Friday, December 16, 2016

UGONJWA WA ZIKA WAGUNDULIKA NCHINI

Virusi vya Zika vyagunduliwa nchini Tanzania

Msitu wa Zika nchini UgandaTaasisi ya utafiti wa magonjwa ya binadamu nchini Tanzania (NIMR) imesema virusi vya Zika vimegunduliwa nchini humo.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Taasisi hiyo, Dkt Mwele Malecela, virusi hivyo vimepatikana mkoani Morogoro, Mashariki mwa Tanzania na Mkoani Geita, kaskazini magharibi mwa Tanzania.
Utafiti huo ulifanyika kutokana na uhalisia kuwa kuna mazingira yanayowezesha kuzaliana kwa mbu wanaoeneza virusi hivyo.
Kati ya watu 533 waliopimwa wakati wa utafiti huo, asilimia 15.6 waligunduliwa kuwa na virusi vya Zika.
Hata hivyo wizara afya nchini humo, imetoa taarifa ambapo inakanusha kuwepo kwa virusi hivyo.
"Kama nilivyoeleza mnamo februari 2016, ugonjwa huu bado haujaingia nchini, na leo pia napenda kuwatoa hofu wananchi kuwa kwa sasa Tanzania haujathibitishwa kuwepo na ugonjwa wa Zika," taarifa ya wizara ya afya imesema.
Wizara hiyo inasema uchunguzi uliofanywa na NIMR ulikuwa wa kuchunguza ubora wa kipimo kipya cha kupima magonjwa ya Zika na Chikungunya.
"Matokeo haya bado yanahitaji kuchunguzwa kwa kina zaidi kupitia vipimo vilivyothibitishwa na Shirika la Afya Duniani," wizara imesema
Dkt Mwele Malecela ameambia BBC kwamba kwa sasa serikali inaangazia kuzuia wajawazito wasiumwe na mbu ambao wanaaminika kueneza virusi hivyo.
"Bado tunajaribu kuangalia ni aina gani ya virusi vya Zika. Lakini hiyo ni dhahiri, tukizingatia kwamba mbu wanaoambukiza Zika wako nchini kwetu na mazingira yaliyoko nchini kwetu hayatofautiani sana na yale ya Amerika ya Kusini na nchi kama Thailand ambako ugonjwa huo unapatikana," amesema Bi Malecela.
"Ugunduzi huu tumeupata kwa watu na tutaendelea kufanya kazi kuangalia kama tutaupata kwa mbu ambao utatuhakikishia basi kwamba ugonjwa huo ina maana umekuwepo nchini ni vile tu ulikuwa haujaonekana."
"Heri nusu shari kuliko shari kamili, kulielewa jambo na kujua kwamba lipo nchini na kujua kwamba wajawazito wanaweza kuzaa watoto wenye matatizo haya kutatuwezesha kuzuia ugonjwa huyu. Tutahakikisha nguvu zetu za kupambana na mbu wanaoeneza virusi hivi zinaongezeka."
Virusi vya Zika zimekuwa vikisababisha watoto kuzaliwa wakiwa na ubongo uliodumaa na vichwa vidogo katika mataifa ya Amerika Kusini na sana Brazil.
Kwa mujibu wa gazeti la Daily News la Tanzania, Dkt Malecela, alipokuwa akitangaza matokeo ya utafiti huo mjini Dar es Salaam alisema uchunguzi wao ulionesha kati ya watoto 80 waliozaliwa wakiwa na matatizo ya kimaumbile, asilimia 43.8 walikuwa na virusi vya Zika.
BBC

No comments:

Post a Comment