Uchambuzi huu wa magazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu Cha Candle Education Centre Tanga. Kituo kinaongoza kufaulisha wanafunzi kidato cha pili hadi cha sita na wanaojiendeleza kielimu. Kituo kinatoa kozi mbalimbali za kielimu na kitaaluma. Wapo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 772746

MWANANCHI
Mawakala wanaoandikisha vitambulisho vya wapigakura kwa kutumia mfumo wa Biometric Voter Registration (BVR), katika Kituo cha Shule ya Msingi Umoja, wamegoma kuendelea na uandikishaji kwa madai ya kutolipwa posho.
Akizungumza kwa niaba ya mawakala wenzake katika manispaa ya Kinondoni, Yusufu Msigiti alisema mkataba wao uliisha jana, lakini walipewa malipo ya siku sita badala ya kumi.
Alisema hata walipofuatilia waliambiwa wanapaswa kulipwa na manispaa au Serikali ya kata.
Hata hivyo, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mabibo, Paul Ngunga
 alidai kuwa alikaa kikao na mawakala hao akawaeleza kuwa katika 
manispaa hiyo, fedha iliyotoka ni ya siku sita tu, hivyo waendelee kuwa 
na subira.
“Sehemu
 nyingine mawakala wanaendelea na kazi, hawa ndiyo hawajaelewa, 
wamegoma…. nimeshaleta mawakala wengine na wanaendelea na kazi ya 
kuandikisha wananchi,” alieleza Ngunga. Hata hivyo, Msigiti alisema: 
“Hatujawahi kulipwa na watu hao, lakini tunashangaa mtendaji wa kata 
anatuambia tuende huko, fedha yenyewe wanayotulipa ni ndogo tunafanya 
kazi ngumu kuanzia saa moja asubuhi hadi saa 12 jioni.”
Msigiti alisema mtendaji huyo aliwajibu 
vibaya baada ya kumhoji kuhusu posho zao za siku nne ambazo hawajalipwa 
badala yake aliwaambia anayetaka kazi aendele na asiyetaka aache.
Mawakala hao wamemtupia lawama mtendaji huyo kwa majibu yake ilihali wana malalamiko ya msingi.
Walisema hakukuwa na haja kwa mtendaji huyo kuita polisi kwa lengo la kuwazuia mawakala hao kudai haki yao.
Wakala Peter Mnyika alisema polisi 
walivyofika eneo hilo walimpiga mwandishi wa habari aliyekuwa eneo hilo 
na kumzuia kukusanya taarifa zake.
“Alikuwa
 amevaa kitambulisho na alijitambulisha baada ya kuona vurugu zinazidi 
lakini askari mmoja wa kiume alimkunja mwandishi huyo na baada ya kuona 
waandishi wenzake wamefika na kamera alikimbilia ofisi ya mwalimu mkuu 
na hajatoka mpaka sasa,” Mnyika.
Mwandishi aliyepigwa ambaye hakutaka 
kutaja jina lake alisema askari ndiyo wamekuwa wa kwanza kumzuia kufanya
 kazi yake badala ya kumpa ushirikiano.
Yusufu Kileme alikiri mtendaji wa kata kutumia lugha mbaya wakati mawakala wakidai haki yao.
Pia, alisema askari wanaofika eneo hilo wanapaswa kuangalia anafanya fujo ili wazuie, na siyo kuwa chanzo cha vurugu.
Mwenyekiti wa kata hiyo, Saimoni Ramo 
alisema askari walipofika aliwasihi wasitumie nguvu kwa sababu 
malalamiko ya vijana hao ni ya msingi.
MWANANCHI
Wakati Mwenyekiti wa Chama cha Democratic Party (DP), Christopher Mtikila akigoma kusaini fomu za kugombea urais akitaka ufafanuzi wa mgombea binafsi, Mwenyekiti wa UPDP, Fahmi Dovutwa amekwama kwenye lifti za jengo lililopo katika Ofisi za Tume ya Uchaguzi (NEC) kutokana na kukatika umeme.
