Friday, January 8, 2016

UCHAMBUZI WA MAGAZETI UNALETWA KWA HISANI KUBWA YA CANDLE

Magazeti yanaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu Cha Candle Education Centre Tanga, kituo kinaongoza kufaulisha wanafunzi na wanaojiendeleza kielimu, Candle Wapo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 772746
MWANANCHI
Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako amelipa siku saba Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) kutoa maelezo kwa kubadili mfumo wa kupanga madaraja ya matokeo ya kidato cha nne na sita, kutoka jumla ya pointi kwenda wastani wa pointi (GPA).
Aidha, waziri huyo aliyewahi kuwa katibu mtendaji wa Necta, kwa miaka tisa, amelitaka baraza hilo kueleza sababu za watahiniwa binafsi kuanza kufanya mitihani ya upimaji endelevu.
Maagizo hayo yalitolewa na Profesa Ndalichako alipokutana na menejimenti ya baraza hilo jana Dar es Salaam baada ya Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde kueleza kuwa walifanya mabadiliko hayo kutekeleza maelekezo kutoka Wizara ya Elimu.
“Hakikisheni mnakuwa na misingi mizuri ya kimaamuzi na msikubali kufanya maamuzi yasiyo na tija kwa Taifa letu,” alisema Profesa Ndalichako huku akitolea mfano jinsi alivyokataa kwa barua watahiniwa binafsi kufanya mtihani wa upimaji endelevu, wakati akiwa katibu mtendaji wa baraza hilo. “Tunawapa wiki moja mtupe maelezo.
Tunataka kujua ninyi kama Baraza mliona sababu gani za msingi kubadili huu mfumo; faida zake nini, na mliwashirikisha watu gani. Kazi ya kuhakikisha utendaji wa taasisi zetu unakuwa mzuri ndiyo imeanza,” alisema Profesa.
Majibizano Sakata hilo lilianza baada ya Dk Msonde kueleza sababu za mabadiliko hayo, huku akisisitiza mara kadhaa kuwa lengo lilikuwa kurahisisha udahili wa wanafunzi wa elimu ya juu.
“Yalikuwa maagizo ya kuzitaka taasisi zote za serikali na serikali yenyewe kuwa na mifumo inayofanana yaani mifumo ya matokeo ya Necta ihusishwe na mifumo ya udahili ya TCU (Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania) na Nacte (Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi),” alisema Dk Msonde.
Aliongeza; “Mfumo wa wastani wa pointi haujabadili chochote kuhusiana na mfumo wa jumla ya pointi. Tumeutumia katika matokeo ya kidato cha pili, cha nne na cha sita na haujaleta matatizo.
Wananchi na wanafunzi wa ngazi zote wanauelewa.” Majibu hayo yalimzindua Profesa Ndalichako na kuhoji, “Hivi ni lini TCU walisema kuna ugumu wa kudahili kwa sababu ya uwapo wa mfumo wa jumla ya pointi? Tueleze kulikuwa na athari gani awali mpaka muanze kutumia GPA?”
Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Simon Msanjila akitoa ufafanuzi kuhusu udahili wa wanafunzi wa elimu ya juu alisema, “Mfumo wa udahili unaangalia taaluma si GPA.
Mtu kama anakwenda kusoma taaluma fulani wanatazama masomo aliyosoma tu. Kama anakwenda kusoma sayansi watatazama masomo ya sayansi aliyosoma.
” Kutokana na kukosekana majibu sahihi, ndipo Profesa Ndalichako alitoa agizo hilo, huku akisisitiza kuwa ili Wizara ilielewe baraza hilo, lazima litoe sababu za msingi badala ya hizo walizoeleza jana.
Kuhusu mtihani wa upimaji endelevu, Profesa Ndalichako alisema haiwezekani watahiniwa binafsi kila somo wakafanya mitihani miwili, na kwamba ikiwa Necta haitatoa majibu ya kuridhisha, mitihani ya upimaji endelevu itafutwa.
Awali, akizungumza na wafanyakazi wa baraza hilo, Profesa Ndalichako alipongeza utaratibu wa kutoa vyeti mbadala kwa waliopoteza vyeti vyao halisi.
