Uchambuzi huu wa magazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cjha Elimu Cha Candle Education Centre Tanga. Kituo kipo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 772746
MWANANCHI
Siku tatu baada ya Baraza Kuu la Chadema kuridhia kumpumzisha kwa muda Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa baada ya kutofautiana na Kamati Kuu kwa kumkaribisha waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kiongozi huyo amesema yupo salama na wakati mwafaka ukifika atazungumza ya moyoni.
Dk Slaa alisema amekuwa akisikia mengi yakisemwa juu yake lakini yote yamekuwa yakimchekesha tu.
Hakuhudhuria vikao muhimu vya chama hicho na vile vya Ukawa, vikiwamo; wakati Lowassa akitambulishwa rasmi, akichukua fomu, kikao cha Baraza Kuu na juzi Mkutano Mkuu na hakuwa akipatikana kwa simu yake ya mkononi.
Wakati kimya kikitawala juu ya hatima yake, baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa vikiandika kuwa amejivua uanachama Chadema.
Lakini jana alisema: “Naangalia mambo mengi yanayoendelea kwenye mitandao halafu ninacheka tu, usifikiri sifuatilii, nafuatilia kinachoendelea na ninabaki nikicheka.”
Kuhusu hatima yake kisiasa na madai ya kujiuzulu uanachama ndani ya Chadema, alisema hawezi kuzungumza lolote kwa sasa na atafanya hivyo wakati mwafaka ukifika. “Usijali wakati wangu wa kuzungumza ukifika nitasema tu, sasa hivi nawaachia mzungumze, lakini nitazungumza,” alisema.
Kadhalika, alipoulizwa kuhusu taarifa zilizozagaa kuwa maisha yake yapo hatarini kwa kuwa anatishwa, Dk Slaa alisema hata hilo pia atalizungumzia wakati mwafaka ukifika.
“Ndiyo hayohayo ninayosema, wala msijali nitazungumza wakati ukifika,” alisema na kusisitiza: “Nipo salama.”
Dk Slaa alisema kwa sasa yupo mapumzikoni nje ya jiji la Dar es Salaam ingawa hakutaka kueleza ni eneo gani.
Juzi, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alifafanua tofauti iliyojitokeza kati ya Kamati Kuu ya Chadema na Dk Slaa wakati wa mchakato wa kumpokea Lowassa.
Katika mkutano huo wa Baraza Kuu la Chadema, Mbowe alisema wamekubaliana katibu mkuu huyo apumzike kwa muda... “Nina hakika kwa tabia na hulka za Dk Slaa… kwa sababu anajua tunampenda na yeye anakipenda chama hiki, tunamwombea kwa Mungu ampe nguvu na ujasiri wa kuona kwamba kauli ya wengi ni kauli ya Mungu.”
Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo na makada wengine wa Chadema, jana walikwenda kuonana na Dk Slaa nyumbani kwake na kufanya naye kikao cha faragha.
Picha zilizomuonyesha Ndesamburo akiwa na Dk Slaa na makada wengine akiwamo Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Jaffar Michael, zilisambaa kwa kasi katika mitandao ya kijamii jana na kuibua mijadala.
MWANANCHI
Mbunge wa Jimbo la Bariadi Magharibi, Andrew Chenge leo atapandishwa kizimbani kuhojiwa na Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma kwa kuhusika katika kashfa ya ‘kuchota’ fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow.
Chenge ni mmoja wa viongozi waliopata mgawo wa fedha kutoka kwenye akaunti hiyo jambo ambalo ni ukiukaji wa sheria namba 13 ya maadili ya viongozi wa umma.
Watuhumiwa wengine ni aliyekuwa waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, mbunge wa Sengerema, William Ngeleja, mkurugenzi wa sheria, Wizara ya Ardhi, Rugonzibwa Mujunangoma na Mnikulu wa Ikulu, Shaaban Gurumo.
Chenge alifungua kesi Mahakama Kuu akipinga kuhojiwa dhidi ya tuhuma za kukiuka maadili ya viongozi baada ya kupokea Sh1.6 bilioni kutoka kwa mkurugenzi wa VIP Engineering, James Rugemalira, fedha ambazo zinahusishwa na akaunti hiyo.
Katika vikao vilivyopita, Chenge alilitaka baraza kutojadili shauri lake kwa sababu kesi yake ya msingi kuhusu fedha za escrow ilikuwa imefunguliwa Mahakama Kuu.
