Thursday, January 21, 2016

UCHAMBUZI WA MAGAZETI NA CANDLE

Uchambuzi huu wa magazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu Cha Candle Education Centre Tanga, Candle wanaendelea kufanya usaili wa wananfunzi pamoja na QT, Wapo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 772746
NIPASHE
Wafungwa wanaotumikia vifungo mbalimbali katika gereza kuu la Lilungu, mkoani Mtwara, wanakabiliwa na hali ngumu kimaisha kutokana na kupewa chakula kibaya na huduma mbovu za vyoo hivyo kutishia kuanzisha mgomo.
Taarifa zilizoelezwa na wafungwa hao, zilisema tatizo la kupewa chakula kibovu limekuwa la muda mrefu na uongozi wa gereza umekuwa hauchukui hatua kila ukielezwa.
Wafungwa hao (majina tunayo) walibainisha mambo sita wanayolalamikia kuwa ni kupewa chakula kibovu na huduma mbaya za ndani na kwamba hadi sasa bado wanatumia mtondoo na hakuna huduma ya matunda hadi wakati wa msimu wa maembe tu.
Malalamiko mengine ni kukosekana kwa mboga za majani kutokana na bustani ya gereza kubinafsishwa kwa mkuu wa gereza hilo ambaye hulazimika kuuza mboga kwa gereza na kutokuwapo huduma ya nyama ambayo wanapewa mare nne tu kwa mwezi.
Kutokana na hali hiyo, Januari 14, mwaka huu, wafungwa katika gereza hilo walianza mgomo baridi baada ya kupikiwa mchele uliodaiwa kuwa na wadudu (funza).
Walisema malalamiko hayo kila wanapowaeleza viongozi wao wamekuwa wakijibu kuwa ni kwa sababu serikali haijawalipa wazabuni wanaotoa huduma ya chakula.
Ofisa Habari Jeshi la Magereza, Deogratius Kazinja, alipoulizwa alisema ofisi yake bado haijapokea malalamiko ya wafungwa hao na kwamba taarifa rasmi za masuala hayo zinaweza kutolewa na viongozi wa juu wa jeshi.
Kazinja alisema migomo ya wafungwa imekuwa ikijitokeza mara kadhaa katika magereza lakini haisababishwi na uongozi wa magereza kushindwa kutatua malalamiko yao.
Kwa upande wake, Mkuu wa Magereza Mkoa wa Mtwara, Mussa Kaswaka, alipoulizwa alisema hawezi kuzungumzia malalamiko hayo kwa sababu kwa utaratibu wa jeshi hilo ni hadi apewe ruhsa ya kuzungumza na Kamishna Jenerali wa Magereza.
“Mimi si msemaji wa Jeshi la Magereza. Nenda  makao makuu kaonane na Kamisha Jenerali wa Magereza halafu yeye ndiye atatoa maelekezo kama niyatolee ufafanuzi,” alisema.
NIPASHE
Serikali imekanusha uzushi unaosambazwa katika mitandao ya kijamii ya ndani ya nchi na nje ya nchi kuwa Rais Dk. John Magufuli, amewafukuza wageni kutoka nje waliokuwa wanafanyabiashara zao nchini kwa kuwa serikali yake haitaki wageni kufanya biashara nchini.
Taarifa iliyotolewa na Ikulu jijini Dar es Salaam kwa vyombo vya habari jana ilisema serikali haijafukuza wageni kutoka nje ya nchi kufanya biashara nchini na haina mpango wa kuwafukuza wageni wanaoishi nchini kwa vibali vilivyotolewa kisheria na Idara ya Uhamiaji.
“Uzushi huo usiokuwa na ukweli umeenezwa kufuatia Idara ya Uhamiaji kutekeleza jukumu lake la kufuatilia wageni wote wanaoishi nchini bila vibali halali vya ukaazi ambapo kwa mwezi Novemba na Desemba, mwaka 2015 wageni 372 walioondoshwa nchini,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Ilifafanua kuwa kazi ya kufuatilia wageni wanaoishi nchini bila vibali halali vya kisheria, haijaanza katika Serikali ya Awamu ya Tano.