Pia, alilitaka baraza hilo kuwasilisha majibu ya mitihani ya watahiniwa wote ili wizara iyapitie. Alisisitiza kuwa wakati mwingine wanafunzi hushindwa kujibu chochote au kwa ufasaha kutokana na matatizo ya walimu.
MWANANCHI
Siku 74 baada ya kushindwa katika Uchaguzi Mkuu mwaka jana, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) jana kimefanya kikao cha kujitathmini na kuweka mpango kazi kwa miaka mitano ijayo.
Katika uchaguzi huo uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana, mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho, Edward Lowassa alishindwa na Rais John Magufuli wa CCM aliyepata kura Milioni 8.8 sawa na asilimia 58.5. Lowassa alipata kura Milioni 6 sawa na asilimia 39.97 ya kura zote.
Chadema pia ilipata wabunge 70, wakiwamo 36 wa viti maalumu huku CCM ikipata wabunge 188. Katika chaguzi ndogo saba zilizofanyika baada ya uchaguzi huo mkuu, CCM iliongeza wabunge takribani tisa, wakiwamo wa viti maalumu watatu na Chadema mbunge mmoja wa kuchaguliwa.
Taarifa iliyotolewa na chama hicho jana, ilieleza kuwa itajadili vipaumbele vyake vya mwaka 2016­2020 na kuwasilisha katika kikao cha kikatiba na uamuzi kwa ajili ya utekelezaji.
“Lengo ni kukiimarisha chama na kuiondoa CCM madarakani ili kuwaletea Watanzania mabadiliko ya kweli kuliko haya yanayofanyika sasa,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo iliyotolewa kwa vyombo vya habari.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho kilichofanyika mkoani Kilimanjaro zinaeleza kuwa moja ya ajenda ilikuwa ni kubadilishwa kwa idara za chama hicho kwa ajili ya kujipanga kwa ajili ya mkutano ujao wa Bunge.
“Pia, watajadili tamko la Waziri Mkuu, Kassim (Majaliwa) la kuzuia mikutano ya vyama vya siasa,” ilieleza taarifa hiyo.
MWANANCHI
Rais mstaafu Benjamin Mkapa amesema yuko tayari kufanya kazi yoyote na kutoa ushirikiano wake kwa serikali ya Rais John Magufuli endapo atahitajika.
Mkapa aliyeambatana na Waziri Mkuu Mstaafu Joseph Warioba ametoa kauli hiyo leo punde baada ya kukutana na Rais John Magufuli Ikulu, Dar es Salaam.
“Rais Mstaafu Mkapa pia amemhakikishia Rais Magufuli kuwa yuko tayari kutoa ushirikiano wakati wote ama kufanya kazi yoyote endapo atahitajika kufanya hivyo,” taarifa iliyotolewa na Ikulu leo mchana imeeleza.
Kwa mujibu wa Ikulu, malengo ya mkuu huyo wa zamani wa nchi kukutana na Rais Magufuli ni kumpongeza kwa dhamana aliyopewa na Watanzania kuiongoza nchi, kuunda serikali na kumtakia heri ya Mwaka Mpya.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, waziri mkuu mstaafu Jaji Joseph Warioba amempongeza katika juhudi zake katika kusimamia ukusanyaji wa mapato, kubana matumizi na kuelekeza matumizi kwenye maeneo muhimu ambayo yanawahusu wananchi yakiwemo afya na maji.
Aidha taarifa hiyo imeeleza kuwa Jaji Warioba amewataka Watanzania wote kumuunga mkono Rais Magufuli kwa kazi anazofanya ikiwemo kukomesha rushwa, ufisadi, matumizi mabaya ya madaraka na wizi wa mali ya umma.
“Lazima kila mmoja amuunge mkono Rais, tusije tukamuachia, pale ulipo kama ni mambo ya rushwa uanzie hapo hapo, kama ni mambo ya matumizi mabaya ya madaraka anzia hapohapo, tusije tukamuachia Rais pekee yake, yeye awe kiongozi wetu, lakini Watanzania wote tushughulike na matatizo hayo,” amesisitiza Jaji Warioba.

HABARILEO
Wizara ya Fedha na Mipango imetoa onyo kwa wakuu wa shule za msingi na sekondari watakaotumia ovyo Sh bilioni 18.77 zilizotolewa na serikali kwa ajili ya kutoa elimu bure.
