Uchambuzi huu wa magazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu Cha Candle Education Centre Tanga. Kituo kinaongoza kufaulisha wanafunzi kidato cha pili hadi cha sita na wanaojiendeleza kielimu. Kituo kinatoa kozi mbalimbali za kielimu na kitaaluma. Kituo kipo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 772746
HABARILEO
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye
amesema wanachama waliokihama chama hicho wamejivua nguo mbele za watu
na kwamba wapinzani wanaowachukua wanahangaika na mafuta machafu.
Aidha, amesema aliyekuwa Mbunge wa Segerea na Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk Milton Mahanga, alikuwa anatafuta sababu za kuihama CCM na anamtakia kila la heri, yeye na rafiki yake, Edward Lowassa.
Nape aliyasema hayo jana katika mkutano
wake na waandishi wa habari katika Ofisi Ndogo ya CCM Lumumba, Dar es
Salaam, alipotakiwa kueleza kuhusu kuhama kwa Lowassa na Dk Mahanga
ambao wote kwa nyakati tofauti wamekimbilia Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA).
Lowassa alijitoa CCM wiki moja iliyopita
baada ya kukwama uteuzi wa CCM wa kuwa mgombea wake wa urais na
kukimbilia Chadema ambako anatarajiwa kuwa mgombea wake wa urais na
kuungwa mkono na Umoja wa Vyama vinne vya Upinzani (UKAWA).
Dk Mahanga naye alijitoa juzi baada ya
kukwama katika kura za maoni jimboni Segerea. “Wanahangaika na oil
chafu. Hawa ni wale wale kama ilivyokuwa Mrema (Augustino) mwaka 1995,
akabebwa kiasi cha Mwalimu Nyerere kusema mwacheni abebwa.
Hebu jiulizeni wanaona ubaya wanapotoka,
lakini mambo yakiwanyookea hawasemi, wakitoka ndio maneno mengi,”
alisema Nape. Alisema kuondoka kwa Lowassa na wengine wachache, si jambo
la kwanza kutokea CCM, na pia si la ajabu wala haliwezi kuwa la mwisho
huku akimtuhumu Dk Mahanga kuwa alikuwa akitafuta sababu ya kuondoka
CCM.
HABARILEO
Rais Jakaya Kikwete
ameliagiza Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, kuanzisha mara moja
mfumo wa ulipaji faini kwa njia ya Benki na mitandao ya simu za mkononi
ili kupunguza ushawishi wa vitendo vya rushwa kwa askari wa kikosi cha
usalama barabarani nchini.
Pia, ameagiza kuanzishwa mfumo wa kuweka
alama kwenye leseni za madereva wanaokiuka sheria na kutumia njia hiyo
kuwafungia, ikiwa ni hatua mojawapo ya kudhibiti wimbi la ajali za
barabarani hapa nchini.
Rais Kikwete alitoa agizo hilo jana
katika viwanja vya Tangamano wakati alipokuwa akizindua Wiki ya Nenda
kwa Usalama Barabarani Kitaifa, inayofanyika mkoani Tanga, ikiwa imebeba
kaulimbiu inayosema ‘Endesha Salama, Okoa Maisha’.
Alisema asilimia 56 ya ajali za
barabarani, zinatokana na uzembe na ukosefu wa umakini kwa madereva na
kwamba hatua hiyo inasababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali na
hata kuathiri ustawi wa Kaya na Uchumi wa Taifa.
“Hivi
mpaka sasa Baraza na Kikosi cha usalama barabarani wanashindwaje
kutumia mifumo ya kidigitali kwa nini mpaka leo hakuna kamera
barabarani? Kwanza ingesaidia kudhibiti ajali na uvunjaji wa sheria,
lakini hata vitendo vya rushwa ambavyo navyo vinachangia ongezeko hili
la wimbi wa ajali hapa nchini,” Rais Kikwete.
Alisema katika kipindi cha miaka mitano
kuanzia mwaka 2010 hadi 2014, jumla ya watu 19,264 walipoteza maisha
kutokana na ajali za barabarani na kwamba idadi ya ya waliokufa katika
kipindi cha mwaka peke yake ni watu 3,534 sawa na idadi ya wanaopeteza
maisha kutokana na ugonjwa wa malaria.
Kufuatia hatua hiyo, amelitaka baraza
hilo kufanya mapendekezo ya marekebisho ya sheria za usalama barabarani
hasa pale penye mapungufu ili kuweza kusaidia kudhibiti wimbi la ajali
linalochangia upotevu wa nguvu kazi ya Taifa.