Ilieleza kuwa Idara ya Uhamiaji nchini tangu Januari hadi Desemba, mwaka jana, iliondosha nchini jumla ya wageni 1,642 waliokuwa wanaishi na kufanya shughuli zao nchini kinyume na sheria.
“Uzushi unaoenezwa hauna ukweli wowote na hauna nia njema na nchi yetu kwani kati ya mwaka 2014 na 2016, Idara ya Uhamiaji imetoa vibali vya ukaazi (Residence Permits) 40,765 kwa wageni wawekezaji na wafanyabiashara, wageni wanaofanya kazi za kuajiriwa, wageni wanaokuja kwa ajili ya masomo, matibabu, dini, utafiti na wastaafu kuishi na kufanya shughuli zao nchini,” iliongeza taarifa hiyo.
Ilisema serikali inawakaribisha wageni kuja nchini kuwekeza na kufanya shughuli zao kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za nchi.
Ilisema aidha, kuna uzushi unaenezwa kuwa Rais Dk. Magufuli, amepiga marufuku wanawake kuvaa nguo fupi kama njia ya kupunguza kasi ya maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi.
“Rais tangu aingie madarakani, hajawahi kuagiza wala kutoa tamko kuhusiana na uzushi wa kukataza uvaaji wa nguo fupi ili kupunguza maambukizi ya Ukimwi kama inavyoenezwa katika mitandao ya ndani na nje ya nchi ambayo inanukuu habari hiyo kuwa imeandikwa na Gazeti la Kenya la `The Standard,’ ilisema.
Ilisema serikali inautangazia umma kuwa uzushi huo unaomhusu Rais Magufuli umetungwa na watu wasioitakia mema Tanzania kwa lengo la kumdhalilisha Rais na hauna ukweli hivyo watu wasishiriki kuueneza kwa njia yeyote ile.
MTANZANIA
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako, amefuta mfumo wa uwekaji   matokeo wa ‘Grade Point Average (GPA) ulioanza kutumiwa na Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA)  mwaka 2014.
Mfumo huo uliofuta mfumo uliokuwapo wa Divisheni,  ulianza kutumika kwa kidato cha nne na sita na vyuo vya ualimu.
Inaelezwa kuwa mfumo huo ulianzishwa   kujaribu kupandisha ufaulu baada ya kuonekana wanafunzi wengi walishindwa  mitihani ya kidato cha nne, hasa mwaka 2013.
Mfumo huo ulilalamikiwa na wadau wa elimu waliodai kuwa ulikuwa unashusha kiwango cha elimu na kuwachanganya wanafunzi.
Profesa Ndalichako, ambaye aliwahi kuwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), alisema baraza hilo limeshindwa kueleza sababu za kutumia mfumo huo badala yake limeishia kutoa utaratibu uliotumika tu.
“Kwa mamlaka niliyonayo chini ya kifungu cha 20 cha Sheria ya Baraza la Mitihani Tanzania, sura ya 107, naliagiza Baraza  kufanya mapitio ya mfumo unaotumika sasa wa wastani wa alama (GPA) kwa lengo la kurudi kwenye mfumo wa awali wa Divisheni.
“Viwango vya ufaulu vizingatie azma ya nchi kuelekea kwenye uchumi wa kati na Tanzania ya viwanda,” alisema Profesa Ndalichako.
Kuhusu mtihani wa pili (Paper two),  aliitaka NECTA kuufuta kwa watahiniwa wa kujitegemea.
Mtihani huo ulianzishwa kama alama ya maendeleo wakati ni mtihani wa mwisho.
“Wizara haiwezi kufikia azma ya kusimamia ubora wa elimu katika ngazi zote bila kuhakikisha   viwango vya ufaulu vinawezesha kutoa wataalamu wenye stadi na maarifa badala ya kuwa na wahitimu wengi wenye vyeti lakini hawakidhi mahitaji ya soko la ajira,” alisema Profesa Ndalichako.
Januari 7 mwaka huu, Waziri Ndalichako alitembelea Necta na kuitaka itoe ufafanuzi wa kuacha kutumia mfumo wa divisheni na kutumia GPA.