Mchungaji Mtikila ambaye aliambatana na 
mgombea mwenza Juma Metu Juma, alitaka ufafanuzi wa kutokuruhusiwa 
kuwania urais akiwa mgombea binafsi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 
wakati Mahakama ya Haki za Binadamu ya Afrika (AfCHPR) imeruhusu.
“Siondoki
 hapa na wala sitaweza kuchukua hizi fomu hadi mniambie ni wapi nitapata
 jibu la tume la kukiuka maagizo ya mahakama ya Afrika.
“Waandishi
 embu subirini kwanza mkurugenzi wa uchaguzi aje hapa ilia atoe 
ufafanuzi na nyie msikilize mkaandike ukweli kwa sababu hii siyo haki ni
 sawa na kudharau mahakama,” alisema.
Baada ya kuzozana na maofisa waliokuwa 
wakimkabidhi fomu hizo, walilazimika kumuita mkurugenzi wa uchaguzi 
Kailima Ramadhani, ambaye alimwambia kwamba sheria hairuhusu.
“Sisi
 tunafuata sheria mwenyekiti kama hicho kipengele kingekuwapo 
tungekuruhusu uchukue fomu hizo, lakini hapa tunabanwa na sheria 
tunaruhusu kutoa fomu kwa watu wanaotoka kwenye vyama vyao,” Ramadhani
Alisema ni vizuri Mtikila angefuatilia 
kwa makini suala hilo ili sheria ipitishwe kwani NEC wanachokifanya ni 
kufuata sheria zilizopo tu na si vinginevyo.
Baada ya kumaliza maongezi Mtikila 
aliamua kuweka sahihi na kuchukua fomu hizo kwa shingo upande huku 
akisema atakiwakilisha vyema chama chake hicho.
Juni 13,2013 Mtikila alishinda kesi 
aliyofungua AfCHPR, mjini Arusha akidai Tanzania inakiuka demokrasia 
inapozuia wagombea binafsi.
Mchungaji Mtikila, ambaye ana historia 
ndefu ya kukwaruzana na Serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM), alifungua
 shauri mahakama ya Afrika mwaka 2011 baada ya jitihada zake za kupindua
 mabadiliko ya kikatiba yaliyofuta ugombea binafsi kugonga mwamba kwenye
 mahakama za kitaifa.
MWANANCHI
 Kada mpya wa Chadema, Edward Lowassa
 jana amerejesha fomu ya kuwania urais, huku akifanikiwa kupata 
wadhamini milioni 1.6, zaidi ya nusu ya kura za urais ambazo chama hicho
 kilipata kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka 2010.
Naibu katibu mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu
 alisema idadi hiyo ya wadhamini inaashiria ushindi wa kishindo, kwa 
maelezo kuwa inakaribia idadi ya kura alizopigiwa katibu mkuu wa chama 
hicho, Dk Willibrod Slaa alipogombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka
 2010.
Katika Uchaguzi huo, Dk Slaa alishika 
nafasi ya pili baada ya kupata kura 2,271,941 sawa na asilimia 26.34, 
huku Rais Jakaya Kikwete akipata kura 5,276,827 sawa na asilimia 61.17.
Lowassa alipochukua fomu za kuomba 
kuteuliwa kuwania urais kwa tiketi ya CCM, kabla ya kuhamia Chadema, 
alidhaminiwa na wanachama 870,000 nchi nzima.
Dk Slaa, ambaye hajaonekana hadharani 
tangu Lowassa ajiunge Chadema, jana hakuwapo kwenye ofisi za chama hicho
 wakati mbunge huyo wa Monduli alipokuwa akirejesha fomu.
Hakuna kiongozi aliyekuwa tayari kuzungumzia suala lake, lakini baadhi ya maofisa wa Chadema walisema wanaendelea kuchapa kazi.
Kama ilivyokuwa juzi katika hafla fupi 
wakati Lowassa akichukua fomu, umati mkubwa ulifurika na kusababisha 
Mtaa wa Ufipa uliopo Wilaya ya Kinondoni kufungwa, watu walijazana tena 
na safari hii umati huo ukiwa umebeba mabango ya kumsifu Waziri Mkuu 
huyo wa zamani.
