Friday, January 15, 2016

UCHAMBUZI WA MAGAZETI NA CANDLE TANGA

Uchambuzi wa magazeti na Candle Education Centre Tanga
MTANZANIA
Aliyekuwa mgombea urais kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ambaye aliungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), Edward Lowassa, amesema anajipanga upya kushinda urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2020.
Lowassa aliweka wazi dhamira yake hiyo, jijini Dar es Salaam jana alipokuwa akizungumza na wafanyabiashara wanaomwunga mkono wanaojulikana kama Timu Mabadiliko wa Soko la Kariakoo ambao walitaka kusikia kauli na hatima yake kisiasa baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu mwaka jana.
Lowassa ambaye alipata kuwa waziri mkuu, alisema bado hajakata tamaa ya kuwaongoza Watanzania, licha ya vizingiti kadhaa alivyowekewa vikiwamo vya kumzuia kufanya ziara za kuwashukuru wananchi waliompigia kura nchi nzima.
“Wale walio na nia ya kutaka kujua mustakabali wangu kisiasa nawaambia kwamba pamoja na kuwepo kwa mambo ya kutaka kunikatisha tamaa, lakini sitakata tamaa na nipo tayari kuwania urais na kushinda kwa kipindi kijacho cha mwaka 2020.
“Niko fiti na morali yangu iko juu naiona kazi hiyo ndiyo kwanza imeanza najua kama Mungu amepanga nitakuwa rais wa Tanzania niko tayari kuanzia sasa na ninaamini tutashinda kama tulivyoshinda katika uchaguzi uliopita Oktoba 25, “alisema Lowassa.
Kiongozi huyo aliwataka wananchi nao pia kutokata tamaa ya kupata mabadiliko ya kweli kwa sababu yuko tayari kugombea hata mara tano ili apate haki yake kwa sababu anaamini kwa nguvu za Mwenyezi Mungu atakuja kuwa rais wa Tanzania.
“Sitakuwa kiongozi wa kwanza kuwania mara tano kwani yupo rais mmoja wa Marekani aliyewahi kuwania zaidi ya mara nne na alipogombea mara ya tano alifanikiwa kupata urais, mwingine ni rais wa Senegal Abdoulaye Wade,” alisema Lowassa.
Katika mkutano huo, Lowassa pia alizungumzia sababu za kutochukua hatua za kuwaruhusu wanachama na wafuasi wake kuingia barabarani kwa maandamano kudai ushindi.
Kwa mujibu wa Lowassa, hatua hiyo ilichangiwa na dhamira yake ya kutaka kulinda amani ya nchi.
“Matokeo yaliwashangaza wengi nikiwamo mimi mwenyewe, hali iliyosababisha wengi kuniomba nitoe kauli ya kuingia mitaani, lakini nikatumia busara kuwatuliza kwani ningewaruhusu wangechinjana lakini sikutaka kuingia Ikulu kwa kumwaga damu.
“Nawashukuru Watanzania kwa kuwa watulivu na kunisikiliza ombi langu lililowezesha Tanzania kuendelea kuwa na amani kwani sikuwa tayari kuona inavurugika kwa muda mfupi wakati imedumu tangu tulipopata uhuru kwa sababu ya kwenda Ikulu,’ alisema.
Lowassa alisema pamoja na kupokonywa ushindi wake, lakini anaamini vyama vya upinzani vimetoa changamoto kubwa kwa CCM na serikali ya awamu ya tano ambao wameamua kutumia baadhi ya sera zilizokuwa kwenye ilani yao ya uchaguzi.
“CCM wanatakiwa kuwa waungwana pindi wanapo nakili Ilani za Chadema, wanatakiwa kusema ukweli pindi wanapoichukua sera ya chama kama ile ya elimu bure kwa kuwa si jambo baya kwa sababu wanatimiza yale tuliyokuwa tukitaka kuwafanyia Watanzania,” alisema Lowassa.
MTANZANIA
Askari wa Jeshi la Polisi na raia wengine watatu wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam wakikabiliwa na tuhuma za unyang’anyi kwa kutumia bastola.
Mbele ya Hakimu Amalia Mushi, Wakili wa Serikali Masini Musa, aliwataja watuhumiwa hao ni askari E.7879 Koplo (CPL) Uswege (44) wa Kituo cha Polisi Mbezi – Kimara, David Kabadi (23), Kasu Gulam (60) na Hilal Ibrahim (70).
Wakili Musa alidai mahakamani hapo kuwa tukio hilo lilitokea Juni 10 mwaka jana maeneo ya Mbezi Afrikana.