Kashfa ya escrow ilisababisha aliyekuwa waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na waziri wa Ardhi, Profesa Tibaijuka kuondolewa katika nyadhifa zao.
HABARILEO
Licha ya kuanza kwa kusuasua, kazi ya uandikishaji wapigakura katika mfumo wa kielektroniki wa BVR katika Jiji la Dar es Salaam, imepata mafanikio na kuvuka lengo la uandikishaji lililokuwa limewekwa.
Awali, ilikadiriwa watu 2,810, 423 sawa na asilimia 98, lakini baada ya kumalizika kwa siku za uandikishaji juzi, waliojiandikisha wamefikia 2,845,256 sawa na asilimia 101.2 Hayo yamethibitishwa na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damian Lubuva katika taarifa yake aliyoitoa kwa vyombo vya habari jana, kuhusu kukamilika kwa kazi hiyo jijini Dar es Salaam.
Alisema hadi Agosti 4 mwaka huu mkoa wa Dar es Salaam, wananchi waliojiandikisha katika wilaya ya Kinondoni walikuwa 1, 157,617 sawa na asilimia 105, ambapo lengo lilikuwa 1,102,565. Wilaya ya Temeke imeandikisha wapigakura 886,564 sawa na asilimia 98.9 lengo lilikuwa 896,142.
Wilaya ya Ilala imeandikisha wapigakura 886,564 sawa na asilimia 98.9 lengo likiwa ni 811,716. Kutokana na kukamilika kwa uandikishwaji huo, NEC ilitangaza rasmi kukamilika kwa uandikishaji katika mkoa wa Dar es Salaam Agosti 4, hivyo kuhitimisha rasmi uandikishaji wa wapiga kura kwa kutumia mfumo wa kielektroniki wa BVR kwa nchi nzima.
Alisema NEC inasisitiza kuwa hakutakuwa tena na muda wa nyongeza wa kuandikisha wapiga kura. Kazi inayoendelea hivi sasa ni kuweka wazi daftari la awali la wapiga kura pamoja na kutoa fomu za kugombea urais, waliopitishwa na vyama vyao vya siasa.
Alisisitiza kuwa NEC inaendelea kuliweka wazi daftari la kudumu la wapiga kura, ambapo hadi sasa tayari mikoa 19 imekwishapelekewa daftari la awali la wapiga kura. Alisema Dar es Salaam na Zanzibar, mchakato wa kuandaa daftari la awali unaendelea na unatarajiwa kukamilika muda si mrefu kuanzia sasa baada ya uandikishaji kukamilika.
Alisema kazi ya kuweka wazi daftari hilo, linafanyika ili kutoa fursa kwa wale wote waliojiandikisha, kusahihisha taarifa zao, kuhamisha taarifa za wapiga kura waliohama kutoka kata au jimbo moja kwenda kata au jimbo lingine, kutoa kadi kwa wapiga kura waliopoteza kadi zao na kuangalia iwapo taarifa za mpiga kura aliyejiandikisha zipo kwenye daftari.
Pia, kuweka pingamizi kwa jina au taarifa za mpiga kura asiye na sifa ya kuwemo katika daftari la kudumu la wapiga kura. Alisema kazi ya uandikishwaji katika mkoa wa Dar es Salaam na nchi nzima imefanyika na kukamilika kwa mafanikio makubwa, licha ya changamoto za zilizojitokeza hasa katika hatua za mwanzo za uandikishaji.
Uandikishaji huo kwa mkoa wa Dar es Salaam ulianza rasmi Julai 22 na kufanyika kwa siku 10, muda ambao haukutosheleza kutokana na idadi kubwa ya wananchi waliojitokeza hali ambayo tume ililazimika kuongeza siku nne zaidi.
“Hii inatafsiriwa kuwa imetokana na mwamko mkubwa wa wananchi waliojitokeza kujiandikisha katika daftri la kudumu la wapiga kura ikilinganishwa na miaka mingine iliyopita,” alisema.
Sambamba na hilo, tume inaendelea na kazi ya utoaji fomu za urais kwa wagombea urais na wenza wao, ambapo hadi kufikia jana jumla ya vyama vya siasa vitano tayari wagombea wake wameshachukua fomu.