Pia aliitaka itoe maelezo ya kuanzishwa kwa mtihani wa pili kwa watahiniwa wa kujitegemea.
Hata hivyo alisema  jana kuwa maelezo yaliyotolewa yalikuwa yamejikita katika kueleza utaratibu badala ya sababu za kuutumia mfumo huo.
“Taarifa imebainisha kuwa uanzishwaji wa mfumo wa GPA ulitokana na maoni ya wadau bila kuwataja wadau  husika na kueleza sababu walizotoa.
“Taarifa ya utafiti uliofanywea na Wizara ya Elimu haijataja idadi ya wadau waliojaza madodoso na wala haionyeshi mikutano ya kupata maoni ya wadau ilihusisha watu gani, ilifanyika wapi na lini,” alisema Profesa Ndalichako.
Kuhusu sababu kuwa NECTA ilipata maelekezo kutoka wa Wizara ya Elimu mwaka 2014, Profesa Ndalichako, alisema uchambuzi unaonyesha kuwa wizara ilikuwa imeelekeza baraza  la mitihani liandae mfumo huo na kuuwasilisha kwa Kamishna wa Elimu   upate kibali cha Serikali kabla ya kuanza kutumika.
“Hata hivyo, jambo hilo halikufanyika na badala yake Baraza hilo likaanza kutumia mfumo huo mwaka 2014. Nyaraka zilizowasilishwa hazionyeshi kama mapendekezo ya mfumo huo yaliwasilishwa kwa Kamishna wa Elimu,” alisema.
Alisema Baraza lilieleza faida ya kutumia GPA kuwa ni kueleweka kwake kwa urahisi na wadau jambo ambalo linapingana na maoni ya wadau yanayojitokeza kwenye vyombo vya habari, huku likishindwa kueleza udhaifu wa mfumo wa Divisheni.
“NECTA wameeleza kuwa mfumo wa GPA umerahisisha udahili wa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu (Collective Admission System- CAS) jambo ambalo si sahihi.
“Mfumo wa CAS ulianza kutumika Aprili 2010 wakati mfumo wa GPA ulianza kutumika mwaka 2014. Isitoshe huzingatia masomo mawili ya fani anayotarajia kusoma mwanafunzi siyo ufaulu wa jumla,” alisema.
Waziri alisema mfumo wa GPA ulikuwa bado kwenye majaribio hivyo haukupaswa kutumika kufanyia majaribio kwenye maisha ya watu.
Kuhusu sababu ya kuongeza mtihani wa pili kwa watahiniwa wa kujitegemea kama mbadala wa upimaji endelevu, alisema maelezo ya NECTA kuwa mtihani huo ni mbadala wa upimaji endelevu hayatekelezeki.
“Kitaalamu ‘paper two’ haiwezi kuwa alama ya maendeleo ya kila siku kwa kuwa inafanyika sambamba na mitihani mingine ya mwisho,” alisema Profesa Ndalichako.
Kwa sababu hiyo, Profesa Ndalichako, alisema kitendo cha baraza hilo kuingiza mfumo huo wa GPA katika marekebisho ya kanuni zake yaliyosainiwa na Waziri Oktoba 28 mwaka jana na kuchapishwa Novemba 6 mwaka jana kwenye gazeti la Serikali, ni kuonyesha kuwa mfumo huo ulianza kutumika bila kukamilika   matakwa ya sheria.
“Mfumo wa GPA ulianza kutumika mwaka mmoja kabla haujaingizwa kwenye kanuni za mitihani,” alisema.
Akizungumzia hasara ya mfumo huo, Waziri Ndalichako alisema baadhi ya watahiniwa waliofaulu mitihani wanaonyesha kiwango kidogo cha maarifa kuliko kiwango cha ufaulu.
Alisema kuwapo  daraja E kwenye alama za ufaulu wakati haihesabiki katika upangaji wa GPA kunawafanya watahiniwa waliopata E zote kwenye mitihani kujiona wako bora kuliko wenye D mbili na F zote, ambaye anahesabika kuwa amefaulu mtihani.
