Friday, December 9, 2016

HADITHI, ALIYEMUUA MCHUMBA WANGU SEHEMU YA 3

HADITHI
 
ALIYEMUUA MCHUMBA WANGU 3
 
ILIPOISHIA
 
Alikuwa karani wa mhakama aliyekuwa amesimamishwa kazi kutokana na tuhuma ya kupoteza kwa makusudi faili la kesi muhimu akiwa na lengo la kupoteza ushahidi.
 
Alikuwa nje kwa dhamana na kesi yake ilikuwa ikiendelea mahakamani.
 
Pamoja na kudai kuwa alikuwa na mchumba, Maria alianza kubadilika kidogo dogo na kuendeleza uhusiano wake na James. Ilifikia wakati ambapo James alimuuliza kuhusu mchumba aliyekuwa naye.
 
“Sina mchumba” Maria akamjibu.
 
“Si uliniambia una mchumba wako?’
 
“Nilikudanganya tu. Nilitaka kukupima nione kama utabadilika na pia nilitaka kukujua vizuri”
 
“Tangu mwanzo nilihisi kuwa unanidanganya”
 
“Unajua nini…nilitaka kukujua vizuri”
 
“Sasa umeshanijua vizuri”
 
“Sana”
 
“Ninafaa kuwa mchumba wako”
 
“Unafaa sana. Kawaone wazazi wangu. Kwa bahati njema wapo hapa Dar”
 
SASA ENDELEA
 
Kwa kuonesha kweli alikuwa na nia ya kumuoa Maria, James hakuchelewa kuwaona wazazi wa Maria na kukamilisha taratibu za uchumba. Sasa wakawa ni wachumba wawili waliotarajia kuoana wakati wowote.
 
                                    ************
 
James Matei alikuwa mngoni aliyesomea Dar. Alipomaliza elimu ya chuo kikuu aliajiriwa na Wizara ya Mambo ya Ndani kama mtaalamu wa kompyuta. Baada ya kufanya kazi kwa mwaka mmoja tu alifanikiwa kununua gari lake alilokuwa akilitumia na alikuwa akiishi kwenye nyumba ya kupanga iliyokuwa Msasani.
 
Siku moja wakati akipata chakula cha mchana kwenye hoteli moja iliyokuwa kati kati ya jiji la Dar, alifika mtu mmoja ambaye alikaa kwenye meza moja na yeye, lakini mtu huyo aliagiza soda.
 
James alikuwa ameshamaliza kula, sasa alikuwa akijiandaa kuondoka.
 
“Samahani, nilikuwa nataka kukuuliza kitu” Mtu huyo aliyekuwa amevaa pama jeusi alimwambia James.
 
“Bila samahani, unaweza kuniuliza”
 
“Mimi naitwa Pascal, kama sikosei wewe ni Mr James Matei?”
 
“Ndiyo mimi”
 
“Sawa. Unamfahamu msichana mmoja anayeitwa Maria, aliwahi kuwa mfanyakazi wa mahakama”
 
James akashituka kidogo.
 
“Namfahamu. Ana nini?”
 
“Ni kweli kwamba ni mchumba wako?”
 
“Ndiyo ni mchumba wangu”
 
“Mnatarajia kuoana lini?”
 
“Kwani wewe ni nani?”
 
“Mtajie Maria jina langu, ananifahamu vizuri tangu Arusha”
 
Mtu huyo akainuka huku akitabasamu.
 
“Sasa ulikuwa na maana gani kuniuliza?” James aliendelea kumuuliza akiwa amepatwa na mshangao.
 
“Usijali, ni kutaka kujuana tu” Mtu huyo alimjibu na kuondoka.
 
James akabaki kumsindikiza kwa macho. Mtu huyo alipotoka kwenye mlango wa hoteli James akampigia Maria.
 
Maria alipopokea simu, James Alimuuliza.
 
“Unamfahamu mtu mmoja anayeitwa Pascal?’
 
“Pascal nani?” Sauti ya Maria ikauliza kwenye simu.
 
“Hakunitajia anaitwa Pascal nani lakini ameniambia nikikutajia jina hilo utamfahamu?”
 
“Mlikutana wapi?”
 
“Tulikutana hapa hoteli sasa hivi”
 
“Bado yupo hapo?”
 
“Ameshaondoka”
 
“Kwa kweli mimi simfahamu”
 
“Ameniambia mnajuana tangu Arusha”
 
“Simfahamu. Mlianzaje maneno yenu?”
 
“Nilikuwa nakula chakula akaja kuniuliza kama mimi ni James Matei. Nikamwambia ndiye mimi. Akaniuliza tena kama ninamfahamu Maria. Nikamjibu ninamfahamu”
 
“Maria wako wengi, alikwambia Maria nani?”
 
“Hakunitajia Maria nani lakini aliniambia aliwahi kuwa muajiriwa wa mahakama, nikajua ni wewe”
 
“Baada ya hapo alikwambia nini?”
 
“Alitaka kujua kama mimi ni mchumba wako”
 
“Ulipomjibu akasemaje?”
 
“Akaondoka”
 
“Huyo mtu mimi simfahamu. Ni wambea tu wa mjini, achana naye”
 
“Alitaka kujua tu kama mimi na wewe tuwachumba na tutaoana lini!”
 
“Huo ndio umbea wenyewe. Achana naye. Umeshakula mpenzi wangu?”
 
“Ndio nataka kuondoka”
 
“Umekula nini?”
 
“Ndizi kwa nyama”
 
“Sawa. Tutaonana jioni ukitoka kazini”
 
“Sawa”
 
James alikata simu akainuka na kutoka. Wakati anatoka alimuona yule mtu ameegemea moja ya magari yaliyokuwa kwenye eneo la maegesho la hoteli akizungumza kwenye simu.
 
Mtu huyo alipomuona James alifungua mlango wa gari akajipakia na kuondoka. Kwa haraka James akalifuata gari lake akaliwasha na  kuliandama gari la mtu huyo.
 
Kwa vile Maria alishamthibitishia kuwa alikuwa hamjui mtu huyo, James alitaka kumfuatilia ili aweze kumuelewa ni nani na anatoka wapi.
 
Lakini kusudio lake halikutimia. Aliweza kuwa nyuma yake katika mitaa miwili tu, kufika mtaa wa tatu gari hilo lilimchenga. Hakuliona tena. Ikambidi James arudi kazini kwake.
 
Wakati wote akiwa ofisini alijiuliza mtu yule ni nani na kwanini alitaka kujua kuhusu uchumba wake na Maria. Alipoona hapati jibu akaamua kuachana na mawazo hayo. Aliendelea na kazi zake hadi jioni alipotoka ofisini.
 
Alikwenda moja kwa moja nyumbani kwa Maria Kinondoni. Wakati anaikaribi nyumba ya Maria alishituka alipoliona gari la yule mtu aliyemuandama likiondoka nyumbani kwa Maria.
 
“Huyu mtu anafahamiana na Maria?” James akajiuliza bila kupata jibu. Alilisimamisha gari akashuka na kuelekea kwenye mlango wa nyumba ya Maria.
 
Aliusukuma mlango na kuingia ndani. Alimkuta Maria akitoka kuoga.
 
“Ndio unafika?” Maria akamuuliza.
 
Badala ya kumjibu James naye alimuuliza.
 
“Ulikuwa na mgeni yeyote humu ndani?” 
 
“Mgeni gani?’
 
“Yule mtu nilimuona akiondoka na gari hapo nje”
 
“Mtu yupi?”
 
“Yule niliyekueleza kwenye simu”
 
ITAENDELEA

No comments:

Post a Comment