Katika shtaka la kwanza, Musa alidai kuwa watuhumiwa waliiba magari mawili aina ya Toyota Prado na Mitsubishi Canter yote yana thamani ya Sh milioni 95 mali ya Abdul Said.
Musa aliongeza kuwa watuhumiwa kabla ya kufanya tukio hilo walimtishia kwa bastola Shaban Kasim ambaye alikuwa mlinzi katika karakana ya magari hayo.
Katika shtaka la pili, watuhumiwa hao wanadaiwa kufanya unyang’anyi kwa kutumia silaha ambapo katika maelezo yaliyosomwa na wakili Musa waliiba gari aina ya BMW yenye thamani ya Sh milioni 30 mali ya Jay Madeleka.
Baada ya kusomewa maelezo hayo watuhumiwa walikana mashtaka hayo na upelelezi bado unaendelea.
Mahakama ilisema kuwa shtaka hilo halina dhamana kisheria hivyo kesi hiyo iliahirishwa hadi Januari 28 mwaka huu ambapo itatajwa tena kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali na watuhumiwa walirudishwa mahabusu.
MTANZANIA
Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA), limeombwa kuiondoa nchi ya Burundi katika uanachama wa jumuiya hiyo na ile ya Umoja wa Afrika (AU) hadi hapo mgogoro wa kisiasa na kijamii utakapomalizika nchini humo.
Ombi hilo limewasilishwa mjini hapa jana na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Wanasheria wa Afrika, Donald Deya, alipowasilisha maombi ya mashirika sita yasiyo ya kiserikali kutoka EAC yaliyoomba kuzungumza na Bunge juu ya mgogoro wa Burundi.
Akizungumza mbele ya Kamati ya Mambo ya Ndani ya Bunge na Usuluhishi wa migogoro ya EALA inayoongozwa na Mwenyekiti Abdullah Mwinyi, Deya alisema nchini Burundi bado kuna shida ya kisiasa na kuna Serikali iliyochaguliwa, lakini si halali kisheria.
Alisema pamoja na maombi ya kuondolewa kwa nchi hiyo, bado itaendelea kushiriki kwa karibu katika meza ya mazungumzo kwa ajili ya kutafuta mwafaka utakaowezesha kupatikana kwa amani na kuondoa shida zinazowakabili kwa sasa.
“Kitu cha msingi ambacho tunaliomba Bunge hili, litumie mbinu zote kuhakikisha Warundi wote wamefika mezani kwenye mazungumzo ya kutoa mwafaka wa shida yao. Na mbinu wanazoweza kutumia zipo nyingi,” alisema Deya na kuongeza:
“Sisi tunasema kwa sasa Serikali ya Burundi iwekwe ‘suspended’ (pembeni) kabisa kwenye uanachama wa Afrika Mashariki (EAC) pamoja na ule wa Umoja wa Ulaya (AU),” alisema Deya.
Akiwasilisha maombi hayo ndani ya ukumbi wa Bunge uliopo Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki mjini hapa, Deya alisema kumekuwapo na ukiukaji mkubwa wa haki za kibinadamu na kijamii huku baadhi wakiogopa na kuiona nchi hiyo inaweza kuteketea na kuingia kwenye mauaji ya kimbari.
“Kwa maoni yetu ukilinganisha mazungumzo ya utatuzi wa mgogoro wa Burundi na mazungumzo yaliyosaidia kuiondoa Kenya kwenye machafuko mabaya ya kisiasa mwaka 2008, utaona tofauti kubwa kabisa,” alisema Deya.
Akifafanua kuhusu mazungumzo yaliyoinusuru Kenya kutumbikia kwenye wimbi la mauaji zaidi, alisema aliyekuwa Mwenyekiti wa AU na Rais wa Ghana, John Kufor, aliiwezesha nchi hiyo kurejea kwenye amani tofauti na ilivyo kwa Burundi leo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge EALA, Mwinyi alisema kwamba maombi yaliyowasilishwa na mashirika hayo sita kupitia jopo la wanasheria wa Afrika yamesikilizwa na wajumbe wa kamati hiyo.
“Kuna mambo mengi wamependekeza, leo wajibu wetu Kamati ya Bunge ni kuyasikiliza na kutafuta ufafanuzi wa kina, ushahidi na baada ya hapo kamati itakaa kwa ajili ya kuyajadili na baadaye tutaandika ripoti na kuipeleka Bunge ili nalo lijadili na kutoa maazimio ya mapandekezo,” alisema Mwinyi na kuongeza:
MWANANCHI
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Edwin Ngonyani ameiagiza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ichunguze iwapo kuna wizi unaofanywa na kampuni za simu kwa wateja wake.
