HADITHI
ALIYEMUUA MCHUMBA WANGU 7
ILIPOISHIA
Jibu hilo la mkato
liliwavunja nguvu polisi hao ambao walilazimika kuondoka ofisini hapo. Dodosa
dodosa ya Inspekta Amour kwenye mitaa ya Temeke ilimfikisha katika nyumba
ambayo ilielezwa alikuwa akiishi Pascal.
Inspekta Amour alipolitaja
jina la Pascal, mwanamke aliyekuwa amemkaribisha kwenye nyumba hiyo alitoa
tabasamu la huzuni.
“Mbona Pascal sasa hivi ni
marehemu, Pascal alishakufa” Mwanamke huyo alimwambia Amour aliyeonekana
kushangaa.
“Alikufa
lini?”
“Sasa
ni karibu miezi mitatu”
“Unamzungumzia Pascal Lazza aliyekuwa
akifanya kazi kiwanda cha mabati?”
“Ndiye yeye ninayekwambia,
alishakufa. Mimi hapa ninayekueleza ni mjane wake”
“Ninapata taabu kuamini kwa
sababu Pascal amekuwa akionekana na anawasiliana na watu”
Mwanamke
huyo akashituka.
“Pascal
ameonekana wapi?”
SASA ENDELEA
“Ameonekana
jana na karibu wiki hii yote”
“Wapi?”
“Hapa
hapa Dar es Salaam”
Mwanamke
huyo licha ya kushituka alitikisa kichwa.
“Si
kweli. Mtu aliyekufa ataonekanaje?’
“Kuna mtu alimuona jana
Kinondoni akiwa na gari aina ya Toyota Corolla ya rangi ya kijani”
“Itakuwa
si yeye. Kwanza marehemu hakuwa na gari”
Inspekta
Amour akatikisa kichwa.
“Ninahisi kwamba unanificha.
Pascal yuko hai, ninaomba uniambie yuko wapi?”
Mwanamke
huyo akanywea.
“Hebu
njoo ndani” alimwambia Amour huku akirudi ndani.
Amour aliingia ndani na
kukaribishwa sebuleni. Aliiona picha kubwa ya Pascal Lazza ikiwa imetundikwa
kwenye ukuta. Sura ya Pascal aliitambua baada ya kuilinganisha na ile aliyoiona
kwenye kivuli cha shahada ya Pascal iliyokuwa imesajiliwa kwenye mtandao wa
simu.
Lakini picha hiyo iliyokuwa
imetundikwa ilimpa alama ya kuuliza baada ya kuona ilikuwa imezungushiwa shada
la maua kuonesha kuwa hakuwa hai.
“Nisubiri” Mwanamke huyo
alimwambia Amour. Akaingia chumbani. Baadaye kidogo alitoka akiwa ameshika
gazeti na kitabu cha picha.
Alimpa
Inspekta Amour lile gazeti.
“Kama unakumbuka kulitokea
ajali ya gari eneo la Kimara miezi miwili iliyopita ambapo watu wawili walipoteza
maisha” Mwanamke huyo alimwambia Amour.
“Kama
kulitokea ajali…?’
“Miongoni mwa hao waliokufa
alikuwa mume wangu, angalia kwenye gazeti habari zao ziliandikwa”
Amour akaliangalia lile
gazeti. Katika ukurasa wake wa kwanza kulikuwa na picha kubwa ilioonesha gari
lililokuwa limegongwa na kuharibika vibaya sehemu ya mbele. Chini yake kulikuwa
na picha ndogo mbili. Picha moja ilimuonesha Pascal na picha ya pili
ilimuonesha mtu mwingine ambaye Amour hakuweza kumfahamu.
Habari iliyoandikwa ilihusu kugongwa
kwa gari hilo na lori la mafuta ambapo watu wawili waliokuwemo kwenye gari hilo
walifariki dunia hapo hapo. Mmoja wa watu hao alikuwa Pascal Lazza!
Amour aliikumbuka ile ajali
na yeye alifika katika eneo la tukio na aliwashuhudia watu hao. Hakuwa na cha
kupinga.
Alinyamaza
kimya kwa sekunde kadhaa akiwaza.
“Umeamini?”
Mwanamke akamuuliza.
“Mimi
mwenyewe pia nilikuwepo katika eneo la tukio”
“Kuna
picha zake nyingine za maziko ziko hapa kwenye albamu”
“Sitahitaji
kuziona. Acha niende, nitarudi tena kwako baadaye”
Amour
alimrudishia gazeti yule mwanamke, akatoka.