Hivyo ni United People Democratic Party (UPDP), Tanzania Labour Party (TLP), Democratic Party (DP), Chama cha Umma (CHAUMMA) na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
HABARILEO
Wanachama wa Chama cha Wananchi (CUF) jana walimbana Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Prof. Ibrahim Lipumba wakimtaka kueleza ukweli juu ya taarifa zinazodai kuwa amejiuzulu wadhifa huo.
Wanachama hao walifika asubuhi na kukusanyika katika Ofisi za Makao Makuu ya CUF Buguruni, Dar es Salaam, kwa lengo la kujua hatma ya kiongozi wao huyo. Walipofika hapo, alikuwa na kikao kirefu na wazee na viongozi wa dini kuhusu kile alichotaka kukieleza mbele ya vyombo vya habari. Baada ya kuwepo kwa kelele nyingi na za muda mrefu, zilizokuwa zikipigwa na wanachama hao zaidi ya 200, waliokuwa wakiimba nyimbo mbalimbali, ilimlazimu Profesa Lipumba kutoka ofisini kwake na kuwatuliza.
Hata hivyo, wanachama hao waliendelea kubaki na sintofahamu kutokana na yale aliyowaambia. Lipumba aliwataka wanachama hao, kuielewa vizuri Katiba ya CUF, kwa kuwa chama hicho kinaendeshwa kwa kufuata Katiba. Alieleza kuwa kila mwanachama kwa nafasi yake, anatakiwa kukijenga chama hicho.
“Mwaka 1995 nilikuwa ni mwanachama wa kawaida na niliteuliwa kuwa mgombea urais. Chama chetu ni taasisi, tena kubwa na sio mtu mmoja, hivyo tujenge chama chetu kama taasisi,” alisema Profesa Lipumba kisha kurudi ofisini kwake.
Hata hivyo, wanachama hao waliendelea kupiga kelele za kutaka ufafanuzi wa kauli hiyo, ambayo wengi walidai kuwa haijaeleweka inamaanisha nini. Mmoja wa viongozi wa dini, aliyejitambulisha kuwa ni Mchungaji Godfrey Sombi alisema hali si shwari, kwani Profesa Lipumba anataka kubaki mwanachama wa kawaida ndani ya chama hicho.
Mchungaji Sombi alisema sababu kubwa ni kutokana na baadhi ya viongozi wa Umoja wa vyama vinne vya upinzani (Ukawa), ambao chama hicho ni miongoni mwa vinavyounda umoja huo, kuvunja malengo yake.
“Hajaridhishwa na ujio wa Lowassa (Edward) ndani ya Ukawa na kupewa nafasi ya kupeperusha bendera kwa nafasi ya urais, kwa hiyo anataka kubaki kuwa mwanachama wa kawaida,” alisema kiongozi huyo wa dini.
Lowassa amejiunga na Ukawa kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wiki moja iliyopita na juzi aliteuliwa kuwa mgombea urais wa chama hicho na umoja huo, wenye vyama vinne vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, baadhi ya wanachama wa CUF walimtaka Profesa Lipumba kuweka wazi kuhusu taarifa zinaripotiwa na vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
Walitaka Profesa huyo maarufu wa Uchumi na aliyegombea urais mara nne tangu mwaka 1995, aendelee kuwa kiongozi wao, kwani wana imani naye. Abdallah Simba alisema kauli iliyotolewa na Profesa Lipumba, bado imewafumba macho, kwani hawaelewi ukweli wa taarifa za kujiuzulu na walitegemea angetoa taarifa za kukanusha kujiuzulu ndani ya chama hicho au kueleza kinachoendelea.
Juzi hakuwapo wakati Lowassa akipitishwa na Mkutano Mkuu wa Chadema kuwa mgombea urais pamoja na Mgombea Mwenza, Juma Duni Haji ambaye alikuwa Makamu Mwenyekiti wa CUF Zanzibar na sasa amehamia Chadema.
Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad alihudhuria mkutano huo, uliofanyika Dar es Salaam na alitangazwa kuwa Mgombea wa Urais wa Ukawa kwa Zanzibar.
HABARILEO
Wizara ya Maliasili na Utalii imeanza kufanya uchunguzi kwa kushirikiana na mamlaka mbalimbali, ikiwemo Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) na vyombo vya ulinzi na usalama ili kubaini waliohusika na upitishwaji wa nyara za serikali katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) hivi karibuni.