Ngonyani alitoa maagizo hayo jana katika hafla ya uzinduzi wa duka la ‘Airtel EXPO’ linalotoa huduma mbalimbali za simu na elimu ya matumizi ya vifaa vya mawasiliano akisema amepokea malalamiko ya aina mbili kutoka kwa Watanzania wanaotumia huduma za kampuni za simu nchini.
Ngonyani alisema kutokana na mazingira hayo, imekuwa ikijengeka taswira kwamba, watumishi wa kampuni za simu wanahusika katika wizi huo.
Aliiagiza TCRA kuchunguza tuhuma hizo huku akiwataka wananchi kuwasilisha malalamiko yao katika mamlaka hayo ili kutafuta ufumbuzi.
Kwa mujibu TCRA, Watanzania milioni 32 wanatumia huduma simu za mkononi, sawa na asilimia 67 huku takriban wateja milioni nane wakitumia za intaneti.
Akizungumzia tuhuma hizo, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Airtel Tanzania, Beatrice Singano alisema malalamiko yote ya wateja wao yamekuwa yakitafutiwa ufumbuzi kwa njia mbalimbali. “Wateja wote tunawasaidia kupitia kituo cha huduma kwa mteja ambacho kinafanya kazi wakati wote.
Kwa upande wetu, wateja wanasikilizwa,” alisema. Msemaji wa TCRA, Innocent Mungy alisema wamepokea maagizo ya naibu waziri na wataanza kuyatekeleza kwa mujibu wa Sheria ya TCRA ya 2003 na ile ya Mawasiliano na Posta ya 2010. “Lakini pia tuna kanuni zinazotusaidia katika utekelezaji wa sheria hizo, kwa hiyo agizo hilo litashughulikiwa, lakini siwezi kusema lini,” alisema.
Mungy alisema malalamiko ya wateja kuhusu hisia za kuibiwa yamekuwa yakiripotiwa kwa wingi kila siku na kupokewa sehemu husika ili kutafutiwa ufumbuzi. “Kwanza malalamiko yanayohusu kampuni fulani yanapokewa na kampuni husika ili kujibiwa, kabla ya TCRA hatujahusika kumaliza malalamiko ya mteja huyo,” alisema.
Hata hivyo, alisema bado elimu inahitajika zaidi katika matumizi ya ofa za vifurushi vya intaneti na muda wa maongezi. “Kuna mambo mengine yanachangiwa na simu zetu za kisasa, kwani unaweza kuliwa fedha zako kwa kosa la kujiunganisha au kutokujua jinsi ya ulaji wa vifurushi kwenye simu,” alisema.
Desemba mwaka jana, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk Ally Simba alitoa adhabu ya faini ya Sh125 milioni kwa kampuni tano za simu za mkononi kwa kushindwa kuweka mazingira salama kwa wateja.
Kampuni hizo ni Airtel, Tigo, Smart, Halotel na Zantel ambazo zilitakiwa kulipa faini kwa sababu zilishindwa kutii agizo la mamlaka hiyo ya kulinda wateja wake huku vitendo vya utapeli wa kutuma ujumbe wa udanganyifu na ulaghai kwenye mitandao vikiendelea.
MWANANCHI
Mvua kubwa iliyonyesha kwa zaidi ya saa nne jijini hapa jana, imesababisha kifo cha mwanafunzi na uharibifu wa mali zenye thamani ya mamilioni ya fedha.
Wananchi wamedai kuwa mvua hiyo, iliyonyesha kuanzia saa 4:00 asubuhi hadi saa 9:00 alasiri, haijawahi kushuhudiwa kwa kipindi cha zaidi ya miaka minne iliyopita.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Mabatini, Ntobi Ntobi pamoja na kaimu kamanda wa kikosi cha Zimamoto jijini Mwanza, Hamidu Nguya walithibitisha kutokea kwa kifo cha mtoto huyo, Jenipher Joseph (6), aliyekuwa mwanafunzi wa Shule ya Msingi Mabatini.
Kamanda Nguya alisema mtoto huyo alisombwa na maji na baba yake, James Joseph walipoteleza na kuangukia mtoni wakati wakivuka daraja la Mto Mirongo uliokuwa umefurika.
“Baada ya kuanguka mtoni, baba alijikuta akimwachia mikono mtoto wake katika harakati za kujiokoa na aliposhtuka tayari mtoto yule alikuwa amesombwa na maji na juhudi za kumwokoa zilishindikana,” alisema Kamanda Nguya.
Miongoni mwa waliopoteza mali ni pamoja na Juma Said, mmiliki wa duka la vifaa vya shule na ofisi zenye thamani ya zaidi ya Sh7.5 milioni.