Alimfuata James nyumbani kwa
marehemu Kinondoni lakini aliambiwa James aliondoka dakika chache zilizopita
kuelekea nyumbani kwake.
Akajipakia tena kwenye gari
na kumpigia simu. James alipopokea simu alimuuliza.
“Uko
wapi James?”
“Wewe
nani?”
“Unazungumza
na Inspekta Amour”
“Oh
Inspekta Amour! Niko nyumbani hapa”
“Nanahitaji
kukuona, nitakupataje?”
“Unaweza
kuja nyumbani au kama ni lazima mimi nije huko”
“Acha
nije nyumbani kwako”
“Njoo”
Amour akakata simu na
kuliwasha gari. Kwa vile alikuwa akiifahamu nyumba ya James alimfuata. Alifika
hadi mbele ya nyumba ya James akampigia tena simu.
“Nimeshafika,
niko nje” alimwambia.
“Sawa,
nakuja”
Sekunde chache baadaye James
alifungua geti. Akaliona gari alilofika nalo Amour. Inspekta Amour hakushuka
kwenye gari. James alilifuata gari hilo.
“Zunguka upande wa pili
uingie kwenye gari” Amour alimwambia James.
James alizunguka upande wa
pili wa gari hilo akafungua mlango na kujipakia.
“Kuna kitu ambacho
kimenishangaza sana” Amour akamwambia James kwa sauti tulivu.
“Kitu
gani?” James akauliza.
“Nilikwenda kwenye ofisi za
kampuni inayomiliki ile namba ya Pascal. Pale nilipata maelezo yote kuhusu
yeye. Usajili wake ulionesha kuwa alikuwa mkazi wa Temeke na mfanyakazi wa
kiwanda cha mabati” Amour akaanza kumuleza James.
“Enhee..?”
James akauliza kwa shauku.
“Lakini nilipokwenda kwenye
hicho kiwanda, niliambiwa kuwa Pascal alishaacha kazi karibu miezi sita
iliyopita. Nikajitahidi kupajua mahali anapoishi, nikafanikiwa kuipata nyumba
yake”
Uso wa James ulikuwa kama
unaotaka kutabasamu kwa kuhisi kuwa Pascal alikuwa ameshakamatwa.
“Nilionana na mwanamke mmoja
aliyenieleza kuwa alikuwa mke wa Pascal. Mwanamke huyo alinipa maelezo ya
kunishangaza. Aliniambia kuwa Pascal alikwisha kufa miezi miwili iliyopita
katika ajali ya gari iliyotokea Kimara”
“Amedanganya! Pascal yuko hai
na ndiye aliyemuua mchumba wangu” James alidakia.
“Amenithibitishia kuwa Pascal
amekufa kweli. Alinionesha picha za magazeti. Ile habari iliandikwa kwenye
magazeti na picha ya Pascal nimeiona ni kati ya watu waliokufa”
“Kwani
wewe unamjua Pascal? Ulimuona wapi?”
“Niliona picha yake kwenye
kivuli cha shahada alichosajilia simu yake”
James
akatikisa kichwa.
“Haiwezekani!”
“Ninajua
kuwa haiwezekani ndio sababu nimekufuata hapa”
James
akanyamaza na kumtazama Inspekta huyo.
“Ninataka twende nyumbani kwa
yule mwanamke ukaitazame ile picha halafu uniambie ndiye Pascal uliyemuona
wewe”
“Sawa.
Twende hata sasa hivi”
James alirudi kufunga mlango
kabla ya kuondoka na gari alilokwenda nalo Inspekta Amour.
“Mimi naamini kuwa Pascal
yuko hai. Kunaweza kuwepo na mbinu za kihalifu za kuonesha kuwa amekufa ili
polisi wasiendelee kumtafuta” James alimwambia Amour kwenye gari.
“Wewe
ndiye utakayetuthibitishia Pascal yuko hai au amekufa”
Walipofika Temeke kwenye
nyumba ambayo Inspekta Amour alifika kwa mara ya kwanza na kuzungumza na
mwanamke aliyemueleza kuwa Pascal alikuwa amekufa, walikaribishwa ndani.
“Umerudi
tena?” Mwanamke huyo alimuuliza Inspekta Amour.
“Ndio. Nilikwambia kuwa
ninaweza kurudi. Nimekuja na mtu ambaye alimuona Pascal katika siku za
karibuni, nataka aone zile picha ili aweze kututhibitishia kama ndiye
aliyemuona au la”
ITAENDELEA kesho usikose uhondo huu
No comments:
Post a Comment