Wednesday, December 28, 2016

AFUKIWA NA JABALI WAKATI AKICHIMBA MAWE AMBONI TANGA



Tanga, MKAZI wa Kongwa Mkoani Dodoma aliefahamika kwa majina ya Thomas Michael (30) amekufa papo hapo baada ya kufukiwa na kifusi wakati akichimba kokoto kijiji cha Mafuriko Amboni Mkoani Tanga.
Tukio hilo lililotokea juzi saa 12 ;30 jioni na kuthibitishwa na kamanda wa polisi Tanga, Benedickt Wakulyamba, baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo walisema walisikia mshindo mkubwa  ndani ya machimbo hayo ya kokoto na mawe.
Wakazi hao walisema Michael kwa miaka mingi amekuwa akijishughulisha na uchimbaji wa mawe na kokoto katika machimbo hayo  na amekuwa akiendesha maisha yake kwa kutegemea kuuza mawe na kokoto.
“Nilikuwa narejea nyumbani baada ya kumaliza uchimbaji ng’ambo ya pili ya machimbo haya, nilisikia kishindo kikubwa lakini nikajua maeneo haya ni kawaida tu” alisema Mussa Ally na kuongeza
“Huyu marehemu alikuwa peke yake na ni mtu anaefahamika sana na alikuwa na bidii kwani huchimba mawe hadi wakati mwengine kiza kinaingia ila niseme kuwa  ni ahadi yake imefika” alisema
Ali alisema wachimbaji wengi wa kokoto na mawe katika machimbo hayo ya Mzizima hawana zana za kuchimbia badala yake wamekuwa wakitumia za asili za mitarimbo na nyundo.
Akithibitisha kutokea tukio hilo, kamanda wa Polisi Mkoani Tanga, Benedickt Wakulyamba, alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa hospitali ya Bombo kusubiri familia ya marehemu kwa ajili ya taratibu za mazishi.
Alisema wakati wa uokozi gari ya kwanza iliyotumwa haikufanikiwa baada ya kuwa na vifaa duni  ambavyo havikuweza kuhimili ufukuzi baada ya jabali hilo kuwa kubwa.
“Kazi utafutaji wa mwili wa marehemu haikuwa kazi rahisi kwani tulidhani ni kifusi cha mchanga bali ni jabali kubwa lililomeguka, tulimaliza kazi ile saa sita usiku na kufanikiwa kuukuta mwili ukiwa umekufa” alisema Wakulyamba
Akitoa wito kwa wachimbaji wa kokoto na mawe katika eneo la machimbo ya Mzizima, kamanda Wakulyamba, aliwataka kuchukua tahadhari kwani miamba hiyo kwa muda mrefu iko na nyufa nyingi.
                                                      



 Wakazi wa kijiji cha Mzizima Amboni Tanga wakiangalia eneo ambalo Thomas Michael alifukiwa na jabali na kufa hapo hapo wakati akichimba mawe.





No comments:

Post a Comment