“Kikosi
cha usalama barabarani kiongeze kasi ya kudhibiti ajali za barabarani
na kuwachukulia hatua za kisheria Askari wanaojihusisha na vitendo vya
rushwa….lakini lisilale katika kutoa elimu ya sheria za usalama
barabarani hasa kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari,” alisisitiza Rais Kikwete.
NIPASHE
Wakati leo ni siku ya mwisho ya
kuandikisha wananchi katika Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa mfumo wa
Biometric Voters Registration (BVR), jijini Dar es Salaam, watu 2,
634, 942 tayari wameandikishwa katika daftari hilo mkoani humo hadi
juzi.
Pia vituo vingi vya uandikishaji hadi
jana mkoani humo vilishuhudiwa kuwa na idadi ndogo ya watu na vingine
vikiwa vitupu huku mashine zikiwa hazina kazi baada ya asilimia kubwa ya
wakazi wa jiji hilo kuandikishwa.
Katika taarifa yake iliyotoka
kujua tathmini ya uandikishaji huo jana, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume
ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Kailima Kombwey, alisema idadi hiyo ni kati ya lengo la kuandikisha watu 2, 810, 423 sawa na asilimia93.76 jijini humo.
“Lengo kwa mkoa mzima ni kuandikisha watu 2, 810, 423. Waliojiandikisha ni 2, 634, 942 sawa na asilimia 93. 7,” Kombwey.
Kati ya idadi hiyo, Manispaa ya
Kinondoni hadi juzi, ilikuwa imeandikisha watu 1, 075, 946 kati ya 1,
102, 565 sawa na asilimia 97.58, wanaotarajiwa kuandikishwa katika
daftari hilo hadi leo.
Kwa upande wa Manispaa ya Temeke, hadi
siku hiyo ilikuwa imeandikisha watu 896, 142 kati ya 815, 214 sawa na
asilimia 90.6 wanaotarajiwa kuandikishwa ifikapo leo.
Manispaa ya Ilala imeandikisha watu 743,
782 kati ya 811, 716 sawa na asilimia 91.63 ya wanaotarajiwa
kuandikishwa hadi leo ambayo ni siku ya 14 na ya mwisho baada ya siku 10
za awali kumalizika Ijumaa wiki iliyopita na tume hiyo kuongeza
nyingine nne kuhakikisha wakazi wote wa jiji hilo wanaandikishwa.
Wiki iliyopita Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mstaafu, Damian Lubuva ,
alisema waliamua kuongeza siku hizo baada ya wakazi wa jiji hilo
kuonyesha mwitikio mkubwa wa kujiandikisha katika daftari hilo.
Kwa mujibu wa Jaji Lubuva, tume hiyo
iliongeza siku hizo chache kutokana na kuwapo kwa mfululizo wa matukio
ya Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.
NIPASHE
Mgombea udiwani kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM, kata ya Mbagala Kuu, jijini Dar es Salaam, Yusuf Manji,
anadaiwa kunusurika kukamatwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (Takukuru) wakiwa kwenye harakati za kugawa rushwa na wapambe
wake.
Inadaiwa kuwa Manji akiwa na wapambe
wake, walikuwa wakifuatiliwa na taasisi hiyo baada ya kupata taarifa
kuwa mgombea huyo alikuwa katika harakati za kugawa fedha ili
achaguliwe.
Tukio hilo lilitokea Jumamosi mchana kwenye ukumbi wa Vigae Pub, ambapo mgombea huyo alionekana kukusanyika na wapambe wake na ndipo walipofuatiliwa na taasisi hiyo kujua kinachoendelea.
Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Temeke, Beutoz Mbwiga,
alithibitisha kuwa taasisi yake iliweka mtego wa kumkamata mgombea huyo
akiwa na wapambe wake lakini mtego huo haukuzaa matunda.
Alisema Manji alikuwa na watu wake
pamoja na mabaunsa katika ukumbi huo uliopo Mbagala na gari la Takukuru
lilipowasili maeneo hayo, mgombea huyo na wapambe wake walitawanyika
katika ukumbi huo.
“Watu
wetu walipoingia kwenye ukumbi huo kufuatilia walishtuka na walianza
kusambaratika, hivyo hawakufanikiwa kumkamata Manji wala wapambe
wake….nahisi huenda gari letu lilionekana ndipo wakaanza kutangaziana na
kuamua kuondoka ukumbini hapo au huenda wamepewa taarifa kuwa
tunakwenda huko,” alisema.
