Tuesday, December 20, 2016

HADITHI, ALIEMUUA MCHUMBA WANGU SEHEMU YA 9

HADITHI
 
ALIYEMUUA MCHUMBA WANGU 9
 
ILIPOISHIA
 
Msichana akakata simu.
 
Amour akampigia tena. Alishamuona alikuwa jeuri.
 
Msichana akapokea simu.
 
“Sasa mbona unanikatia simu, kwani wewe ni nani wake?”
 
“Kwani alipokupa namba hii alikwambia mimi ni nani wake?”
 
“Mbona tunaulizana maswali dada’ngu, kwani ukinijibu itakuwaje?’
 
“Ulichokuwa unataka wewe ni kujua Pascal yuko wapi au kujua uhusiano wetu?’
 
Amour akajidai kutoa kicheko.
 
“Umekuwa mkali sana lakini ndio tabia ya warembo wengi wa jiji hili, si kitu niambie nitampata wapi Pascal”
 
“Kwa sasa sijui yuko wapi”
 
“Ni muda gani mtakutana?” Amour aliendelea kumuuliza.
 
Msichana akang’aka.
 
“Tukutane wapi? Kwani alikwambia ana mpango wa kukutana na mimi. Wewe kama unamtaka njoo hapa saa mbili usiku. Kama atakuja kunywa utamkuta”
 
SASA ENDELEA
 
“Hapo ni wapi?”
 
“ABC Club Kimara”
 
“Sawa. Bila shaka wewe ni shemeji yangu”
 
“Zamani si sasa”
 
“Una maana siku hizi hampo pamoja”
 
“Yuko pamoja na mke wake, si mimi”
 
“Kwani Pascal anaishi wapi?’
 
“Mimi mwenyewe pia simuelewi, njoo umuulize mwenyewe”
 
“Nikija hapo niulize nani?”
 
“We njoo tu utanikuta”
 
Msichana akakata tena simu. Amor hakumpigia tena. Kutokana na maelezo ambayo Amour aliyapata kutoka kwa msichana huyo, Amour aligundua mambo manne.
 
 Kwanza aligundua kuwa mtuhumiwa aliyekuwa akimtafuta alikuwa amejipachika jina hilo la Pascal na alikuwa akilitumia sehemu nyingi.
 
Pili aligundua kuwa Pascal huyo alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na msichana ambaye aliongea naye kwenye simu lakini kwa muda ule walikuwa wameachana.
 
Tatu aligundua kuwa Pascal alikuwa na mke.
 
Nne aligundua Pascal alikuwa hajulikani anaishi wapi.
 
Na tano Amour aligundua kuwa Pascal alikuwa na kawaida ya kwenda kupata kilevi katika klabu ya ABC iliyokuwa Kimara kila saa mbili ya usiku.
 
Amour akajimbia kama atakula sahani moja na msichana huyo ambaye hakutaka kumtajia jina, huenda akafanikiwa kumtia mbaroni mtu huyo.
 
Dakika chache kabla ya saa mbili usiku Amour alisimamisha gari lililokuwa na namba ya kiraia kwenye eneo la kuegesha la klabu ya ABC Kimara. Ingawa hakuwa amewahi kufika katika klabu hiyo, aliigundua kirahisi kutokana na mabango yaliyokuwa yakimuongoza tangu alipoingia katika eneo hilo.
 
Klabu yenyewe haikuwa na hadhi yoyote ya kuitwa klabu ingawa alikuta magari kadhaa pamoja na pikipiki vilivyokuwa vimeegeshwa nje.
 
Amour alipoingia humo ndani alikuta kumechangamka kiasi. Kulikuwa na wateja wa kuridhisha ingawa hawakuwa wengi. Kazi kubwa ambayo ilimpata Inspekta Amour ambaye wakati ule alikuwa amevaa kiraia, ilikuwa ni kumpata yule msichana aliyeongea naye mchana ambaye hakuwa akimfahamu.
 
Alikaa kwenye meza ya peke yake akawa na kazi ya kuwamulika watumishi wanawake wa mle ndani. Mhudumu mmoja alimfuata akamuagiza bia ya Kilimanjaro ingawa Amour hakuwa akitumia ulevi wa aina yoyote.
 
