na mwingine
ni mwanamke na wanatoka Manispaa ya Kinondoni. Mkuu huyo wa Mkoa alisema
ugonjwa huo umethibitika baada ya vipimo vya maabara vya watu hao,
kuthibitisha.
“Watu wawili akiwemo mwanamume na mwanamke wamefariki dunia baada ya
vipimo vya maabara kuthibitisha ugonjwa huo. Hata hivyo, hakuna taarifa
zozote za ugonjwa huo katika manispaa za Temeke na Ilala,” alisema
Sadiki.
Alisema endapo hali hiyo itaendelea kuwa mbaya, itabidi mamlaka za
Dar es Salaam kusogeza mbele kampeni za kisiasa, zinazotarajiwa kuanza
mwisho mwa wiki hii ili kuepusha mikusanyiko ya watu.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Mussa Natty, alisema wagonjwa
wengine 30 wapo chini ya uangalizi maalumu katika hospitali za
Mwanayamala na Sinza, ambapo 19 wapo Sinza na 11 Hospitali ya
Mwananyamala. Wengine wanne wameruhusiwa na kurudi nyumbani.
“Sampuli za wagonjwa sita zilizochukuliwa, wanne kati yao wamethibitika kuwa na vimelea vya ugonjwa huo,” alisema Natty.
Alisema wamepata dawa kutoka Bohari Kuu ya Dawa nchini (MSD) kwa
ajili ya kukabiliana na ugonjwa huo. Jitihada mbalimbali zinaendea
kuchukuliwa ikiwemo kupulizia dawa kwenye madimbwi ya maji.
Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam, Dk Jackson Makanjo,
aliwataka wakazi wa Dar es Salaam kuchukua tahadhari, ikiwemo kunawa
mikono kwa sabuni kabla ya kula, na unapotoka chooni. Alitoa wito kwa
wakazi wa Dar es Salaam, kuhakikisha wanachemsha maji ya kunywa na
kuepuka kula ovyo vyakula vya mitaani.
Alisema ugonjwa huo ulianzia eneo la Kwa Ali Maua huko Kijitonyama na
kisha kuenea maeneo ya jirani ya Tandale, Manzese na Mwananyamala.
Kwa habari, matukio na michezo ni hapahapa tangakumekuchablog
No comments:
Post a Comment