Juzi, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhan Mababida,
alisema wagombea wa CCM mkoa huo watakaothibitika kugawa rushwa,
watanyang’anywa ushindi wao haraka na kupewa wengine wanaowafuatia
katika ushindi.
Madabida aliyasema hayo wakati
akizungumza na waandishi wa habari waliotaka kujua uwapo wa malalamiko
ya rushwa kwa baadhi ya wagombea wa chama hicho.
Alisema wagombea wote na wanachama
wamepewa mwongozo kuwa anayetaka uongozi kwa kuhonga hafai kwa kuwa
anayefaa hawezi kuhonga na kwamba wanachama wanajua uwezo wake na
watamchagua wanayeona anafaa.
NIPASHE
Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amevunja ukimya juu ya kinachomsibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa, ambaye amekuwa haonekani kwenye shughuli za chama hicho.
Akifungua mkutano wa Baraza Kuu la chama
hicho jijini Dar es Salaam jana, Mbowe alisema kuwa Dk. Slaa ameamua
kupumzika shughuli za chama baada ya kutofautiana na wenzake juu ya ujio
wa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, ambaye atapeperusha bendera
ya Chadema kupitia Umoja wa Kutetea Katiba ya Wananchi (Ukawa) kuwania
urais katika uchaguzi mkuu Oktoba 25, mwaka huu.
Mbowe alisema kuwa Dk. Slaa
alitofautiana na wajumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho juu ya kuteuliwa
kwa Lowassa ambaye alijiunga na chama hicho, na kwa pamoja wameamua
kumwacha apumzike na kama ataona inafaa atawaunga mkono mbele ya safari.
Alisema kwa muda mrefu sasa kumekuwa na
minong’ono, manung’uniko, malalamiko na nderemo kuhusiana na kujiunga
kwa Lowassa katika chama hicho.
“Dk. Slaa tunampenda sana na yeye
anatupenda na kwa hulka yake, Katibu Mkuu wetu hawezi kupingana na
maamuzi ya chama ya kumkaribisha Lowassa, tunamuombea kwa Mungu ampe
ujasiri kwa kuona kuwa ujio wa Lowassa ni mipango ya Mungu,” alisema
Mbowe.
Mbowe alisema kabla ya Lowassa na
wenzake kujiunga na chama hicho, vilifanyika vikao vya mashauriano ya
muda mrefu na kujiridhisha kuwa hakuna shaka kuhusiana na mwanasiasa
huyo kujiunga na Chadema.
Aliongeza kuwa katika hatua zote hizo, Dk. Slaa alishiriki.
Hata hivyo, Mbowe alisema katika hatua
za mwisho, Dk. Slaa alitofautiana na baadhi ya watu, lakini chama
kinaendeela kuzungumza naye ili kufikia muafaka.
“Hata
jana (juzi) niliongea naye na kimsingi, Dk. Slaa amekubaliana kwamba
sisi tuendelee na mchakato huu, tukifikia sehemu atatu-join (ataungana
nasi) mbele ya safari, ifahamike kuwa katika suala la maamuzi siyo
lazima kila mmoja akubali kwa asilimia 100,” Mbowe.
Mbowe alisema mtu anaweza kujiunga na
chama chochote cha siasa, lakini Chadema hakiwezi kufanya udalali kwa
sababu chama kimefika hapo kilipo kutokana na kuungwa mkono na
Watanzania wengi.
“Ni
dhahiri kuwa CCM ndio adui yetu mkuu, na ukipata nafasi ya kumjeruhi
adui yako usipoitumia lazima utakuwa mwendawazimu,” alisema na kuongeza:
“Ilijengeka imani kuwa hatuwezi kuwa na chama cha upinzani cha kuwa na uwezo wa kupambana na chama tawala.”
Mbowe aliwaeleza wajumbe kuwa
yamejitokeza makundi ya watu wengi toka ndani ya CCM ambao wanataka
kujiunga na Chadema na katika makundi hayo aliyekuwa anabinywa zaidi ni
Lowassa.
Alisema katika siasa hakuna rafiki wala adui wa kudumu, lakini ndani ya Chadema kinachoangaliwa ni maslahi ya Taifa ya kudumu.