Wizara hiyo pia imeeleza kupokea kwa masikitiko makubwa taarifa hizo za kukamatwa kwa nyara za serikali katika Uwanja wa Ndege wa Zurich nchini Uswisi zikiwa njiani kwenda China kutokea Uwanja huo wa Ndege wa Kimataifa wa JNIA wa jijini Dar es Salaam.
Taarifa ya wizara hiyo kwa vyombo vya habari iliyosainiwa na Waziri Lazaro Nyalandu ilisema wizara hiyo inaupongeza uongozi wa Uwanja wa Ndege wa Zurich na Serikali ya Uswisi na watu wote walioshiriki kubaini na kukamata nyara hizo.
Waziri Nyalandu alisema, nyara hizo zinajumuisha meno ya tembo yenye uzito wa kilo 262, kucha na meno ya simba vyenye uzito wa kilo moja.
Alisema tukio la kukamatwa kwa nyara hizo lilitokea kwenye uwanja huo Julai 6, mwaka huu zikiwa ndani ya masanduku manane zikiwa njiani kwenda Beijing China kutokea uwanja wa ndege wa Dar es Salaam kupitia Zurich.
“Wizara imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa hizi na kwamba nyara hizo zimesafirishwa kupitia Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere. Tukio hili linadhihirisha kuwa tatizo la ujangili bado linaendelea ndani na nje ya nchi yetu” alisema.
HABARILEO
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohammed Othman Chande amesema kitendo cha Rais Jakaya Kikwete kufanya uteuzi wa mara kwa mara wa majaji nchini, kimeongezea kwa kiasi kikubwa utendaji wa Idara ya Mahakama na hadi sasa kuna Majaji takribani 100, jambo ambalo halijawahi kutokea miaka ya nyuma.
Aidha, ameahidi kutokana na wingi wao, sasa wana uhakika wa kuongeza uchapaji kazi na kwa kuanzia, wameweka lengo kwamba, kesi zote katika Mahakama Kuu na Mahakama ya Biashara zisiendeshwe zaidi ya miezi 10.
Jaji Chande alikuwa akizungumza na waandishi wa habari Ikulu, Dar es Salaam jana mara baada ya Rais Kikwete kuapisha Majaji wa Mahakama Kuu 13 na Jaji mmoja wa Mahakama ya Rufani. “Tunamshukuru Rais kwa ongezeko hili la majaji ambalo sasa linaifanya Tanzania kuwa na majaji 100, hawa ni wengi haijawahi kutokea,” alisisitiza.
Alisema ongezeko hilo, litasaidia sekta hiyo kushughulikia tatizo la mlundikano wa kesi hasa katika kanda za Mahakama Kuu, ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikielemewa na kesi nyingi.
Alitaja kanda ambazo zina mzigo wa kesi nyingi, ambazo sasa zitapunguziwa mzigo huo kutokana na ongezeko hilo la majaji kuwa ni Kanda ya Mahakama Kuu ya Bukoba, ambayo Jaji mmoja alikuwa akishughulikia kesi 3,000 na Mwanza jaji mmoja kesi 600.
Aidha, alisema ongezeko hilo litasaidia maeneo mengine yenye kesi nyingi pia, ambayo ni Tabora na vitengo vya Mahakama Kuu kama vile Idara ya kazi, Ardhi na Biashara. Alisema tayari sekta ya Mahakama ilishajiwekea mikakati ya kushughulikia changamoto zinazoikabili sekta hiyo, ikiwa ni pamoja na kubadilisha ratiba, ambapo kwa upande wa Majaji walipangiwa Jaji mmoja sasa kusikiliza kesi 220, Hakimu Mkazi wa wilaya na Mkoa kesi 250 na Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo kesi 260.
“Kila Mahakama pia imewekewa malengo yake na lengo kubwa ni kuhakikisha kesi hazichukui muda mrefu kusikilizwa, kwa mfano kwa mujibu wa mabadiliko haya kitengo cha Biashara cha Mahakama Kuu kesi zake hazitosikilizwa kwa muda wa zaidi ya miezi 10 hadi mwaka mmoja,” alisisitiza.
Aliwataka majaji walioteuliwa na kuapishwa jana kutambua kuwa waliteuliwa katika nyadhifa hizo, kutokana na utendaji, uzoefu na uadilifu wao, hivyo wanapaswa kuhakikisha wanadumisha sifa hizo katika utendaji wao.