“Uwepo wa pointi za mfiko kwenye madaraja ya ufaulu kwa ngazi mbalimbali za elimu kunaleta mkanganyiko kwani inakuwa vigumu kueleza tafsiri ya madaraja hayo. Kwa mfano ‘Distinction’ ya kidato cha nne inaanza pointi 3.6 wakati ya ualimu inaanzia pointi 4.4,” alisema Waziri Ndalichako.
Pamoja na hatua hiyo aliyochukua, Profesa Ndalichako alisema bado Serikali haijaamua kuwachukualia hatua viongozi wa NECTA.
MTANZANIA
Mvua kubwa iliyonyesha Dar es Salaam usiku wa kuamkia jana   imesababisha maji kuingia na kujaa ndani ya jengo maarufu la maduka ya biashara la Mlimani City lililopo pembezoni mwa barabara ya Sam Nujoma.
MTANZANIA ilifika eneo hilo na kushuhudia maji yakiwa yametuama na kujaa katika maduka mbalimbali likiwamo duka kubwa la Nakumat, Duka la Sumsung na benki ya KCB Tawi la Mlimani City huku wafanyakazi wa jengo hilo wakihangaika kuyatoa nje kwa kuyachota.
Mmoja wa wafanyakazi wa Benki ya KCB, alisema mvua hiyo ilisabababisha maji kujaa katika eneo ambalo ujenzi unaendelea, lililopo pembezoni mwa jengo hilo na baadaye maji hayo yaliingilia mlango wa nyuma uliopo karibu na benki hiyo.
Alisema maji hayo yamesababisha athari kubwa kwa benki hiyo ikiwamo kuungua  baadhi ya vifaa vya umeme na kuchelewesha muda wa kufungua benki.
MTANZANIA
Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limepinga uamuzi wa serikali wa kulifuta kwenye daftari la msajili gazeti la Mawio kwa madai ya kuandika habari za uchochezi.
Pia limeitaka Serikali kutafakari upya na kwa kina uamuzi wake huo ambao TEF inautafsiri kama mwendelezo wa ukandamizaji wa tasnia ya habari.
Tamko la TEF lilitolewa   Dar es Saalam jana na Mwenyekiti wake, Absalom Kibanda na Katibu wake, Neville Meena.
Walieleza kutoridhishwa na nia ya serikali ya kupatikana kwa sheria bora ambazo imeahidi kuzifanyia kazi kuhusu tasnia ya habari.
“Hii ni aina mpya ya ukandamizaji wa uhuru wa vyombo vya habari nchini kwani serikali zilizopita zilikuwa zikipambana na vitendo vya kufungiwa kwa magazeti kwa muda maalum lakini si kuyafuta”.
Meena alisema katika serikali zilizopita adhabu kubwa iliyowahi kutolewa ilikuwa ni kulifungia kwa muda usiojulikana gazeti la MwanaHalisi kabla gazeti hilo kurejeshwa kwa umma na mahakama, kufungiwa siku 90 gazeti la Mtanzania na siku 14 gazeti la Mwananchi.
“Kwa kuwa hii inaonekana ni dhamira rasmi ya Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Magufuli kutumia sheria kandamizi kudhibiti demokrasia na uhuru wa habari, tunatoa wito kwa watawala wetu kutafakari upya suala hili na kuachana kabisa na dhamira hiyo isiyokuwa na tija kwa nchi yetu.
“Uamuzi wa kufuta Mawio (hata kama lilifanya makosa) umetufikirisha sana, tumetafakari kwa kina na kujiuliza kwamba habari ambazo ziliandikwa na gazeti hili zilikuwa hatari kwa kiasi gani kwa nchi kiasi cha kufikiwa uamuzi huo? Ni magazeti mangapi yatafuata baada ya Mawio ikiwa serikali itaendelea na ubabe wa aina hii?” alihoji Meena.
Katika hoja zake TEF imesema mfumo wa sasa wa kushughulikia matatizo au kasoro za taaluma katika vyombo vya habari ni kandamizi kwa vile  unamfanya Waziri kuwa ‘Mhariri Mkuu’ na ana mamlaka ya kutoa adhabu kwa kuzingatia mtizamo wake, hata kama utakuwa unakinzana na misingi ya taaluma.