Katika kuhakikisha fedha hizo zinatumika ipasavyo, wahusika wametakiwa kuweka wazi fedha walizopokea kutoka serikalini ili wananchi wafahamu alichopewa mhusika na matumizi yake.
Bodi za shule zimepewa kazi ya kuhakikisha zinasimamia matumizi ya fedha hizo na kutoa taarifa kwa atakayebainika kutumia fedha hizo vinginevyo ili ashughulikiwe.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alitoa maagizo hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mapato na namna Serikali ya Awamu ya Tano ilivyovunja rekodi katika ukusanyaji.
Aliwataka pia wakuu wa wilaya, mikoa na wakurugenzi wote nchini kusimamia fedha hizo ambazo Sh bilioni 14.7 zimepelekwa kwenye shule na Sh bilioni tatu zimepelekwa katika vyombo vya usimamizi wa mitihani.
Akizungumzia ukusanyaji wa mapato, Dk Mpango alisema Desemba mwaka jana walifikia Sh trilioni 1.592 ikiwa ni nyongeza ya asilimia 18.9 ya lengo la mwezi huo.
Alisema lengo la kukusanya mapato ya ndani kwa mwezi huo ilikadiriwa kuwa Sh trilioni 1.338 huku mwaka 2014 mwezi kama huo zilikusanywa Sh trilioni 1.104 ongezeko ambalo ni asilimia 44.2.
Alisema lengo la serikali ni kuongeza ukusanyaji mapato kufikia hadi Sh trilioni mbili kwa mwezi. Alisema dhamira ya serikali ya awamu ya tano ni kujitegemea na kuacha kuwa ombaomba.
Waziri Mpango alisema ukusanyaji mapato unavyozidi kuongezeka inasaidia kupunguza kutegemea wafadhili hivyo serikali itahakikisha inaziba mianya ya ukwepaji kodi kwa kukusanya ipasavyo huku kila Mtanzania akitimiza wajibu wake wa kulipa kodi.
Alisema wanaendelea kuweka mkazo katika ukusanyaji kodi katika maeneo mbalimbali ikiwemo utalii, tozo mbalimbali za misitu na uvuvi pamoja na viza na kujielekeza katika maeneo mengine yenye fursa kama ukusanyaji kodi za majengo.
Kaimu Kamishna wa TRA, Alphayo Kidata alisema awali waliweka lengo la kukusanya mapato ya Sh trilioni 1.04 Januari lakini kwa kuwa Desemba ilifikia Sh Trilioni 1.4 hawatashuka, badala yake wataongeza makusanyo.
Alisema wataalamu wako katika hatua za mwisho za matayarisho ya sheria ya majengo ili kuweza kukusanya kodi ipasavyo.
HABARILEO
Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), imesema inaendelea na mchakato wa kupokea maoni ya wadau mbalimbali kuhusu nauli zitakazotumika kwa ajili ya usafiri wa mabasi yaendayo kasi, na itahakikisha inatoa nauli zinazoendana na halisi halisi.
Meneja Mawasiliano wa Sumatra, David Mziray alisema wanafanyia kazi taarifa ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ya kukataa mapendekezo ya nauli yaliyotolewa na kampuni ya UDA Rapid Transit (UDA-RT) .
“Kama alivyosema Waziri Mkuu kuwa mapendekezo ya nauli hizi ni ya gharama kubwa na hata tulivyokutana na wadau kujadili mapendekezo haya wengi waliyapinga sasa sisi tunaendelea kukusanya maoni hadi Januari 13, baada ya hapo tutatoa uamuzi wa nauli ambazo hazitakandamiza upande wowote,” alisema Mziray.
Alisema mamlaka hiyo haitarejea tena mchakato wa kupokea mapendekezo mapya ya nauli kutoka kampuni ya UDA-RT bali itaendelea na utaratibu wa kukusanya maoni kutoka kwa wadau ambapo itatoa uamuzi kulingana na maoni hayo ya wadau.
Kampuni ya UDA-RT hivi karibuni ilitoa mapendekezo ya nauli inayotarajia zitumike katika mradi wa usafiri wa mabasi yaendayo haraka (DART) ambazo ni safari kwenye njia kuu kuwa Sh 1,200 na safari katika njia kuu na pembeni kuwa Sh 1400 na wanafunzi nusu ya nauli hizo.