Alisema kabla ya majaji hao hawajaanza rasmi kazi, wataandaliwa mafunzo maalum ili waweze kuendana na utaratibu wa kimahakama kwa kuwa kati ya majaji hao, watano walikuwa mawakili wa kujitegemea, watano mawakili wa Serikali na watano walikuwa mahakamani.
Akizungumzia suala la uchaguzi, Chande, alisema tayari wamejipanga kuhakikisha kuwa kesi za uchaguzi zinasikilizwa kwa haki na muda ambapo hazitosikilizwa kwa zaidi ya miezi sita.
Kuhusu Majaji waliotuhumiwa kupatiwa mgawo wa fedha za akaunti ya Escrow, alisema tume iliyoundwa kufanya uchunguzi na upelelezi, tayari imekamisha upelelezi wake wa awali na itakapokamilisha kuuandaa, itaukabidhi rasmi kwa mamlaka ya uteuzi (Rais) kwa hatua zaidi.
Majaji hao ni Profesa Eudes Ruhangisa anayedaiwa kupata Sh milioni 400.25 na Aloysius Mujulizi Sh milioni 40.4. Awali, akizungumza na gazeti hili kuhusu uteuzi wake, Jaji wa Mahakama Kuu Ignas Kitusi, alisema kuna mipango mingi ya kuboresha huduma za Mahakama, ambapo aliahidi pamoja na wenzake kutekeleza mipango hiyo ikiwemo kurejesha imani ya wananchi dhidi ya Mahakama ambayo kwa sasa imepotea.
NIPASHE
Mahakama ya Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam, imemhukumu Ofisa Mhifadhi Wanyamapori wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Richard Nchasi, kulipa faini ya Sh. 900,000 au kwenda jela miaka mitatu baada ya kukutwa na makosa matatu.
Hukumu hiyo ilisomwa na Hakimu Mkazi, Juma Hassan, juzi baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri na kumtia mshtakiwa hatiani kwa makosa hayo matatu.
“Kati ya makosa manne, mahakama imemtia hatiani mshtakiwa kwa makosa matatu ya kutumia nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri kwa kutoa hati za uwindaji wa wanyama,” Hakimu Hassan.
Hata hivyo, mahakama hiyo ilisema upande wa Jamhuri umeshindwa kuthibitisha shitaka la kuisababishia wizara hiyo hasara ya Dola 1,860 za Marekani (sawa na Sh. 2,976,000).
NIPASHE
Matukio ya uvamizi wa vituo vya polisi yanayokwenda sambamba na kupora silaha, kuua askari na kujeruhi imebainika kuwa yanasukwa na baadhi ya watumishi wasiokuwa waaminifu waliopo ndani ya Jeshi la Polisi au waliofukuzwa kwa makosa mbalimbali ukiwa ni mkakati wa kumdhoofisha kiutendaji Mkuu wa Jeshi hilo IGP, Ernest Mangu.
Uchunguzi wa kina umebaini kuwa hatua ya baadhi ya askari polisi kuasi ndani ya jeshi hilo kunatokana na kuchukizwa na mambo kadhaa yaliyofanywa na IGP Mangu tangu alipoteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kushika wadhifa huo.
Baadhi ya watumishi wa serikali waliozungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti walisema mambo ambayo yamechukizwa baadhi ya watu ndani ya jeshi hilo ni kutokana na kufukuzwa kazi askari wengi na wengine kubadilishwa vituo vyao vya kazi kwa sababu mbalimbali, mambo ambayo yamefanyika kipindi cha IGP Mangu.
“Unakumbuka wakati Sanya (Laurance Sanya) alipokuwa RPC Mbeya kulitokea tukio moja la uvamizi wa Kituo cha Polisi Tunduma lakini kipindi cha utawala wa IGP Mangu yamejitokeza mengi hapa kuna sababu,” alisema.
Alisema IGP Mangu amekuwa mkuu wa Jeshi la Polisi ambaye ameongoza kufukuza askari hususani wanaokula rushwa ambao hakuwavumilia na ndiyo hao hao wamegeuka kuwa adui wa jeshi hilo kwa kushirikiana na jamaa na ndugu zao ambao bado wapo ndani ya utumishi wa jeshi hilo.
Jambo la pili lililojenga hasira kwa askari hao ni hatua ya IGP Mangu kutoa tishio kwamba askari wote ambao wana vyeti vya kughushi wajisalimishe.