Mhudumu huyo alipoondoka Amour alitoa simu yake akampigia msichana aliyekuwa ameongea naye mchana. Wakati anapiga simu hiyo macho yake yalikuwa yakiwamulika wasichana wahudumu wa mle ndani. Alitaka kuona nani atapokea simu.
 
Simu ilikuwa inaita lakini hakumuona yeyote aliyekuwa akishughulika na simu. Msichana aliyekuwa amemuagiza bia alikuwa anakuja. Yeye ndiye aliyetoa simu na kuipeleka sikuoni.
 
Amour akasikia sauti ya msichana ikimwambia “Hallo!”
 
Amour akagundua kuwa msichana mwenyewe alikuwa ndiye yule.
 
“Ninayekupigia ni mimi niliyekuagiza bia”
 
“Wewe si ulinipigia mchana?”
 
“Niletee bia yangu tuzungumze”
 
Amour akakata simu.
 
Msichana akairudisha simu yake mfukoni. Akamtazama Amour kwa macho ya kuchangamka. Alikuwa amebakisha hatua chache sana kuifikia meza aliyokuwa amekaa Amour.
 
“Bia ni ya kwako, mimi situmii bia unaweza kunywa sasa hivi au baadaye” Amour alimwambia msichana huyo alipomuwekea chupa ya bia mezani.
 
“Wewe utakunywa nini?” Mhudumu huyo akamuuliza lakini. Sauti yake sasa ilikuwa ya heshima na adabu.
 
“Labda nikusumbue tena, niletee soda na wewe ongeza bia nyingine kama utapenda”
 
Amour alitoa noti mbili za elfu kumi kumi akampa.
 
“Nikuletee soda gani kaka’ngu?”
 
“Niletee cocacola baridi halafu uje tuzungumze”
 
“Usijali”
 
Msichana aliondoka tena na bia yake. Amour alimtazama kwa nyuma. Alikuwa msichana wa kuvutia lakini mwenye uso ulioonesha kiburi. Alikuwa mweupe. Amour aligundua kuwa weupe huo haukuwa halisi. Ulikuwa weupe uliotokana na mkorogo.
 
Alipanga jinsi ya kuzungumza naye. Alijiambia kama takosea kidogo tu huenda msichana huyo akasita kumpa habari sahihi za Pascal.
 
Msichana aliporudi tena alimuwekea chupa ya cocacola, akaifungua na kummiminia kwenye bilauli. Ile chupa ya bia hakurudi nayo. Amour alishukuru alipomuona msichana huyo akiketi naye. Akajua ni ile bia ya bure aliyompa pamoja na pesa.
 
“Mhu…niambie, ulikuwa unasemaje kaka?” Msichana huyo akamuuliza Amour.
 
Amour aliionja cocacola baridi. Alipoirudisha bilauli alimwambia.
 
“Mimi naitwa Amour, wewe unaitwa nani?”
 
“Naitwa Mage”
 
“Pascal aliniambia kama ninamuhitaji nikuone wewe”
 
“Kwani Pascal ni nani wako?”
 
“Ni rafiki yangu tu, sema mji mkubwa huu hatukutani mara kwa mara”
 
Amour alipiga tena funda la cocacola akamtazama Mage.
 
“Pascal alikuwa mpenzi wangu zamani lakini tangu alipooa hana stori na mimi”
 
“Alioa lini?”
 
“Ni muda sasa. Inaweza kufika miaka miwili”
 
“Hivi rafiki yangu yule anafanya kazi gani?’
 
Mage akabetua mabega.
 
“Sijui anafanya kazi gani. Kwani wewe hujui anafanya kazi gani?’
 
“Mimi sijui, sijawahi kumuuliza”
 
“Mimi pia sijui. Dar es Salaam hii watu hawana muda wa kuulizana. Mimi namuona tu akija hapa kunywa na kuondoka”
 
“Ana kawaida ya kuja hapa kila siku?”
 
“Kila saa mbili usiku lazima aje hapa. Mimi na yeye pia tulijuana hapa hapa”
 
ITAENDELEA kesho Usikose Uhondo huu

No comments:

Post a Comment