Waziri Mkuu aliagiza taasisi zinazohusika; Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), ya Ujenzi na ya Uchukuzi, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) pamoja na kampuni ya UDA-RT kukutana haraka kujadili viwango vipya vya nauli vinavyoendana na hali halisi ya maisha ya wananchi.
Licha ya Waziri Mkuu kupinga nauli hizo, wadau wengine hususan Baraza la Walaji la Sumatra (Sumatra CCC), walihoji sababu za mabasi hayo yanayobeba watu wengi kwa safari moja na yanayotumia barabara zisizo na foleni, kutoza nauli kubwa.
NIPASHE
Mwanamke mmoja (jina linahifadhiwa)  anayedaiwa ni mke wa mtu, amefariki dunia katika nyumba ya kulala wageni katika Manispaa ya Bukoba, akiwa na mwanaume mwingine inayesemekana ni hawara yake.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Augustine Ollomi, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa, watu hao walienda katika nyumba hiyo ya kulala wageni iliyopo eneo la Hamugembe Januari 3, mwaka huu na kuchukua chumba namba nane.
Alisema siku iliyofuata saa 6:00 mchana, polisi walipokea taarifa kutoka kwa wahudumu wa nyumba hiyo ya kulala wageni kuwa katika chumba hicho kuna watu waliingia jana yake lakini hadi muda huo mlango wa chumba ulikuwa haujafunguliwa na kuna ukimya uliowatia hofu.
Alisema wahudumu hao waliambatana na polisi na walipofika eneo la nyumba hiyo walimkuta mmiliki wake ambaye alitoa funguo za akiba na kufungua chumba hicho.
“Polisi walipofungua chumba walikuta godoro liko chini lakini kitandani lilipopaswa kuwa kulikuwa na mwili wa mwanamke ukiwa umefunikwa shuka na kuuchukua kwenda kuuhifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera,” alisema.
Kamanda huyo wa polisi mkoa wa Kagera, alisema mtu aliyekuwa pamoja na mwanamke huyo (jina linahifadhiwa) ambaye ni dereva wa basi la abiria linalofanya safari zake kati ya Bukoba na Mwanza, hakukutwa katika chumba hicho na alifunga mlango kwa nje na kuondoka na funguo.
Hata hiyo, alisema chanzo cha kifo hicho hakijajulikana lakini kutokana na taarifa walizopata kutoka kwa msaidizi wa dereva huyo wamefanikiwa kumpata mtu aliyejitambulisha kuwa ni mume wa marehemu.
Kamanda Ollomi aliongeza kusema kuwa,  mume wa marehemu mkazi wa Butimba, jijini Mwanza, amepatikana na kukabidhiwa mwili wa mkewe, huku uchunguzi wa tukio hilo ukiendelea na kwamba wafanyakazi wawili wa nyumba hiyo ya kulala wageni wanashikiliwa na polisi kwa upelelezi zaidi lakini pia kwa kitendo cha kuficha taarifa za wageni wanaolala katika nyumba hiyo.
NIPASHE
Operesheni kubwa ya kubomoa nyumba zaidi ya 15,000 zilizojengwa katika maeneo yasiyostahili jijini Dar es Salaam, imekumbana na changamoto ya aina yake baada ya mmoja wa wasimamizi wa kazi hiyo kutoka Baraza la Taifa la Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira (NEMC), Heche Suguti, kuanguka ghafla akiwa ofisini kwake na kuwahishwa hospitali akiwa hoi.
Chanzo  kutoka ndani ya Nemc kimeiambia Nipashe kuwa Suguti ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Sheria katika baraza hilo, alianguka ofisini kwake majira ya saa 9:30 alasiri baada ya kurejea kutoka katika Mahakama Kuu kitengo cha ardhi kushughulikia kesi inayoikabili Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi dhidi ya wakazi 681 wa eneo la Mkwajuni, Kinondoni ambao wanapinga nyumba zao kubomolewa.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa baada ya Suguti kuanguka ghafla ofisini kwake eneo la Mikocheni, baadhi ya wafanyakazi wenzake (wa Nemc) walimsaidia haraka kwa kumbeba na kumpakiza kwenye gari na kumpeleka hospitali mbili tofauti ambako kote vipimo vya awali havikubaini tatizo.