Licha ya ubovu wa miundombinu, eneo la Mabatini hukumbwa na mafuriko ya mara kwa mara kutokana na ujenzi holela uliobana kingo za Mto Mirongo. Hadi saa 12:00 jioni jana, Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji kilikuwa kikiendelea na juhudi za uokoaji na kutafuta miili ya watu wanaodhaniwa kuwa wamesombwa na mafuriko hayo.
MWANANCHI
Wakati Serikali ya Awamu ya Tano ikisisitiza kutoa elimu bure kwa shule za msingi na sekondari, mpango huo umesababisha adha kwa baadhi ya shule ikiwamo kukosekana walimu wa ziada, kuibwa vifaa vya kufundishia na ongezeko la wanafunzi.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili katika shule za msingi na sekondari katika wilaya za Ilala, Kinondoni na Temeke, umebaini kuwa mpango huo badala ya kuwa msaada kwa walimu umekuwa mzigo unaowapasua kichwa.
Fedha za ruzuku zinazopelekwa katika shule kwa mchanganuo maalumu kulingana na idadi ya wanafunzi, hazikidhi matumizi ya shule hizo hata kwa wiki mbili.
Mchanganuo wa fedha za ruzuku Wilaya ya Kinondoni, unaonyesha kuwa ni shule tano pekee ambazo zimepewa fedha ya chakula ni Kawe A, Mbuyuni, Msasani A, Msewe na Sinza Maalumu, huku nyingine zote zikiwa hazina fedha za kulipa walinzi, bili ya maji, umeme, ukarabati wa madawati, madarasa na vyoo.
Katika Wilaya ya Temeke, shule kadhaa zimevunjiwa madarasa, ofisi za walimu na kuibwa vifaa vya kufundishia, meza, viti kutokana na kukosekana walinzi ambao walikuwa wakilipwa kwa ushirikiano wa shule na wazazi.
Mlinzi mmoja hulipwa kati ya Sh150,000 hadi 200,000. Mpango huo umekuwa mwiba mchungu kwa walimu wa shule hasa za sekondari ambao walitakiwa kuwa wabunifu kwa kutafuta jinsi ya kuongeza ufaulu wa wanafunzi na kushirikiana na wazazi kulipa walimu wa ziada hasa wa masomo ya sayansi.
“Nimeajiri walimu sita wa masomo ya sayansi kwa kushirikiana na wazazi, ambao hapa kwangu nina mahitaji makubwa huku akiwapo mmoja aliyeajiriwa na Serikali.
Kwa mwezi nawalipa Sh300,000 hadi 350,000, najiuliza nitawalipa nini na fedha ya ruzuku haina fungu hilo? Bado mlinzi, bado maji, bado umeme, nimechanganyikiwa natamani kurudi kijijini nikalime kuliko fedheha hii, ”alisema mmoja wakuu wa shule ya sekondari wilayani Temeke ambaye hakuwa tayari jina lake liandikwe gazetini.
Alisema mwaka huwa ana mitihani minne wa Machi, Juni, Septemba na Desemba, ambayo kila mmoja hadi unamalizika humgharimu Sh1.5 milioni, kwa bahati mbaya fedha ya ruzuku aliyopata kwa mchanganuo wote ni Sh4.8 milioni hivyo kwa mitihani pekee anatumia Sh6 milioni ambazo hafahamu atazitoa wapi huku fedha za ruzuku zikiacha hayo yote bila majibu wala ufafanuzi. “…Wazazi wametangaziwa elimu bure kwa kishindo, sielewi itakuwaje na waliendelea kufundisha mwezi uliopita wananidai na sifahamu mwezi huu nitawapa nini,” alisema mwalimu mwingine.
Katika shule za msingi, tatizo kuu lililojitokeza ni wanafunzi kuwa wengi kuliko uwezo wa shule. “Mwaka jana na mwaka juzi, wiki ya kwanza shuleni nilikuwa nimekadiria kuandikisha wanafunzi 250, wakaongezeka hadi 300, lakini hadi asubuhi ya leo (jana) nimeandikisha wanafunzi 600, ” alisema mwalimu mkuu wa shule moja wilayani Temeke ambaye pia aliomba jina lake lisiandikwe gazetini.
Alisema kwa ongezeko hilo kila darasa watakaa wanafunzi 150 badala ya 50 waliokuwa wanakaa awali. “Hatuwezi kuwakataa tutaambiwa tunakataa wanafunzi, bado wanakuja hadi Machi, sijui itakuwaje,” alisema mwalimu mwingine wa shule ya msingi wilayani humo.
Alisema mbali ya hilo wamelazimika kutoa elimu ya ziada kwa wazazi, kutokana na wengi wao kuwaleta wanafunzi wakiwa hawana kitu chochote hadi begi la kubebea madaftari.