“Taarifa za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) inaonyesha kuwa zaidi ya watumishi 10,000 wa Jeshi la Polisi wana vyeti vya kughushi lakini kwa bahati mbaya katika awamu zote za utawala wahusika wamekuwa wakiachwa bila kuchukuliwa hatua na sasa IGP Mangu amekuja kuyavumbua,” kilisema chanzo kutoka ndani ya serikali.
Chanzo hicho kilieleza kuwa baada ya IGP Mangu kutoa tamko la kutaka watumishi ndani ya jeshi hilo wenye vyeti vya kughushi wajisalimishe ndipo matukio ya uvamizi wa vituo vya polisi yalipoibuka kwa kasi ili mkuu huyo wa Jeshi la Polisi aonekane ameshindwa kazi na kufukuzwa.
Anaeleza kuwa kuhusisha matukio ya uvamizi huo na suala la ugaidi inaweza kuwa siyo kweli kwa asilimia kubwa kwa sababu mara nyingi magaidi wanaofanya matukio makubwa mfano nchi jirani wanakuwa na silaha kubwa kama AK-47 sasa inawezekanaje kama kweli ni magaidi hapa kwetu wawe wanapora bunduki ndogo za SMG.
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Hellen Kijobisimba, alisema matukio ya uvamizi wa vituo vya polisi yameanza kujitengeneza pole pole na sasa yamekuwa makubwa.
Alisema wakati hali ya kiuslama ikibadilika, Jeshi la Polisi kwa upande wake bado halijabadilika ili kukabiliana na matukio hayo.
“Zamani usingeweza kuona askari anayetembea barabara ananyang’anywa silaha hata kama huyo askari yukoje, lakini hivi sasa polisi wapo kwenye doria wanavamia na kunyanng’anywa silaha, wanaenda kama vile nyumbani kwao na bahati mbaya polisi wenyewe hawajashtuka,” alisema.
Kijobisimba alisema polisi wangekuwa wamebadilika kiutendaji matukio hayo yasingetokea.
Alisema sababu nyingine ya kuibuka kwa matukio hayo ni ndani ya Jeshi la Polisi lenyewe kuna tatizo ambalo inabidi litafutiwe ufumbuzi.
NIPASHE
Idadi ya wahandisi waliosajiliwa nchini imeongezeka kutoka 6,868 na kufikia 15,364 katika kipindi cha miaka 10.
Kati ya wahandisi hao 15,364, wahandisi wazalendo ni 13,901 na wa kigeni 1,463.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi, Steven Mrope, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam juzi.
Mhadisi Mrope alisema katika kipindi hicho, jumla ya kampuni za ushauri wa kihandisi 279 zilisajiliwa na kati ya hizo, 201 ni ya kizalendo na 78 za kigeni.
Aidha, alisema idadi ya wahandisi washauri ni 459 ambapo kati yao, 356 ni wazalendo na 103 wageni.
“Bodi imeendelea kutembelea na kukagua hali ya uhandisi katika halmashauri zote Tanzania bara, ukaguzi huo umewezesha halmashauri nyingi kutambua umuhimu wa kuajiri wahandisi na kuwatumia katika miradi ya ujenzi,” alisema Mrope.
Alisema hiyo pia imewezesha idadi ya wahandisi katika halmashauri kuongezeka kutoka 129 mwaka 2003 hadi kufikia 508 mwaka 2015.
“Ingawa idadi hiyo ya wahandisi bado ni ndogo, lakini ni dhahiri ubora wa kazi katika halmashauri umeongezeka,” alisema.
Aliongeza kuwa Bodi imefanikiwa pia kuongeza idadi ya wahandisi wataalam wanawake kutoka 20 waliosajiliwa mwaka 2011/12 hadi 80 waliosajiliwa mwaka 2013/14 mpaka kufikia 176 kwa sasa.
Aliongeza kuwa baada ya mabadiliko ya Sheria, Bodi imeanza kusajili mafundi sanifu ambao ndiyo wasaidizi wakuu wa wahandisi na mpaka sasa mafundi sanifu 157 wamesajiliwa.
Mhandisi Mrope alisema moja ya majukumu ya Bodi ni uendelezaji wa taaluma ya kihandisi ili kufanya wahandisi waende sambamba na mabadiliko ya kisayansi na kiteknolojia.
Kwa habari,matukio na michezo ni hapa hapa tangakumekuchablog
No comments:
Post a Comment