Friday, August 7, 2015

MKUU WA WILAYA HANDENI ALIA NA MADEREVA WALEVI


Tangakumekuchablog

Handeni, MKUU wa Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga, Husna Rajab, amekiagiza kikosi cha usalama barabarani Wilayani hapa kufanya ukaguzi wa leseni za madereva wa magari makubwa na madogo lengo likiwa ni kuwabaini madereva feki na kupunguza ajali za barabarani.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni ya  upimaji wa afya kwa madereva wa magari uliofanywa na kampuni ya Bia Tanzania (TBL)  jana kituo kidogo  cha mabasi cha Segera, Husna alikiagiza kikosi hicho kukomesha ajali zinazoweza kuepukika na  kutoa adhabu kali kwa madereva walevi.

Alisema ajali nyingi zitokeazo barabarani zinatokana na uzembe wa madereva ambao wengi wao amedai huwa wamelewa jambo ambalo kikosi cha usalama barabarani kimeshindwa kulikomesha.

“Kitendo hiki cha leo ambacho kimefanywa na wenzetu wa jeshi la polisi makao makuu kwa kushirikiana na kampuni ya bia Tanzania kwa kweli nakiomba kiwe endelevu” alisema Husna na kuongeza

“Kuanzia leo mimi nitakuwa mmoja wa wanaharakati wa kupinga matumizi ya vilevi wakati wa kazi iwe ni maofisini ama kwa madereva baraarani wa magari makubwa na madogo pamoja na mabasi” alisema

Wakati huo huo, Afisa uhusiano kampuni ya Bia Tanzania, Doris Kalulu, aliwataka madereva kuwa na ada ya kupima  afya zao jambo ambalo litawawezesha kuleta ufanisi ndani ya kazi zao.

Alisema kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kwa kushirikiana na kikosi cha Usalama Barabarani kitakuwa na utaratibu wa kupima afya madereva kwa kutumia kifaa maalumu cha kuwabaini madereva wanaotumia bombe wakati wakiwa safarini .

“Utaratibu huu ni imani yetu kuwa madereva walevi wakiwa safarini utakoma---tutahakikisha kila dereva wa basi anafanyiwa kipimo cha kubaini watumiaji waotumia pombe wakiwa safarini” alisema Kalulu na kuongeza

“Sisi wajibu wetu ni kuwapima na jeshi la polisi kwa upande wao wako na utaraibu kama ni faini au kuzuiliwa kwa leseni ya dereva endapo amekutikana na kosa hilo ni la kwao” alisema

Alisema endapo utaratibu huo utakuwa endelevu unaweza kupunguza ajali na vifo barabarani na hivyo kuwataka wamiliki na madereva wa magari kutoa ushirikiano ili kuweza kukomesha matumizi ya vilevi wakati wa safari.

                                               Mwisho

 Afisa upimaji Afya wa madereva wa mabasi na magari makubwa ya masafa marefu, Lazaro John, akimpima presha dereva wa lori, Rashid Hashily, wakati wa zoezi la upimaji  afya kwa madereva wa mabasi la malori ikiwa ni maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama lililofanywa na Kampuni ya Bia Tanzania kwa kushirikiana na jeshi la polisi makao makuu zoezi lililofanyika kituo kidogo cha mabasi cha Segera Wilayani Handeni Mkoani Tanga jana.

 Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Hasna Rajab, akimkabidhi cheti, fulana na stika ya nenda kwa usalama barabarani, dereva wa lori, Mzinga Saleh mara baada ya kufanya vipimo vya macho, presha, sukari, na HIV wakati wa zoezi la upimaji wa afya kwa madereva wa mabasi na malori yaendayo Mikoani katika kituo kidogo cha Segera Wilayani Handeni Mkoani Tanga jana zoezi lililofanywa na kampuni ya Bia Tanzanzania (TBL) katikati ni Kamanda wa polisi Makao Makuu Dar es Salaam (SACP) Johansen Kahatano.

No comments:

Post a Comment