Mbowe alisema kumezuka hofu ndani ya
Baraza Kuu, wagombea ubunge na wagombea udiwani na hofu hiyo inapokelewa
kwa hisia tofauti na kwamba chama kitahakikisha hofu hiyo inapatiwa
ufumbuzi ili kupata nguvu ya kuishinda CCM katika uchaguzi mkuu wa mwaka
huu.
“Hofu ambazo zinatokana na minyukano ya
kisiasa lazima tuishinde, na mimi kama kiongozi mkuu wa chama
nitahakikisha hofu hii tunaishinda,” alisema.
Mbowe hata hivyo, alisema Dk. Slaa aliomba kwenda likizo kwa mapunziko na baadaye ataungana nao.
Dk. Slaa alipotafutwa katika simu yake ya kiganjani jana kuzungumzia hatma yake hakupatikana.
Kwa takribani wiki mbili sasa kumekuwa
na hofu ambayo imetanda ndani ya Chadema na wananchi kwa ujumla kutokana
na kutoonekana kwa Dk. Slaa, katika matukio ya kisiasa yanayohusu
mustakabali wa chama hicho.
NIPASHE
Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa
Arusha kimesema viongozi ambao wameweka mguu mmoja CCM na mwingine
upinzani na kuhujumu chama ni bora watoke mara moja wawaachie chama chao
kuliko hujuma, vinginevyo watashughulikiwa.
Katibu wa CCM Wilaya ya Arusha, Feruzy Bano, alisema wakati wa uchaguzi wa kura za maoni wamegundua hujuma zilizofanywa na baadhi ya viongozi wa CCM.
“Mfano
unakuta wanachama wanatishwa na hasa maeneo ya Umasaini, na kusababisha
wapiga kura kujitokeza wachache 7,251 kati ya wanachama hai 27,000,” alisema.
Alisema ni bora wakatoka wamfuate wanayemtaka kuliko kubaki wakati kimwili na roho hawako huko.
“Ila tupo katika uchunguzi baada ya muda si mrefu dawa yao inachemka maana wanajulikana,” alisema.
Aliwaonya wagombea nafasi ya udiwani
waoshinda nafasi zao, ambao wana mpango wa kujitoa baadaye ili kuipa
ushindi Chadema waache kufanya hivyo maana cha moto watakiona.
NIPASHE
Baadhi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha
Katoliki Ruaha (RUCU) mkoani Iringa, wamelalamika kutokupewa fedha za
kujikimu na za mafunzo kwa vitendo.
Wanafunzi hao ambao hawakutaka majina
yao kuandikwa, walisema wamekuwa wakifuatilia fedha hizo kwa muda mrefu
kwenye uongozi wa chuo pamoja na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya
Juu (HESLB) bila ya mafanikio.
Walisema wenzao waliokuwa wanadai fedha hizo walikuwa wengi, lakini ni wanafunzi wachache waliofanikishwa kutatuliwa tatizo lao.
“Tulikuwa
wengi tunaodai fedha hizo, lakini ni wanafunzi wawili tu ambao
walipewa, sisi wengine bado tunahangaika hatujui tumfuate nani kwa kuwa
HESLB tumeshaenda na hakuna kitu,” alisema mmoja wao.
Wanasema kuwa uongozi wa chuo umekuwa ukiwapa majibu kuwa HESLB hakuna fedha, hivyo wanapaswa kuwa wavumilivu.
Waziri wa Mikopo wa Wanafuzi Rucu, Walter Raymond, alithibitisha kuwapo kwa tatizo hilo.
Alisema kuna wanafunzi wa mwaka wa tatu
wanaosomea Ualimu hawajalipwa fedha za utafiti, mwaka wa tatu waliosomea
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT), wanafunzi wa mwaka wanne
waliomaliza Sheria, mwaka wa tatu waliomaliza Sayansi ya Kompyuta pamoja
mwaka wa tatu waliomaliza Sayansi ya Mazingira.
Afisa mikopo wa chuo hicho, Chesco
Mwalongo, alipotafutwa, simu yake iliita bila kupokelewa na hata
alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno (sms) hakujibu.
Mkurugenzi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa HESLB, Cosmas Mwaisobwa, alisema bodi ilishakatatua tatizo la mikopo kwa wanafunzi wa chuo hicho muda mrefu.
Alisema kama kuna mwanafunzi ambaye bado ana tatizo la mikopo afike katika ofisi za bodi na kuwaona maofisa na watamsadia.