“Baadaye alipelekwa katika Hospitali ya Aga Khan ambako alilazwa kuanzia siku hiyo (Jumanne) na kutolewa leo asubuhi (jana) baada ya kupata nafuu… ila kwa kifupi ni kwamba afya yake imeyumba na hadi sasa madaktari bado wanachunguza kujua ni kitu gani hasa kinachomsumbua,”
Mkurugenzi wa Nemc, Bonaventure Baya, alikiri kuwa Suguti aliugua baada ya kuanguka ofisini Jumanne wiki hii na kulazwa katika Hospitali ya Aga Khan, lakini haoni kama ni sahihi kuzungumzia afya yake kwani hayo ni masuala binafsi.
“Nadhani ni uchovu ndiyo uliokuwa unamsumbua… hata hivyo, hayo ni masuala binafsi.
Alipotafutwa kwa njia ya simu jana mchana, Suguti aliyekuwa akizungumza kwa taabu, alikiri kupatwa na tatizo asilolifahamu na kuanguka ofisini kabla ya kujikuta akiwa amelazwa katika wodi mojawapo ya Hospitali ya Aga Khan.
“Kwakweli sielewi kilichotokea. Nilipoingia ofisini kwangu baada ya kutoka kwenye kesi ya nyumba za watu wa Kinondoni, ghafla nikahisi kizunguzungu, giza kutanda na mwishowe nikaanguka… sijui kilichotokea baada ya hapo ila fahamu ziliponirudia nikajikuta nikiwa hospitali,” alisema Suguti.
Alipotakiwa kueleza zaidi kuhusiana na tukio hilo, Suguti hakuwa tayari kwa maelezo kuwa bado hajisikii vizuri.
“Kwa sasa naomba uniache tu, sijisikii kuzungumza zaidi,” alisema na kukata simu.
Baadhi ya watumishi wa Nemc waliozungumza na Nipashe, walisema wamestushwa na tukio hilo kwani halijawahi kutokea hapo kabla kwa Suguti kuanguka ghafla na kuugua kiasi kwamba asijitambue wakati wakimuwahisha hospitali.
Mmoja wa watumishi hao alisema siku hiyo, baada ya kurudi ofisini akitokea mahakamani, Suguti alikuwa mzima wa afya.

NIPASHE
Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, amesisitiza umuhimu wa wazazi kufuatilia maendeleo ya elimu ya watoto wao shuleni ili hatua mbalimbali zinazochukuliwa na serikali kuimarisha elimu zifikie malengo yaliyowekwa.
Amesema mabadiliko ya sera ya elimu yaliyofanywa na serikali  ambayo pamoja na mambo mengine, yatawawezesha vijana wa Zanzibar kumaliza elimu wakiwa na umri wa wastani kama nchi zingine, yanahitaji ushirikiano wa karibu kati ya serikali na wazazi ili yatekelezeke.
Amesema utaratibu wa sasa wa watoto kumaliza elimu ya msingi baada ya miaka sita badala ya saba, yatawafanya watoto kuingia sekondari wakiwa na umri mdogo, hivyo wazazi wanapaswa kufuatilia kwa karibu na kwa umakini zaidi kuhusu  maendeleo ya watoto wao kwa kushirikiana na walimu.
Dk. Shein aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na wananchi kwenye hafla ya uzinduzi wa Skuli ya Msingi ya Mnarani, wilayani Micheweni,  ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Aliwahakikishia wananchi kuwa serikali itaendelea kuimarisha sekta ya elimu ili kutimiza Malengo ya Mapinduzi ya mwaka 1964 ya kuwapatia elimu wananchi wote.
Katika kuimarisha elimu, Dk. Shein alisema serikali imeangalia upya ramani za shule nchini ambapo kutokana na ukosefu wa ardhi, shule sasa zitajengwa za ghorofa kwa kadiri hali itakavyoruhusu.
Aidha, Dk. Shein aliishukuru Taasisi ya Milele Zanzibar Foundation kwa kuchangia kwa kiwango kikubwa ujenzi wa skuli hiyo ambayo ujenzi wake wote uligharimu Sh. milioni 359.377.
Akitoa maelezo kuhusu ujenzi wa skuli hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali.
Kwa habari, matukio na michezo ni hapa hapa Tangakumekuchablog

No comments:

Post a Comment