“Ukiwauliza wazazi mbona mtoto hana kitu zaidi ya sare alizovaa anakuambia wametangaziwa elimu bure, kibaya zaidi hata nembo hawana, tunashindwa kuwaambia walipe Sh500 au 1,000 ya nembo watasema tunawalipisha,” alisema. Alifafanua ikitokea wanafunzi wamepata matatizo itakuwa ngumu kuwatambua, kutokana na kutokuwa na nembo,” alisema.
Akizungumzia changamoto ya ruzuku, Ofisa Elimu Mkoa wa Dar es Salaam, Raymond Mapunda alisema shule zinazopata tabu ya ruzuku ni zenye wanafunzi wachache kwani zilizo na wengi hazipati adha hiyo kwa kuwa zinapata fedha nyingi.
Alisema Serikali imepanga kila mwanafunzi kwa mwaka atumie Sh10,000 hivyo zitatolewa kidogokidogo hadi zitimie: “Hizo changamoto zilizopo zitafanyiwa.
NIPASHE
Mwalimu wa Shule ya Msingi Peramiho, Songea mkoani Ruvuma, Baraka Mwakajila (29), amekutwa amefariki dunia baada ya kujinyonga kwa kutumia shati ndani ya nyumba alimokuwa akiishi.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Revocatus Malimi, alisema jana kuwa tukio hilo limetokea juzi saa sita mchana katika mji mdogo wa Peramiho, nje kidogo ya Manispaa ya Songea.
Malimi alisema inadaiwa kuwa siku hiyo ya tukio, Mwalimu Mkuu Msaidizi, Rashid Pilly, aligundua kujinyonga kwa mwalimu huyo, baada ya kupita eneo la nyumba aliyokuwa anaishi na kuona nzi wengi wametapakaa kwenye eneo la dirisha la chumba alichokuwa analala.
Alifafanua zaidi kuwa Mwalimu Pilly baada ya kuona hali hiyo, alisogea hadi mlangoni na kukutwa mlango ukiwa umefungwa huku eneo hilo likiwa na harufu kali iliyoashiria kuna kitu ambacho kimeoza.
Alisema baadaye Mwalimu Pilly alilazimika kwenda kutoa taarifa kwenye kituo kidogo cha Polisi cha Peramiho na baadaye askari polisi wakiwa wameongozana na mganga, walifika eneo la tukio.
Baada ya kufika, alisema walivunja mlango na kuingia ndani ya nyumba hiyo ambako walimkuta Mwalimu Mwakajila akiwa tayari ameshakufa muda mrefu baada ya kujinyonga.
Alisema Mwakajila alijinyonga ndani ya nyumba ambayo ni mali ya shule na askari walikuta barua chini ya sehemu aliyojinyongea iliyokuwa imeandikwa Januari 4 mwaka huu na mwanamke (jina linahifadhiwa), anayedaiwa kuwa ni mpenzi wake, ambaye alimtaka aachane naye na aendelee na maisha yake.
Malimi alisema polisi baada ya kuiona na kuisoma, waliendelea kuufanyia upekuzi mwili wa marehemu na kukuta pia karatasi kwenye mfuko wa suruali yake, ambayo Mwakajila aliandika Januari 2, mwaka huu, akimtuhumu mpenzi wake huyo kuwa amekuwa malaya na mlevi
Kamanda Malimi alisema polisi wanaendelea na uchunguzi zaidi kuhusiana na tukio hilo na mwili wa marehemu umekabidhiwa kwa ndugu kwa ajiki ya taratibu za mazishi.
NIPASHE
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Prof. Makame Mbarawa, amesema ni umuhimu taasisi zote za serikali kuwa na mfumo wa kielekroniki (EAR) wa mahudhurio kazini ya watumishi wake.
Akizungumza mara baada ya kujisajili katika nfumo huo katika wizara yake jijini Dar es Salaam jana, Prof. Mbarawa alisema kwa kuanzia utaratibu huo utatumika katika sekta uchukuzi na ujenzi na kisha utafungwa katika taasisi zote za serikali ili kuhakikisha watumishi wa umma wanafika ofisini kwa wakati na kupunguza utoro.
“Hakikisheni watumishi wote wanatumia mfumo huu wa kielektroniki ili kudhibiti utoro na watu kufanyakazi kwa muda unaokubalika kiserikali”, amesema.
Aidha, waziri huyo aliwataka wafanyakazi wa mapokezi wa wizara hiyo kuacha kuwafungulia wafanyakazi watoro na wanaochelewa kuingia ofisini bila ya kupitia mfumo huo ili kuwatambua watumishi watoro waweze kuchukuliwa hatua stahiki.