“Tunajiuliza ikiwa kwa miezi takriban mitatu tu tangu kuanza kazi  serikali mpya (Novemba 5 mwaka jana alipoapishwa kuwa rais), serikali ya Dk Magufuli tayari imefuta gazeti moja itakuwaje katika safari ya miaka mitano ambayo atakuwa madarakani?” alihoji Meena.
Katibu huyo alisema kwa taaluma ya habari, Serikali bado imeendelea kujipa mamlaka ya “kukamata, kushtaki, kusikiliza kesi, kuhukumu na kufunga” kwa sababu  kama ilikuwa ni kesi iliyozaa hukumu ya kufutwa, basi uendeshaji wake ulifanyika katika “mahakama ya siri”.
Alisema  usiri huo matokeo yake ni hukumu ya siri ambayo haikuwapa wahusika kutoa utetezi wa kile kilichokuwa kikilalamikiwa dhidi yao.
MTANZANIA
Rais John Magufuli jana aliongoza mamia ya waombolezaji kuaga mwili wa Leticia Nyerere nyumbani kwa familia ya hayati Mwalimu   Nyerere, Msasani  Dar es Salaam.
Rais  aliwasili nyumbani hapo akiongozana na mkewe Janeth na moja kwa moja alikwenda kusaini kitabu cha maombolezo.
Viongozi wengine waliohudhuria ni pamoja na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sifue, marais na mawaziri wakuu wastaafu, Ali Hassan Mwinyi, Jakaya Kikwete, Mizengo Pinda   na Spika mstaafu,   Anna Makinda.
Mwili wa Leticia aliyefariki dunia  Marekani  alikokuwa amelazwa uliwasili  juzi saa 9 alasiri na kupokewa na ndugu, jamaa na marafiki katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam.
Baadaye  ulipelekwa katika Kanisa la Mtakatifu Peter kwa ajili ya Ibada   na neno la faraja kwa familia.
Viongozi mbalimbali wa Serikali akiwamo Rais mstaafu, Benjamin Mkapa waliongoza waombolezaji katika ibada hiyo. Wengine waliohudhuria ibada hiyo maalum ni Spika mstaafu, Anna Makinda na Jaji Joseph Warioba.
Jana mwili wa marehemu Leticia ulisafirishwa kupelekwa kijijini Butiama kwa  mazishi.
Leticia ambaye ni mtoto wa mwanasiasa mkongwe, Musobi Mageni alizaliwa wilayani Kwimba mkoani Mwanza 1954 na kupata elimu yake ndani na nje ya Tanzania kwa vipindi tofauti.
Marehemu Leticia ambaye ni mtalaka wa mtoto wa baba wa taifa, Madaraka Nyerere ameacha watoto watatu.
HABARILEO
Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda amewataka wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kujenga hoja vizuri katika Bunge linalotarajia kuanza vikao vyake wiki ijayo mjini Dodoma, kwa kuwa wabunge wa vyama vya upinzani wameongezeka bungeni.
Hayo yalisemwa jana Dar es Salaam na Pinda, baada ya kuaga mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu, Leticia Nyerere, aliyefariki akiwa Maryland nchini Marekani akipatiwa matibabu.
Akizungumzia Bunge la sasa, Pinda aliwashauri wabunge wanaounda Bunge hilo ambao wengi wao ni vijana, kuzingatia maslahi ya taifa na sio itikadi za vyama vyao na kuwasisitiza wabunge wa CCM, kujipanga na kwenda na hoja.
“Kila upande ujiandae kwenye kuwasilisha hoja, kuna ongezeko la wabunge wa upinzani, sasa wabunge wa CCM ni lazima nao wajipange na kujenga hoja vizuri,” alisema Pinda.
Alisema kwa mtazamo wake, Bunge ni zuri na sio la mivutano kwa kuwa kila mmoja amejipanga kuwasilisha hoja zitakazomgusa mwananchi kwa lengo la kumsaidia.
