Friday, January 29, 2016

SERIKALI YAKITWAA KIWANDA CHA CHAI CHA MPONDE




Tangakumekuchablog
Lushoto, SERIKALI imekitwaa kiwanda cha Chai cha Mpondwe kilichopo Bumbuli na kusema kuwa mwekezaji alivunja mkataba wa uendeshaji jambo lililowawasababishia wakulima na mwekezaji kuingia katika mivutano ya mara kwa mara.
Utwaaji wa kiwanda hicho ulifanywa kwa ulinzi mkali wa kikosi cha polisi waliokuwa na silaha kwa kushirikiana na, Msajili wa Hazina, Laurence Mafuru, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mwantumu Mahiza, Kamanda wa Polisi Tanga, Mihayo Misikhella pamoja na Mbunge wa jimbo la Bumbuli, Januari Makamba.
Kiwanda hicho ambacho kwa zaidi ya miaka mitatu kimesimama uzalishaji na kuingia migogoro ya mara kwa mara baina ya wakulima na mwekezaji jambo lililopelekea wakulima kutishia kubadilisha aina ya kilimo badala ya Chai.
“Kwa mamlaka niliyonayo niliyopewa na Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli, kuanzia sasa kiwanda hiki cha chai cha Mponde kinatwaliwa na Serikali" alisema Msajili wa Hazina Laurenced Mafuru
Mafuru alisema mwekezaji ambaye alikuwa ni Umoja wa Wakulima wa Chai, Korogwe na Lushoto (UTEGA) walishindwa kukiendesha kiwanda hicho na kuvunja mikataba ya uendeshaji kiwanda.
Alisema kwa kipindi chote hicho Serikali ilikuwa inafuatilia kwa umakini kisha kubaini kuwa kuna ukiukwaji mkubwa wa mkataba wa uendeshaji hivyo kuona ni vyema kukichukua na kuliokoza zao la Chai Wilayani humo.
“Katika ufuatiliaji wetu tuliona zao la chai hapa linatoweka na wakulima wengi wamebadilisha aina ya kilimo na kulima mahindi, hakuna sababu yoyote wakati kiwanda chenye mitambo iliyokamilikka kufa hivi hivi” alisema Mafuru
Akizungumza na wananchi mara baada ya kiwanda hicho kuchukuliwa na Serikali, Mbunge wa Bumbuli, January Makamba, aliwataka wakulima kurejea mashambani na kulima Chai na kusema kuwa neema inakuja.
Alisema hakutakuwa na mivutano tena ya bei na uendeshaji wa kiwanda kwani Serikali inatambua hivyo ni wajibu wa kila mkulima kurudi shambani na kusema kuwa kiwanda hicho karibuni kitaanza kununua na kuanza uzalishaji.
“Wazee wangu na wajomba na mashangazi kile kilio chenu cha muda mrefu leo kimetimia, hakuna jambo lisilo na mwisho na leo najua kila mmoja hapa kwa furaha ataenda kupika biriani” Alisema Makamba
Aliwataka wakulima hao kila mmoja kurejea katika eneo lake la na wale ambao waliuza au kubadilisha aina ya kilimo kurejea kulima Chai kwani Serikali imejipanga kuwakomboa na umasikini wakulima wa Chai.
                                              Mwisho



  Aliekuwa mwenyekiti wa Umoja wa Wakulima wa Chai (UTEGA) kiwanda cha Chai cha Mponde Bumbuli Wilayani Lushoto Mkoani Tanga, William Shelukindo, akilalamika mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mwantumu Mahiza mara baada ya Serikali kukitwaa kiwanda hicho baada kukaa zaidi ya miaka mitatu bila uzalishaji na wakulima kuteseka kutafuta masoko ya kuuza Chai.

 Aliekuwa Mwekezaji kiwanda cha Chai Cha Mponde Lushoto Tanga, Nawab Mullah, akilalamika kutwaliwa kiwanda hicho na Serikali mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mwantumu Mahiza, Msajili wa Hazina, Laurence Mafuru na maofisa wengine wa Serikali.




 Msajili wa Hazina, Laurence Mafuru akipokea maelekezo ya kiwanda cha Chai Cha Mponde ambacho amekitwaa na kukikabidhi kwa Serikali baada kushindwa kufanya kazi kwa miaka mitatu baada ya Mwekezaji Umoja wa Wakulima Lushoto na Korogwe (UTEGA) kushindwa kutekeleza mkataba wa kuendesha kiwanda hicho.
Msajili wa Hazina, Laurence Mafuru (kulia) akiwana Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mwantumu Mahiza (kushoto) wakitoka nje baada ya kukagua mitambo ya kiwanda cha Chai Cha Mponde baada ya Serikali kukitwa kutoka kwa Mwekezaji (UTEGA) kushindwa kutekeleza mkataba wa kukiendesha kiwanda.

No comments:

Post a Comment