Katika hafla ya jana, makamu mwenyekiti 
wa Chadema-Bara, Profesa Abdallah Safari alieleza jinsi Chadema 
ilivyojipanga kuchukua nchi na siyo kushinda ubunge na udiwani pekee na 
kwamba Lowassa amebakiza hatua mbili tu kuingia Ikulu, jambo walilodai 
kuwa limeichanganya CCM.
Wakati Lowassa ambaye alitangaza rasmi 
kujiondoa CCM na kujiunga na Chadema Julai 28 mwaka huu akisubiri 
kupitishwa na Mkutano Mkuu wa chama hicho utakaofanyika Agosti 4, habari
 za ndani zinaeleza kuwa vigogo kadhaa wa CCM watatambulishwa katika 
mkutano huo.
Habari hizo zinaeleza watakaotambulishwa
 siku hiyo ni wenyeviti wa CCM wa mikoa, wilaya na waliokuwa wabunge wa 
chama hicho ambao wanamuunga mkono Lowassa.
Jana Lowassa, aliyekuwa amevaa shati 
jeupe na suruali nyeusi na aliyekuwa katika gari aina ya Toyota Land 
Cruiser VX, alifika makao makuu ya Chadema saa 9:35 alasiri akiwa pamoja
 na familia yake na alipokewa na umati mkubwa wa watu waliokuwa wamebeba
 mabango yenye ujumbe mbalimbali.
Baadhi ya ujumbe huo ni “Chini ya 
Lowassa umaskini haupo”, “Kwa Lowassa hata maskini atapata ajira” na 
“Kingunge Ngombare-Mwiru karibu Ukawa”. Kingunge ni kada mkongwe wa CCM 
na anamuunga mkono Lowassa.
Mbali na kubeba mabango, watu hao 
walikuwa wakiimba nyimbo mbalimbali za kumsifu Lowassa na kushangilia 
pale ilipokuwa ikitajwa mikakati ya chama hicho kushika dola.
Akieleza taratibu na kanuni za kudhamini
 mgombea urais, mkurugenzi wa Oganaizesheni na Mafunzo wa chama hicho, 
Benson Kigaira alisema mgombea urais anatakiwa kudhaminiwa na wanachama 
wasiopungua 200.
“Naamini
 fomu za Lowassa zitakuwa na idadi hiyo ya wadhamini. Ila baada ya 
mgombea kuchukua fomu jioni yake wanachama wa Chadema, wapenzi na 
Watanzania walifurika katika ofisi za Kanda, mikoa na majimbo nchi nzima
 wakiomba kumdhamini,” Kigaira.
Alisema wanachama hao walidhani fomu 
hizo zimepelekwa kila mkoa, kutokana na kuepuka kuwanyima fursa hiyo 
chama hicho kilipeleka fomu ili wanachama wamdhamini na kupewa masharti 
kuwa lazima wawe wamejiandikisha kupiga kura, wataje namba zao za simu.
HABARILEO
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
 (TAKUKURU) LINDI, imekanusha tuhuma za rushwa zilizoelezwa na baadhi ya
 vyombo vya habari dhidi ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri 
Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC-CCM), Nape Nnauye.
Kamanda wa Takukuru mkoani hapa, Steven Chami
 alisema, taasisi hiyo haikumkamata Nape kwa sababu ya kuhusika na 
rushwa, bali ilitaka kujiridhisha na kiwango cha fedha kilichokuwa 
kikitolewa kwa mawakala.
Alisema, “Uhakiki
 ulifanywa kwa watu wote walioomba ridhaa ya kugombea nafasi mbalimbali 
mkoani humu, ikiwa ni pamoja na ubunge, ambao Nnauye na wengine 
waliomba.”
Kutokana na maelezo yake, Nape alikuwa 
miongoni mwa wanasiasa walioomba ridhaa ya CCM kugombea ubunge katika 
jimbo la Mtama, na alikuwa pia miongoni mwa watangaza nia walioingia 
kuchukua fedha katika Benki ya NMB ya mjini hapa, iliyotajwa na vyombo 
vya habari.