Akizungumzia utawala wa Awamu ya Tano wa Rais John Magufuli, Pinda alisema kila zama zina kitabu chake; na kwa utawala wa Rais Magufuli ameanza vizuri na kuomba Watanzania kumuunga mkono ili kufanikisha azma ya maendeleo ya taifa.
Alisema katika uongozi wake, ndio muda wa kuhakikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo inayoisha baada ya miaka 10 ijayo, inapaswa kuwa imetekelezwa, hivyo hatua mbalimbali anazozifanya rais, ikiwa ni pamoja na kubana matumizi, ni mambo muhimu.
“Hatua zinazofanywa na Rais Magufuli ni za msingi katika kuhakikisha dira ya Taifa ya Maendeleo inatekelezwa, ni vyema Watanzania wote tumuunge mkono juhudi zake”, alisema Waziri Mkuu mstaafu Pinda. Katika hatua nyingine, wabunge wa CCM wamepewa semina elekezi za namna ya kutekeleza ilani ya chama hicho.
Katibu wa Uenezi na Itikadi wa CCM, Nape Nnauye alisema hayo jana wakati akizungumzia kikao cha wabunge wa CCM, kilichofanyika kwa muda wa siku mbili. Alisema kikao hicho kilikuwa cha mashauriano juu ya wajibu wa mbunge wa CCM kwa jimbo na chama chake, kwani asilimia 68 ya wabunge ni wapya na wamefunzwa namna wabunge watakavyotekeleza Ilani ya CCM.
Pamoja na hayo, aliwataka waandishi wa habari wasiwe na mijadala yao kwani taarifa nyingi za magazeti wakati wa kikao hicho, zilikuwa za mitaani kwani mengi yaliyoripotiwa hayakujadiliwa kwenye semina elekezi. “Bora mngeniuliza kuliko kutafuta habari za mtaani, mengi ya yaliyoandikwa ni ya kutunga,” alisema Nape.
Wakati huo huo, vikao vya Kamati za Bunge vinaanza leo mjini Dodoma kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai kutoa majina ya uteuzi wa wajumbe wa kamati. Atafanya hivyo kwa mujibu wa Kanuni za Bunge.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha Bunge, Owen Mwandumbya alisema kwa mujibu wa ratiba, leo kutakuwa na uteuzi wa Kamati za Kudumu za Bunge na kufuatiwa na uchaguzi wa Wenyeviti na Makamu wao na wajumbe wa kamati kuelezwa wajibu, kazi na mipaka ya kazi za kamati, kupokea na kujadili mpango kazi wa kamati unaoisha Juni 2016.
Mwandumbya alisema Januari 22 kutakuwa ni mkutano wa wabunge wote na mada zitakuwa ni kanuni za kudumu za Bunge na uendeshaji wa Bunge, nadharia ya mgawanyo wa madaraka katika mhimili wa dola, haki na kinga na madaraka ya bunge, mamlaka ya spika na bunge, kazi, wajibu na masharti ya mbunge.
Pia Januari 23 mkutano wa wabunge wote, utaendelea na mada zitakuwa pamoja na maadili na miiko ya wbaunge, nafasi ya mbunge katika usalama wa taifa na itifaki ya mbunge.
Jumapili kutakuwa na kikao cha Kamati ya Uongozi na Jumatatu Januari 25 ni maelezo ya wabunge wote kuhusu Mpango wa Taifa wa Miaka Mitano, unaokusudiwa kutekelezwa katika Jamhuri ya Muungano.
HABARILEO
Chama cha Waongoza Watalii nchini(TTGA) kimetoa msaada wa dawa za kupambana na kipindupindu mkoani Arusha.
Mwenyekiti wa TTGA, Zadocvk Mgeta alimkabidhi Mkuu wa Mkoa Arusha, Felix Ntibenda dawa hizo huku akisema dawa na vifaa walivyotoa vinaweza kusaidia kaya 840 kudhibiti kipindupindu.
Alitaja dawa hizo kuwa ni sabuni, dawa za kuweka kwenye maji na dawa za kuzuia kuharisha.
Alisema wao kama mabalozi wa utalii, wanajua athari za Arusha kuwa na kipindupindu kwani tayari watalii wameanza kuogopa vyakula.