Amesisitiza mfumo huo utakapofungwa katika taasisi zote za umma utadhibiti watoro kwa kuwa unaweka kumbukumbu  ya muda mtu anaokuwa kazini na hivyo kuwawezesha viongozi kupata taarifa sahihi za mahudhurio.
NIPASHE
Jeshi la Polisi Mkoani Katavi linamshikilia mkazi wa mji wa Mpanda, kwa tuhuma za kumnyanyasa kwa kumnyima mahitaji muhimu mtoto wake ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa juzi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari, alisema polisi walipata taarifa hiyo kupitia kituo kimoja cha radio kilichopo mkoani humo wakati mtoto huyo akihojiwa.
Alisema baada ya polisi kusikia kipindi hicho, walifuatilia na kumpata mtoto huyo na kumhoji na kubaini kuwa mzazi wake amekuwa akimnyima mahitaji muhimu ya kimaisha kama mavazi, chakula, matibabu na mahitaji ya shule.
Kamanda Kadavashari alisema mtoto huyo tangu mama yake mzazi afariki dunia mwaka jana na baba yake kuoa mke  mwingine, maisha yake yalibadilika na kuanza kuishi maisha ya manyanyaso na mateso, hali iliyomsababisha hata kushindwa kuendelea vizuri na masomo.
Alisema katika kanisa ambalo mzazi huyo anasali pamoja na mtoto huyo, imekuwa ikitolewa michango kwa lengo la kumsaidia lakini mtoto huyo hamfikii na kwamba hivi karibuni baba yake alimfukuza nyumbani na kuanza kuishi kwa kutangatanga mitaani.
Kamanda huyo wa polisi mkoa wa Katavi, alisema baada ya baba wa mtoto huyo kusikia kipindi hicho cha radio, alikwenda polisi kutoa taarifa za kupotelewa na mtoto wake huyo na polisi kumshikilia na walipomuhoji walibaini amekuwa akimnyanyasa mtoto wake na tayari amefunguliwa mashtaka na atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.
NIPASHE
Zikiwa zimepita siku tano tangu Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, aagize mabasi ya mwedo kasi yaanze kutoa huduma jijini Dar es Salaam, Nipashe limebaini kwamba mbali ya kasoro lukuki zinazotajwa, mabasi yaliyoingizwa nchini kwa kazi huduma hiyo, hayajalipiwa kodi.
Itakumbukwa kwamba mradi huo ulitarajiwa kuanza kutoa huduma jijini Dar es Salaam Oktoba, mwaka jana, lakini haikuwa hivyo.
Waziri Mkuu Majaliwa alitembelea mradi huo Desemba, mwaka jana na kuagiza kuwa mabasi hayo ya mwendo kasi yaanze kutoa huduma jijini Dar es Salaam Januri 10, mwaka huu, agizo ambalo halijatekelezwa.
Agosti 16, mwaka jana, serikali ilizindua mafunzo kwa madereva 330 wa kuendesha mabasi hayo.
Aidha, Septemba 20, mwaka jana, mabasi 138 yaliwasili katika Bandari ya Dar es Salaam na kuelezwa kwamba yataanza kutoa huduma Oktoba, mwaka jana.
Akiwa bandarini hapo kushuhudia mabasi hayo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick, alisema:
“Tumefikia hatua nzuri na naipongeza Kampuni ya Uda Rapid Transit (Uda-RT) kwa kuleta mabasi haya kwa ajili ya kuanza kutoa huduma ya usafiri katika kipindi cha mpito. Hii itasaidia kuondoa adha ya usafiri kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam.”
Alisema kampuni hiyo imepewa jukumu la kuendesha kipindi cha mpito ili wapate uzoefu na zabuni ya mwendesha mradi kipindi cha kudumu itakapotangazwa itasaidia wao kushindana.
Hata hivyo, uchunguzi wa gazeti hili umeonyesha kwamba sehemu kubwa ya mabasi hayo bado yapo chini ya Kamishna wa Forodha kutokana na kutolipiwa kodi.
Jana, Mkurugenzi wa Idara ya Elimu na Huduma kwa Walipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo, alithibitisha kuwa magari hayo yapo chini ya Kamishna wa Foforodha ikiwa ni taratibu za kawaida kwa magari ama vitu vingine ambavyo havijalipiwa kodi.
“Sisi kwa kawaida mzigo mpaka ulipiwe kodi ndipo unapotolewa. Kama haujalipiwa kodi unakuwa chini ya Msimamizi wa Forodha. Huu ni utaratibu wa kawaida sana.