Alifafanua kuwa, kitendo cha maofisa wa 
Takukuru kumfuata Nnauye ili wajiridhishe na kiwango cha fedha 
alichokitoa kwa ajili ya mawakala, kilichukuliwa kuwa ni kumkamata kwa 
rushwa jambo ambalo si kweli.
“Vijana
 wangu walimuomba Nnauye aongozane nao hadi ofisini ili wahakiki kiasi 
cha fedha alichokuwa amekitoa benki. Alifanya hivyo na kutumia dakika 
kati ya 30 na 45 kutoa maelezo yaliyowaridhisha maofisa wa Takukuru 
waliomwachia baada ya mahojiano mafupi. “…Ninapenda kuwathibitishia 
kuwa, Nnauye alikuwa na kiwango cha kawaida cha fedha ambacho 
kinaruhusiwa kutolewa kwa mawakala. Haikuwa rushwa kama ilivyopotoshwa 
na baadhi ya wanahabari walioandika na kutangaza habari hiyo,” Chami alisema na kuongeza kuwa alikutwa na Sh milioni tatu tu.
Alisema, Nnauye aliieleza Takukuru kuwa 
fedha hizo zilikuwa kwa ajili ya kuwalipa mawakala wake 156, aliowaandaa
 kusimamia uchaguzi katika vituo vyote jimboni humo.
HABARILEO
Mchoraji maarufu katika Mji wa Namanyere wilayani Nkasi, Gilbert Paul,
 ambaye alishaanza kujiandalia maziko kwa zaidi ya miaka 15 sasa akiwa 
hai buheri wa afya, anatarajia kuanza kujichimbia kaburi miezi mitatu 
ijayo, ili liwe tayari kuhifadhi mwili wake mara mauti yatakapomfika.
Kijana huyo ambaye amekuwa gumzo mjini 
Namanyere na kwingineko, amedai alianza kujiandalia maziko yake kwa 
kujichongea msalaba mkubwa na kuusimika juu ya paa la kibanda chake 
kilichopo katika Mtaa wa Sasala mjini Namanyere.
Msalaba huo mweupe mkubwa umeandikwa 
tarehe aliyozaliwa Desemba 24, 1977 lakini kufa ameweka alama ya ulizo, 
huku baadhi ya wageni wanaotembelea mtaa huo wakidhani ni nyumba ya 
ibada na wengine wakifikiri ni kaburi la mtu mashuhuri.
“Wageni
 wanapoona msalaba huu kwa mara ya kwanza ukiwa umesimikwa juu ya 
kibanda hicho, hudhani kuwa ni kaburi kubwa alimozikwa mtu maarufu au 
mtawala maarufu wa kimila, kwani kipo katikati kabisa ya mji huu,“ alisema Jackson Nkwabi mkazi wa mjini humo.
Nkwabi alisema msalaba uliopakwa rangi 
nyeupe kwa maandishi meusi, umekuwa kivutio cha aina yake kwa wageni 
wanaofika mjini hapo ambao ni mara yao ya kwanza kuuona.
Akizungumza na gazeti hili juzi mjini 
Namanyere, Paul alisisitiza kuwa msalaba huo ndio utakaosimikwa katika 
kaburi lake ambalo anatarajia kuanza kulichimba Oktoba mwaka huu.
Alisema yuko katika harakati za 
kukusanya fedha anazodai kutoka kwa wasitiri wake, ili ifikapo Oktoba 
mwaka huu, aanze maandalizi ya kuchimba kaburi ambalo atazikwa mauti 
yatakapomkuta.
“Ningekuwa
 nimekaribia kuchimba na kusakafia kaburi langu hilo lakini 
kinachonikwamisha ni baadhi ya wateja niliowafanyia kazi… nawadai 
hawajanilipa wameniahidi kunilipa baadaye mwezi huu wa Agosti,” alisema.
Hii kazi ya uchimbaji wa kaburi 
nitaianza Oktoba mwaka huu, ikiwa ni pamoja na kusakafia na kuwekea 
nakshi…kaburi langu natarajia ligharimu si chini ya Sh milioni moja 
kisha nitatengeneza jeneza litakalo gharimu zaidi ya Sh milioni moja,” 
alisema.