Alisema matatizo ya mikopo kwa wanafunzi yanatatuliwa na bodi na siyo sahihi wanafunzi kukimbilia kwenye vyombo vya habari.
NIPASHE
Mshambuliaji aliyekuwa amekosa uhakika wa namba katika Kikosi cha Yanga, Mliberia Kpah Sherman, amesaini mkataba wa miaka mitatu kwenye klabu ya Mpumalanga Black Aces ya Afrika Kusini.
Mitandao mbalimbali ya michezo ya Afrika
Kusini ilimwonyesha Sherman akitambulishwa jana kwenye klabu hiyo baada
ya kusaini mkataba juzi huku taarifa kutoka ndani ya uongozi wa Yanga
zikieleza kuwa Wanajangwani hao watalamba Dola za Marekani 150,000 (Sh.
milioni 312 za Tanzania) ikiwa ni zaidi ya mara mbili ya fungu ambalo
walitumia kumnasa ambalo lilielezwa kuwa ni Dola 60,000 Desemba, mwaka
jana.
Taarifa hizo zilieleza kuwa Mliberia
huyo aliyekuwa analipwa Dola 3,000 na Yanga kwa mwezi, akiwa huko sasa
atalipwa Dola 5,000 na klabu hiyo mpya, lakini kiasi hicho kikiwa kabla
ya kukatwa kodi.
Akizungumza jana jijini, Katibu Mkuu wa Yanga, Jonas Tiboroha,
huku akikataa kutaja dau walilomuuza, alisema mchezaji huyo alifuzu
majaribio pamoja na vipimo vya afya, hivyo klabu hao inamtakia mafanikio
kwenye timu yake hiyo mpya.
Katibu huyo alisema hiyo ni nafasi nzuri
kwa mchezaji huyo, na itamsaidia kwa sababu isingekuwa jambo la busara
kuendelea kukaa naye hali ya kuwa haendani na mfumo wa sasa wa Kocha
Mkuu, Hans van der Pluijm.
“Ni kweli ameshapata mkataba, si mchezaji wetu tena,” alisema kwa kifupi katibu huyo.
Kuondoka kwa Sherman kunaipa nafasi Yanga ya kusaini mchezaji mwingine wa kigeni kwenye kikosi chake ili kujiimarisha.
Kanuni za ligi msimu ujao utakaoanza Septemba 12, mwaka huu zinaruhusu klabu kusajili wachezaji wa kigeni wasiozidi saba.
Wachezaji wa kigeni ambao wako Yanga ni pamoja na Haruna Niyonzima, Mbuyu Twite kutoka Rwanda, Andrey Coutinho (Brazil), Joseph Zutah (Ghana) na Donald Ngoma (Zimbabwe)
MWANANCHI
Chama cha Mapinduzi (CCM), kimesema
kitatumia ‘panga’ lilelile lililotumika kumpata mgombea wake wa urais
katika kuchuja wagombea ubunge na udiwani kupitia vikao vyake halali ili
kupata wagombea safi.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnaye
alisema hayo jana Dar es Salaam katika mkutano na waandishi wa habari,
kuzungumzia mchakato wa vikao vya kamati za chama hicho ili kupata
wagombea wa ubunge, uwakilishi na udiwani baada ya mchakato wa kura za
maoni kukamilika.
Alisema mchakato huo utaanza kwa kikao
cha Kamati Maalumu ya CCM Agosti 6 na 7 kuchuja na kupitisha wagombea
ubunge na uwakilishi. Agosti 8 na 9, Sekretarieti itakutana ikifuatiwa
na Kamati Kuu pia kwa siku mbili kabla ya Halmashauri Kuu kukutana
Agosti 12 na 13 kuteua wagombea ubunge na uwakilishi.
“Kura
za maoni siyo mwisho wa safari, ni hatua ya kwanza ya kuona ni nani
anayekubalika… siyo kibali cha kupeperusha bendera ya CCM, kama kuna
upungufu vikao vitachukua hatua. Kura ya maoni si kigezo… kama wamecheza
rafu au kutumia rushwa, hata kama wameshinda kwa kura nyingi,
ikithibitika wanaweza kuondolewa,” alisema Nape na kuongeza:
“Tutafanya
kama ilivyokuwa kwa wagombea urais, kama maadili hayakufuatwa wanaweza
kuondolewa siyo tu wa kwanza, hata wanne, hata kufuta matokeo.