Kwa hiyo haya mabasi yapo chini ya Msimamizi wa Forodha, ni kama magari mengine yaliyo huko `show room’  (maeneo ya kuuza magari), hayajalipiwa kodi, lakini yakiuzwa, wahusika huja kulipia kodi na hivyo kuanza kufanya kazi,” alisema Kayombo.
Hata hivyo, Kayombo hakuwa tayari kusema ni kiasi gani kinachodaiwa kwa magari hayo kwa maelezo kwamba hilo ni suala la kujadili na mlipa kodi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Uda, Simon Kisehna, alisema tayari ofisi yake iko katika mchakato wa kukamilisha masuala ya kodi TRA na kwamba mradi utaanza kama ilivyoagizwa na Waziri Mkuu ili kutoa huduma kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam.
Kisehna alisema miundombinu ya mradi huo kwa sehemu kubwa iko sawa na huduma zitaanza kutolewa hivi karibuni.
NIPASHE
Wakati utekelezaji wa kuanza darasa la kwanza mpaka kidato cha nne ukiendelea kuleta mkanganyiko kwa wazazi kutojua wanachopaswa kuchangia ama kutochangia, imebainika kwamba mwongozo uliotolewa na serikali unaelekeza wazazi kuendelea kujitolea nguvu na mali kwa shule zilizo maeneo hayo.
Katika mwongozo huo, eneo linalozungumzia majukumu ya wazazi na walezi, linasema: “Wazazi na wananchi wengine pia wanatakiwa kuendelea kujitolea nguvukazi na mali ili kuleta ustawi na maendeleo ya shule zilizoko ndani ya jamii.”
Kutokana na kipengele hicho, ni wazi kwamba baadhi ya shule bado zitaendelea kuwatoza wazai michango ama kuchangia vitu vingine tofauti na ambavyo wazazi wengi waliamini kwamba kwa sasa hawatachangia chochote kwa elimu ya watoto wao.
Tayari kumekuwa na malalamiko kutoka kwa baadhi ya wazazi wakisema watoto wao wamerudishwa nyumbani wakitakiwa kuchangia vitu mbalimbali ikiwa ni pamoja na chakula na fedha tasilim.
Kwa mujibu wa mwongozo huo wa Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, wazazi wanatakiwa pia kununua sare za shule na michezo, vifaa vya kujifunzia yakiwamo madaftari na kalamu na chakula kwa wanafunzi wa kutwa pamoja na matibabu kwa watoto wao.
“Wanatakiwa pia kulipia nauli ya kwenda shule na kurudi kwa wanafunzi wa kutwa na wanafunzi wa bweni wakati wa likizo, kununua magodoro, shuka, vifaa vya usafi binafsi kwa wanafunzi wanaosoma shule za bweni na wanaoishi katika hosteli,” unasema mwongozo huo.
Alipopigiwa simu kutoa ufafanuzi, Kamishna wa Elimu, Prof. Eustella Bhalalusesa, baada ya kuulizwa swali na mwandishi alikata simu na kusema yupo kwenye kikao.
Katika hatua nyingine, Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mukoba, alisema mishahara midogo kwa walimu, mazingira mabovu ya kazi na ongezeko la wanafunzi lisiloendana na miundombinu, ni changamoto nyingine kwenye kutimiza lengo hilo la elimu bure.
“Serikali haijaangalia matatizo ya walimu kama mishahara midogo. Siku zote walimu wamekuwa wakilipwa mishahara midogo na ujue hata watoto ambao hawakutaka kuja shule watakuja,” alisema.
Alisema mishahara midogo ni kikwazo kwa kuwa walimu wanakata tamaa.
Taarifa zinaonyesha kuwa mwalimu mpya wa Daraja 3A wa shule ya msingi aliyeajiriwa Julai, mwaka jana, anaanza na mshahara wa Sh. 477,000 kwa mwezi ambao baada ya makato hupokea Sh. 360,000.
HABARILEO
Wizara  ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeagiza kukamatwa kwa watu waliohusika kuwaozesha watoto wao wa umri wa miaka 13 na kuwakatisha masomo katika mkoa wa Shinyanga na Dodoma.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Wizara hiyo, Erasto Ching’oro alisema hayo katika taarifa yake aliyoitoa kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam.
Ching’oro alisema wakati mtoto ambaye ni mwanafunzi wa shule ya msingi Wishiteleja wilayani Kishapu mkoa wa Shinyanga ameozeshwa kwa nguvu kwa mahari ya ng’ombe 13 na kukatishwa masomo akiwa darasa la sita, mtoto mwingine wa mtaa wa Chikole kata ya Msalato, Dodoma inasemekana ameozeshwa kwa mahari ya Sh 600,000.