Akizungumzia msalaba huo, aliousimika 
kwenye kibanda chake cha kazi, Paul alisema aliutengeneza mwenyewe kwa 
gharama ya Sh 40,000.
Paul aliyehitimu kidato cha nne katika 
Shule ya Sekondari Nkasi mjini Namanyere mwaka 2001, ameoa mke, 
Paschalia Salvatory (26) na wamejaliwa mtoto wa kike.
Baadhi ya wakazi wa mjini humo na 
kwingineko wanaamini kuwa Paulo anafahamu siku atakayofikwa na umauti, 
huku wengine wakimwona amechanganyikiwa, lakini mwenyewe akidai kuwa na 
akili timamu na kwamba hajui lini atafikwa na mauti na kwamba anaamini 
ataishi miaka mingi ijayo.
HABARILEO
Tume ya Uchaguzi (NEC),
 imesema imeandikisha zaidi ya watu milioni 21 nchini tangu uandikishaji
 uanze Februari 23, mwaka huu na kwamba, Dar es Salaam pekee, 
wameandikishwa watu zaidi ya milioni mbili.
Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji mstaafu Damian Lubuva
 alisema juzi Dar es Salaam kuwa, uandikishaji wa wapiga kura katika 
Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa mfumo wa Biometric Voters 
Registration (BVR) unaendelea jijini humo hadi Agosti 8.
Kwa mujibu wa Jaji Lubuva, baada ya siku hizo zilizoongezwa, hakutakuwa na muda mwingine utakaoongezwa.
“Tumieni
 muda ulioongezwa kujiandikisha, vinginevyo mtaikosa haki yenu ya kupiga
 kura kwa sababu ya kutoandikishwa katika Daftari la Wapigakura,” Jaji Lubuva alisema.
JAMBOLEO
Kura za maoni ndani ya Chama Cha 
Mapinduzi (CCM), zimefanyika kwa utulivu katika maeneo mengi nchini, 
huku baadhi ya maeneo kukiibuka hitilafu zilizosababisha baadhi ya 
wanachama kulala mahabusu.
Mbali na kura hizo za ndani ya CCM 
zilizopigwa jana nchi nzima, ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo 
(Chadema), kutokuwepo kwa mmoja wa wagombea wa ubunge katika jimbo jipya
 la Kibamba, kumesababisha chama hicho kuahirisha uchaguzi.
Mkoani Arusha Katibu wa CCM Kata ya Mjini Kati jijini Arusha, Ally Meku na Katibu wa tawi wa CCM katika kata hiyo, Yakub Shamban wametiwa mbaroni na Polisi, baada ya kukutwa na karatasi za kupigia kura za ubunge na udiwani nyumbani wakipiga tiki.
Meku na mwenzake walitiwa mabaroni 
majira ya saa sita mchana wakati kazi ya kupiga kura ikiendelea katika 
ukumbi wa CCM Mkoa, kutokana na ofisi ya kata hiyo kuungua kwa moto siku
 chache zilizopita.
Akithibitisha kukamatwa kwa makada hao, 
Katibu wa CCM Wilaya ya Arusha, Feruz Banno alikiri kukamatwa kwa 
wanachama hao na kuongeza kuwa alikwenda Kituo Kikuu cha Polisi kupata 
taarifa lakini ilishindikana kuwawekea dhamana.
“Ni
 kweli wametiwa mbaroni na Polisi tangu saa sita mchana… nimefika Kituo 
cha Polisi na nitafuatilia dhamana zao baada ya uchaguzi ndani ya chama 
kumalizika,”  Banno.
Alipoulizwa kwa nini katibu huyo 
alipeleka karatasi nusu kituoni na nyingine kubakiza nyumbani kwake, 
alisema amefanya kosa kwa kukiuka taratibu za uchaguzi na maelekezo 
aliyopewa kwa kuwa walikubaliana kila kitu kifanyike hadharani.
Akizungumzia tukio hilo kwa njia ya simu
 yake ya kiganjani, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, alisema hana 
taarifa rasmi kwa kuwa yupo nje ya ofisi.
Mkoani Mbeya hali ilikuwa shwari isipokuwa kasoro chache zilizojitokeza kwenye baadhi ya maeneo.