“Tumetoa msaada huu kama mchango wetu waongoza watalii lakini tuna imani wadau wengine watajitokeza kutoa misaada,” alisema.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Ntibenda alisema amewapa siku saba watendaji wa serikali katika ngazi mbali mbali mkoani hapa kuhakikisha kipindupindu kinamalizika.
Alisema hadi sasa Arusha ina wagonjwa wanne wa kipindupindu waliolazwa.
Alisema ametoa maagizo kwa wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri na watendaji wengine, kuhakikisha wanafika katika maeneo ambayo yamekuwa yakitoa wagonjwa na kudhibiti maambuikizi mapya.
“Leo nilikuwa na kamati ya ulinzi na usalama mkoa, nimetoa siku saba kipindupindu kiwe kimekwisha Arusha,”alisema.
Ntibenda alishukuru msaada wa TTGA wa dawa na vifaa mbalimbali vya kupambana na kipindupindu walivyokabidhi.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Dk Frida Mokiti alisema msaada huo utapelekwa kwenye maeneo ambayo yamekuwa na wagonjwa wa kipindupindu.
“Msaada huu utawafikia walengwa na tuna hakika utasaidia sana kupambana na ugonjwa huu,” alisema.
Chama cha waongoza watalii, kina jumla ya wanachama 6,512 ambao wanafanya kazi ya kuwaongoza watalii katika hifadhi za taifa na mbuga za wanyama na maeneo ya vivutio vya utalii.
MWANANCHI
Wakati Serikali ikihaha kuandaa mwongozo kwa vyuo na shule binafsi za msingi na sekondari ili kudhibiti viwango vya ada, hali ni tofauti kwenye shule za kimataifa ambazo zinaonekana kama zinachuana kwa kuwa na ada kubwa.
Wakati ada ya juu kwa shule zinazotumia Kiingereza kuanzia elimu ya msingi ni kati ya Sh2 milioni na Sh3 milioni, ada ya shule za kimataifa zilizopo nchini inafikia hadi Sh60 milioni mwa mwaka, kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na Mwananchi kwenye shule mbalimbali za jijini Dar es Salaam na baadhi ya mikoa.
Uchunguzi huo unaonyesha kuwa mwanafunzi wa chekechea hutakiwa kulipa hadi Sh35 milioni kwa mwaka na fedha hizo hulipwa kwa kutumia dola ya Marekani.
Baadhi ya shule zinapokea wanafunzi wenye asili ya Asia, nyingine hupokea wanafunzi kutoka nchi tofauti bila ya kubagua na ni dhahiri kuwa hata wazazi wa watoto ni wale wa kipato kikubwa.
Shule nyingi zinatumia Kiingereza katika kufundisha masomo yote darasani kwa mitalaa ya kimataifa na walimu wa kigeni ambao wanalipwa mishahara kwa viwango vya kimataifa.
Wanafunzi wanaosoma katika shule hizo wanaishi mazingira tofauti na wanaosoma katika shule za kawaida. Mwananchi lilishuhudia baadhi ya wanafunzi wa kike wakiwa wamevaa kaptura, bukta na sketi zinazoacha wazi mapaja, kufuga rasta huku wavulana wakiwa huru kufuga nywele, na kuvaa hereni bila kubanwa na sheria.
Shule na ada ni balaa Kwa kuzingatia nyaraka za kujiunga na shule ya International School of Tanganyika (IST) iliyoko Masaki, ada ya mwanafunzi wa mwaka wa kwanza na wa pili wa chekechea ni Sh35.9 milioni; darasa la tatu hadi la tano ada ni Sh 39.8 milioni na kwa wale wanaoingia darasa la sita, la saba na la nane ni Sh46. 3 milioni huku darasa la tisa na la kumi ada ni Sh49.2 milioni.
Mchanganuo wa ada kwa mwanafunzi anayeingia darasa la 11 na 12 ni Sh 59.4 milioni. Mbali ya ada hiyo, mwanafunzi hutakiwa pia kulipiwa gharama za ujenzi, ada ya dharura, fomu ya kujiunga shuleni pamoja na michango mingine ambavyo jumla ni Sh 19.8 milioni.