Alisema kutokana na kuwepo kwa matukio hayo, Wizara ilivitaka vyombo vya dola kwa kushirikiana na Kamati za Ulinzi wa Mtoto katika mikoa yote, kuhakikisha kuwa watuhumiwa wanachukuliwa hatua kali.
“Tukio la kuwaoza watoto wadogo katika umri mdogo siyo tu linakinzana na haki za msingi za mtoto bali pia linamkosesha mtoto haki ya kuendelezwa akiwa ni pamoja na kuhatarisha uhai wake kwa kupatiwa majukumu ya mtu mzima katika umri mdogo,” alisema Ching’oro.
Alisema wizara inawataka wazazi na walezi kubadilika na kuachana na tabia ya kuwaoza watoto wao katika umri mdogo, maana vitendo hivyo ni vya kikatili.
Aliongeza kuwa jamii inatakiwa kutambua kuwa vitendo vya kikatili kama hivyo, vinapofanywa katika familia vinarudisha nyuma juhudi za serikali za kupambana na ukatili, maana kwa kiasi kikubwa familia inatakiwa kuwa mahala salama panapofaa watoto kuishi na kulindwa.
Pia alisema wizara inakumbusha wazazi, walezi na wadau wengine kuwa ndoa za utotoni ni kinyume cha Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009 na mikataba ya kimataifa kuhusu haki na ustawi wa mtoto.
Alisema ni wajibu wa kila mtu, kuhakikisha kuwa watoto wanaishi katika usalama na kuhakikishiwa haki zao zote za msingi, ikiwemo kulindwa, kuendelezwa, kuishi na kushirikishwa katika maisha ya kila siku ili kujenga taifa linaloheshimu maslahi ya watoto.
Juzi gazeti hili liliripoti kuwa mtoto mwenye umri wa miaka 13 anayesoma darasa la sita katika shule ya msingi Wishiteleja wilayani Kishapu, ameozeshwa kwa nguvu na wazazi wake baada ya kupokea mahari ya ng’ombe 13.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Shirika la AGAPE, John Myola, mwanafunzi huyo alifungishwa ndoa ya kimila Septemba 25, mwaka jana katika kitongoji cha Nyamikoma kijiji cha Buchambi wilayani Kishapu.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Hawa Ngh’umbi aliyekiri kupokea nakala ya barua kutoka Agape iliyozungumzia juu ya kufungishwa ndoa kwa mtoto huyo, alikemea kitendo hicho na kuahidi kumsaka mtuhumiwa akamatwe na kufikishwa mahakamani.
Mkoani Dodoma, mama mmoja anatuhumiwa kutaka kumuozesha mtoto wake mwenye miaka 13 (jina linahifadhiwa) baada ya kupokea mahari ya Sh 600,000 na ng’ombe wanne.
HABARILEO
Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Morogoro imewatia mbaroni wahamiaji haramu 48 na kuwafukuza nchini na baadhi yao kufikishwa mahakamani kwa kuingia nchini na kufanya kazi kinyume cha sheria.
Wahamiaji haramu hao walikamatwa kwa nyakati tofauti kuanzia Septemba mwaka jana hadi Januari mwaka huu kutokana na msako mkali uliofanywa na maofisa wa idara hiyo katika maeneo mbalimbali ndani ya mkoa huo.
Naibu Kamishna wa Uhamiaji wa Mkoa wa Morogoro, Agustino Haule, alisema hayo jana ofisini kwake mjini hapa alipokuwa akielezea hatua mbalimbali zinazochukuliwa na idara hiyo katika hatua ya kukabiliana na wimbi la wahamiaji haramu na walioingia nchini na kufanya kazi kinyume cha sheria.
Alisema wahamiaji haramu kutoka mataifa mbalimbali walipatikana katika msako uliofanyika maeneo mbalimbali ikiwemo viwandani, shuleni, majumbani na katika taasisi mbalimbali zilizopo mkoani Morogoro. Hivyo aliwataja wahamiaji haramu hao ni kutoka katika nchi za Kenya, Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
“Msako huu wa kuwakamata wahamiaji haramu unaendelea kufanyika katika maeneo mbalimbali mkoani Morogoro na hadi sasa wahamiaji haramu 48 wamekamatwa katika maeneo mbalimbali kwa kipindi cha Septemba mwaka jana hadi Januari mwaka huu,” alisema Naibu Kamishna wa Uhamiaji Mkoa wa Morogoro.
Hivyo alisema baadhi ya wahamiaji hao tayari wameshafikishwa mahakamani na kutozwa adhabu na pia kurejeshwa nchini kwao na wengine kesi zao zikiendelea kusikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa.
Kwa habari, matukio na michezo ni hapahapa Tangakumekuchablog

No comments:

Post a Comment