NIPASHEWakati uvumi wa kujiuzulu cheo na kujivua uanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Wilbroad Slaa, ukiwa umetawala kupitia mitandao ya kijamii na magazeti, taarifa zinadai kuwa sababu ya kuchukua hatua hiyo ni shinikizo kutoka kwa mkewe.
Taarifa zilizochapishwa na gazeti moja likimnukuu Dk. Slaa mwenyewe, zilisema ameachana na siasa na kujivua wadhifa wake na atabaki kufanya shughuli zingine.
Dk. Slaa amedaiwa hakubaliani na namna chama chake kilivyompokea Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa.
Lowassa aliyekuwa Mbunge wa Monduli alitangaza kuhamia Chadema, Julai 28, mwaka huu baada ya kutoridhishwa na mchakato wa CCM wa kumpata mgombea wa urais.
Habari za uhakika kutoka vyanzo vyetu vya habari ndani ya Chadema zinadai, Dk. Slaa alishiriki katika mchakato mzima wa kumpokea na kuridhia Lowassa, kusimamishwa kuwa mgombea urais kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Hata hivyo, chanzo kingine cha habari kinadai kuwa mke wa Dk. Slaa, Josephine Mashumbusi, alitoa shinikizo kwa mumewe la kujiuzulu baada ya kuruhusu kusimamishwa mgombea mwingine (Lowassa).
“Josephine alikuwa na uhakika mume wake ndiye atakayesimama ugombea urais kwa upande wa Ukawa, hali ilivyobadilika, akakasirika na kumwambia mumewe ama yeye au Chadema,” chanzo kilidokeza.
Kupitia ujumbe uliosambaa kwenye mitandao ya kijamii, unaoonyesha kutoka kwa Mashumbusi, aliandika “Ni kweli Frida na kwa hili Dk. Slaa amejivua wadhifa wake wa ukatibu mkuu na kuachana na siasa.
Hata hivyo, Dk. Slaa alipotafutwa kupitia simu yake ya mkononi kuthibitisha madai hayo, iliita mara moja na kuzimwa. Juhudi za kumpata ziligonga mwamba baada ya simu yake kutopatikana hali kadhalika simu ya Mashumbusi.
Baadhi ya wasomi walisema kama Dk. Slaa amejiuzulu nafasi yake na kujivua unachama atakuwa amejijengea heshima na uaminifu na kwamba Chadema kitapata pigo.
Mhadhiri wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, alisema kwa upande wake aliamini kitu kama hicho kitatokea kutokana na tukio hilo kuwa la haraka na kulifananisha sawa na mapinduzi ya ghafla ndani ya chama.
Mhadhiri huyo alisema anaamini Slaa aliweza kukifufua chama hicho mwaka 2010 kwa kuweka misingi yake ya kukemea ufisadi, hivyo hawezi kurudi nyuma kwa kuivunja.
Dk. Kitlya Mkumbo kwa upande wake alisema anaheshimu maamuzi ya pande zote mbili kwani zinaonyesha demokrasia na ukomavu wa kisisa.
Septemba 15 mwaka 2007 katika viwanja vya Mwembe Yanga jijini Dar es Salaam, Dk. Slaa alimtaja Lowassa kuwa miongoni mwa mafisadi 11 waliochota fedha Benki kuu katika akaunti ya Epa.
Kauli hiyo alikuwa akiitamka kila mahali alipokwenda na kusisitiza kwamba Lowassa na viongozi wenzake wa CCM wamechafuka kwa ufisadi.
NIPASHE
Jeshi la Polisi Mkoa wa Ilala linamshikilia mtu mmoja anayedaiwa kuhusika na shambulio lililofanywa na wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambalo lililotokea Msongola kijiji cha Kidole, Chanika na kusababisha watu kujeruhiwa na wanawake kudhalilishwa.
Vurugu hizo zinadaiwa kufanywa na moja ya kundi la watia nia Jimbo la Ukonga.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Mkoa wa Ilala, Lucas Mkondya alisema, tukio hilo lilitokea juzi alasiri wakati wafuasi wa kundi la mtia nia mmoja lilipovamia na kuliteka gari lililokuwa limebeba wafuasi wa CCM.