Shule nyingine ambayo tozo zake ­ ada na michango mingine – imefuata mkondo huo Braeburn iliyoko barabara ya Bagamoyo, Africana.
Ada ya mwanafunzi wa chekechea ni Sh 12.7 milioni kwa mwaka. Mwaka wa kwanza na wa pili ambao ni sawa na darasa la kwanza na la pili hulipa Sh19.3 milioni.
Darasa la tatu hadi la sita Sh21.1 milioni na darasa la saba hadi la tisa (sekondari) ni Sh25.4 milioni. Mwanafunzi anayejiunga na shule ya msingi ya Readers Rabbit iliyoko Masaki hutakiwa kulipa kiasi cha Sh24.1 milioni kwa mwaka.
MWANANCHI
Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT) Zanzibar, Asha Bakari Makame amefariki dunia leo huko Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu.
Taarifa zilizothibitishwa na wanafamilia pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa umoja huo visiwani Zanzibar, Salama Aboud Talib zinasema kiongozi huyo alikuwa ametoka nchini India kwa matibabu.
Naibu Katibu huyo amesema kuwa baada ya Makame kutoka India kwa matibabu, alipitia Dubai kwa mwanae, mahali ambapo mauti ilimkuta mapema leo.
Mbali na wadhifa huo ndani ya UWT, Asha Bakari Makame ameshawahi kuwa Waziri wa Wanawake na Watoto katika serikali ya awamu ya tano visiwani Zanzibar iliyokuwa chini ya Rais Salmin Amour.
Mbali na wadhifa huo, mwanasiasa huyo ameshawahi kuwa mwakilishi katika Baraza la Wawakilishi Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) na aliwahi kuwa mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba.
MWANANCHI
Polisi wilayani Mwanga Mkoa wa Kilimanjaro, wanadaiwa kumlinda raia wa China, anayetuhumiwa kufyatua risasi kiholela na kuwatisha wananchi.
Hata hivyo, Kamanda Polisi Mkoa Kilimanjaro, Ramadhan Mungi alisema jana kuwa, hana taarifa ya tukio hilo lililotokea Julai mwaka jana lakini atalifuatilia.
“Kila mtu anatakiwa kuheshimu sheria za nchi awe ni mgeni au Mtanzania, matumizi ya silaha yana masharti yake ambayo ni lazima yaheshimiwe. Nitafuatilia jambo hili,” alisema.
Mlalamikaji katika tukio hilo, Ally Ng’anzo ambaye ni mkurugenzi mwenza wa Kampuni ya Mega Copper alisema alishatoa maelezo yao polisi. “Siku hiyo nilipigiwa simu na wafanyakazi na wananchi wanaoishi jirani na Mchina aliyefyetua risasi kwenye mgodi wangu.
Nilikwenda lakini namshukuru nilikuta hakuna aliyejeruhiwa,” alisema Ng’anzo.
Alifafanua kuwa wafanyakazi walimweleza kuwa raia huyo alifyatua risasi tatu, mbili alizielekeza kwenye njia ya mgodi na nyingine alifyatua hewani na hawakujua sababu.
Hata hivyo, alisema baada ya kufungua jalada hilo, yeye na mashahidi waliandikisha maelezo yao lakini hadi sasa wanasubiri kuitwa mahakamani kutoa ushahidi.
Diwani wa Kata ya Shighatini, Enea Mrutu alisema raia huyo hana uhusiano mzuri na majirani zake lakini wanashangaa polisi kutochukua hatua dhidi yake.
“Hivi tujiulize kuna Mtanzania anaweza kwenda China akapewa kibali cha kumiliki silaha. Tuseme amepewa, anaweza kutisha watu kiasi hiki?” alihoji Mrutu.
Diwani huyo aliwataka polisi kukamilisha haraka uchunguzi wake akisema ushahidi dhidi ya Mchina huyo ulikuwa dhahiri lakini hajashtakiwa.
Kwa habari matukio na michezo ni hapa hapa Tangakumechablog

No comments:

Post a Comment