Tutachukua hatua kwenye ubunge, tutachukua hatua kwenye udiwani kwa wale
watakaojihusisha na rushwa. Hawatapata nafasi ya uteuzi kwenye chama
chetu. Hatuna muda wa kuanza kuosha watu na madodoki.”
Alikumbusha jinsi chama hicho
kilivyomteua Dk Khamis Kigwangallah kuwania ubunge wa Nzega alikoteuliwa
licha ya kushika nafasi ya tatu katika kura ya maoni.
Kuhusu changamoto kwenye upigaji kura za
maoni ikiwamo vitendo vya rushwa, Nape alisema kwa takwimu walizonazo,
changamoto zilizojitokeza ni kidogo ikilinganishwa na miaka ya nyuma…
“Hii ni kwa sababu tumeboresha utaratibu tofauti na huko nyuma. Maeneo
mengi yamemaliza na hata yale ambayo yamekuwa na kasoro za hapa na pale
tumezitatua.
“…Kura za maoni katika chama chetu
zimetoa demokrasia na bila shaka tumefundisha vyama vingine. Vyama vingi
vinatoa wagombea mfukoni, lakini sisi tunawapeleka kwa wanachama
wanapigiwa kura,” alisema Nape.
Alisema kuwa kutokana na kukua kwa
demokrasia katika chama hicho na kujenga mfumo mzuri zaidi wa upigaji
kura za maoni, hata vigogo wasiofanya vizuri wameanguka katika kura za
maoni.
Kauli hiyo ya Nape imekuja huku kukiwa
na ripoti ya baadhi ya mawaziri na wabunge wanaomaliza muda wao kuanguka
katika kura za maoni.
Alipoulizwa kuhusu kuhama chama hicho
kwa waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa na Mbunge wa Segerea, Dk
Makongoro Mahanga na wanaCCM wengine, Nape alisema siyo jambo la ajabu
na kwamba si wa kwanza na wala hawatakuwa wa mwisho. “Wapo wanaotoka CCM
kwenda vyama vingine na wapo wanaotoka vyama vingine na kuja CCM.
Lakini niseme tu kwamba wapo ambao wanataka uongozi na wapo ambao
wanataka kwenda kuongoza watu:
“Anayetaka
kuongoza watu ni mvumilivu, mtulivu na hufuata taratibu. Lakini wapo
ambao lengo siyo kwenda kuongoza watu, lengo ni masilahi binafsi.
Wakikosa uongozi huonyesha tabia zao waziwazi.”
MWANANCHI
Muasisi wa Tanu na baadaye CCM, Mzee Peter Kisumo amefariki dunia.
Mwanasiasa huyo mkongwe nchini ambaye
aliwahi kushika nyadhifa kadhaa katika Serikali ya Awamu ya Kwanza,
alifariki Dunia jana saa moja usiku katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Mtoto wa marehemu, Michael Kisumo
alilithibitishia gazeti hili jana juu ya kifo cha baba yake akisema
kilitokana na maradhi ya figo ambayo yamekuwa yakimsumbua kwa muda
mrefu.
“Tulikuja
hapa Muhimbili kwa ajili ya mzee kufanyiwa dialysis (usafishaji damu
katika figo) sasa ikajitokeza complication (utata) akaanza kuharisha
damu,” alisema.
Michael alisema baba yake alilazwa wodi ya kawaida juzi ili jana apatiwe tiba hiyo kabla ya hali yake kubadilika ghafla.
“Daktari
wake alipokuja leo (jana) na kumwangalia aliagiza atolewe wodi ya
kawaida ahamishiwe ICU lakini ilipofika saa moja usiku akatutoka”Michael.
Kifo cha mwanasiasa huyo kimekuja
takribani mwezi mmoja tangu arejee kutoka India ambako amekuwa akienda
mara kwa mara kuchunguzwa afya yake.
Hali ya ugonjwa wake huo ilifikia katika
kiwango cha juu na kulazimika kufanyiwa uchujaji wa figo mara tatu kwa
wiki kila Jumatatu, Jumatano na Ijumaa.
Kisumo aliwahi kuwa mmoja wa mameneja wa
kampeni wa Rais Jakaya Kikwete mwaka 2005 akisimamia kanda ya kaskazini
iliyojumuisha mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Tanga.
Mbali ya kuwa waziri, aliwahi pia kuwa mkuu wa mkoa na mdhamini wa CCM.
Kwa habari, matukio na michezo ni hapa hapa tangakumekuchablog
No comments:
Post a Comment