Alisema walioshambuliwa walikuwa kwenye gari aina ya Noah ambao walikuwa wanatoka kwenye mkutano na walipofika eneo hilo walikutana na gari aina ya Jeep ambalo watu waliokuwamo ndani walifanya unyama huo.
Kamanda alisema baada ya shumbulio, watu wanane waliokuwa kwenye Noah walitoa ripoti polisi zilizowezesha kukamatwa kwa mtu mmoja ambaye jina lake wamelihifadhi.
“Tunaendelea kumhoji mtu huyu kwa kesi iliyofunguliwa ya shambulio, kati ya waliofungua kesi wanawake ni wanne,” alisema.
Alisema jeshi la polisi linaendelea kufuatilia wengine waliohusika kwenye vurugu hizo.
Chanzo cha habari cha kuaminika kilichofanikiwa kufika eneo la tukio na kushuhudia waliofanyiwa unyama huo, baada ya watu hao kuliteka gari hilo walilipeleka kwenye vichaka na kuanza kuwavua nguo wanawake na kuwafanyia udhalilishaji huo.
Chanzo hicho kimesema kuwa, watu hao waliwajeruhi wanaume sita ambao mmoja alitobolewa tumboni na kukimbizwa hospitali ya Temeke kwa matibabu.
Chanzo kilieleza kuwa, waliotekwa walisema watekaji hao walikuwa wanawahoji kwa nini wameamua kumsapoti mgombea wa jimbo la Ukonga (jina tunalo).
NIPASHE
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) inawashikilia makada wanane wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa tuhuma za kujihusisha na utoaji rushwa katika matukio tofauti ya mchakato wa kura za maoni za ubunge na udiwani, jijini Dar es Salaam na Lindi.
Kadhalika Takukuru inashikilia kiasi cha Sh. 1,677,000 kilichokutwa kwa makada hao kupitia mtego uliowekwa kwenye majimbo ya Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam.
Makada hao ni pamoja na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT) kata ya Goba, Pili Mustafa, aliyekamatwa saa 3 usiku akiwa na Sh. 1,330,000, Rehema Luwanja, anayegombea udiwani kata ya Goba na Sh. 95,000, huku akiwa ameshagawa 110,000.
Wengine ni Katibu Itikadi wa CCM kata ya Kibamba, Babu Kimanyo, aliyekamatwa saa 4:30 usiku akiwa na Sh. 252,000 na tayari alishagawa sh. 330,000, Katibu CCM kata ya Kibamba, Elias Nawera ambaye anagombea Ubunge Kawe, Siraju Mwasha anayegombea udiwani Msigani.
Kaimu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Kinondoni, Denis Manumbu, alisema kuwa mbali na watuhumiwa hao, wamepokea malalamiko 28 yanayohusu rushwa ambayo wanayafanyia uchunguzi ili hatua zichukuliwe.
Alisema katika kipindi hiki cha kura za maoni za kuwapata wagombea katika ngazi ya udiwani na ubunge katika vyama vya siasa majimbo manne ya Wilaya ya Kinondoni, ofisi yake imepokea taarifa mbalimbali kutoka kwa wananchi zinazohusu vitendo vya rushwa.
Manumbu alisema vitendo hivyo vinafanywa na watangaza nia na wapambe wao na baada ya kupitia taarifa hizo ofisi ilizifanyia kazi na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao na kuwahoji.
Alisema ofisi yake ina mamlaka kisheria ya kumuita mtu yeyote kutoa maelezo ili kusaidia uchunguzi wa tuhuma husika na mamlaka hayo kwa mujibu wa kifungu cha 10(a) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007, atakayekiuka wito huo atakuwa amekwenda kinyume cha sheria.
Hata hivyo, alisema Takukuru inafanya kazi yake kwa mujibu wa sheria na hawatasita kumchukulia hatua mgombea wa chama chochote na upelelezi utakapokamilika watafikishwa kwenye vyombo vya dola.
Ungana nami kwa habari, matukio na michezo hapa hapa tangakumekuchablog
 
No comments:
Post a Comment